6 Aug 2011




JK: Nawajua wala rushwa kwa majina
By Richard Williams | Published  02/22/2006 | Habari za Kitaifa |Rating:
.Asema tabasamu lake lisipotoshe watu
.Maamuzi yake si nguvu ya soda




RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amesema anawajua kwa majina wala rushwa katika wizara na kwamba nguvu anayokwenda nayo siyo ya soda.

Alikuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika jana katika uwanja wa michezo wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, mkutano ambao lengo lake lilikuwa ni kuwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa ushindi wa kishindo waliompatia yeye na Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa Desemba 14, mwaka jana.

Rais Kikwete ambaye mkoa wa Rukwa ulikuwa ni wa nne katika ziara zake za kuwashukuru wananchi, amesisitiza kwamba kauli mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa katika ziara zake za kutembelea wizara mbalimbali na idara za serikali ni kauli ambazo hazitoi kwa kutania, bali ni kauli za mambo anayoyafahamu vyema na kwamba mengine ameyaweka akiba. 

"Sizungumzi kwa utani nayajua ninayoyasema. Nilichoweka akiba ni kuwataja watu kwa majina, wasidhani nikienda wizarani nikasema watu hawa wanakula rushwa wasidhani siwajui kwa majina, ninawajua, bali kwa sasa ninatoa muda kwa watu hao wajisahihishe. Mwenye masikio nadhani atakuwa amesikia," alisisitiza.

Katika mazungumzo yake na wananchi hao ambayo mara kwa mara yalikuwa yakikatishwa na vigelegele na nderemo; Rais alirudia tena kauli yake kwamba Mwenyezi Mungu amemuumba akiwa na sura ya tabasamu jambo alilosema kuwa hawezi kulibadili, lakini tabasamu hilo lisiwapotoshe watu, kwani yanapokuja mambo ya msingi huwa hana mchezo na mtu. 

Alisisitiza kuwa kila kiongozi katika nafasi wajibu wake ni kuwatumikia wananchi na kwamba wananchi wanayo haki ya kupata huduma kutoka kwa kiongozi huyo. 

"Ikifika mahali Mtanzania akitaka huduma kutoka kwa mtumishi wa serikali anayelipwa mshahara, basi ni lazima kwanza kabla ya kupewa huduma hiyo, amlipe mtumishi yule, tukifika huko basi huo ni ukiukwaji wa maadili ya kazi na mtu kama huyo hastahili kuwa mtumishi wa umma.

"Tumejipanga vizuri ndani ya serikali katika kuwatumikia wananchi, na hii siyo nguvu ya soda, ukisimama mbele yetu utasukumwa," alisema na kushangiliwa na wananchi.

Rais amebainisha kuwa wale watumishi ambao wamekuwa wakidhani kuwa kutokana na unyeti wa taaluma zao basi hata wakinyanyasa wananchi hawataondolewa katika nafasi zao, wakidhani hivyo wanajidangaya.

"Anayedhani kuwa ataendelea kuharibu kwa sababu katika taaluma yake itachukua muda kuwafundisha watu wengine, anajidanyaganya, tuko tayari kuanza upya. Bora tabu kuliko kuwa na mtu wa aina hiyo ambaye badala ya kuwatumikia wananchi yeye anawatesa," alisema.


Alisema maamuzi mbalimbali ambayo serikali inayachukua hivi sasa na hapo baadaye yanalenga katika kuurejesha utumishi wa umma katika mstari ulionyooka na kwa sababu hiyo amewataka watumishi wa serikali kuu na serikali za mitaa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maadili ya kazi na viapo walivyokula



Alisema mfanyakazi atakayetekeleza kazi zake kwa kuzingatia maadili ya kazi yake, hata nishani anaweze kupewa na serikali, lakini kwa yule ambaye atafanya kinyume chake serikali haitakuwa na muda naye.



"Hatuna ugomvi na mtu wala hatuna chuki na mtu, tunachotaka kutoka kwako ni utumishi wako uliotukuka kama ulivyoapa kufanya kazi kwa kuzingiatia maadili," alisisitiza Rais na kuufanya umati wa wananchi wa Sumbawanga kumshangilia.



Alisema kuwa anachotoa ni ilani na kukumbushana kama gari lilikuwa linapita kwenye majani, basi sasa lirejee barabarani ili kule lilikokuwa linapita lisije kuwakanyaga watu.



Kikwete alisema uwajibikaji huo wa watumishi wa serikali kuu na mitaa unawahusu vilevile wakuu wa mikoa ambao tayari alishazungumza nao, na atarudia tena kwa wakuu wa wilaya na wakuregenzi wakati atakapokutana nao mara baada ya kukamilisha kazi ya kuwateua.



Akiwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kumpatia ushindi wa asilimia 86, Rais alisema kuwa ahadi ya serikali ya kuwajengea barabara ya lami kutoka Sumbawanga hadi Tunduma, iko palepale na kwamba kazi ya uchoraji imekwisha kamilika na zabuni za kutafuta kandarasi ili kazi ianze inaendelea. 



Kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha katika mkoa huo, Rais amewaomba wananchi hao kuzitumia vizuri ili waweze kuzalisha chakula cha kuwatosha wao na ziada itumike kuwalisha Watanzania wengine ambao mikoa yao imekosa mvua.



Rais Kikwete alishindwa kuhutubia jana mjini Iringa kwa sababu ya mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na radi na hivyo atahutubia leo na baadaye atakwenda kutembelea mabwawa yanayotoa umeme ya Kihansi na Mtera.



Mikoa ya Rukwa na Mbeya ambayo hivi sasa mvua zinanyesha, ingawa zilichelewa kuanza, hali ya mashamba na mazao ni ya kuridhisha hali inayoashiria kuwa kama mvua hizo zinataendelea basi kuna uhakika wa kupata chakula kwa wingi.



Mkoa wa Rukwa hauna matatizo ya njaa isipokuwa katika wilaya ya Mpanda ambako bei ya mahindi imepanda hadi kufikia sh. 10,000 kwa debe, kupanda kwa bei huko kumetoka na wananchi wa maeneo hayo kuuza kwa wingi mahindi yao za ziada 
katika nchi jirani ambako kuna njaa.



Mkoa huo wa Rukwa unatarajia kuzalisha tani milioni 1.2 za mahindi wakati mahitaji halisi ya mkoa ni tani 500,000.


Kutoka gazeti la Uhuru
ISSN 0876-3896 NA.19240
Na Maura Mwingira, Sumbawanga

HABARI HII ILICHAPIHSWA KWENYE MTANDAO WA HABARI TANZANIA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.