Showing posts with label RIDHIWANI KIKWETE. Show all posts
Showing posts with label RIDHIWANI KIKWETE. Show all posts

6 Aug 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Sina muda kujadili upuuzi huu kuhusu Ridhiwani – Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni mkusanyiko wa upuuzi mtupu madai kuwa yeye Rais alishiriki kumwokoa mtoto wake, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ambaye alikuwa amekamatwa na madawa ya kulevya nje ya nchi.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Urais ni taasisi kubwa sana nchini na hivyo yeye akiwa Rais hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo wanataka baadhi ya watu wanamsukuma ili ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.

“This is nonsense – ni mkusanyiko wa upuuzi. Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo,” amesema Rais Kikwete usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati alipozungumza na Watanzania wanaoishi katika Marekani kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.

Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani alitoa majibu hayo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi, mwaka juzi, 2012 na Katibu Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Wilbroad Slaa, madai hayo yamempeleka mahakamani.

Amesema Rais Kikwete: “Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania.’
Amesisitiza Rais Kikwete: “Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa.”
Kuhusu swali jingine aliloulizwa kuhusu suala hilo, kuwa Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, Rais Kikwete amesema:

“Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria hata kuiweka rehani. Haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania.”

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti, 2014

6 Mar 2014

 
Mshindi wa kura za maoni za kugombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya CCM, Ridhiwani Kikwete amesema siasa anazofanya sasa hazina uhusiano wala ubia na baba yake.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura za maoni za chama hicho katika jimbo hilo kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Msata alisema anafanya siasa kwa maisha yake na si kwa mgongo wa baba yake kwani aliingia katika siasa akiwa na umri wa miaka mitano na hakuwahi kufanya hivyo kwa sababu ya baba yake.
“Siasa ninayofanya haina uhusiano na baba yangu, nafanya siasa kwa maisha yangu na sina ubia na baba yangu katika hili” alisema mtoto huyo wa Rais Jakaya Kikwete.
Akijibu swali la kwa nini amejiingiza katika siasa tofauti na maneno yake aliyowahi kutamka mwaka 2010 kuwa hawezi kushiriki katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo, Ridhiwani alisema wakati huo hakuwa tayari.
“Kwenye siasa usiwe muwazi katika kila kitu, ukiwa hivyo unawapa nafasi maadui kukushambulia, mimi hapa Chalinze ni kwetu, kwa wazazi wangu na kule Bagamoyo tunakwenda tu kikazi na ndiyo maana nikaamua kurudi nyumbani kuomba ridhaa. Nashukuru kuongoza katika kura za maoni ninaona ni kiasi gani ninaungwa mkono,” alisema.
Katika kura hizo za maoni Ridhiwani alibuka mshindi kwa kura 758, akifuatiwa na Imani Madega aliyepata kura 335, Ramadhan Maneno (206) na Mkwazu Changwa (17).
Kamati Kuu ya CCM (CC), inatarajiwa kukutana Machi 8, mwaka huu kupitisha jina mgombea wake wa ubunge katika jimbo hilo nafasi ambayo iliachwa wazi na Said Bwanamdogo aliyefariki dunia Januari 22, mwaka huu.

10 May 2011



Leo ni tarehe 10/05/2011,na deadline aliyotoa Ridhiwani Kikwete,mtoto wa Rais Jakaya Kikwete,kwa Katibu Mkuu wa Chadema,Dkt Willibroad Slaa,na Mwenyekiti wa DP,Mchungaji Christopher Mtikila,imemalizika jana.Ridhiwani alitoa dealine ya siku saba kuwataka Dkt Slaa na Mtikila wamwombe radhi kufuatia tuhuma zao dhidi yake kuwa amekuwa bilionea kwa njia za kutilia shaka.

Ni mapema mno kubashiri chochote lakini habari ifuatayo inaweza kutoa mwangaza kuhusu uwezekano wa Ridhiwani kwenda mahakamani kama livyotishia au kutokwenda (which would imply tuhuma hizo dhidi yake ni za kweli).Soma kwanza habari yenyewe


Mtoto wa Rais Kikwete ang’aka

na Janet Josiah

MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani, amesema hataki kufuatiliwa maisha yake na wanasiasa hasa wanaomtuhumu kuwa ni bilionea huku akisisitiza kuwashughulikia waolimchafua.

