Nimekuwa nikipokea shutuma na lawama nyingi kwamba ninaichukia CCM na uongozi wake (sana sana nikituhumiwa kuwa na "chuki binafsi").Kadhalika,nimekuwa nikilaumiwa kuwa ninamchukia Rais Jakaya Kikwete,huku wengine wakidai mimi nia Chadema damu damu.
Kawaida yangu ni kutojihusisha na malumbano na wasomaji wa blogu hii.Hata hivyo,ninapotupiwa shutuma kwa lugha ya kistaarabu huwa najaribu kutoa ufafanuzi kuhusu mtizamo na msimamo wangu.Naomba nirejee position yangu.Kwanza,mimi ni Mtanzania,na japo nimekuwa nje ya nchi yangu kwa takriban muongo (decade) moja sasa,haijanipunguzia japo kwa asilimia 0.0001 utanzania wangu.Baba yangu,kaka na dada zangu,wadogo zangu,marafiki,ndugu na jamaa wengi (zaidi ya asilimia 99.9) bado wapo Tanzania.Kwahiyo uwepo wangu hapa Uingereza haunipunguzii utanzania wangu.Kwa mantiki hiyo,kila kinachowagusa Watanzania wenzangu kinanigusa pia,regardless Watanzania hao wapo huko nyumbani au nje ya nchi.
Pili,mimi ni mwanafunzi wa stadi za siasa (political studies).Japo siwezi kujiita mtaalamu wa siasa au kujimilikisha uelewa wa hali ya juu wa siasa,ukweli ni kwamba angalau ninaielewa siasa at an advanced stage.Sasa kuna faida gani ya kuelimika pasipo kuitumikia jamii?Kwa wasiofahamu definition ya elimu,neno hilo linamaanisha jitihada za binadamu katika kukabiliana na mazingira yake.Sasa kama nimeelimika kwenye fani ya siasa,kisha nikaacha kutumia elimu hiyo kuisaidia jamii yangu kwa namna moja au nyingine,basi sintokuwa na tofauti na mafisadi.Ufisadi wa kitaaluma sio tu kufoji vyeti au kutelekeza taaluma na kukimbilia fedha bali pia kutoitumia taaluma ipasavyo.
Tatu,uwepo wangu nje ya nchi umenisaidia kulinganisha na kutofautisha baadhi ya mambo yanayotokea huko nyumbani.Actually,wakati naanzisha blogu hii niliweka bayana approach yangu katika mambo mbalimbali nitakayokuwa nayaongelea humu.Nilibainisha kuwa napendelea kujadili mambo katika namna ya kukosoa.Natambua kuwa sie waswahili hatupendi kukosolewa (at least wengi wetu).Lakini tatizo sio kukosoa bali kukosoa fyongo,kwa mfano kumkosoa mtu kwa vile tu humpendi.Mara kadhaa nimejaribu kuwaeleza wasomaji wangu kuwa,kwa mfano,sina tatizo na Mtanzania mwenzangu aitwaye Jakaya Kikwete bali nina matatizo na kiongozi wa nchi yetu,Rasi Jakaya Kikwete.Na sina matatizo na naye kwa vile yeye ni Mkwere na mie ni Mndamba (by the way wote ni Watanzania) bali tatizo langu kubwa lipo kwenye udhaifu wa uongozi wake.
Kuhusishwa kwangu na Chadema kunatokana na kushabihiana kimtizamo.Chama hicho kimejidhihirisha kuwa mahiri katika mapambano dhidi ya ufisadi na maovu mengine katika jamii yetu.Nami pia hilo ndilo jukumu langu kubwa.Kwangu,faida pekee ya elimu yangu ni pale itakapotumika ipasavyo kuitumikia nchi yangu.Kwa kugusia tu,hata kabla ya kuanza uandishi nilikuwa naitumikia nchi yangu katika namna mbayo Watanzania wengi hawajapata fursa kama hiyo.Nisingependa kufafanua kwa sababu za kimaadili na kisheria lakini tu ieleweke kuwa nami ni miongoni mwa Watanzania wachache kabisa waliokuwa wakikesha macho for several nights a week kuifanya Tanzania yetu kuwa nchi stahili ya kuishi.You could feel the blanks by yourself,if you wish to.
Sasa,pamoja na mabaya mengi ya CCM,kuna baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao kwa hakika kuna nyakati wanastahili pongezi.Na makala hii inamhusu January Makamba.Najua madhara ya kumsifia kiongozi; watu hawakawii kuhitimisha kuwa "aah anajikomba huyu".Well,let anybody make such a silly conclusion lakini penye ukweli sharti tuseme au tuandike.
