11 Aug 2014

                   
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba nusura wapigane baada ya kupishana kauli wakati wa mjadala wa ndani ya Kamati Namba Sita inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo inayofanyia vikao vyake katika moja ya kumbi za Dodoma Hoteli zinasema, mvutano huo ulitokea Alhamisi iliyopita na kusababisha Wassira kusitisha kwa muda kikao hicho, kisha kwenda kuwasuluhisha.
Jana, Wassira licha ya kukiri kutokea kwa mvutano huo, alikanusha taarifa kwamba aliahirisha kikao hicho kwa ajili ya kuwasuluhisha.
“Kupishana katika masuala haya makubwa ni jambo la kawaida, hivyo mimi sidhani kama ni jambo linalopaswa kwenda mpaka kwenye magazeti maana kila wakati hutokea tofauti hizi na ndiyo maana sisi wenyeviti tupo ili kusimamia mijadala,” alisema Wassira na kuongeza:
“Lakini kwamba eti hilo jambo lilisababisha kikao kuahirishwa au kusitishwa hapana, kikao kiliendelea na kazi yake baada ya hilo lililoleta na ubishani kumalizwa”.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema mvutano huo ulitokea wakati kamati hiyo ilipokuwa ikijadili Sura ya Nne na Tano, hususan suala la uraia wa nchi mbili. Sura ya tano ndiyo inayozungumzia masuala ya uraia.
“Sophia Simba yeye anataka uraia wa nchi mbili wakati Werema alikuwa akisema hilo jambo haliwezekani kutokea kwa sasa,” kilisema chanzo chetu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mvutano huo uliendelea baina ya viongozi hao na ndipo Jaji Werema aliposimama katika mchango wake na kuhoji elimu ya Simba, hivyo kuamsha hasira za waziri huyo ambaye pia alijibu mapigo.
“AG alipopewa nafasi ya kuzungumzia baada ya mabishano ya muda alihoji shule (elimu) ya Simba kwamba amesoma shule gani akimaanisha kwamba ni mgumu kuelewa, kwa hiyo waziri alikasirika na yeye alianza kujibu mapigo,” kiliongeza chanzo hicho.
Baada ya kutokea mvutano huo, baadhi ya wajumbe waliingilia kati kusitisha mzozo huo, ndipo Mwenyekiti Wassira alipositisha kikao hicho kwa muda kisha kuwasuluhisha wahusika.
Walipotafutwa jana kwa nyakati tofauti kuzungumzia mzozo wao, Werema na Simba hawakuwa tayari kubainisha kilichotokea.


Werema alitaka aachwe apumzike na kwamba mambo ya kamati yaachwe kwenye kamati.
“Jamani hamtuachi hata tupumzike Jumapili yote hii? Tafadhali bwana niache nipumzike, hayo mambo kama ni ya kamati, yaachwe kwenye kamati,” alisema Werema na kukata simu.
Simba baada ya kuulizwa alisema: “Heeeee hayo makubwa… I have no comment (sina cha kusema”), kisha alikata simu.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema ofisi yake haikuwa imepata taarifa kuhusu mzozo huo na kwamba angefuatilia ili aweze kufahamu kuhusu kilichojiri.
“Nina maofisa wa kutosha katika kila kamati, sasa nashangaa kwamba jambo kubwa kama hilo litokee halafu nisipate taarifa, lakini ngoja nifuatilie lakini kwa sasa sina taarifa yoyote,” alisema Hamad.
Werema
Juni mwaka huu, Jaji Werema alitaka kumtia adabu Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila bungeni Dodoma baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuahirisha kikao cha Bunge, ikiwa ni muda mfupi baada ya Werema na Kafulila kurushiana maneno bungeni.
Jaji Werema alichukia baada ya Kafulila kumwita mwizi, akijibu mapigo baada ya mbunge huyo kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya kutofautiana kauli kuhusu mgogoro wa fedha za akaunti ya Escrow kulipwa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
CHANZO: Mwananchi 
ANGALIZO: Picha ni kielelezo tu 

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.