Ridhiwani, alisema hayo jana alipozungumza na Tanzania Daima akitakiwa kueleza hatua atakazochukua baada ya muda wa siku saba aliowapa Mwenyekiti wa Demokratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willbrod Slaa kupita.

Awali, mtoto huyo wa Rais aliwataka wanasiasa hao wamwombe radhi katika kipindi cha siku saba vinginevyo angewapeleka mahakamani kwa kuwa wamemchafua pamoja na familia yake.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa njia ya simu, ili kujua lini angekwenda mahakamani kuwafungulia mashtaka viongozi hao, alijibu kwa jazba kwamba jambo hilo linahusu maisha yake hivyo haoni sababu ya kufuatiliwa na vyombo vya habari.

“Jambo la kuwafikisha wanasiasa hao mahakamani si jambo lenu, hilo ni jambo linalonihusu mimi na maisha yangu hivyo nitachokifanya nakijua mwenyewe,” alisema Ridhiwani huku akisisitiza kwamba hata alipozungumza na waandishi wa habari juma lililopita alisema lengo lake ni kuueleza umma na sio kufuatiliwa maisha yake.

Kwa nyakati tofauti Mchungaji Mtikila na Dk. Slaa, walimtuhumu Ridhiwani kwa ukwasi huku wakiitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumchunguza.



Pasipo nia ya kufanya hitimisho lolote,nashindwa kumwelewa Ridhiwani anaposema "jambo la kuwafikisha mahakamani wanasiasa hao si jambo lenu..."Hivi sio Ridhiwani huyuhuyu aliyeitisha mkutano na waandishi wa habari,ambapo pamoja na mambo mengine alikanusha tuhuma zilizotolewa na wanasiasa hao,na akawataka wamwombe rahdi vinginevyom angewafikisha mahakamani?Sasa kama jambo la kuwafikisha mahakamani wanasiasa hao si jambo lao (wanahabari) kwanini basi aliitisha mkutano nao na kuwaelezea same thing anachodai hakiwahusu?

Waandishi wa habari wana kila sababu ya kumhoji kama atawafikisha Slaa na Mtikila mahakamani au la.Kwanini?Kwa sababu,kwanza,alitamka hayo mbele ya waandishi hao hao wa habari,na pili,yeye ni mtoto wa Rais na ametuhumiwa kuwa bilonea kwa mgongo wa baba yake.Sasa hakuna Mtanzania asiyependa kujua kama madai ya wanasiasa hao ni zushi mtupu au yana ukweli ndani yake.

Wito wangu kwa Ridhiwani ni huu:TIMIZA AHADI YAKO YA KWENDA MAHAKAMANI.Tuhuma za wanasiasa hao dhidi yako si ndogo,kwani licha ya kukugusa wewe binafsi zinamgusa pia baba yako ambaye ni Rais wetu (na ambaye siku za karibuni ametangaza kuwa anadhamiri kuukalia kooni ufisadi).Usipokwenda mahakamani itaonyesha kuwa tuhuma hizo zina ukweli.

And to make matter even worse,Dkt Slaa na Mtikila wanaweza kukufungulia kesi ya kuwakashifu,kwani ulidai ni wazushi tu.Sasa kama sio wazushi then go to the court as you promised,bearing in mind kwamba wewe ni mwanasheria.

Enewei,tunasikiliza WHAT'S NEXT!

Ngoma inogire!

3 May 2011


Sakata linalomhusu Ridhiwani Kikwete,mtoto wa Rais Jakaya Kikwete-kwa upande mmoja,na Katibu Mkuu wa Chadema Dkt Willibroad Slaa na Mwenyekiti wa chama cha DP,Mchungaji Christopher Mtikila-kwa upande mwingine,linaanza kupamba moto baada ya wanasiasa hao kumjibu Ridhiwani.Kimbembe hicho kilianza kwa kauli zilizotolewa na Dkt Slaa na Mtikila ambao katika nyakati tofauti walimtuhumu Ridhiwani kuwa bilionea aliyepata fedha isivyo kihalali akitumia mgongo wa baba yake,Rais Kikwete.

