14 May 2010

Kuna wakati najiuliza kwanini sie masikini wa kutupwa ni hodari sana kwenye matumizi ya ovyo ovyo.Moja ya kumbukumbu za serikali ya awamu ya nne ilikuwa kuongeza mishahara ya wabunge licha ya hali yetu mbovu kabisa ya uchumi.Sambamba na hilo ni utitiri wa magari ya kifahari ambayo kimsingi si miongoni mwa vipaumbele kwa taifa masikini kama letu.

Wakati sie tunaendeleza matumizi ya kutapanya huku tukitembeza bakuli kwa wafadhili,serikali mpya ya hapa Uingereza chini ya David Cameron imetangaza kuwa mishahara ya mawaziri itapunguzwa kwa asilimia 5 na hakutakuwa na nyongeza katika mishahara hiyo (pay freeze) kwa miaka mitano.Mshahara wa sasa wa Waziri Mkuu Cameron utakuwa pungufu ukilinganisha na mishahara wanayolipwa meya wa manispaa mbalimbali 61 (kila manispaa hapa inajipangia kiwango cha mishahara ya viongozi wao kulingana na uwezo wa manispaa husika.Kukupa picha nzuri,alichofanya Cameron ni kama JK angeamua alipwe mshahara pungufu kulinganisha na meya wa manispaa ya Temeke au Kinondoni...ah,naota tu.Afanye hivyo achekwe!!!?)



Yah,unaweza kusema hizi ni mbwembwe tu za serikali mpya,au manjonjo tu,lakini ukweli ni kwamba serikali makini ni ile inayoonyesha kwa vitendo kuwa inatambua hali inayolikabili taifa.Cameron ameingia madarakani wakati Uingereza ikiwa kwenye msukosuko wa uchumi,na moja ya vipaumbele vya serikali yake ni kurekebisha uchumi mapema iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun la hapa,mshahara wa Waziri Mkuu Cameron umepunguzwa kwa pauni 7,500 na kubaki pauni 142,500.Mishahara ya Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg na mawaziri wengine waandamizi itakatwa pauni 7,082 na kubaki pauni 134,565 huku mawaziri wa kawaida wakikatwa pauni 5,197 na kubaki pauni 98,740.Mishahara ya mawaziri 'wadogo' itakatwa pauni 4,707 na kubaki 89,435.Hatua hiyo ya kukata mishahara kwa asilimia 5 itaokoa pauni milioni 3.

Wakati hayo yanatokea,gazeti la Mwananchi lina habari kuwa nchi wahisani wanaochangia bajeti ya serikali yetu wameamua kuunguza mchango wao kwenye bajeti ya serikali kwa mwaka 2010/2011 kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ni pamoja na kasi ndogo ya serikali katika kutekeleza mageuzi kwenye sekta za umma.

Taarifa ya wahisani hao iliyotolewa jijini Dar es Salaam juzi, inaeleza kuwa mwaka huo wa fedha, watatoa dola za Marekani 534 milioni sawa na Sh721bilioni, ambazo ni pungufu kwa Dola za Marekani 220 milioni sawa na Sh297 bilioni walizotoa mwaka 2009/2010.

Wahisani wa bajeti ya serikali ni Benki ya Maendeleo Afrika (ADB), Canada, Denmark, Jumuiya ya Ulaya (EU), Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Uholanzi, Norway, Sweden, Uswisi, Uingereza na Benki ya Dunia (WB) mwaka jana walichangia Sh1.9 trilioni katika bajeti ya serikali kupitia miradi ya maendeleo na mifuko ya kisekta.

Taarifa hiyo ilitaja maeneo ambayo serikali ilishindwa kufikia malengo kuwa ni mabadiliko ya haraka katika menejimenti ya sekta ya fedha za umma, mategemeo ya kuboreka kwa hali ya mazingira ya uwekezaji na uboreshaji wa huduma kwa kutoka sekta za umma.

Hii ni mara ya nne kwa wahisani hao kuiwekea ngumu serikali katika kuchangia bajeti yake kila inapofikia mwisho wa mwaka, kwa kushindwa kutekeleza mambo wanayofikiria wao kuwa ni muhimu zaidi katika maendeleo ya nchi.

Mwaka juzi wahisani hao waligoma kutoa fedha baada ya serikali kusuasua kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wakiwemo wa fedha za EPA mpaka zilipofunguliwa kesi kadhaa ambazo mpaka sasa zinanguruma mahakamani.

Tatizo la viongozi wetu sie ni porojo nyingi na ulaghai mwingi wa kisiasa.Majukwaani wanahubiri kama watu wenye uchungu kweli na nchi yetu,lakini matendo yao tofauti kama kiza na mwanga.Tunapenda kuishi kifahari wakati uwezo wetu ni duni kabisa.Yani kuna wakati naangalia msafara wa Waziri Mkuu hapa,kisha nikikumbuka misafara ya viongozi wetu wakuu nabaki na maswali mengi kuliko majibu.Hebu angalia video hii hapo chini inayoonyesha msafara wa Gordon Brown siku alipokwenda makazi ya Malkia Elizabeth (Buckingham Palace) kuwasilisha ombi lake la kujiuzulu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.