7 Oct 2011


Raia Mwema Ughaibuni
Kama hali ni hii, ustaarabu wa kisiasa tuusahau 2015!
Evarist Chahali
Uskochi
5 Oct 2011
Toleo na 206
HATIMAYE uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga umefanyika. Kama zilivyo chaguzi mbalimbali nchini tumeshuhudia kila aina ya vituko.
Kama kuna lolote la kujifunza, basi ,ni ukweli kwamba safari yetu ya kidemokrasia bado ni ndefu. Waingereza wana msemo kuwa katika jambo lililofanyika muda mrefu uzoefu una umuhimu wake (tafsiri isiyo rasmi ya in long run experience counts).
Lakini inapokuja kwenye masuala ya siasa zetu, uzoefu wa muda mrefu wa chama tawala CCM unageuka kuwa mithili ya kikwazo cha demokrasia.
Kwa vyovyote vile; matokeo ya uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Igunga, yamezidi kudhihirisha kuwa CCM ipo tayari kufanya lolote lile ili mradi ibaki madarakani.
Haihitaji kuwa mchambuzi mzuri wa siasa kupata picha kwamba kama chama hicho tawala kimeweza kutumia kila mbinu katika kampeni zake kwenye uchaguzi huo wa jimbo tu, basi, ni dhahiri kuwa kama ilivyo kwenye chaguzi kuu zilizotangulia, mwaka 2015 tutashuhudia tena mambo yasiyoendana kabisa na ustaarabu wa kisiasa.
Pengine kabla ya kuendelea zaidi na makala hii niweke wazi msimamo wangu kisiasa. Mara kadhaa nimekuwa nikihusishwa na CHADEMA; huku wengine wakinituhumu kuwa kujiweka kwangu karibu na chama hicho ni kwa matarajio ya kupata madaraka iwapo kitafanikiwa kukamata dola.
Ni kweli kuwa maandiko yangu mengi yameonyesha kuiunga mkono CHADEMA; lakini hiyo haimaanishi kuwa mimi ni mfuasi au mwanachama wake. Msimamo wangu kisiasa ni kutofungamana na chama chochote cha siasa.
Kwa vile dhamira yangu ni kuwa mchambuzi ‘halisi’ wa siasa, kufungamana na chama fulani kunaweza kuathiri utekelezaji wa majukumu yangu.
Itikadi yangu kisiasa ni uzalendo. Japo kwa mujibu wa Katiba yetu yenye mapungufu ni vigumu kwa mwananchi kushiriki katika siasa kwa ukamilifu pasipo kuwa mwanachama wa chama cha siasa, binafsi ninaamini njia bora ya kuutumikia umma ni kutanguliza maslahi ya taifa bila kujali uanachama wa chama cha siasa.
Katika siasa tunafundishwa kuwa nchi ni lazima iendelee kuwepo; ilhali vyama vya siasa vinazaliwa na vinaweza kabisa kufa kwa sababu moja au nyingine. Lakini linapokuja suala la uhai wa nchi, kila mwananchi anapaswa kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa sio tu inaendelea kuwepo bali pia inakuwepo katika hali inayostahili.
Sasa, kwa muda mrefu CHADEMA imejitambulisha kwa umma kama mtetezi wa kweli wa wanyonge na maslahi ya nchi yetu. Chama hicho kumekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi na mafisadi.
Kwa namna fulani, harakati za chama hicho zimeweza hata kuifanya CCM ijiangalie kama kweli ipo madarakani kuwatumikia Watanzania na si mafisadi pekee.
Kwa mantiki hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kila anayeipenda Tanzania yetu kwa dhati kuungana na harakati za CHADEMA katika safari yake ya kuhamasisha na hatimaye kufikia ‘uhuru wa pili.’
Naam, vita ya uhuru ‘wa kwanza’ ilikuwa ya kumwondoa mkoloni, mgeni aliyetunyanyasa kwa vile -pamoja na sababu nyingine - hakuwa na uchungu na nchi hii.
Vita hii ya sasa ni dhidi ya Watanzania wenzetu ambao kwa tamaa na ulafi wao wameweka mbele maslahi yao pasipo kujali wanalipeleka wapi taifa letu.
Kama nilivyoandika katika makala yangu katika toleo la wiki iliyopita mazingira ya chaguzi zetu, na kama ilivyoshuhudiwa huko Igunga, hayatoi fursa kwa vyama vya upinzani kuchuana na CCM kwa haki.
Uhuni uleule wa kila siku ambapo timu moja ya soka yenye wachezaji 11 inalazimika kuchuana na timu pinzani yenye wachezaji 15 (kwa maana ya wachezaji 11 wa kawaida wakisaidiwa na refa, washika vibendera wawili na kamisaa).
Watendaji wa serikali wanaopaswa kusimamia chaguzi pasipo upendeleo wanalazimika (aidha kwa uoga wao au kwa kufuata maelekezo ya serikali) kuipendelea CCM waziwazi.
Na chanzo kikubwa cha tatizo hili ni kufeli vibaya kwa harakati za kuondoa itikadi za kisiasa kwenye utumishi wa umma serikalini.
Katika mazingira ya kawaida, huwezi kumzuia Mkuu wa Wilaya asiipendelee CCM; ilhali anajua bayana kuwa iwapo chama hicho tawala kitashindwa kwenye uchaguzi unaofanyika kwenye jimbo lililopo kwenye wilaya ya DC huyo, basi naye atakuwa matatani.