Tuhuma hizo zilipelekea Ridhiwani kuitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo licha ya kukanusha kuwa sio bilionea-na kudai kuwa magari ya kifahari anayoonekana akiendesha mara kwa mara ni ya kuazima kutoka kwa marafiki zake-alitoa siku saba kwa Dkt Slaa na Mtikila kuthibitisha madai yake vinginevyo atawafikisha mahakamani.

Sasa,kama habari ifuatayo inavyoonyesha,wanasiasa hao wamemtaka Ridhiwani awahi kwenda huko mahakamani,na wao watatumia fursa hiyo kuthibtisha madai yao.Nisikumalizie uhondo,soma mwenyewe hapa chini

Slaa, Mtikila wamtega mtoto JK

Tuesday, 03 May 2011 21:50
Leon Bahati na Raymond Kaminyoge

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amemtega mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani, akisema akifanikiwa kukifikisha chama hicho mahakamani atakuwa amefanikiwa kula mfupa ambao uliwashinda vigogo waliowatangazwa hadharani kuwa ni mafisadi nchini.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa kutoa msimamo wake kuhusu kauli ya Ridhiwani aliyoitaoa Dar es Salaam juzi, kuwa atamfikisha mahakamani ili kuthibitisha kauli yake kwamba mtoto huyo wa rais ni bilionea aliyepata utajiri wa kutisha kipindi kifupi.

Ridhiwani alimpa siku saba Dk Slaa, kuanzia jana awe amekanusha kauli hiyo ya kumtuhumu kuwa fisadi, vinginevyo atamfikisha mahakamani.
"Sisi tunasema atangulie huko mahakamani sisi tutakuja nyuma," alisema Dk Slaa.

Dk Slaa ambaye katika uchaguzi uliopita aligombea urais na kutoa upinzani mkubwa kwa Rais Kikwete aliyetangazwa kuwa mshindi, alisema kauli za kushtakiwa wanapotangaza taarifa za ufisadi hadharani zimekuwa za kawaida.

Alisema wengi waliwahi kutoa kauli kama hiyo kupitia vyombo vya habari baada ya kuwatuhumu hadharani kuwa ni mafisadi, lakini wakashindwa kwenda mahakamani.

"Chadema tuna uzoefu tulipotaja orodha ya mafisadi walitutishia kuwa watatushtaki mahakamani tukawaambia watangulie sisi tutakuja nyuma, lakini walishindwa kutekeleza ahadi yao," alisema Dk Slaa na kuongeza kuwa, iwapo Ridhiwani atafanya hivyo atakuwa amevunja rekodi ambayo imewashinda watu wazito.

Katibu huyo ambaye umaarufu wake ulikuja kwa kasi kipindi cha miaka 15 aliyokuwa Mbunge wa Karatu, Arusha, alijigamba kuwa hawazungumzi jambo bila vielelezo ndio maana wanajiamini kwa kila wanachokisema hadharani.

Dk Slaa alitupia lawama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwamba amekuwa akisisitiza ifutwe kwa sababu inashindwa kufanya kazi yake, ikiwamo kufanya uchunguzi kwa watu wanaotuhumiwa kupata utajiri katika mazingira yenye utata.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Ridhiwani alikanusha kuwa kijana bilionea kama Dk Slaa anavyomtuhumu.Alisema anamiliki shamba mkoani Pwani, lenye ukubwa wa ekari 1.5, gari ndogo na akaunti kwenye benki ya CRDB, NBC na Stanbic, ambazo hakutaja kiasi cha fedha.

Dk Slaa alipinga vikali kauli hiyo na kwamba, alimaliza shule miaka michache iliyopita, lakini sasa ni bilionea na utajiri huo aliupata kwenye mazingira ya utata.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, alisema atatoa uthibitisho mahakamani kuhusu mali alizozitaja kuwa zinamilikiwa na Ridhiwani.“Siwezi kumuomba radhi mtu, nina uhakika wa kuwa kijana yule anamiliki mali ambazo hajazipata kwa njia halali, itakuwa vizuri ikiwa atanipeleka mahakamani, kwani huko ndiko nitakakoonyesha uthibitisho wangu,” alisema Mchungaji Mtikila.

