3 May 2011


Sakata linalomhusu Ridhiwani Kikwete,mtoto wa Rais Jakaya Kikwete-kwa upande mmoja,na Katibu Mkuu wa Chadema Dkt Willibroad Slaa na Mwenyekiti wa chama cha DP,Mchungaji Christopher Mtikila-kwa upande mwingine,linaanza kupamba moto baada ya wanasiasa hao kumjibu Ridhiwani.Kimbembe hicho kilianza kwa kauli zilizotolewa na Dkt Slaa na Mtikila ambao katika nyakati tofauti walimtuhumu Ridhiwani kuwa bilionea aliyepata fedha isivyo kihalali akitumia mgongo wa baba yake,Rais Kikwete.

Tuhuma hizo zilipelekea Ridhiwani kuitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo licha ya kukanusha kuwa sio bilionea-na kudai kuwa magari ya kifahari anayoonekana akiendesha mara kwa mara ni ya kuazima kutoka kwa marafiki zake-alitoa siku saba kwa Dkt Slaa na Mtikila kuthibitisha madai yake vinginevyo atawafikisha mahakamani.

Sasa,kama habari ifuatayo inavyoonyesha,wanasiasa hao wamemtaka Ridhiwani awahi kwenda huko mahakamani,na wao watatumia fursa hiyo kuthibtisha madai yao.Nisikumalizie uhondo,soma mwenyewe hapa chini

Slaa, Mtikila wamtega mtoto JK

Tuesday, 03 May 2011 21:50
Leon Bahati na Raymond Kaminyoge

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amemtega mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani, akisema akifanikiwa kukifikisha chama hicho mahakamani atakuwa amefanikiwa kula mfupa ambao uliwashinda vigogo waliowatangazwa hadharani kuwa ni mafisadi nchini.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa kutoa msimamo wake kuhusu kauli ya Ridhiwani aliyoitaoa Dar es Salaam juzi, kuwa atamfikisha mahakamani ili kuthibitisha kauli yake kwamba mtoto huyo wa rais ni bilionea aliyepata utajiri wa kutisha kipindi kifupi.

Ridhiwani alimpa siku saba Dk Slaa, kuanzia jana awe amekanusha kauli hiyo ya kumtuhumu kuwa fisadi, vinginevyo atamfikisha mahakamani.
"Sisi tunasema atangulie huko mahakamani sisi tutakuja nyuma," alisema Dk Slaa.

Dk Slaa ambaye katika uchaguzi uliopita aligombea urais na kutoa upinzani mkubwa kwa Rais Kikwete aliyetangazwa kuwa mshindi, alisema kauli za kushtakiwa wanapotangaza taarifa za ufisadi hadharani zimekuwa za kawaida.

Alisema wengi waliwahi kutoa kauli kama hiyo kupitia vyombo vya habari baada ya kuwatuhumu hadharani kuwa ni mafisadi, lakini wakashindwa kwenda mahakamani.

"Chadema tuna uzoefu tulipotaja orodha ya mafisadi walitutishia kuwa watatushtaki mahakamani tukawaambia watangulie sisi tutakuja nyuma, lakini walishindwa kutekeleza ahadi yao," alisema Dk Slaa na kuongeza kuwa, iwapo Ridhiwani atafanya hivyo atakuwa amevunja rekodi ambayo imewashinda watu wazito.

Katibu huyo ambaye umaarufu wake ulikuja kwa kasi kipindi cha miaka 15 aliyokuwa Mbunge wa Karatu, Arusha, alijigamba kuwa hawazungumzi jambo bila vielelezo ndio maana wanajiamini kwa kila wanachokisema hadharani.

Dk Slaa alitupia lawama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwamba amekuwa akisisitiza ifutwe kwa sababu inashindwa kufanya kazi yake, ikiwamo kufanya uchunguzi kwa watu wanaotuhumiwa kupata utajiri katika mazingira yenye utata.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Ridhiwani alikanusha kuwa kijana bilionea kama Dk Slaa anavyomtuhumu.Alisema anamiliki shamba mkoani Pwani, lenye ukubwa wa ekari 1.5, gari ndogo na akaunti kwenye benki ya CRDB, NBC na Stanbic, ambazo hakutaja kiasi cha fedha.

Dk Slaa alipinga vikali kauli hiyo na kwamba, alimaliza shule miaka michache iliyopita, lakini sasa ni bilionea na utajiri huo aliupata kwenye mazingira ya utata.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, alisema atatoa uthibitisho mahakamani kuhusu mali alizozitaja kuwa zinamilikiwa na Ridhiwani.“Siwezi kumuomba radhi mtu, nina uhakika wa kuwa kijana yule anamiliki mali ambazo hajazipata kwa njia halali, itakuwa vizuri ikiwa atanipeleka mahakamani, kwani huko ndiko nitakakoonyesha uthibitisho wangu,” alisema Mchungaji Mtikila.

Jumamosi iliyopita, Mtikila alikaririwa na vyombo vya habari akisema, Ridhiwani ni bilionea anayemiliki nyumba za ghorofa, malori, kampuni za ujenzi wa barabara na ardhi.
CHANZO: Mwananchi

Uzuri wa sakata hili upo katika pembe nyingi.Kwanza,Ridhiwani ni mwanasheria kitaaluma,kwahiyo yayumkinika kuamini kuwa tishio lake (la kuwapeleka Dkt Slaa na Mtikila mahakamani iwapo watashindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake) lilikuwa sio danganya toto.Pili,Ridhiwani ni mtoto wa Rais Kikwete,na kwa vile tuhuma hizo zinamhusisha pia baba yake (kwa maana ya kutumia fursa ya urais kumnufaisha mwanaye) inatarajiwa kuwa suala hapa sio kujisafisha yeye tu bali pia baba yake.

Lakini kwa upande wa pili ni wasifu wa Dkt Slaa,na pengine Mtikila.Wengi tunafahamu kuwa Mtikila na mahakama ni kama mtu na nyumbani kwake.Japokuwa siku za karibuni amekuwa na msimamo unaoyumba lakini bado anatambulika kuwa anapoamua kupigania haki basi atakwenda umbali wowote ule pasipo kuchelea madhara ya kufanya hivyo.

Kwa Dokta Slaa,wengi tunamfahamu kama mmoja wa wanasiasa adimu kabisa ambao ni nadra kutoma matamshi pasipo kuyafanyia utafiti wa kutosha na kuwa na uthibitisho.Yayumkinika kuamini kuwa Dkt Slaa alikuwa akifahamu vema kuwa kwa vile Ridhiwani ni mwanasheria,na pia asingependa kuona jina lake na la baba yake yanahusishwa na ufisadi hadharani,ni lazima angetishia kwenda mahakamani kama sio kwenda kabisa huko mahakamani kufungua kesi ya madai.Kwa mantiki hiyo,na kwa kurejea historia ya Dkt Slaa,inawezekana kuamini kuwa alikuwa na uhakika na alichosema,sambamba na kuwa na ushahidi mzito kuhusu madai hayo.

Enewei,siku saba si nyingi.Leo ni siku ya pili,tumebakiwa na siku tano.Tusubiri kusikia kauli kutoka kwa Ridhiwani Jumatatu ijayo ambapo siku saba alizotoa zitakuwa zimekwisha muda wake.

Ngoma inogire!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.