Showing posts with label MAAFA TABORA. Show all posts
Showing posts with label MAAFA TABORA. Show all posts

4 Oct 2008


Picha kwa hisani ya BONGOPICHA

Kumbe mauaji ya watoto Tabora yangeweza kuepukwa
Victor Kinambile, Tabora na Kizitto Noya

KAMA mamlaka za mkoa mkongwe wa Tabora zingejua kusoma alama za nyakati, basi maafa ya watoto 19 kwenye ukumbi wa Bubbles Night Club yaliyotokea siku ya Iddi Mosi, yasingetokea.

Ukumbi huo ulishapata hitilafu kwa miaka miwili mfululizo na kusababisha watoto kadhaa kuzirai, lakini wakanusurika kifo, lakini hakukuwepo na hatua zozote thabiti zilizochukuliwa kuepusha uwezekano wa maafa kabla ya msiba huo mkubwa wa kitaifa.

Watoto hao, waliofariki kwa kukosa pumzi na kukanyagana, walizikwa jana mjini Tabora na Kigoma.

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Abeid Mwinyimsa, aliwaambia waandishi wa habari njana kuwa ukumbi huo, ulio katika jengo la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ulianza kuwa na hitilafu tangu mwaka 2006 wakati watoto 26 walipopata tatizo kama hilo, lakini wakaokolewa na kukimbizwa hospitalini ambako maisha yao yaliokolewa.

Siku hiyo pia ilikuwa ni siku kuu ya Idd el Fitr.

Mwaka jana, tukio kama hilo lilitokea kwenye ukumbi huo na watoto wapatao 14 walidhurika kutokana na hitilafu kama hizo na wakakimbizwa haraka kwenye Hospitali ya Mkoa ya Kitete, ambako kwa mara nyingine madaktari walifanya kazi ya ziada kuokoa maisha yao.

Miongoni mwa walionusurika alikuwemo mtoto wa mbunge wa viti maalum Tabora, Mwanne Mchemba.

"Mkoa uliunda tume iliyowashirikisha watu muhimu kutoka katika makundi mbalimbali muhimu ya kijamii, lakini mpaka linatokea tukio hili tume ilikuwa haijatoa ripoti," alisema Mwinyimsa.

Mkuu huyo wa mkoa hakutaja watu waliokuwemo kwenye tume hiyo na kama ripoti yake walikuwa wakiitarajia lini.

Mji wa Tabora ulikuwa umekumbwa na simanzi baada ya watoto hao waliokosa hewa baada ya viyoyozi viwili vilivyo kwenye ukumbi huo wa disko, ambao ulijengwa ili utumike kwa mikutano, kuzima ghafla. Inasemekana kutokana na umeme kuzima na viyoyozi kushindwa kufanya kazi, watoto walikosa hewa na baadaye kukanyagana wakati wakijaribu kujiokoa na hivyo kusababisha maafa hayo.

Jengo hilo linamilikiwa na NSSF na awali ukumbi unaotumiwa kwa disko ulikuwa maalum kwa ajili ya mikutano, ambayo huchukua watu wachache, lakini uligeuzwa na kuwa wa burudani na hivyo kufunikwa sehemu za kutolea hewa ili kuzuia sauti kutoka nje.

Shirika hilo la hifadhi ya jamii, lilikuwa la kwanza miongoni mwa watoa ubani baada ya kutoa ubani wa Sh 500,000 kwa kila familia iliyopoteza mtoto na Sh100,000 kwa kila familia ambayo iliathirika, ahadi ambazo pia zilitolewa mapema kabisa na Rais Jakaya Kikwete, ambayo aliahidi viwango hivyo kwa familia zilizoathirika.

Wakati huohuo, Mwinyimsa alisema Jeshi la Polisi mkoani Tabora, linawashikilia wakurugenzi wawili na mameneja waliokuwa wakiendesha disko toto katika siku hiyo ya Idd.

Aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wakurugenzi hao na mameneja wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya kuhojiwa na polisi kuhusu chanzo cha tatizo lililosababisha watoto hao kupoteza maisha.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni mkurugenzi wa disko hilo, Oneten Teck, Projestus Fidelis na meneja wake Jaffar Rashid. Wengine ni mkurugenzi wa Bubbles Night Club, Shashikant Manji Patel na meneja wake Vituko Salala.

Alisema jeshi hilo limempa taarifa rasmi ya kushikiliwa kwa watu hao, huku likimuarifu kwamba walinzi wa milangoni katika madisko hayo mawili "mabaunsa", nao wanasakwa ili waweze kuhojiwa kuhusu sakata hilo.