Jumamosi iliyopita, Mtikila alikaririwa na vyombo vya habari akisema, Ridhiwani ni bilionea anayemiliki nyumba za ghorofa, malori, kampuni za ujenzi wa barabara na ardhi.
CHANZO: Mwananchi

Uzuri wa sakata hili upo katika pembe nyingi.Kwanza,Ridhiwani ni mwanasheria kitaaluma,kwahiyo yayumkinika kuamini kuwa tishio lake (la kuwapeleka Dkt Slaa na Mtikila mahakamani iwapo watashindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake) lilikuwa sio danganya toto.Pili,Ridhiwani ni mtoto wa Rais Kikwete,na kwa vile tuhuma hizo zinamhusisha pia baba yake (kwa maana ya kutumia fursa ya urais kumnufaisha mwanaye) inatarajiwa kuwa suala hapa sio kujisafisha yeye tu bali pia baba yake.

Lakini kwa upande wa pili ni wasifu wa Dkt Slaa,na pengine Mtikila.Wengi tunafahamu kuwa Mtikila na mahakama ni kama mtu na nyumbani kwake.Japokuwa siku za karibuni amekuwa na msimamo unaoyumba lakini bado anatambulika kuwa anapoamua kupigania haki basi atakwenda umbali wowote ule pasipo kuchelea madhara ya kufanya hivyo.

Kwa Dokta Slaa,wengi tunamfahamu kama mmoja wa wanasiasa adimu kabisa ambao ni nadra kutoma matamshi pasipo kuyafanyia utafiti wa kutosha na kuwa na uthibitisho.Yayumkinika kuamini kuwa Dkt Slaa alikuwa akifahamu vema kuwa kwa vile Ridhiwani ni mwanasheria,na pia asingependa kuona jina lake na la baba yake yanahusishwa na ufisadi hadharani,ni lazima angetishia kwenda mahakamani kama sio kwenda kabisa huko mahakamani kufungua kesi ya madai.Kwa mantiki hiyo,na kwa kurejea historia ya Dkt Slaa,inawezekana kuamini kuwa alikuwa na uhakika na alichosema,sambamba na kuwa na ushahidi mzito kuhusu madai hayo.

Enewei,siku saba si nyingi.Leo ni siku ya pili,tumebakiwa na siku tano.Tusubiri kusikia kauli kutoka kwa Ridhiwani Jumatatu ijayo ambapo siku saba alizotoa zitakuwa zimekwisha muda wake.

Ngoma inogire!


Mtoto wa Rais Kikwete aukana ubilionea

na Betty Kangonga

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), Ridhiwan Kikwete, amekanusha tuhuma zilizoelekezwa kwake juu ya kumiliki mali na mabilioni ya fedha.

Ridhiwan alikanusha madai hayo baada ya nyakati tofauti Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Mchungaji Christopher Mtikila kutoa madai kuwa Ridhiwan pamoja na kumaliza shule miaka michache iliyopita, hivi sasa ni tajiri bilionea.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Ridhiwan, alisema habari hizo si za kweli bali za kizushi na kwamba zimejaa uongo unaolenga kumchafua yeye pamoja na baba yake Rais Jakaya Kikwete huku wakipandikiza chuki kwa umma.

Ridhiwan alisema kwa sasa anamiliki shamba la hekari moja na nusu, gari aina ya Toyota Cami na akaunti tatu tofauti zilizo katika benki ya NBC, Stanbic na CRDB.

Alipoulizwa mbona anaonekana akitembelea magari ya kifahari, mtoto huyo wa Rais alisema: “Hapa mjini unaweza kumuona mtu amevaa suti ukadhani ya kwake kumbe ameazima. Mimi nina marafiki wengi, huwa wananiazima magari yao nitembelee, juzijuzi hapa nilikuwa na benzi ya rafiki yangu….jamani miundombinu ya mjini si mnaijua?”

Alisema kutokana na kuwaheshimu wazee hao na umri walionao ni bora watumie busara na kujitokeza ili watoe ushahidi juu ya hayo waliyoyasema na hatua zaidi zichukuliwe.

Aliongeza kuwa iwapo itadhihirika kuwa habari walizozieleza ni za uongo basi atakuwa tayari kuwasamehe; lakini alidai leo atawafikishia barua wazee hao ambapo ndani ya wiki mbili amewataka wathibitishe taarifa hizo walizozitoa juu yake.

