Showing posts with label KULIKONI UGHAIBUNI. Show all posts
Showing posts with label KULIKONI UGHAIBUNI. Show all posts

4 Jul 2012


Hatimaye ninyi wasomaji makini wa blogu hii mmeitembelea mara MILIONI MOJA.Japo kuna blogu kadhaa za Kitanzania zilizopita idadi hiyo,binafsi najiskia faraja kubwa hasa kwa vile nimemudu kufikisha idadi hii ya watembeleaji pasipo msaada wa picha.Kimsingi,blogu za uchambuzi/habari pekee hazipati watembeleaji wengi kwani wengi wa Watanzania wanapendelea zaidi picha kuloko maneno.

Nawashukuru sana kwa kutumia muda wenu muhimu kufika hapa.Sina cha kuwalipa zaidi ya kuwaahidi kuwatumikia kwa uadilifu zaidi na kufanya marekebishi kila inapobidi.

MUNGU AWABARIKI SANA 

20 Jan 2012



Unaweza kusema "aah,"kwani wasomaji laki tano ni wengi?Mbona kuna blogu kadhaa zimeshafikisha wasomaji milioni na ushee?" You could say that again,lakini kwangu haya ni mafanikio makubwa.Ni kweli kwamba blogu hii imekuwa hewani kwa takriban miaka 6 sasa,na pengine ingetarajiwa kuwa ingeshakuwa imetembelewa na idadi kubwa zaidi ya wasomaji kuliko hao laki 5 waliokwishatembelea hadi sasa.Ukweli mchungu ni kwamba Watanzania wengi si wapenzi wa habari zisizo za watu binafsi,au zile zisizoambatana na picha za "flani kafanya hiki,kavaa kile,kafumaniwa,kampora flani,nk."

Kuendesha blogu ya habari,uchambuzi na maoni kunataka moyo hususan iwapo bloga husika anatamani kuona wasomaji wengi wanatembelea blogu yake.Moja ya mambo ninayojivunia ni ukweli kwamba tangu ianzishwe,blogu hii ime-focus kwenye malengo yaleyale ya awali pasipo kushawishika kuingia kwenye nyanja nyingine kwa minajili tu ya kupata wasomaji wengi.Kinachonifariji zaidi ni uwepo la wasomaji waaminifu,yaani watu ambao angalau mara kadhaa kwa wiki ni lazima waipitie blogu hii hata kama haina post mpya.Ninafahamu kuhusu hilo kupitia michanganuo mbalimbali ya takwimu za wasomaji wa blogu inayoonyesha mahali walipo wasomaji  (kwa mfano Google Analytics,Stat Counter,nk).

Na kwa vile tangu mapema leo asubuhi "kaunta" ilikuwa inaonyesha kila dalili ya kutimia idadi hiyo ya wasomaji,niliamua kuongeza "feature" mpya ambapo sasa msomaji anaweza kuisoma blogu hii katika mionekano (sura) mbalimbali kama zinavyoonyesha picha zifuatazo.

Mwonekano wa CLASSIC

Mwonekano wa FLIPCARD

Mwonekano wa MAGAZINE

Mwonekano wa MOSAIC

Mwonekano wa SNAPSHOT

Mwonekano wa TIMELINE

Mwonekano wa SIDEBAR
Ili kwenda kwenye minekano hiyo,cha kufanya ni kubonyeza maandishi  mekundu "yanayotembea" kama inavyoonyesha picha ifuatayo


Utahamishiwa kwenye ukurasa utakaokupa uchaguzi wa kuamua unataka kuisoma blogu hii kwa mwonekano upi kati ya mionekano iliyotajwa hapo juu.Ukitaka kurejea kwenye mwonekano wa asili wa blogu hii (kama unavyoonekana katika picha ifuatayo),cha kufanya ni kurejesha nyuma ukurasa kwa ku-click kimshale ←
 ambapo utarejeshwa ukurasa wa awali hadi hatimaye kurejea kwenye ukurasa wenye mwonekano wa asili/kawaida wa blogu hii


NAOMBA KUTOA SHUKRANI NYINGI KWA KILA MMOJA WENU ANAYEKUMBUKA KUTEMBELEA BLOGU HII.NAWASHUKURU PIA WALE WOTE WANAONITUMIA MICHANGO KWA NJIA YA MAONI NA NINAWAKARIBISHA WASOMAJI WOTE KUTUMA MAONI.

WAKATI TUNAINGIA AWAMU YA PILI KUELEKEA WASOMAJI MILIONI MOJA,NINAPENDA KUWAHAKIKISHIA UBORA WA HALI YA JUU WA CONTENTS NA MWONEKANO WA BLOGU HII,SAMBAMBA NA MAREKEBISHO MBALIMBALI YENYE LENGO LA KUBORESHA BLOGU YENU HII.