Gazeti la Mwananchi toleo la leo lina habari kuwa Wizara ya Nishati na Madini imeingia kwenye kashfa ya kuhonga wajumbe wa kamati ya bunge ya nishati na madini ili "bajeti ya wizara hiyo ipite kiulaini huko bungeni".And guess what,aliyefanikisha kufahamika kwa taarifa hizo za kushtua si mwingine bali mwenyekiti wa kamati hiyo,yaani January.Huu ni uzalendo wa kupigiwa mstari.Ukiweka kanda political rhetorics and sentiments ambazo zimezoeleka kwenye competitive politics,January ana mitizamo inayoshairia kuweka mbele maslahi ya nchi badala ya maslahi ya chama chake.Of course,kama kiongozi wa CCM analazimika kuisifia na kuwarushia madongo wanasiasa wa upinzani,lakini hatuwezi kumhukumu kwa yale tusiyayapenda tu.Ndio maana hata katika makala niliyoandika kwenye jarida la Raia Mwema kumkosoa baba wa taifa Julius Nyerere nilibainisha wazi kuwa wengi tunafahamu mazuri ya Nyerere lakini "mabaya" yake yamebaki kuwa muted au taboo kuyaongelea.Kama kuongelea "mabaya" ya Nyerere hakumaanishi kumchukia,kumsifia January Makamba hakumaanishi kuipenda CCM (at least kwa madudu yake na ulezi wake kwa mafisadi).It simply means giving credit where it's due...au kwa kiswahili ni mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
Kwahiyo Mheshimiwa January,natumaini hutoishia tu kwenye kufichua uovu ndani ya kamati yako bali pia utajaribu kusambaza jitihada zako za kizalendo na kwenye maeneo mengine pia.CCM inahitaji viongozi watakaotanguliza maslahi ya nchi mbele ya maslahi ya chama.Haimaanishi msiwe mashabiki wa chama chenu bali nchi yetu ni muhimu zaidi ya chama cha siasa.
Anyway,habari husika ni hii hapa chini
Kashfa nzito Wizara ya Ngeleja
Monday, 04 July 2011 08:44
MAOFISA WA JUU WATUHUMIWA KUIHONGA KAMATI YA MAKAMBA
Mwandishi Wetu
WIZARA ya Nishati na Madini imeingia katika kashfa nzito ambapo baadhi ya maofisa wa wizara hiyo wanatuhumiwa kuwahonga baadhi ya wabunge katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kile kinachodaiwa kutaka bajeti ya wizara hiyo kupita kwa urahisi, Mwananchi limebaini.
Habari zilizopatikana kutoka Dodoma na Dar es Salaam zimedokeza kuwa taarifa za uovu huo tayari zimefikishwa mezani kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amesema atalishughulikia baada ya kuwa amewasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Kwa mujibu wa habari hizo suala hilo pia tayari limefikishwa kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kwamba kamati ya uongozi ya bunge anayoiongoza pia imearifiwa kuhusu suala hilo.
Kashfa hiyo imeikumba wizara hiyo katika kipindi kigumu ambacho nchi iko gizani huku wizara hiyo ikilaumiwa kutokana na uhaba wa nishati ya umeme kiasi cha Waziri Ngeleja kutangaza mgawo wa saa 10 wakati wa mchana na saa sita wakati wa usiku "ni janga la kitaifa".
Habari zaidi zinasema miongoni mwa mambo muhimu ambayo kamati hiyo ilikuwa ikitaka maelezo ni mapendekezo ya wizara hiyo kutaka kujenga jeno la makao yake makuu jijini Dar es Salaam kinyume cha ilani ya CCM ambayo inaweka wazi kwamba hakutakuwa na ujenzi wa makao makuu ya wizara jijini humo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Habari zilizolifikia Mwananchi zilidai kwamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge, January Makamba ndiye aliyewasilisha malalamiko kwa Pinda na Makinda baada ya kubaini 'ulegevu' miongoni mwa wajumbe wa kamati yake wakati wa mchakato wa kujadili mapendekezo ya bajeti ya Wizara hiyo na kwamba mapema alikuwa ameishapokea taarifa kuhusu baadhi ya wajumbe wake kuhongwa.
"Mwenyekiti (January) alipewa taarifa za wajumbe wawili wa kamati yake ambao walikataa hongo hiyo, na baada ya kufanya uchunguzi alibaini kwamba kuna kila dalili kwamba baadhi ya wabunge katika kamati yake walikuwa wamebadili msimamo katika baadhi ya mambo," kilieleza chanzo chetu mjini Dodoma.