“Kama haitoshi narudia tena niliwaahidi ushirikiano na endapo watataka ili kuthibitisha yote hayo waliyosema na hata yale wanayoyasikia, wakithibitisha habari walizopewa ni za uongo basi wasisite kuueleza umma,” alisema Ridhiwan.

Ridhiwan alienda mbali zaidi na kudai kuwa si mara ya kwanza kwa Dk. Slaa kuongopewa, akidai kuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, watu wasiopungua 50 walikutana katika mji wa Mwanza kwenye Hoteli ya La Cairo ili kuhujumu uchaguzi.

“Mchungaji Mtikila ambaye yeye amewahi kukiri wazi kuwa alishawahi kuongopewa hivyo, imani yangu kwamba atakapojiridhisha juu ya maroli, maghorofa na hiyo kampuni ya kutengeneza barabara atatumia busara ili hatua za kisheria zifuatwe,” alisema.

Aliwataka wazee hao kutokuwa makanjanja wa kutengeneza habari katika njia ya kutafuta sifa za kisiasa na kuonekana wanajua kuongea.

Ridhiwan alieleza kutokana na kutokuwa na kinga ya aina yoyote na kutambua nchi inaendeshwa katika misingi ya utawala bora ambao unaheshimu haki za binadamu, yuko tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo mbalimbali ili ukweli uwekwe wazi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mchungaji Mtikila alimtuhumu Rais Jakaya Kikwete kuitumia Ikulu kumtajirisha mwanawe, ambaye anaaminika kuwa tajiri bilionea.


1 May 2011

Mimi ni Rais wenu,na huyu ndiye mwanangu mpendwa ninayependezwa na ufisadi,oops..ujasiriamali wake

na Mwandishi wetu

RAIS Jakaya Kikwete anakabiliwa na kashfa nzito kutokana na utajiri wa mtoto wake, Ridhiwani. Sasa anatuhumiwa kuitumia Ikulu kumtajirisha mwanawe, ambaye anasemekana ni bilionea.

Kwa nyakati mbalimbali, ukwasi wa mtoto huyo wa rais uliibuliwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.

Katika moja ya mikutano yake ya hadhara hivi karibuni mkoani Tabora, Dk. Slaa alisema Ridhiwani amemaliza shule miaka michache iliyopita, lakini hivi sasa ni tajiri bilionea na kwamba ameupata utajiri huo katika mazingira ya kutatanisha.

Jana Mtikila alizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Travertine, akidai Ridhiwani amegeuka bilionea kwa muda mfupi “kwa mgongo wa baba yake.”
Akibainisha zaidi uwezo wa kifedha wa kijana huyo, Mtikila alisema hivi karibuni mtoto huyo ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), aliingiza magari makubwa ya mizigo aina ya “semi trailer” zaidi ya 100 na kudai kuwa yanafanya kazi ya kusomba mizigo DRC na mengine ameyauza.

Alidai pia mtoto huyo wa rais anamiliki makampuni ya ujenzi wa barabara na maeneo mengi ya ardhi kwa lengo la kujenga maghorofa ya kupangisha.

“Huyu ni mtoto mdogo, kamaliza shule juzi, pesa za utajiri wote huu kazipata wapi?” alihoji Mtikila.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Ridhiwani alikaririwa na moja ya vyombo vya habari akisema kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano kwa Dk. Slaa kuonyesha kila anachomiliki.

Kutokana na tuhuma hizo, Mtikila alimtaka Rais Kikwete naye ajivue gamba kwa kuonyesha mfano, vinginevyo ni uendawazimu kujivua gamba bila mkuu huyo wa nchi kujiuzulu urais na uenyekiti wa CCM.

Huku akionekana kuwatetea Edward Lowassa (Monduli), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi) na Rostam Aziz (Igunga), Mtikila alisema Kikwete anawachezea wana CCM na Watanzania kwamba ana nia ya kuwatimua makada hao kwa madai kuwa ni mafisadi wakati yeye ni mshirika wao.

