13 Oct 2009


Hivi mwenzangu unapoiangalia CCM kwa mtazamo wa kawaida tu (yaani usiohisha uchambuzi wa kitaaluma) unaielezeaje?Pengine huafikiani na mtizamo wangu wa “kawaida” na kitaaluma kwamba pamoja na hadi lukuki za kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye lindi la umasikini,chama hicho hakijaonyesha dhamira ya dhati kutimiza ahadi hizo.

Naamini kuwa baadhi ya ahadi hizo zilikuwa za dhati,hususani ile ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.Naamini hivyo kwa vile ni dhahiri kwamba chama hicho kilikuwa kinatambua hali ngumu inayowakabili Watanzania baada ya miongo kadhaa ya utawala wake.Kwa kutambua tatizo,CCM ilileta dalili za matumaini kwamba sio tu inataka kuendelea kutawala lakini pia inataka kuwa chachu ya mabadiliko.Japo chama hicho kinafahamika kwa usugu wa kukiri mapungufu ya utendaji wake,uamuzi wake kugusia maeneo yanayowakera wananchi ilikuwa ishara ya kutambua mapungufu katika awamu zilizotangulia na kudhamiri kufanya marekebisho.

Binafsi nilitarajia kwamba kama ilivyokuwa mwaka 2005 ambapo CCM “ilikiri mapungufu yake kiaina” kwa kuahidi kuboresha maisha sambamba na kukabili chanzo kikuu cha kuzorota/kudidimia kwa maendeleo (rushwa),basi safari hii pia kingepata ujasiri wa kutueleza bayana kwamba kumekuwa na mapungufu makubwa zaidi katika utekelezaji wa ahadi hizo.

Ni nani asiyejua kuwa kiwango cha rushwa kinazidi kupaa siku hadi siku?Ni nani asiyejua kuwa rushwa na uhujumu mwingine wa uchumi umechukua sura mpya kwa kuzaa tabaka “jipya” la mafisadi?Ni nani pia asiyejua kuwa kwa kiasi kikubwa ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania imekuwa na maana zaidi kwa mafisadi kuliko walalahoi?Ni dhahiri kwamba Watanzania wenzetu kama wamiliki wa kampuni ya Kagoda wanaishukuru CCM kwa ukarimu na huruma yake to an extent that inaona aibu kuwataja hadharani.Matapeli wa Richmond (achana na yule Mhindi aliyegeuzwa mbuzi wa kafara mahakamani) wanaishukuru sana CCM kwa huruma yake kwao ambapo kila kikao cha bunge kinazugwa kuwa “taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya kamati ya Mwakyembe itatolewa katika kikao kijacho”,na porojo nyingine kama hizo.

Kinachokera sasa sio tu madudu yanayoendelea kufanywa na CCM bali hizi kauli za kukera kwamba eti chama hicho kimeweka rekodi ya mapambano ya rushwa kuliko nyakati yoyote ile.Hii ni sawa na kuwasanifu Watanzania.Ni mithili ya kuwafanya wajinga,wasioona madudu yanayoendelea,wasiosikia maumivu ya vibano wanavyopewa na mafisadi,na wasiofahamu kuwa watuhumiwa kadhaa wa ufisadi hawajaguswa hadi leo (na hakuna dalili kuwa wataguswa licha ya ahadi kuwa kuna kesi tatu kubwa zitafunguliwa hivi karibuni....na kila mara tunaambiwa “hivi karibuni).”

Ni kweli kwamba hatua dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi hazipaswi kuchukuliwa kutokana na utashi wa watu flani bali kwa kuzingatia sheria na kanuni.Lakini utashi ni muhimu katika kuchukua hatua,na hapa hatuzungumzii utashi wa wananchi wasio na uwezo wa kuuamua,kwa mfano “Chenge na tuhuma za vijisenti vyake huko Jersey hastahili kuwa kwenye kamati ya maadili ya CCM.”Kwanza kuwa na utashi wa kufanya jambo jema si dhambi,kama CCM inavyotaka kutuaminisha.Kuwa na utashi wa kuchukua hatua dhidi ya mafisadi ndio itapelekea chama hicho kuwatenga mafisadi inaowakumbatia,na hivyo kuwa rahisi kwake kuchukua hatua dhidi yao.Utashi unapaswa kuepukwa ni kama ule wa wanamtandao unaoendelea kuwaangalia wana-CCM wasio wanamtandao kuwa mithili ya wahaini.

