2 Aug 2014

Kiuhalisia, kuna aina lukuki za watumiaji wa mitandao ya kijamii. Lakini katika kuweka mambo sawia, isingipendeza kuwa na 'makundi makuu' kama makabila vile kisha ukijitanabaisha upo 'kabila' lipi miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii?

Kimsingi, mitandao ya kijamii ni nyenzo ya kukuunganisha na watu-aidha kusikia au kutaka kusikika. Na kwa maana hiyo, ni muhimu kwa mtumiaji kujitambua mapema, na kujiweka katika kundi analodhani linamfaa au lina manufaa zaidi kwake.

Kwahiyo,katika uchambuzi huu, kuna makundi 10 ya msingi ya watumiaji mbalimbali wa mitandao hiyo ya kijamii. Ni matarajio ya makala hii kwamba utapomaliza kuisoma,utabaini upo kundi gani, au ungependa kuwa katika kundi gani. Enjoy!

068ecf0a8e7ac52b676ef4afe6a5a811

Kundi la kwanza ni MSIKILIZAJI: Huyu anapendelea sana mitandao ya kijamii lakini mara nyingi yupo kinya, hataki kuonekana wala kusikika. Kama jina lilivyo, yeye ni msikilizaji tu.Anaweza kuipenda post yako kwenye Facebook lakini akakaa kimya.

Kundi jingine ni MWANAHARAKATI: Huyu ni mtu anayetambua nguvu ya mitandao ya kijamii katika kufikisha ujumbe,na anafanya kila awezalo kuitumia ipasavyo ili kufikisha sauti yake iskike na hatimaye kuleta tofauti inayokusudiwa. (Binafsi nadhani ninaangukia katika kundi hili)

Kundi la tatu ni MCHAFUZI WA HALI YA HEWA: Huyu ni mtu anayedhani kwamba mabandiko yake mtandaoni ni ya kiwango cha hali ya juu, kiasi cha kuamini kuwa kila mtu anastahili kutumiwa kwenye inbox yake (tena pasi kujali ridhaa ya mtumiwa). Nadhani ushakutana na DM au meseji Facebook yenye ujumbe 'angalia picha hii...' na ukilogwa kubonyeza link husika waweza kujutia nafsi yako.

Kundi la nne ni MWENYE MAHABA NA ISHU FLANI: Ushakutana na mtu anapenda mpira kupita kiasi, na ukifuatilia mabandiko yake kwenye mitandao ya kijamii utadhani ni chombo cha habari. Mtu wa aina hii anaendeshwa na mahaba ya akipendacho-iwe siasa, burudani, uchumi au ishu nyingine yoyote ile, na anatumia muda kuifuatilia ishu hiyo na ku-share na jamii. Kimsingi watu wa aina hii wanaweza kuufanya mtandao wa kijamii kuwa mahala pa kujifunza kama sio kuburudisha. (Nahisi pia ninaangukia kundi hili kwa mada nizipendazo, yaani siasa, teknolojia, habari na intelijensia)

Kundi la tano ni KIPEPEO WA JAMII Huyu ni yeye na picha. Atakjuonyesha kila sehemu aliyotembelea, kila shughuli aliyofanya, na kila hachoki ku-tag watu kwenye picha hizo. Pengine ni mtu wa watu lakini pengine ni msumbufu tu anayetaka kuonyesha maisha yake kwa njia ya picha. Kipepeo wa jamii anaweza kutengeneza idadi kubwa ya marafiki kwa sababu mara nyingi huwa kama analazimisha kila mtu awe rafiki yake kwa njia ya picha.

Kundi la sita ni WASUMBUFU MTANDAONI: Huyu ni mtu anayeweza kuvuka mpaka kati ya kupishana hoja kistaarabu hadi kufikia kashfa,matusi na udhalilishaji. Mara nyingi mtu wa aina hii hung'ang'ania ishu zisizo za msingi lakini zenye madhara kwa hadhi au heshima ya mlengwa katika jamii. Njia pekee ya kukabiliana na mtu wa aina hii ni kum-block, kwa sababu jaribio lolote la kumuelimisha-hata liwe la kistaarabu kiasi gani-litaishia kuzua mabalaa zaidi.

Kundi la saba ni MWALIMU: Huyu ni kama yuole wa kundi la nne hapo juu (mwenye mahaba na ishu flani) lakini yeye hana ishu maalumu bali anapenda ku-share uelewa (knowledge). Mara nyingi anakuwa na uelewa wa kutosha lakini haridhika kukaa na uelewa huo peke yake na badala yake anashirikisha wengine.Mtu wa aina hii anaweza kuwa muhimu sana katika mtandao wa kijamii kwani anatoa elimu bure (nami najihisi kama nipo kundi hilo,japo siwezi kujihukumu).

Kundi la nane ni ALIYEANZA KITAMBO: Mara nyingi utamgundua mtu huyu katika katika mtandao mpya (angalau kwake), ambapo kwa vile alikuwepo tangu zama za Facebook haijawa maarufu kama sasa basi anataka kila mtandao wa kijamii anaojiunga nao 'ufuate kanuni' za Facebook ya zamani. Watu wa aina hii hupatikana zaidi Twitter ambapo hufanya kiola wawezalo kuigeuza Twitter kuwa Facebook. Huyu anaweza kukukera kirahisi kwa sababu anataka kulazimisha matamanio yake yawe ya watu wote.

Kundi la tisa ni la MWENYE KITABU CHEUSI: Kama hufahamu, kitabu cheusi ni kama diary yenye kumbukumbu mbalimbali za kila siku pamoja na namba za simu au anwani za watu mbalimbali. Mara nyingi mtu wa aina hii yupo kwenye mtandao wa kijamii kwa ajili ya mawasiliano na wengine. Si ajabu kuona mtu wa aina hii akiwa na 'marafiki' au 'wafuasi' kibao kwa sababu yupo kwenye mtandao wa kijamii kwa ajili hiyo.

Kundi la kumi na la mwisho ni MTU WA FAMILIA:Huyu anaweza kuwa mtu asiye na uzoefu sana na teknolojia lakini mara baada ya kufahamu jinsi ya kuitumia basi anataka kuhakikisha anakuwa karibu na 'familia' yake. Mara nyingi mtu wa aina hii yupo katika mtandao wa kijamii kwa minajili ya kifamilia zaidi, na ninaposema familia inajumuisha pia watu wa karibu na mhusika.

Kama nilivyobainisha awali, mitandao ya kijamii ina aina lukuki za watumiaji japo hizi 10 zinaweka pamoja watu hao katika makundi hayo makuu. Je hadi kufikia hapa unadhani upo katika kundi gani?

CHANZO: Makala hii imetafsiriwa kutoka tovuti ya DAILYGENIUS

Endelea kutembelea blogu hii ili kupata makala na habari mbalimbali, na iwapo ni mpenzi wa teknolojia kama mie basi usikose kubonyeza hapo juu ya blogu palipoandika TEKNOLOJIA ili kupata kila kilicho bora katika anga hizo. 



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.