“Kikwete aanze kutoka yeye ndipo awanyoshee vidole hawa Mapacha Watatu alioshirikiana nao kwenye ufisadi wa EPA, Richmond na Dowans, vinginevyo anawadanganya Watanzania. Aanze yeye,” alisema Mtikila.

Alisema anashangazwa na Kikwete kuibuka na dhana ya kujivua gamba kwa kuwatosa marafiki zake watatu wakati chama hicho kina mafisadi lukuki.

Mchungaji Mtikila pia aliorodhesha miradi ya ufisadi aliyomhusisha nayo Kikwete na watendaji wengine serikalini kuwa ni pamoja na IPTL, uuzaji wa iliyokuwa Benki ya NBC, Meremeta, Richmond, Dowans, EPA na nyingine, kwamba zinawahusu watendaji wengi na si mapacha watatu pekee.

”Kikwete aliunda tume kubaini waliochota fedha za EPA na kutakiwa warudishe, lakini hadi sasa hatujui kina nani wamehusika, na kiasi gani cha fedha kilichorudishwa. Kama rais hahusiki na ufisadi huu, usiri wa nini?” alihoji Mtikila.

Alisisitiza kuwa hana maana kuwa Lowassa, Rostam na Chenge ni wasafi, bali anataka orodha ya kuwatimua mafisadi wa CCM iwe kubwa, akiwamo Rais Kikwete kwani ndilo gamba kubwa kuliko yote.

Kuhusu hatima ya CCM na kile alichokiita usanii wa kujivua gamba, Mchungaji Mtikila alisema chama hicho kina ugonjwa wa ‘Nambulila’ ambao mgonjwa hufa na kuzikwa akijiona.

“Wapangwa wana ugonjwa unaitwa Nambulila. Ni ugonjwa unaotokana na tego la mke. Mtu akitembea na mke wa mtu anaupata na anapokufa, anawaona watu wanavyomlilia, wanavyomuingiza kwenye kaburi, lakini hana uwezo wa kusema, hivyo anazikwa akiwa hai, akiona kila kitu. Ndivyo ilivyo CCM, inakufa ikijiona. Hii ndiyo Nambulila,” alisema Mtikila.

Alisema usanii wa kujivua gamba hauwezi kuinusuru CCM kwani ni dhana ya uendawazimu yenye lengo la kuwaghilibu Watanzania.

Sambamba na hilo, Mtikila aliwataja mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye, Joseph Warioba na Cleopa Msuya, kuwa ni miongoni mwa watu wachache wasafi ndani ya CCM.

Alipobanwa kueleza usafi wa Sumaye wakati miaka sita iliyopita alipata kumtaja kwamba ni fisadi namba moja, Mtikila alikiri kutoa kauli hiyo na kuongeza kwamba baada ya kufuatilia walibaini kashfa dhidi yake zilikuwa za uongo na zilipikwa ili kumrahisishia Kikwete njia ya kuwa rais.

“Kweli niliwahi kumtaja kama fisadi namba moja, tulipofuatilia tulibaini kwamba haikuwa sahihi na ndiyo maana leo namtaja kama mmoja ya viongozi wachache wasafi,” alisema.

Aliwataka wana CCM kutobeza ushauri wa viongozi hao wachache wasafi na kutolea mfano wa Warioba na Sumaye walivyoshambuliwa na UVCCM walipotoa mawazo yao.


20 Aug 2010

Pamoja na kumtetea mwanaye,JK alisema (namnukuu)"...hata kama aliyegombea hakuridhishwa na mazingira ya namna aliyeshinda alivyoshinda, ndiyo ameshapata,hivyo jambo la msingi ni kuacha makundi yaliyokuwepo wakati wa kura za maoni, bali wajielekeze katika kutafuta ushindi wa kishindo huku wakijiandaa kwa kugombea kipindi kingine..."SWALI.Je kama kutoridhishwa huko kunatokana na matumizi ya rushwa?Au kwa vile Awamu ya Nne ilikuwa na huruma kwa mafisadi basi wagombea waliofisadiwa nao waige mfano wa serikali hiyo?Soma habari kamili HAPA.

20 May 2010

Nadhani unamfahamu Christina Aguillera,na kama unamfahamu basi ni dhahiri utakuwa unakumbuka 'singo' yake ya kwanza kabisa Genie in a Bottle (Kama huukumbuki basi cheki video hii hapa).