Mamlaka husika zinapozembea kuchukua hatua sahihi halafu tunaishia kuambiwa kuwa hatua haziwezi kuchukuliwa kwa utashi wa watu flani...jibu jepesi ni kwamba matatizo yetu hayawagusi wanaotuongoza.Wanaona tunapiga kelele zisizo na msingi,ndio maana kwao haki za binadamu za mafisadi ni muhimu zaidi kuliko za walalahoi walio wengi.

Hivi kweli CCM inataka kutuzuga kuwa haifahamu kwamba Watanzania wengi wangependa kuona wahusika “halisi” wa utapeli wa Richmond wakifikishwa mahakamani badala ya kile tunachoelezwa kuwa “walijiuzulu kwa maslahi ya taifa”?CCM haijui kwamba kwa kuendelea kuminya taarifa kuwa nani anamiliki Kagoda ni mithili ya kuwapuuza Watanzania?Au CCM haifahamu kuwa kuwaachia mzigo Waingereza kudili na vijisenti vya ujambazi wa rada ni kukwepa majukumu?

Au chama hicho kinapotulaghai kwamba tumwache mhusika mkuu wa ufisadi katika mgodi wa Kiwira apumzike kwa amani ni sawa na kuruhusu kila mtu aibe kisha aachwe apumzike kwa amani?Kwanini basi vibaka wanajazana magerezani ilhali wezi wakubwa wanatetewa kwa nguvu zote?

Watanzania wana kila sababu ya kuiadhibu CCM hapo mwakani.Kinachofanywa na chama hicho kinapodai kuwa “kimeweka rekodi ya kupambana na rushwa” ni mithili ya vibaka wanaokuibia kisha wanakupigia ukelele wa mwizi na kupelekea wewe mwathiriwa wa uporaji huo kushushiwa kipigo kitakatifu huku kibaka “akiyeyuka kiulaini.”Badala ya kukiri kwamba kasi yao ya kupambana na ufisadi ni ndogo, wao wanatukejeli kuwa wameweka rekodi!Halafu bado tutegemee lolote kutoka kwa wababaishaji hawa?

Hakuna haja ya kubishana au kupigiana kelele nao.Dawa yao ni hapo mwakani.Kama unataka kuendelea kuona mafisadi wakitetewa huku wanaowapinga wakikemewa basi irejeshe CCM madarakani hapo mwakani.Kama unadhani maisha bora yaliyoahidiwa 2005 yamepatikana zaidi ya matarajio yako basi hutofanya kosa kutoa kura ya ndio kwa chama hicho.

Tukiendeleza mazowea tutazidi kuumia.Kuna wanaodhani kwamba Tanzania haiwezi kuwa kisiwa cha amani pasipo utawala wa CCM.Wanachosahau kuwa hata hao CCM ni Watanzania wenzetu japo wanawathamini zaidi wageni (wawekezaji) kuliko sie wenye nchi.Wanasahau pia kuwa wingi wa wabunge wa CCM unakwaza jitihada wa wapambanaji kama akina Dokta Slaa kuwakalia kooni wababaishaji waliojazana chini ya utawala wa CCM.

Atakayenuna na anune lakini nchi hii ni yetu sote na kila Mtanzania ana haki ya kudai haki yake.Tukiruhusu kuendelea kwa ngojera za “tunaendelea na mchakato wa blah blah blah” au “kesi kadhaa zkubwa zitapelekwa mahakamani hivi karibuni...” na hadithi nyingine kama hizo basi tutaendelea kuwa watu wa kulalamika kila siku japo ni sie wenyewe tunaoweza kukomesha usanii wa kisiasa wa aina hiyo.Kama imewezekana Ghana basi hata kwetu inawezekana.Si kweli kwamba chama mbadala kitashindwa kutupeleka tunakostahili kwenda hasa ikizingatiwa kuwa hakuna uwezekano wa chama hicho mbadala kupata idadi kubwa ya wabunge zaidi ya CCM,which means itakuwa rahisi kukidhibiti iwapo kitaonyesha dalili za kurejea madudu ya CCM.

Kusanya hasira zako lakini usipigane bali pugie kura ya kujiletea maisha yako bora wewe mwenyewe kwa kuwaondoa wanaokwaza uwezekano huo.Ifike wakati tusema tumechoshwa na ahadi na maneno matamu (na mengine si matamu bali ya dharau kama hayo ya kudai wameweka historia ya kupambana na rushwa wakati wanajua waziwazi kuwa wamekuza rushwa kupindukia).

It can be done if you play your part.

Inawezekana ukiamua kutimiza wajibu wako.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.