9 Oct 2011



Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete,

Kwanza naomba kukupa salamu za heri kwa siku yako ya kuzaliwa uliyoadhimisha jana.Mungu akuzidishie uhai,afya njema na nguvu ya kuendelea kututumikia Watanzania wenzako.

Baada ya salamu hizo,naomba niende kwenye mjadala usio rasmi ulioanzia juzi huko Twitter.Katika majibu yako kwa swali langu tunawezaje kuuelezea umasikini unaowakabili wakazi wa wilaya Kilombero (ambapo ulizuru majuzi) licha ya utajiri mkubwa wa raslimali-hususan ardhi yenye rutuba ambayo imelifanya eneo hilo kuwa maarufu kwa kilimo cha mpunga na nafaka ya mchele-ulieleza, naomba nikunukuu, "In Kilombero we've extension officers,SACCOS,market facilitation and mechanization initiatives.Some are using these opportunities" (kwa Kiswahili,Kilombero tuna maafisa ugani,vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa,uwezeshaji masoko,jitihada za matumizi ya mashine.Baadhi ya watu wanatumia fursa hizi."

Labda nikuulize,Mheshimiwa Rais,je uliona umasikini usiofichika unaowagubika wakazi wengi wa wilaya ya Kilombero?Ninatumai uliouna japo watendaji wengi wana tabia ya kuificha taswira zisizopendeza ili waonekane wanatekeleza wajibu wao ipasavyo.Hapa ninamaanisha si ajabu iwapo watendaji wa serikali wilayani Kilombero wangeamua kukupa picha ya "kila kitu ni shwari" ili uridhishwe na utendaji kazi wao.

Tuje kwenye jibu lako with an assumption kwamba uliona umasikini unaowakabili "matajiri" wa Kilombero (in the sense of kuwa wakazi kwenye sehemu yenye utajiri lukuki).Mheshimiwa Rais,tatizo la Tanzainia yetu halipo kwenye uwepo wa maafisa wenye majukumu fulani bali ni iwapo maafisa hao wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.Mara kadhaa,Mheshimiwa Rais,umelazimika kutumia madaraka yako kuwasaidia wananchi licha ya uwepo wa waziri husika,naibu wake,katibu mkuu,naibu katibu mkuu,mkurugenzi wa idara husika,mkuu wa mkoa,mkuu wa wilaya na pengine diwani kama si mwenyekiti wa serikali ya mtaa.

Mheshimiwa Rais,kama ilivyo kwenye sheria zetu nzuri na ambazo kwa hakika zingesimamiwa ipasavyo tungemedu kukabiliana na matatizo kama ufisadi kwa ufanisi (kwa mfano kwa kiutumia ipasavyo Sheria ya Uhujumu Uchumi) ni wazi pia kuwa laiti wengi wa watendaji unaoamini kuwa wanaweza kuwasaidia wananchi kufikia malengo yao ya kimaendeleo wangetimiza wajibu wao ipasavyo basi tusingeendelea kuwa moja ya nchi masikini kabisa duniani licha ya utajiri lukuki wa raslimali tulionao.

Ni wazi,Mheshimiwa Rais,kuwa laiti maofisa ugani unaowazungumzia huko Kilombero wangekuwa wanatimiza wajibu wao ipasavyo sio tu baadhi ya wakazi au wazawa wa neo hilo kama mie tusingekuwa na cha kulalamikia bali pia eneo hilo lingeweza kabisa kuwa mithili ya Saudi Arabia ya Tanzania (kwa kulinganisha uzalishaji mafuta wa Saudi na mchele wa wilaya ya Kilombero).Wnachofanya maofisa ugani unaosifia uwepo wao ni kukupatia ripoti nzuri zenye kutia matumaini lakini kimsingi wao ni miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya eneo hilo.

Mheshimiwa Rais,ninaomba kuafikiana nawe kuwa uwepo wa SACCOs umelta ukombozi mkubwa kwa wananchi hususan wa vijijini.Masikini hawa ambao hawana amana za kuwawezesha kukupa benki wamepata ukombozi mkubwa kupitia SACCOs.Hata hivyo,nyingi ya taasisi hizo zimekuwa zikikabiliwa na na tatizo sugu la mtaji mdogo ambao unapelekea kuhudumia wananchi wachache kuliko ilivyopaswa.

Mhehimiwa Rais,utakumbuka jinsi wajanja (polite word for mafisadi) walivyo-misuse "Mamilioni ya Kikwete" na sehemu ya fedha hizo kuishia mifukoni mwao badala ya kuwafikia walengwa.Moja ya taasisi ambazo zingenufaika sana na mpango huo ni SACCOs mbalimbali nchini.

Lakini pia,Mheshimiwa Rais,katika kuonyesha namna serikali yako isivyotoa kipaumbele cha kutosha kwa wakulima waodogo wadogo,fedha za stimulus package zilielekezwa zaidi kwa viwanda na kampuni (ikiwa pamoja na zilizo hewa) badala ya kuwatupia macho wakulima hawa.