Ushaikumbuka?Well,lengo la makala hii si kumjadili mwanamuziki huyo au wimbo huo uliovuma sana.Nacho-focus hapa ni hiyo ishu ya 'jini kwenye chupa'.

Lakini kabla sijainyambua,ngoja nikupe stori moja fupi.Mwaka 2005 nilipokwenda nyumbani kwenye fieldwork,nilikutana na rafiki yangu mmoja wa zamani ambaye ni mtoto wa Sharifu huko Tanga.Baada ya mahojiano yetu nilimdadisi kuhusu suala la majini.Nae bila hiana akanipa darasa kutoka A mpaka Z.Actually,alikwenda mbali zaidi hadi kunionyesha namna jini linavyotengenezwa.Bila kuingia kwa undani sana,alichovya maandishi flani kwenye chupa na kutengeneza kitu alichokiita kombe,kisha akafunga hiyo chupa.Akaeleza kuwa katika muda aliokusudia,jini litatoka katika hiyo chupa na 'kufanya vitu vyake' (kwa mujibu wa manuizo/dua.Bado nakumbuka jinsi nilivyosisimka baada ya 'kuonyeshwa jini mtarajiwa'

Naamini usemi 'jini ndani/kwenye chupa' unaendana na mantiki ya utengenezaji jini (yaani linawekwa kwenye chupa kisha 'linalipuka' katika muda ulokusudiwa).Kwa mujibu wa yule mtoto wa Sharifu ni kwamba jini likishatengenezwa na kuhifhadhiwa ndani ya chupa tayari kwa 'maangamizi' haliwezi kurejeshwa.Na la zaidi ni kwamba jini likishatoka kwenye chupa haliwezi kurudisha.Kwahiyo basi,usemi 'jini kwenye/ndani ya chupa' unamaanisha kitu ambacho 'kikitoka kimetoka',yaani ni kama maji yakimwagwa ardhini,hayawezi kuzoleka.

Kwanini basi nimeamua kutumia msemo huu katika makala hii?Well,katika uchambuzi wangu kuhusu kauli za/matendo ya Rais wetu (Chaguo la Mungu) Jakaya Kikwete,naanza kupatwa na wasiwasi huohuo wa 'jini ndani/kwenye chupa'.Simaanishi kuwa JK ndio jini.Hapana.Nazungumzia kauli na matendo yake ya hivi karibuni.

Sijawahi kuzungumzia lolote kuhusu hotuba yake kali alotoa kwa wafanyakazi wa serikali waliokuwa wametishia kugoma.Kwa kifupi,baadhi ya kauli zake hazikupaswa kutolewa na kiongozi anayejali utawala wa sheria.Kwa kutaja maneno kama risasi za moto au namna wafanyakazi wangeweza kukumbana na nguvu za polisi ilikuwa ni mithili ya kubariki ukatili.Hata kama wafanyakazi wangegoma bado isingehalalisha matumizi ya nguvu 'to an extent baadhi yao wangeweza kukumbana na makali ya risasi za polisi'.Hivi sio JK huyuhuyu alosema kuwa yeye anathamini haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi?Tuliache hilo kwa sasa.

Juzijuzi akaibuka tena na kudai suala la takrima ni gumu kukwepeka.Mkuu wa nchi anaposema hivyo ni sawa na kubariki matumizi ya rushwa kwa jina la takrima.Kauli kama hiyo haipaswi kutolewa hata na katibu kata,let alone Mkuu wa nchi.Ugumu wa jambo haumaanishi liachwe kama lilivyo.Yaani kwa vile mapambano dhidi ya ukimwi ni magumu kwahiyo tuache watu 'watembee pekupeku'?Au kwa vile ugonjwa wa malaria umekuwa ukitusumbua miaka nenda miaka rudi basi tuuache kwa vile ni vigumu kupambana nao?Sasa alipohamasisha kampeni ya ZINDUKA na wapambe wake wa bongoflava alikuwa anamaanisha nini?Rais alipaswa kuelewa kuwa kwenye mapambano dhidi ya udhalimu,giving up is not an option.Laiti Nyerere na wapigania uhuru wengine wangekuwa na mtizamo finyu kama huo wa 'jambo hili gumu kwahiyo tuliache kama lilivyo' basi hadi leo tungekuwa bado koloni la Mwingereza.

