Showing posts with label KANSA YA MATITI. Show all posts
Showing posts with label KANSA YA MATITI. Show all posts

6 Oct 2013

Kuanzia sasa , blogu hii itakuwa ikiwaletea makala muhimu za mtaalam wa afya, Dokta Joachim Mabula. Makala hizo pia hupatikana katika tovuti ya Fikra Pevu, na unaweza kufuatilia mada mbalimbali kutoka kwa Dkt Mabula kwa kum-follow huko Twitter, ambapo anatumia handle @DrMabula au Google+ +Joachim Mabula au Facebook https://www.facebook.com/DrMabula

Makala yake ya leo inazungumzia ugonjwa wa saratani ya matiti (breast cancer): chanzo, dalili na matibabu. Ungana nae hapa chini


Kansa ya matiti ni aina ya kansa inayojitokeza toka tishu za matiti hasa mirija myembamba inayopitisha maziwa. Ugonjwa huu (Saratani ya matiti) hutokea kwa binadamu na mamalia wengine. Idadi ya wanaume wanaopatwa na kansa ya matiti ni ndogo sana ikilinganishwa na ya wanawake. 
Ulimwenguni pote, kansa ya matiti hubeba asilimia 29 nukta tisa ya kansa zote kwa wanawake. 
Licha ya maendeleo ya kitiba, bado kansa ya matiti ndiyo kansa inayosababisha vifo vingi zaidi vya wanawake. 
Nchi zilizoendelea za Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi ndizo zenye idadi kubwa zaidi ya watu walio na kansa, lakini idadi ya wanawake walio na kansa ya matiti inaongezeka katika bara la Asia na Afrika ambako kwa kawaida kumekuwa na idadi ndogo kiukweli. 
Idadi ya wanaokufa kati ya wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huo huko Asia na Afrika ni ya juu kwasababu kansa hiyo haigunduliwi mapema. Wagonjwa wengi huja ikiwa tayari imeenea sana. 
Kansa ya matiti huanza wakati ambapo chembe moja inajigawanya haraka sana isivyo kawaida na bila utaratibu, na hatua kwa hatua inafanyiza uvimbe. 
Uvimbe unakuwa kansa wakati chembe zake zinapovamia tishu nyingine. Uvimbe fulani unaweza kuchukua miaka kumi hivi kabla ya kugunduliwa. 
VIHATARISHI/VISABABISHI

Hatari ya kupatwa na kansa hiyo huongezeka dadiri umri unavyosonga. Asilimia 80 hivi ya wanawake wenye kansa ya matiti wana umri unaozidi miaka 50. 
Lakini jambo linalofariji ni kwamba kansa ya matiti ni mojawapo ya kansa zinazoweza kutibiwa kwa urahisi. 
Watakao tibiwa kabla ya kansa hiyo kuenea wanaweza kuishi muda mrefu kwa ukawaida. 
Visababishi vya kansa ya matiti bado ni fumbo. 
Baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba kansa ya matiti hutokana na hatua nyingi tata ambazo huanza wakati ambapo chembe fulani ya urithi yenye kasoro inapofanya chembe zitende kwa njia isiyo ya kawaida, yaani, zigawanyike kwa kasi sana, zishambulie tishu nyingine na kuepuka kuharibiwa na mfumo wa kinga, kisha pole pole chembe hizo zinashambulia na kuharibu viungo muhimu vya mwili. 
Jambo lingine linalohusishwa na kansa ya matiti ni homoni ya estrojeni ambayo huenda inachochea aina fulani za kansa hiyo. 
Kwa hiyo, mwanamke anaweza kupatwa na kansa hiyo ikiwa alianza kupata hedhi mapema maishani au ikiwa aliacha kupata hedhi akiwa amechelewa isivyo kawaida, ikiwa alipata mimba ya kwanza umri wake ukiwa umesonga au ikiwa hakuwahi kupata mimba, au ikiwa alipata matibabu ya kurudisha homoni fulani mwilini. 
Kwa kuwa chembe za mafuta hutokeza estrojeni, huenda wanawake walionenepa kupita kiasi waliofika umri wa kuacha kupata hedhi na hivyo ovari zao hazitokezi tena homoni, wakawa katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo. 
Pia watu walio na viwango vya juu vya insulini na watu walio na viwango vya chini vya homoni ya usingizi inayoitwa melatonia kama vile watu wanaofanya kazi usiku, wako pia katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo. 
Uvutaji wa tumbaku umeonekana kuongeza hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti, kiwango kikubwa cha tumbaku iliyovutwa na kuanza kuvuta tumbaku katika umri mdogo hufanya hatari kuongezeka zaidi. 
Mionzi na kemikali za viwandani huongeza hatari ya kansa ya matiti. Kemikali kama polychlorinated biphenyls, polycyclic aromatic hydrocarbons na dawa za kuulia wadudu huchangia kutokea saratani hiyo. 
DALILI

- Uvimbe wowote au kuongezeka kwa unene wa ngozi kwenye makwapa au titi. 
- Umajimaji wowote unaotoka kwenye chuchu ambao si maziwa. 
- Mabadiriko yoyote ya rangi au ngozi ya titi. 
- Chuchu iliyodidimia kwa njia isiyo ya kawaida au inayowasha. 
UCHUNGUZI KUJUA KAMA NI KANSA

Ili kuchunguza ikiwa uvimbe una kansa sindano nyembamba hutumiwa kutoa tishu kutoka kwenye uvimbe huo na kufanyiwa uchunguzi. 
MATIBABU

Uvimbe ukiwa na kansa hufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo na tishu zinazozunguka titi. Upasuaji husaidia kuonyesha uvimbe ulipofikia (ukubwa, aina na kuenea kwake) na kuchunguza uvimbe unakua upesi kadiri gani. 
Chembe zenye kansa zinaweza kutoka kwenye uvimbe na kusafiri kupitia mfumo wa damu au mfumo wa limfu na kuanza kukua tena mahali pengine mwilini. 
Kuenea kwa kansa hadi kwenye viungo na tishu muhimu kama vile ubongo, ini, uboho wa mfupa au mapafu ndio hufanya ugonjwa huo uwe hatari. 
Hivyo baada ya upasuaji, wagonjwa wengi hupata matibabu mengine ambayo yatazuia kansa isirudi na kuenea. 
Kwasababu ya maendeleo katika matibabu ya kansa ya matiti, kumekuwa na matibabu mbalimbali ikitegemea umri, afya historia ya kansa katika familia, na aina ya kansa. 
Wanasayansi wanajifunza mambo mengine kuhusu kansa kutia ndani kuelewa ni kwa nini kansa huenea, kudhibiti chembe za kansa ambazo haziharibiwi kupitia matibabu ya kemikali, kuzuia kugawanyika kwa chembe na kutibu kila uvimbe kwa njia hususa.


ABOUT THE AUTHOR: 
Clinician | Programme Officer & Social Media Manager (Cvs-Tanzania) | Bussinessman
- See more at: http://www.fikrapevu.com/saratani-ya-matiti-breast-cancer-chanzo-dalili-na-matibabu-yake/#sthash.vAwVieVu.dpuf



Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.