Kwa hakika inapendeza kumwona mwekezaji wa kigeni akiwekeza katika kilimo cha mpunga.Lakini ni wazi,Mheshimiwa Rais,ingependeza zaidi iwapo uwekezaji huo ungefanywa na wakulima hao masikini.Sio tu uwekezaji huo ungeinua hali za maisha za walalahoi hawa lakini pia ungeweza kutoa ajira za kutosha na kusaidia harakati za maendeleo ya eneo hilo na nchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Rais,kuhusu kuwezesha upatikanaji wa soko,ninaamini kuwa laiti ungepeata wasaa wa kusikia kilio cha wakazi wa eneo hilo (na pengine maeneo mengine ya uzalishaji) ungebaini kuwa licha ya utajiri wa mpunga/mchele,wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na tatizo sugu la masoko.Kimbilio kubwa limekuwa kwa walanguzi ambao hujazana huko kila unapojiri msimu wa mavuno.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba wakati tunaadhimisha mika 50 ya uhuru wetu,baadhi ya wakazi wa Kilombero hullazimika kurejea njia za kale za uuzaji wa mazao yao ambapo barter trade hutumika kuwawezesha baadhi ya wakulima kumudu kupata bidhaa kama mitumba ya nguo,sukari na hata chumvi.Hivi Waziri husika ana mpango gani mahsusi ya kusaidia wakulima wa aina hii?Tumesikia kuhusu Kilimo Kwanza na Mapinduzi ya Kijani lakini kama ilivyokuwa katika zama za Ujamaa na Kujitegemea kauli mbiu hizo zimesihia kuwa matamko tu yenye malengo mazuri lakini utekelezaji sio wa kuridhisha.

Kuhusu sapoti katika matumizi ya teknolojia kwa maana ya mashine za kilimo,laiti Mheshimiwa Rais ungeongea na wananchi wa eneo hilo wangekufahamisha kuwa wanakabiliwa na tatizo sugu la uhaba wa matrekta.Machache yaliyopo ni mabovu na gharama zake ni kubwa mno kiasi kwamba wakulima wanalazimika kutegemea jembe la kono.Miaka 50 ya uhuru lakini mkulima wa Kitanzania bado anategemea zaidi jembe la mkono badala ya mashine za kisasa.

Mheshimiwa Rais,moja ya sababu zilizowashawishi Watanzania kukupa kura nyingi mwaka 2005 (na baadaye mwaka 2010) ni dhamira uliyoonyesha mwanzoni kuwa unataka kupunguza (kama si kumaliza kabisa) matatiao yanayowakabili Watanzania.Kihistoria,unafahamika kama miongoni mwa viongozi wachache walio karibu sana na wananchi (hata kabla hujaingia Ikulu).Uelewa wako kuhusu matatizo ya Watanzania ulitarajiwa kutoa suluhisho la tatizo la umasikini wa kutupa unaowakabili Watanzania wengi.

Binafsi siamini kuwa wewe binafsi ndio pekee wa kulaumiwa bali baadhi ya watendaji wako.Sasa,Mheshimiwa Rais,mwaka 2006 ulionya watendaji wabovu wasitafsiri vibaya upole wako kwani usingesita kuwawajibisha.Lakini ukweli ni kwamba wengi wa watendaji wako hao wameendela kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Rais,mwezi huu wa Oktoba utakuwa unatimiza mwaka mmoja mzima tangu uingie madarakani kwa awamu nyingine ya Urais.Lakini kama unakumbuka vyema,nyingi ya hadi ulizotoa mwaka 2005 hazijatekelezwa,na ukichanganya na za mwaka 2010 utaona kuwa una kazi ya ziada kumaliza utekelezaji wa ahadi hizo kabla hujang;atuka rasmi mwaka 2015.

Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa ili tuendelee tunahitaji WATU,ARDHI,SIASA SAFI na UONGOZI BORA.Sasa Mheshimiwa Rais,sio tu kwamba watu wapo bali pia   wana nia na kiu ya maendekleo yao binafsi na ya jamii zao.Ardhi ipo ya kutosha ikama ulivyoona huko Kilombero.Nadhani kinachokosekana na SIASA SAFI na UONGOZI BORA.

Mheshimiwa Rais,umebakiwa na miaka minne tu kabla hujamaliza muda wako kwa mujibu wa sheria.Hivi  ungependa umalize muda wako ukiwa na legacy isiyopendeza kuhusu masikini wa kutupa ambao hawana mbele wala nyuma.

Mwaka 2005 uliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania lakini baadhi yetu sasa tumekuwa tukitafsiri kama Mauisha Bora kwa kila fisadi.Ninaamini kabisa,Mheshimiwa Rais uliota ahadi hizo ukiamini kuwa zinatekelezeka.Lakini kwa bahati mbaya-au makusudi- hali yetu ni mbaya sana.Maendeleo tunayodaiwa kuyafikia yameendelea kubaki ndoto ya mbali.

Sasa Mheshimiwa kwa vile umebakiwa na miaka minne tu na rundo la ahadi zinazosubiri utekelezaji basi ninaomba utumie muda huu ulisailia kufanya jtihada za makusudi kuhakikisha unakumbukwa kwa jambo moja au jingine la msingi.

Basi Mheshimiwa Rais naomba nisikuchoshe sana na makala hii ndefu.Ninaamini una kila SABABU,na UWEZO lakini kiachokosekana ni NIA ya kuifikisha Tanzania mahala inapostahili kuwepo kimaendeleo.Kama Rwanda wamemudu kupiga hatua licha ya mauaji ya kimbari huko nyuma kuathri umoja wao kitaifa,na kama Botswana na Sychelles zinamudu kuwa majabali ya uchumi barani japo tunaweza kuwa na utajiri mkubwa wa raslimali kuliko nchi hizo,hivi tuna sababu gani ya kuendelea kusuasua kiuchumi na kimaendeleo kiujumla?

UKIAMUA,INAWEZEKANA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.