24 Nov 2013


KAMA nilivyoahidi katika makala yangu ndani ya toleo lililopita la gazeti hili maridhawa, wiki hii nitafanya uchambuzi kuhusu kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015.
Kwa wanaofuatilia safu hii, niliwahi kugusia mada hii katika toleo la Oktoba 26, 2011 ikibeba kichwa cha habari “Mizengwe na mitego ya mgombea urais kutoka CCM.” Mengi yametokea kati ya wakati huo na sasa, na kwa vile Uchaguzi Mkuu unazidi kujongea, nimeona ni muhimu kurejea tena mada hii.
Pengine msomaji unaweza kubaini mabadiliko kidogo katika mtizamo wangu kuhusu uwezekano wa CCM kung’oka madarakani 2015. Ninaomba kukiri kwamba chokochoko zisizo na msingi zinazoendelea ndani ya chama kikuu cha upinzani (na tegemeo la wengi kuiondoa CCM madarakani, CHADEMA, zinanifanya nikubaliane na ukweli mchungu kuwa fursa za chama tawala kushinda tena katika uchaguzi mkuu ujao zinazidi kuongezeka.
Na moja ya mambo ya kusikitisha zaidi kuhusu CHADEMA ni kuibuka kwa kundi la ‘wahuni wa kisiasa’ waliojipachika joho la uanaharakati. Kwa wababaishaji hao, kuanza kukubalika kwa chama hicho kumetoa fursa kwao kufahamika kwa namna moja au nyingine. Ni tatizo lilelile sugu katika jamii yetu la kusaka umaarufu hata kwa mambo ya kipuuzi, Waingereza wanasema ‘famous for nothing.
Sasa ‘wahuni’ hawa wamebinafsisha ajenda ya CHADEMA kupambana na ufisadi na kujipa hakimiliki kuwa wao pekee ndio wenye uelewa na mbinu za kukiwezesha chama hicho kufanikisha ajenda hiyo. Pasi kujali madhara ya uhuni wao kwa hatma ya chama hicho, wamejikuta wakitumiwa na maadui wa CHADEMA kwa njia isiyo ya moja kwa moja - kwa ‘remote control.’
Lakini kuashiria kuwa chama hicho kina wakati mgumu japo uongozi wake wa juu unaendeleza porojo za “njama za CCM na Usalama wa Taifa,” imefika mahala Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya mkoa anabandika tuhuma nzito dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, kwenye blogu yake. Hivi pamoja na madudu ya CCM unatarajia ‘utoto’ wa aina hiyo?
Tuelekee huko CCM sasa. Kwanza ninaomba kuweka bayana kuwa uchambuzi huu umeelemea katika uelewa wangu wa siasa za huko nyumbani, maongezi yangu na watu walio karibu na siasa hizo, na taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari (vya ‘asili’ na vya ‘kisasa’)
Kwa mtizamo wangu, hadi muda huu wanasiasa wawili wanaoongoza katika kinyang’anyiro cha kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete hapo 2015 ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Kwa ‘pembeni’ kidogo kuna Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta. Kimsingi, majina mengine yanayosikika kama William Ngeleja, John Magufuli na wengineo ni ya ‘kuchangamsha gumzo’ zaidi kuliko kuwa na uzito wowote wa maana.
Pengine baadhi ya wasomaji wangetamani nisiandike hivi lakini kimsingi hauepukiki, kama mazingira yatabaki kama yalivyo muda huu (constant) ni vigumu kwa mwanasiasa yeyote yule ndani na nje ya CCM kumzuia Lowassa kuwa rais mwaka 2015. Ninaomba nikiri kuwa ninatamani isiwe hivyo (kwa sababu binafsi ninaamini kuwa hafai kuwa Rais) lakini ukweli una tabia moja: kuuchukia hakuufanyi uwe uongo.
Turufu kubwa ya Lowassa ni uwezo wake mkubwa wa kifedha japo mwenyewe amekuwa akikanusha na kudai kuwa mamilioni anayoyamwaga katika harambee mbalimbali ni michango ya rafiki zake (hajawahi kuwataja wala kutueleza vyanzo vya utajiri wao).
Inaelezwa pia kuwa mwanasiasa huyo amejijenga mno ndani ya CCM kiasi cha kuwa sahihi kuhitimisha kuwa ana nguvu zaidi ya Mwenyekiti wa Taifa, Kikwete.
Sasa, huhitaji japo kozi ya muda mfupi ya siasa za nchi yetu kufahamu kuwa katika zama hizi fedha ndio nyenzo muhimu zaidi ya kumwezesha mwanasiasa kushinda uchaguzi kuliko kitu chochote kile. Mpigakura mwenye njaa hana habari na sera ya chama bali anachofikiria ni pishi ya mchele, doti ya khanga au kilo ya sukari.