ASANTENI SANA NA MUNGU AWABARIKI

13 Oct 2011


Kuna tofauti kati ya kujipa ujiko na kuongea ukweli.Na japo kujipa ujiko si dhambi as long as ujiko huo ni stahili,lakini ukweli ni shurti usemwe hata kama utaleta tafsiri ya kujipa ujiko,which as pointed out earlier sio kosa la jinai.

Nimekuwa kwenye ulingo huu wa kublogu kwa kitambo sasa.Mara ya kwanza niliandika post ya kwanza bloguni mwezi April mwaka 2006-yaani miaka mitano iliyopita.Lakini mie si muumini sana wa maadhimisho na ndio maana hata blogu hii ilipotimiza miaka mitano nilisahau kuandika chochote kile.Kwa kawaida siku zangu za kuzaliwa husherehekewa kwa sala na simu kwa mzazi,na zaidi ni tafakuri ya wapi nimetoka,nilipo na niendako.Kuna maana gani ya "kusumbua dunia nzima" kwa vifijo na vigeregere kisa umetimiza miaka 50 ilhali akili yako ni haba zaidi ya mwenye miaka 10? (huo ni mfano tu,don't get me wrong).

Anyway,leo nimeamua kuweka flashback ya makala yangu ya kwanza kabisa katika blogu hii.Kimsingi,makala hiyo haikuwa kwa minajili ya kuwekwa bloguni kwa sababu niliiandika kwa ajili ya makala zangu kwenye lililokuwa gazeti maarufu la kila wiki huko nyumbani la KULIKONI.Na ni makala hizo ndizo zilizozua jina la KULIKONI UGHAIBUNI (ie safu hiyo ilibeba jina hilo la Kulikoni Ughaibuni)

Anyway,makala husika ni hii hapa chini

KULIKONI UGHAIBUNI


Asalam aleykum waungwana.

Nadhani kabla ya kubwabwaja mengi ingekuwa ni vema tukatambuana. Lakini kabla ya hapo, ngoja nikunong’oneze kitu kimoja kuhusu gazeti hili mwanana la KULIKONI.Hili sio gazeti la kawaida. Japokuwa hili ni toleo la pili tu, lakini nimeshuhudia kwa macho na masikio yangu maelfu kwa maelfu ya wapenda habari wakisema kwamba gazeti hili tayari limeshakidhi kiu ya wasomaji japo ndio kwanza linaanza. Na nawahakikishia wenye mtizamo huo kuwa hawajakosea. Ama kwa hakika huu ni mwanzo wa tofauti na mazoea. Japokuwa yapo baadhi ya magazeti yanayotoka mara moja kwa wiki ambayo ukilikosa linapotoka usitarajie kulipata siku inayofuata, kwa KULIKONI ukilikosa Ijumaa basi uwezekano wa kulipata kesho yake ni finyu sana. Kwa kifupi, ni gazeti linalokidhi matakwa ya kila aina ya msomaji: mtu mzima kwa kijana, kinababa kwa kinamama, waliojiajiri kwa walioajiriwa, na kadhalika na kadhalika.

Nirejee kwenye kujitambulisha. Mimi ni Mtanzania mwenzenu, na hadi naandika makala haya nipo hapahapa nchini, lakini nitakuwa nikiwaletea makala kutoka huko Ughaibuni ninakoishi. Naamini kuna mengi yanayotokea huko Ughaibuni ambayo ninyi wasomaji watukufu mngependa kuyapata sio kwa mtizamo wa CNN, Newsweek au Times, bali kwa mwenzenu ambae anayaona katika macho ya ki-Tanzania. Labda nifafanue. Mara ya kwanza nilipoombwa sigara na Mzungu nilidhani ni utani. Nilipompatia alinishukuru nusura anilambe miguu.Kumbe yule Mzungu alikuwa ombaomba kama rafiki yangu Matonya (japo ile staili ya Matonya inaweza kuwa kali kuliko zote ulimwenguni).Nilipokutana kwa mara ya pili na jamaa yule alieniomba sigara ,ambapo safari hii aliniomba pauni moja,ndipo nilipogundua huenda akawa ni ombaomba kweli.Uthibitisho niliupata nilipokutana nae kwa mara ya tatu lakini safari hiyo nikiwa na rafiki yangu mmoja Mghana ambae alikuwa hapo Ughaibuni kabla yangu.Huyo mjukuu wa Kwame Nkrumah ndiye alienithibitishia kuwa hapo Uingereza kuna ombaomba lukuki.Niliposimulia hadithi hiyo kwa jamaa zangu hapa baadhi walinibishia.Na walikuwa na hoja.”Mbona tunaangalia BBC kila siku na tunaowaona ni wazungu wanaoonekana kuwa hawana shida hata kidogo”,ilikuwa hoja ya mmoja wao.Ukweli ni kwamba hawa wenzetu wanapenda zaidi kuonyesha yale wanayoyaona kuwa yanaleta picha nzuri ya nchi zao.Angalau balaa la Katrina lilisaidia kuwafumbua macho watu kwamba hata huko kwa George Bush kuna masikini kama hapa kwetu,na wamesahaulika.