Alisema wakurugenzi hao watahojiwa pia na tume huru iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza mkasa huo, ambayo alisema imeanza kazi jana na kuwataka wananchi watoe ushirikiano kwa tume hiyo ili iweze kupata taarifa za ukweli zitakazofanyiwa kazi na serikali.

Akizungumzia watoto waliokuwa bado wamezirai hospitalini, alisema wamepatiwa huduma nzuri za afya na kwamba wote wamelazwa wodi za daraja la kwanza.

Alisema vijana wanne waliruhusiwa mara baada ya maendeleo ya afya zao kuwa nzuri na kuwataja vijana hao kuwa ni Msimu Rehani, Sakina Alli, Kulwa Idd na Tatu Hamad, huku akibainisha kuwa vijana wawili bado wako hospitalini ambao ni Jumanne Mashaka na Naomi

Joseph.

Naye Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Prof. Juma Kapuya

alisema kuwa serikali itachukua hatua madhubuti dhidi ya wote

watakaobainika kuhusika katika kadhia hiyo, na kueleza kuwa nia ya

serikali ni kuona tukio hilo lililotekea Tabora, halijirudii tena wala

kutokeza katika sehemu nyingine hapa nchini.

Hadi kufikia jana, idadi kamili ya watoto waliokuwa kwenye kumbi hizo mbili za disko haijajulikana na imebainishwa kuwa idadi hiyo itajulikana baada ya tume iliyoundwa kukamilisha kazi yake.

Wakati huohuo, mazishi ya watoto waliokufa kwenye ukumbi huo yalianza juzi jioni na baadhi kuzikwa jana mjini hapa, huku miili

ya watoto wawili ikisafirishwa kuelekea Kigoma na Goweko.

Mazishi ya watoto hao yamevuta umati wa wakazi wa Tabora.

Mkazi mmoja, Sheikh Ali Kondollah, akizungumza mara baada ya maziko ya ndugu wawili - Mwanahamis Waziri na Hadija Waziri- yaliyofanyika Rufita, aliitaka serikali iharakishe kutoa ripoti ya uchunguzi wa tume na kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika kwani wananchi wanahitaji kuona hatua zikichuliwa badala ya kuwepo kwa mlolongo wa tume zisizokuwa na majibu.

Nacho Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kulisema maafa hayo ni matokeo ya ufisadi unaotokana na uporaji wa viwanja vya wazi.

Mkurugenzi mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya alisema jana kuwa watoto wamekosa maeneo ya wazi ya kucheza kutokana na viwanja vingi kuporwa na mafisadi na kubadilishwa matumizi.

Alisema Tamwa inaamini kwamba watoto wa Tabora waliokufa ama kuumia kwa kukosa hewa hawakupaswa kucheza disko ndani ya kumbi za starehe na badala yake wangeweza kucheza kwenye eneo la wazi lililoandaliwa kwa shughuli hiyo.

"Tamwa tunaamini kuwa kuvamiwa kwa maeneo ya wazi na hasa mijini kunatokana na kushamiri kwa vitendo vya ufisadi hasa rushwa na uroho wa watu wachache waliopewa mamlaka katika ngazi za serikali za mitaa, kata, halmashauri na wizara inayohusika na ardhi," alisema.

Kwa mujibu wa Nkya, katika miaka ya hivi karibuni rushwa na ufisadi vimechangia maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya viwanja vya michezo na burudani hasa mijini, kugeuzwa viwanda vidogo, gereji, mabaa, migahawa, maduka, hoteli na vituo vya mafuta.

Alisema kutokana na hali hiyo watoto mijini wamekuwa hawana mahala pa kucheza badala yake wanalazimika kutumia haki yao ya msingi kucheza katika maeneo hatari ikiwamo barabarani na kwenye kumbi za starehe.

"Tunawaomba Watanzania wote tutafakari ni watoto wangapi wamepoteza maisha yao kwa kugongwa na magari wanapokuwa wakicheza barabarani? Watoto wangapi wanafanyiwa vitendo vya kikatili kama vile kubakwa kutokana na kucheza kwenye baa ambazo nyingi ziko katikati ya maeneo ya makazi ya watu," alihoji.

"Sisi Tamwa tunaamini serikali ikitaka kuhakikisha janga kama hili la Tabora halitokei tena nchini kwetu, basi ihakikishe kuwa viwanja vyote vilivyotengwa kwa ajili ya shughuli za umma mijini na vijijini, vinarejeshwa hata kama waliopora watakuwa wamejenga vitega uchumi vyenye thamani kubwa ya fedha."

SOURCE: Mwananchi


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.