Kwa upande wa Membe, turufu zake muhimu zaidi ni tatu. Kwanza, nafasi yake kama Waziri wa Nje inamweka karibu sana na Rais Kikwete kwani wanasafiri pamoja takriban katika kila ziara ya Rais nje ya nchi. Huhitaji kuwa mdadisi kufahamu kuwa watu wanaosafiri pamoja kwa miaka 10 mfululizo wana ukaribu kiasi gani.
Pili, kuna taarifa zisizo rasmi kuwa Membe anaungwa mkono na familia ya Kikwete. Katika moja ya mahojiano, mmoja wa watoto wa Kikwete, Ridhiwani, alikiri bayana kuwa anadhani Membe anaweza na anafaa kuwa Rais. Siasa za kifamilia zinaweza kubadilika lakini kwa angalau kwa sasa hali ipo hivyo.
Tatu, na kwangu hii ndio turufu muhimu zaidi, Membe ni ‘shushushu mstaafu.’ Pengine ni vigumu kuelezea kwa undani umuhimu wa kigezo hiki, lakini kwa kifupi, ni vigumu sana kwa mwanasiasa kuingia Ikulu pasi kuungwa mkono na Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi husika (angalau katika ‘demokrasia changa’). Mashushushu, kama watumishi wengine wa vyombo vya dola, wana tabia moja ya kumuunga mkono ‘mwenzao.’
Lakini sambamba na hilo ni kile kinachofahamika kama ‘sanaa za giza’ (dark arts), yaani kwa lugha ya kawaida, zile mbinu zinazosababisha kura kuyeyuka katika mazingira ya ajabu. Tukiamini kuwa mashushushu watamuunga mkono Membe, kwa nini basi wasiende mbali zaidi kuhakikisha kuwa anashinda kwa ‘gharama yoyote’ (na ‘gharama’ hapa si lazima iwe fedha)?
Kwa hiyo licha ya uwezo mkubwa wa kifedha wa Lowassa (tukiweka kando kukanusha kwake kuwa yeye si tajiri), Membe anaweza kumshinda kwa mbinu (ambazo kwa mtizamo wangu zinaweza kuhusisha watumishi wa sasa na wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa)
Kuhusu Sitta, nafsi yangu inanituma kuamini kuwa haitokuwa jambo la kushangaza endapo miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 tukakutana na kichwa cha habari kama hiki “Sitta: Lowassa ni chaguo la Mungu.” Kwa nini nina hisi hivyo? Binafsi ninamwona kama mwanasiasa asiyeaminika, anayeendeshwa na siasa za kusaka umaarufu na hata ‘rahisi kutulizwa.’ Kwa kifupi, Sitta anaendeshwa zaidi na imani (kuwa anaweza kuwa rais) kuliko uhalisia.
Kwa Sumaye, japo pengine ni mapema mno ‘kumpuuza,’ nafasi pekee ya yeye kuwa rais ni nje ya CCM. Tatizo kubwa kwa mwanasiasa huyu ni kwamba lugha anayoongea haieleweki ndani ya chama hicho. Naam, amejitokeza kuwa msemaji wa wanyonge na mkemeaji mkubwa wa ufisadi lakini sote tunafahamu kuwa hiyo sio sera ya CCM (angalau kwa vitendo na si kauli za majukwaani).
Nafasi hairuhusu kuangalia ‘odds’ dhidi ya Lowassa na Membe (ninataraji kufanya hivyo katika matoleo yajayo), lakini muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii nilishiriki katika mjadala mzito kuhusu hatma ya Tanzania yetu hususan jinsi ya kuzuia uwezekano wa kumpata Rais atakayetokana na rushwa. Pia tulijadili tatizo la rushwa na namna ya kulimaliza.
Kwa bahati nzuri, mjadala huo uliofanyika katika mtandao wa kijamii wa Twitter ulimvutia mwanasiasa kijana na Mbunge wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi. Kwa kifupi, alitueleza kiini cha tatizo la rushwa, na nini kinaweza kufanyika kupambana na tatizo hilo sugu. Bila kuingia undani kuhusu mjadala huo, ulipofikia tamati takriban kila mshiriki alikiri kuwa “kumbe CCM bado ina hazina zaidi ya hayo majina tunayoyasikia kila siku.”
Je, wanasiasa kama Abdullah, mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi wanaweza kuwa chaguo mbadala (alternative choice) hasa ikizingatiwa kuwa hawana ‘mawaa’ kama ya Lowassa au Membe (nitayajadili mbeleni)?
Nihitimishe makala yangu kwa kusisitiza jambo moja: japo kwa jinsi hali ilivyo ni muhimu kujiandaa kisaikolojia kuiona CCM ikiendelea kuwa madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, bado kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kikongwe kupumzishwa kwani kimeshindwa kazi.
Si Lowassa, Membe, Sitta au Sumaye anayeweza kuibadili CCM irejee misingi aliyoasisi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Tegemeo dogo katika chama hicho ni damu mpya kama za akina Abdulla Mwinyi, japo pengine ni mapema mno kuhitimisha hilo.
ITAENDELEA...


- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015#sthash.fO09a0nd.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.