Leo ni siku ya kuzaliwa ya mmoja ya wasanii maarufu kabisa huko nyumbani na hata duniani, Ommy Dimpoz. Nilifahamiana na Ommy kupitia Twitter, na tangu wakati huo sijawahi hata siku moja kujilaumu kufahamiana nae. Tofauti na hisia zilizotapakaa katika jamii kuwa watu maarufu mara nyingi huwa 'watu wa kujiskia,' kwa Ommy ni tofauti kabisa. Katika mawasiliano tuliyowahi kuwa nayo kupitia Twitter ameonyesha ni kijana mstaarabu, mwenye heshima na ni vigumu kuamini kuwa ni mmoja wa watu maarufu kabisa kwa sasa huko nyumbani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
Na sio Ommy Dimpoz pekee. Kitu kimoja nilichojifunza katika kufahamiana na wengi wa ma-celeb wetu ni utu wao. Orodha ni ndefu lakini kwa uchache tu, nilichokutana nacho kwa Ommy Dimpoz ndicho nilichokutana nacho kwa Mwana FA, Profesa Jay, AY, Fid-Q,Solo Thang,Lameck Ditto, Cindrulz,Grace Matata,Mkoloni, Albino Fulani na hata wakongwe wa fani ya Bongoflava kama @XamiaSiku4Saa4 wa waasisi wa Bongoflava Kwanza Unit, na wengineo wengi.Tumekuwa tukiheshimiana tangu siku ya kwanza 'tulipofahamiana' mtandaoni.
Lakini si kwa Bongoflava tu kwani hata mastaa wengine kama Sinta, Flaviana Matata, Sporah Njau, Batuli, Seki, Masanja Mkandamizaji, Sheria Ngowi, Michael Mlingwa Masudi Kipanya na wengineo wengi ni watu ambao kwa hakika sijawahi kujutia kufahamiana nao kwenye mitandao ya kijamii.
Na kwenye 'anga' nyinginezo VIPs kama Mawaziri Lazaro Nyalandu, Januari Makamba, wanasiasa kama John Mnyika, Faustine Ndugulile, Halima Mdee, Hamis Kigwangalla, William Ngeleja na Lawrence Masha, sambamba na waheshimiwa wana-Afrika Mashariki Shyrose Bhanji na Abdullah Mwinyi, hali ni hiyo hiyo, unafahamiana na watu mtandaoni na wanakuwa kama 'asset' muhimu maishani kwa aidha kujifunza kutoka kupitia mafanikio yao au ustaarabu walionao mtandaoni.
Makala hii haitoshi kuwataja watu wote maarufu niliofahamiana nao kupitia mitandao ya kijamii, lakini ninachoweza kubainisha bayana ni ukweli kwamba kuwa-follow watu maarufu kunapunguza sana usumbufu kwenye mitandao ya kijamii. Pengine ni kwa sababu wanatunza heshima yao lakini pengine ni ukweli kwamba mafanikio ni mwalimu mzuri wa maisha, na wengi waliofanikiwa watakwambia kuwa moja wa mitaji mikuu ya mafanikio ni kuwaheshimu watu wengine kama wanavyokuheshimu.
Lakini ninaomba nibainishe waziwazi kwamba kama ilivyo katika maisha halisi 'mtaani' au duniani, heshima haihitaji mtu awe maarufu au wa kawaida. Kwa mantiki hiyo, ninachopigia mstari hapa si kwamba watu wote nilofahamiana nao mtandaoni nimaarufu, au watu wasio na umaarufu hawana faida. Hapana. Kuna maelfu ya watu 'wa kawaida tu' ambao kwa hakika wamenisaidia sana kuwa mtu bora zaidi ya nilivyokuwa kabla ya kufahamiana nao.
`Binafsi, moja ya vitu ninavyovithani ni mno ni utu na unyeyekevu. Kwa bahati mbaya (au pengine bahati nzuri) nilikulia katika familia isiyo na uwezo mkubwa. Sijisifu, lakini laiti nisingekuwa na akili ya darasani basi hata kuhitimu kidato cha nne ingekuwa mgogoro kwani wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kumudu gharama japo kiduchu za wakati ninasaka elimu maana hata ada ya elimu ya O'Level ikuwa mgogoro japo mwanzoni ilkuwa Shilingi 1,500 tu. Kubwa lililonisaidia ni kuishi na watu vizuri, unyenyekevu na heshima kwa kila mtu.
Lakini kibaya nilichojifunza katika maisha yangu mtandaoni ni ukweli usiopendeza kwamba wengi wa wasumbufu mtandaoni ni wale wasio na moja la kujivunia: wenye umaarufu kutokana na mambo ya ovyo ovyo kama matusi na bullying, na wengine ni wenye kamera zenye IQ kubwa kuliko wao wenyewe lakini wanahangaika kusaka umaarufu kwa kuwachafua watu waliowazidi kiakili/uwezo kuliko ukoo wao mzima.
Japo yawezekana kuwapo kwa watu maarufu wenye tabia zisizopendeza (japo sijawahi kukutana nao mtandaoni, na hata ningetakana nao ningewakwepa kwa sababu kanuni yangu kuu ni kuthamini utu wa mtu na si vitu alivyonavyo), lakini kwa hao niliofahamiana nao wamewezesha maisha yangu mtandaoni na katika dunia halisi kuwa ya amani na furaha. Uzoefu waonyesha kuwa watu wasumbufu sana, hususan mtandaoni, ni wale wasio na kitu chochote cha maana lakini wanajaribu kuihadaa dunia kuwa 'nao wamo.' Ushauri wangu mwepesi ni huu: kamwe usifuatane na mtu asiye na mwelekeo unless awe mtu anayejielewa kuwa mtaji wake mkubwa licha ya 'kutokuwa na kitu' ni utu wake.
Basi nimalizie makala hii maalum kwa ndugu yangu Ommy Dimpoz kwa kumtakia kila la kheri maishani nikitaraji watu wengine 'wenye majina' watajifunza mengi kupitia unyenyekevu wake ambao nina hakika unachangia sana katika mafanikio yake makubwa. Ninamwombea aendelee kuwa mfano kwa watu wengine maarufu kwa kujali utu kuliko vitu, kuendelea kuwa mnyenyekevu hasa kwa vile unyenyekevu una mvuto zaidi kuliko nyodo, mapozi na tabia nyingine zisizopendeza.
Na kwa wasumbufu wanaosaka umaarufu kwa kuwasumbua wenzao, sina maneno mazuri wala ushauri wa busara wa kuwaeleza zaidi ya kuwakumbusha kuwa huwezi kumwangusha mtu mwema/bora. Kujuana na watu maarufu hakukufanyi nawe kuwa maarufu. Na hata kama watu maarufu watakuwa karibu nawe kwa 'upuuzi wako' basi ni wazi kuwa umaarufu huo utabaki kuwa kama mapovu, muda si mrefu hupasuka.
Happy birthday Ommy Dimpoz na shout out kwa kila mtu maarufu anayejali utu, mwenye heshima, mnyenyekevu na anayetambua kuwa mtaji mkubwa wa binadamu ni watu- marafiki- kuliko maadui.