5 Oct 2008


JAJI Kiongozi, Salum Massati, amesema kuanzia sasa madereva watakaosababisha vifo katika ajali za barabarani watanyang’anywa leseni na hata kufungwa miaka miwili jela ili kupunguza matukio hayo.

Akizungumza mjini hapa, Jaji Massati alisema ili kufanikisha mkakati huo, Mahakama ya Tanzania imewaagiza mahakimu wake kutafsiri vizuri na kwa usahihi sheria ya makosa ya barabarani ili kuwabana madereva wazembe. 

Agizo hilo lilitolewa alipokuwa akizungumza na watumishi wa mahakama hiyo Kanda ya Iringa. 

Alisema kwa kipindi kirefu madereva wanaopatikana na hatia za kuua kutokana na makosa ya barabarani wamekuwa wakipata adhabu ndogo, jambo linalolalamikiwa kuchochea matukio ya ajali. 

“Hivi sasa mahakama zimebebeshwa mzigo huu wa lawama kana kwamba sisi ndio chanzo cha kuendelea kwa ajali nyingi barabarani kwa kuwa adhabu tunazotoa haziwiani na makosa yanayofanywa yakiwamo ya kusababisha vifo,” alisema. 

“Sheria inataka anayesababisha kifo kwa makosa ya barabarani ahukumiwe miaka miwili jela na anyang’anywe leseni yake, lakini mahakimu wetu hawatoi hukumu hiyo,” alisema. 

Alisema badala yake madereva wengi wanaokutwa na hatia za makosa hayo hupigwa faini ndogo na kuachiwa. 

Jaji Massati alisema mianya iliyopo katika sheria ya Usalama Barabarani imesababisha wakati mwingine dereva aliyesababisha ajali ambayo hata kama imeua watu 20 apigwe faini na kurudishiwa leseni yake. 

“Pale Kibaha, Pwani aliwahi kukamatwa dereva mwenye leseni feki aliyesababisha ajali na kuua, hata hivyo alipofikishwa mahakamani alihukumiwa kwa faini ya Sh 10,000 na kurudishiwa leseni yake. 

“Sidhani kama hukumu hiyo ilikuwa sahihi na inatoa fundisho kwa madereva wengine kuzingatia sheria zote za barabarani,” alitoa mfano.


Kwa mujibu wa sheria,kila mvunja sheria anapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria (kifungo ikiwa ni mojawapo ya adhabu hizo).Ajali za barabarani zinapoteza maisha ya Watanzania wenzetu kila kukicha,lakini ufisadi nao unaathiri (na pengine hata kupoteza) maisha ya mamilioni ya Watanzania kila dakika.Madereva wanaosababisha ajali na mafisadi wote ni wavunja sheria na wanapaswa kudhibitiwa kwa kuchukuliwa hatua kali ili,kwa upande mmoja,iwe fundisho kwa wengine,na kwa upande mwingine,wavunja sheria wavune wanachopanda.

Lakini pamoja na kuunga mkono mtazamo wa Jaji Kiongozi,nadhani kuna umuhimu wa kwenda mbali zaidi kuangalia vyanzo vya ajali mbali ya uzembe wa madereva.Tuchukulie madereva wa daladala kwa mfano.Mazingira yao ya kazi yanafanywa kuwa magumu na wamiliki wa daladala wenye uchu wa faida pasipo kujali sana mazingira ya kazi ya wanaowaletea faida hiyo.Na hapo tumewaweka kando askari trafiki wenye kudai rushwa waziwazi kana kwamba ni haki yao.