Habari zaidi zilidai kuwa kufuatia hali hiyo, January aliitisha kikao cha wabunge ambao ni wajumbe wa kamati yake na kugeuka mbogo, huku akiweka bayana kuchukizwa kwake na taarifa za wajumbe wake kuhongwa na kwamba alikwenda mbali zaidi akitishia kujiuzulu nafasi ya uenyekiti ili kutoa nafasi kwa wabunge hao kuchagua mwenyekiti mwingine ambaye atakuwa tayari kuvumilia uovu huo.
"Yule kijana (January) alikasirika sana, alichukizwa kweli kweli na hali hiyo kwa sababu ni kama wajumbe waliopokea hizo bahasha walikuwa wakimzunguka kwani tayari walikuwa wanajua nini wanachopaswa kufanya ili kuziokoa sekta za nishati na madini,"kilieleza chanzo hicho.
Kadhalika suala hilo la hongo lilijadiliwa katika kikao cha pamoja baina ya wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, ambapo Waziri Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima waliomba radhi kutokana na tukio hilo, hivyo kamati hiyo kuagiza maofisa wa wizara waliohusika wachukuliwe hatua.
"Ni kama Ngeleja na Malima walimalizana na kamati, si unajua maana ni kama January alikuwa peke yake, kama kulikuwa na wanaomsapoti (wanaomuunga mkono) walikuwa ni wachache, hivyo kama waziri na naibu wake waliomba radhi hakukuwa jinsi zaidi ya kumalizana nao," zilidai taarifa hizo na kuongeza:
"Hata hivyo Mwenyekiti na baadhi ya wajumbe walimwagiza Ngeleja na Malima kuwachukulia hatua maofisa waliohusika na ugawaji wa fedha hizo kwa baadhi ya wabunge".
Kauli za viongozi
Mwananchi liliwasiliana na January ili kufahamu undani wa suala hilo, lakini mbunge huyo wa Bumbuli hakukanusha wala kukubali kuhusu baadhi ya wajumbe wake kupokea rushwa.
"Nani kakwambia bwana, mimi siwezi kuzungumza lolote, mambo ya kamati jamani si yote tunayoweza kuweka wazi, lakini siku hizi hatufanyi vikao bila kuwaruhusu waandishi wa habari, kama hayo yangetokea si yangeonekana wakati huo?,"alihoji January.
Waziri Ngeleja kama ilivyo kwa January naye hakukubali wala kukanusha kuwepo kwa tuhuma hizo na badala yake alisisitiza kwamba anayeweza kuzizungumzia ni mwenyekiti wa kamati akimaanisha January.
"Unasikia, kama jambo limetokea kwenye kamati mimi sina mamlaka ya kulizungumzia hata kidogo maana nitakuwa navunja kanuni, kama wengine nilivyowaambia maana naona leo wengi wananitafuta kwa habari hii, mpigieni mwenyekiti wa kamati yeye ana mamlaka, mimi kwangu no comment (siwezi kusema chochote),"alisema Ngeleja kwa simu.
Spika wa Bunge, Makinda kwa upande wake pia alikanusha kupokea taarifa hizo. "Mimi ndiyo nazisikia kutoka kwako, pengine kama zimeletwa kwa barua sijaiona, lakini sifahamu kitu kama hicho," alisema Makinda alipozungumza kwa simu na Mwananchi.
Kwa upande wake Naibu Spika Job Ndugai alisema kuwa hana taarifa hizo kwa kuwa yeye alikuwa nje ya nchi kikazi. "Ndugu yangu, pengine ukimpata Spika anaweza kukusaidia, mimi nimerudi jioni hii (jana jioni) ndio naingia hapa Dodoma najiandaa kwa ajili ya kesho,"alisema Ndugai.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kuwa it's high time Ngeleja has to go.Sijui afanye madudu yepi ili Rais Kikwete agunude kuwa Waziri huyu hafai kuendelea kuongoza Wizara hiyo nyeti lakini ni matarajio yetu kuwa skandali hili jipya ni kitanzi cha mwisho kwa Ngeleja.He has to go..NOW!
Kadhalika,Spika Anne Makinda sasa anapaswa kuhamishia udikteta wake kwa wabunge wa upinzani to wajumbe wa kamati waliopokea mlungula.Na jeshi la polisi ambalo ni mahiri kwa kuwabana wapinzani linapaswa kuanza uchunguzi wa mara moja kuhusu suala hili,sambamba na TAKUKURU.