Kilichonishtua zaidi hadi kufikia hatua hii ya kuleta ulinganifu na 'jini kwenye/ndani ya chupa' ni mkanganyiko uliojitokeza katika sakata la Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM).Awali ilielezwa kuwa kuna vipeperushi vilivyosambazwa kumtuhumu aliyekuwa Mwenyekiti ya jumuiya hiyo,Hamad Yusuph Masauni.Baadaye gazeti moja likabainisha kuwa mtoto wa JK,Ridhiwani,anatuhumiwa kuivuruga jumuiya hiyo na kuchochea suala hilo la Masauni.Lakini,akihutubia mkutano wa Jumuiya hiyo huko Iringa,JK aliweka bayana kuwa (namnukuu) "Tulipochunguza ilibainika ni kweli alighushi, wakati wa uchaguzi alisema alizaliwa mwaka 1979, lakini ukweli alizaliwa mwaka 1973 na alianza darasa la kwanza mwaka 1979".Je hii haimaanishi kuwa hata vipeperushi vilivyosambazwa kumhusu Masauni vilikuwa na uhusiano na 'uchunguzi' huo anaozungumzia JK?Kama ni hivyo,je si hatari inapotokea kiongozi wa nchi anaporuhusu michezo michafu kama hiyo kwa minajili tu ya kukidhi matakwa flani?

Kinachokasirisha ni kauli yake kuwa  "kijana huyo (Masauni) mpole na mzito kufanya maamuzi magumu na haraka...ni mkakamavu na mchapakazi atapangiwa kazi nyingine hapo baadaye".Yaleyale ya Mwilima.Mtu anaboronga huku kisha anazawadiwa uongozi.Kama ni kweli Masauni alifoji umri wake,hivi hiyo haimpotezei sifa za kuwa kiongozi mahala kwingine?Sasa JK anapotuambia kuwa aatapangiwa kazi kwingine anamaanisha nini?Au huko atakapopangiwa hakuhitaji uadilifu?Na kama 'kudanganya umri' si big deal kwanini basi wameshinikiza aondolewe UVCCM?Nauliza hiyo kwa vile,kwa mujibu wa 'Chaguo la Mungu',kufoji umri kulikopelekea Masauni kujiuzulu sio big deal ndio maana 'atapewa kazi nyingine baadaye'.

Habari nyingine zinazoweza kuashiria kuwa 'jini lililo ndani/kwenye chupa linaweza kutoka muda wowote ule' ni katika jarida la Raia Mwema kwamba Mawaziri Wakuu wastaafu wanafuatiliwa.Ukisoma habari hiyo utabaini kuwa kwa vyovyovte vile,Mkuu wa Nchi anafahamu kuhusu suala hilo.Lakini sidhani kama tunapaswa kushangaa sana kwa vile kama Masauni alichunguzwa (which is equivalent to kufuatiliwa kwa ex-PMs hao) na hatimaye vipeperushi vikasambazwa,basi katika utawala huu lolote linawezekana,hususan uzandiki na character assassination.

Na hili suala la promotion ya familia kwenye uongozi,japo si kosa,linaweza kutafsiriwa kwa namna ya maandalizi ya udikteta.Baba/mume rais,mama/mke naye mwanasiasa 'kiaina',kaka wa rais naye mwanasiasa,mtoto naye mwanasiasa,na hadi kitinda mimba naye kaingizwa kwenye siasa.Na hapa sizungumzii siasa kwa maana ya hamasa tu bali siasa za mizengwe na kugombea kwa kutumia jina.Hapa tunazalisha mfalme au dikteta?

Kwa Watanzania wengi ni business as usual.Lakini kwa wanaoangalia ishu na kukumbuka kuweka alama za kuuliza,yayumkinika kufananisha suala hili na ' jini ndani/kwenye chupa'.LIKITOKA LIMETOKA,hakutokuwa na jinsi ya kulirejesha kwenye chupa.

Kwa atakayechukizwa na uchambuzi huu (kama yule mjinga alontumia comment ya matusi) all I could tell them is SUCK IT UP!


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.