Hivi anayeamua kuweka chasis ya lori kwenye basi la abiria ni dereva au mmiliki wa basi hilo?Je linapopata ajali kutokana na mechanical corruption hiyo wa kulaumiwa ni dereva au mmiliki wa basi hilo?Na vipi kuhusu trafiki wanaokagua mabasi ya abiria?Au vipi kuhusu wiki ya usalama barabarani ambayo inaadhimishwa kila mwaka?Kwa mmiliki wa basi bovu kulikabidhi kwa dereva kwa ajili ya biashara inamaanisha kwamba ametoa baraka kwa lolote litakalotokea,ikiwa ni pamoja na ajali.Same could be concluded about mamlaka zinazoruhusu gari bovu kuwepo barabarani.

Hapa tunarudi kwenye tatizo lilelile la kila mara la kuangalia matokeo badala ya chanzo.Au kwa mtazamo mpana zaidi,kuhukumu vidagaa badala ya papa.Madereva wengi wa mabasi ya abiria wanalazimika kuyakubali mazingira magumu ya kazi hiyo sio kwa vile wanaipenda sana bali kutokana na tatizo zima la ajira huko nyumbani.Hakuna mtu mwenye akili timamu aliye tayari kuendesha "jeneza linalotembea" (a walking coffin),yaani magari ambayo yako barabarani kwa kudra za Mwenyezi Mungu pekee.

Sawa,madereva wanaosababisha ajali wanapaswa kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kifungo.Lakini pasipo kukomesha tatizo la kuwepo kwa magari mabovu barabarani,vifungo vitaendelea na ajali zitaendelea pia.By the way,kama vifungo pekee vingekuwa kizuizi cha kuvunja sheria,idadi ya wafungwa waliopo magerezani (na mazingira ya kutisha wanayoishi huko) ingetosha kukomesha uvunjifu wa sheria unaoweza kupelekea mtu kwenda gerezani.Pasipo kuangalia upande wa pili wa tatizo,yaani wamiliki wa vyombo vya usafiri wanaoweka mbele faida kuliko uhai wa abiria wao,na trafiki wanaothamini rushwa kuliko maisha ya Watanzania wenzao,basi ajali zitaendelea hata kama adhabu kwa kosa la kusababisha ajali itakuwa hukumu ya kifo.

1 comment:

  1. Hakuna juhudi za dhati kupambana na rushwa na ubadhirifu pia wavunja sheria katika tanzania..hii ndiyo msingi wa hayo matatizo...barabara hazina viwango vinavyotakiwa kutoa wanaoshinda hizo tenda ni kwa kutoa mlungula kwa wahusika...matokeo yake barabara zinajengwa kama vile miujiza...angalia barabara ya Morogoro mjini kutoka msamvu kufika mjini morogoro...haiwezi hata kuingilia akilini kwamba huyo kandarasi amejenga nini....barabara ya Morogoro kutoka ubungo kwenda mpaka kibaha analia hiyo mitaro iliyopo pembeni...gair likienda tuu huko pembeni tuu barabara basi ni balaa....jaji masati iwapo kama mtaweza kushughulikia wala rushwa ambao wanashabikiwa na serikali tena bila kuguswa na wanaogopwa na serikali iliyopo basi mtaahishia kuwafungiwa madereva wote bila kupungua hizo ajali za barabarani....Hivi juzi tuu umesikia wafanyakazi wakitoa maombi ya kuongezewa malipo...je jeshi la polisi malipo yao wanayopewa yanaweza wao kumudu maisha!?Jibu hapana sasa unategemewa ufanisi wa kazi utatokana nini kam siyo rushwa ambayo inaendeleza uzembe na uvunjaji sheria....nafikiri sheria zilizopo zinatosha isipokuwa zinatoa adhabu kwa hadhi yako katika jamii...iwapo ni hoe hae basi sheria itachukua mkondo wake...na iwapo wewe ni Rais,2waziri mkuu mstaafu ama unachnagia pesa jingi CCM basi hiyo sheria haitakugusa...Msingi mkuu hatuna uwajibikaji katika kutekeleza sheria zilizopo kwa sababu ya Rushwa. Rushwa ni adui wa maendeleo na uahi wa mtanzania.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.