Ni vigumu kwa Mkuu wa Mkoa ambaye amezawadiwa u-RC kutokana na ushiriki wake ndani ya CCM kumudu kusimamia uchaguzi kwa uhuru na haki na hatimaye kuruhusu CCM ishindwe kihalali.
Hali ni hivyo hivyo kwa Tume ya Uchaguzi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo utendaji kazi wa taasisi hizo ni kama kwa njia ya ‘remote control’ kwa matakwa ya chama tawala, kiasi kwamba malalamiko yoyote ya vyama vya upinzani huchukuliwa kama ‘kelele za mpangaji ambazo hazimnyimi usingizi mwenye nyumba’.
Ni kweli kwamba mawaziri wote tulionao ni wana CCM, lakini jukumu la waziri na wizara, kama ilivyo serikali, ni kuwatumikia Watanzania wote pasipo kujali itikadi zao.
Sasa waziri anapokwenda kwenye kampeni za uchaguzi na kuwatisha wapiga kura kwamba wakidiriki kuchagua mbunge wa chama cha upinzani watanyimwa maendeleo, ni uhuni wa hali ya juu wa kisiasa.
Katika kampeni huko Igunga tulisikia ‘hadithi’ kwamba CHADEMA wameingiza magaidi kutoka nje ya nchi kwa minajili ya kufanya vurugu kwenye uchaguzi huo. Hizi si tuhuma ndogo na zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa taifa letu.
Wanasema, moja ya athari za ugomvi kati ya wanafamilia ni uwezekano wa watu walio nje ya familia hiyo na ambao wana chuki na familia husika kutumia migongano huo wa kifamilia kuihujumu; huku wakijua fika itakapofika hatua ya ‘kusaka mchawi’ macho yataelekezwa kwa miongoni mwa wanafamilia wanaokorogana.
Kwa kutumia mfano huo wa kinadharia, iwapo kuna magaidi wanaotaka kuidhuru Tanzania wanaweza kutumia propaganda hizo mufilisi za CCM kuja kutudhuru; huku wakielewa fika uwepo wa imani fyongo kuwa ‘magaidi tishio kabisa kwa Tanzania wanalelewa na CHADEMA.’
Tunafanya yote hayo kwa faida ya nani? Sote tunawajua wabunge wetu na utendaji wa bunge lenyewe. Hivi kweli tunakubali kufarakanishwa kwa ajili ya watu ambao wengi wao wakishaingia bungeni wanakuwa bize zaidi na kutafakari namna ya kutumia mamilioni wanayolipiwa kama posho na mishahara?
Hivi kweli wapiga kura wanakuwa radhi kusikia porojo za Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ambaye alikuwepo madarakani kwa miaka 10 na kumbukumbu kubwa aliyotuachia ni tuhuma dhidi yake kuwa aliigeuza Ikulu kuwa sehemu ya kufanyia biashara?
Kwa vyovyote vile; matokeo ya uchaguzi huo mdogo wa Igunga yanamaanisha kuwa waathirika wakubwa ni wana Igunga wenyewe. Rushwa mbalimbali zilizoambatana na burudani kutoka ‘mjini’ hazitadumu muda mrefu, na busara au ukosefu wa busara kwa kumchagua mbunge asiyeweza kulitumikia jimbo kwa manufaa, zitaanza kuonekana muda si mrefu.
Kwa CHADEMA, uchaguzi huu mdogo unapaswa kuendelea kuwa darasa zuri kwao kujiimarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kilicho wazi kwa kila aliyefuatilia mwenendo wa uchaguzi huo ni ukweli kwamba chama hicho kilikuwa kinapambana na CCM, CUF na serikali kwa ujumla.
Idadi ya kura ambazo CHADEMA imepata ni ‘mithili ya ushindi’; kwani upinzani dhidi yao ulikuwa mkubwa kuliko umri wa chama chenyewe.
Kwa ndugu zangu wa CUF, ninachoweza kuwatahadharisha ni kwamba pasipo umakini wa kujua kwa nini chama hicho kilianzishwa, kuna hatari ya sio tu kupoteza nafasi yake kama wapinzani nambari mbili nyuma ya CHADEMA, bali pia kinaweza kujichimbia kaburi.
Siasa za Zanzibar zinakiweka chama hicho katika nafasi ngumu ya kupambana kwa dhati dhidi ya CCM, na badala yake kinaelekeza mapambano yake dhidi ya wapinzani wenzao wa CHADEMA.
Lakini CUF wanafahamu fika kuwa CHADEMA si chama tawala, na kuiandama kunaweza kuzua hisia kuwa CUF ipo ipo tu na ‘inatumia uhasama usiokuwepo na CHADEMA kwa minajili ya umaarufu tu na kuinufaisha CCM.
Nimalizie kwa kuwakumbusha tena Watanzania wenzangu kuwa kamwe tusikubali kufarakanishwa kwa ajili ya maslahi ya chama au mtu binafsi. Maendeleo na ustawi wa Tanzania yetu ni jukumu letu kama wananchi na sio kuliacha mikononi mwa wanasiasa wasioishiwa na ahadi ambazo hata wasipozitekeleza bado wana uhakika wa kuingiza mamilioni kwenye akaunti zao.
Inawezekana, timiza wajibu wako


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.