Kwa hiyo basi,makala hii itawasaidia Watanzania wenzangu kujua mambo mbalimbali-mazuri kwa mabaya-yanayojiri huko Ughaibuni ambayo ni nadra kwa mtu wa kawaida kuyapata.Naahidi wasomaji watukufu kwamba kama ambavyo hamtopenda kukosa nakala za KULIKONI basi ndivyo hamtotaka kukosa uhondo nitakaokuwa nawaandalia kutoka huko nje.Kama azma ya gazeti hili ilivyo-kuupatia umma chakula cha kila wakati-nami nitahakikisha nawapatia mlo wa kila wakati.Labda tofauti itakuwa ni kwamba mlo huo unaandaliwa kutoka nje.Lakini ugali si ugali tu.Ukitoka Uingreza au ukipikwa Manzese si bado ni ugali.Cha msingi upikwe kwa kuzingatia kanuni za upishi wa ugali.Pengine kingine ni kwamba mapishi haya ya kutoka nje yatakuwa tofauti ni yale uliyoyazowea.Haya yatamlenga mlaji wa kawaida.Kwa ufafanuzi,ni kwamba utofauti wa makala hii ni kwamba kama lilivyo gazeti lenyewe,itakuwa tofauti ni makala mlizozizowea katika baadhi ya magazeti ya kila wiki.Na tofauti yenyewe ni kwamba kipaumbele kitawekwa kwa watu wa kawaida na mambo ya politiki yatakuja tu pale yanapowagusa watu wa kawaida.

Basi hadi Ijumma ijayo,nawaomba make mkao wa Kula ambapo makala motomoto zitaanza kuwajia kutoka Ughaibuni.Ahadi yangu na ya timu nzima ya KULIKONI ni kubeba sauti za watu wa kawaida,na kwahakika hilo linawezekana.

Alamsiki

10 Feb 2011







BLOGU HII YA Kulikoni Ughaibuni INAPENDA KUWAFAHAMISHA KUWA INAHAMIA KATIKA ANWANI MPYA MTANDAONI.AWALI BLOGU HIYO IMEKUWA IKIPATIKANA KATIKA ANWANI http://chahali.blogspot.com/
 LAKINI SASA INAHAMIA KATIKA ANWANI MPYA YA http://www.blogger.com/goog_939388498
.
http://www.chahali.com

PAMOJA NA MABADILIKO HAYO,AMBAYO NI SEHEMU TU YA MABADILIKO MAKUBWA ZAIDI YA UBORESHAJI NA HATUA YA KUELEKEA KUWA TAASISI KAMILI YA HABARI NA UTAFITI,ANWANI YA AWALI ITAENDELEA KUWA HEWANI KWA MUDA WOTE WA ZOEZI HILI LA UHAMAJI (MIGRATION).SAMAHANI SANA KWA USUMBUFU WOWOTE UTAKAOJITOKEZA

ASANTENI NA KARIBUNI SANA http://www.chahali.com/






8 Mar 2010


Blogu yako inaendelea kuja na mabadiliko ya hapa na pale lengo likiwa kukupatia wewe msomaji mpendwa 'ile kitu roho inapenda'.Katika kutekeleza azma hiyo,blogu hii inatarajia kuwaleta mahojiano na watu mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wana mchango katika kulitangaza jina la nchi yetu. Kadri mambo yatakavyokwenda sawa,walengwa wa mahojiano hayo ni pamoja na wasanii wetu,wanasiasa (hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu),wanamichezo,pamoja na makundi mengine ya kijamii

Kwa vile blogu hii ni yako wewe msomaji mpendwa,na mimi ni mtumishi wako tu,basi nakaribisha maoni ya nani ungependa kuona anafanyiwa mahojiano.Mimi nitajaribu kutuma maombi ya mahojiano hayo,na nikifanikiwa,nitayatundika hapa bloguni.Ili kutoweka ubaguzi wa aina yoyote,blogu hii inakaribisha pia Mtanzania yeyote anayeona kuwa kwa nafasi yake na popote pale alipo anaiwakilisha Tanzania yetu kwa namna moja au nyingine.

Mahojiano hayo yatakuwa katika mfumo wa maandishi japokuwa mipango ya muda mrefu ni kuwa na mahojiano ya sauti pia,na ikiwezekana,mahojiano ya video.Kwa watakaotumiwa maombi ya mahojiano,au kwa wanaotaka kuhojiwa,hii inaweza kuwa fursa nzuri kwao kutangaza vipaji vyao au shughuli zao hususan nje ya Tanzania.Kadhalika,mahojiano hayo yatakuwa aidha kwa Kiswahili au Kiingereza kutegemea maafikiano na mhojiwa.Baadhi ya mahojiano hayo yatafanyika kwa Kiswahili na kutafsiriwa kwa Kiingereza ili kutoa fursa sawa kwa wasomaji wa blogu hii ambao hawafahamu Kiswahili.

Stay tuned, more to come in 2010.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.