11 Jan 2017

Kwamba Rais wa Russia, Vladimir Putin na watu wake wa karibu, walitaka mgombea urais wa chama cha Republican cha Marekani, Donald Trump, ashinde uchaguzi wa Urais uliofanyika Novemba mwaka jana, wala sio siri. 

Ilishafahamika kabla ya uchaguzi huo kuwa Putin na "watu wake" hawakutaka Trump awe rais kwa vile wanampenda bali walikuwa na ajenda na maslahi binafsi. Hata hivyo, hadi muda huu ilikuwa haifahamiki ni kitu gani hasa kilichokuwa kikimfanya Rais huyo wa Russia na mashushushu wake kupigana kufa na kupona kuhakikisha Trump anashinda katika uchaguzi huo, kitu ambacho kwa hakika kilitokea.

Kadhalika, Putin na Russia walishapata ushindi hata kabla ya uchaguzi baada ya duru za kiintelijensia, ndani na nje ya Marekani, kuthibitisha kuwa kiongozi huyo wa Russia na mashushushu wake walikuwa wakihujumu uchaguzi huo. Kiintelijensia, huo ni ushindi hata kama matokeo yake hayakujulikana muda huo.

Kwa 'kumwezesha Trump kushinda,' Putin na mashushushu wake waliibuka na ushindi mkubwa zaidi, pengine wa kihistoria katika 'vita ya muda mrefu ya kijasusi kati ya Russia na Marekani.' Kwa 'macho ya kawaida,' nchi hizo mbili zilionekana kama zina maelewano bora kuliko ilivyokuwa katika zama za Vita Baridi. Lakini 'kizani,' nchi hizo zimekuwa kwenye vita kali ya kijasusi, na ambayo inaelezwa kuwa pengine ni kubwa kuliko ilivyokuwa katika zama za Vita Baridi. Hiyo ni mada ya siku nyingine.

Ijumaa iliyopita, wakuu wa taasisi za ushushushu za Marekani walikutana na Rais Mteule Trump kumfahamisha kuhusu uchunguzi wao uliohitimisha kwamba Russia ilihujumu uchaguzi wa Rais wa Marekani, ambao Trump aliibuka kidedea.


Awali kabla ya mkutano huo nyeti, bosi mkuu wa taasisi za ushushushu za Marekani, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (DNI), James Clapper (pichani chini), aliieleza kamati ya bunge la seneti kuwa hujuma zilizofanywa na Russia zipo katika sura nyingi zaidi ya kudukua taarifa za chama cha Democrats, na kumhujumu mpinzani wa Trump, mwanamama Hillary Clinton.

2017-01-05t153806z-1958236086-rc17375221c0-rtrmadp-3-usa-russia-cyber-clapper.jpg

Lakini sasa taarifa zilizopatikana baada ya mkutano wa wakuu hao wa taasisi za ushushushu na Trump zinaeleza kuwa Russia ina kitu kinachofahamika kishushushu kama 'compromising information' kumhusu Trump. Maelezo ya kina kuhusu 'compromising information' yapo katika kitabu changu cha SHUSHUSHU (kinunue hapa), lakini kwa kifupi, ni taarifa ambazo mashushushu wanazo dhidi ya mtu na wanaweza kuzitumia kumshurutisha afanye wanachohitaji wao. Mfano hai, mwanasiasa mmoja huko nyumbani aliwahi kunaswa akifanya 'kitu flani,' kikanukuliwa na 'wahusika,' na amebaki kuwa 'compromised' pengine milele.


Muhtasari wenye kurasa mbili ulioambatana na taarifa ya taasisi hizo za kishushushu za Marekani kuhusu hujuma za Russia ulijumuisha madai kwamba mashushushu wa Rusia wana 'compromosing information' kuhusu Trump. 

Taarifa hiyo imechangiwa na kazi iliyofanywa na jasusi mmoja mstaafu wa Uingereza ambaye kazi zake huko nyuma zinachukuliwa na taasisi za kishushushu za Marekani kuwa ni za kuaminika.

Imefahamika kuwa shirika la ushushushu wa ndani la Marekani, FBI, hivi sasa lipo katika uchunguzi kubaini ukweli kuhusu hizo 'compromising information' kuhusu Trump.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba tetesi kwamba Russia 'ina nyeti kuhusu Trump' zimekuwa zikizagaa kitambo japo hazikuwahi kuzungumzwa na taasisi za kishushushu.

Taarifa moja ya kishushushu 'iliyotolewa usiri' (unclassified) iliyowekwa hadharani Ijumaa iliyopita ilitanabaisha kuwa Putin binafsi alitoa amri ya Russia kumsaidia Trump  kwa kumuumbua mpinzani wake, Hillary. 

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Idara ya ushushushu wa kijeshi ya Russia, GRU, ilikitumia kikundi cha wadukuzi cha WikiLeaks kuvujisha baruapepe mbalimbali kumhusu Hillary na wasaidizi wake wakati wa kampeni za urais zilizomalizika Novemba mwaka jana na Trump kuibuka mshindi.

Endelea kutembelea tovuti hii kwa habari kama hizi kuhusu USHUSHUSHU (bonyeza hapo juu kabisa mwa ukurasa huu palipoandikwa 'intelijensia') na habari nyinginezo.

CHANZO: Habari hii imetokana na vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na HIKI.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube