“Magufuli ni dikteta. Yeye ni nani hasa wa kutupangia mikutano ya kisiasa?” Ni kauli ya mtu mmoja kwenye mtandao wa kijamii wa twitter. “Kama Magufuli ni dikteta, basi hamia Sudan ya Kusini…au Somalia,” lilikuwa jibu la mtumiaji mwingine wa mtandao huo.
Mada ya ‘Magufuli ni dikteta/Magufuli si dikteta’ ndiyo inayotawala zaidi kwenye mijadala mbalimbali, hususan, ya kijamii, ambako kwa uzoefu wangu, ni kati ya maeneo muafaka kupima maoni na mitazamo ya watu wa kada mbalimbali.
Kwa kiasi kikubwa, kambi inayodai kuwa ‘Magufuli ni dikteta,’ inajumuisha wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao sasa wanahamasishana kuhusu mkakati wao mpya uanaofahamika kama ‘UKUTA,’ yaani ‘Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania.’ Sina hakika neno ‘umoja’ limeingiaje hapo kwa sababu tofauti na ‘Umoja wa Katiba ya Wananchi’ (UKAWA) ulioijumisha Chadema na CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ‘umoja’ wa UKUTA unakihusisha Chadema pekee.
Kwa upande mwingine, kambi inayomtetea Dk. Magufuli kuwa si dikteta, inaundwa na wafuasi wa chama tawala CCM, na idadi kubwa tu ya Watanzania wengine wanaoamini kuwa si tu kwamba kiongozi huyo anafanya kazi nzuri bali pia kuna masuala ya muhimu zaidi kwa nchi yao kuliko mikutano/maandamano ya kisiasa.
Hoja ya Chadema, au UKUTA yao, ni kwamba agizo la serikali kuzuia mikutano na maandamano ya kisiasa ni la kidikteta, linakandamiza haki yao ya kikatiba ya kufanya shughuli za kisiasa, na hawahitaji ruhusa ya Rais katika utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
Sambamba na hilo, malalamiko dhidi ya Dk. Magufuli na serikali yake ni kamata-kamata inayoendelea dhidi ya viongozi na wanachama wa vyama vya Upinzani. Kwa wapinzani, huo si udikteta tu bali pia mkakati wa kuviua vyama hivyo.
Pengine katika hatua hii ni muhimu kuweka bayana maslahi yangu. Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, nilimuunga mkono na kumpigia kampeni Dk. Magufuli, kwa kutumia haki yangu ya kikatiba na utashi wangu.
Kwangu, uchaguzi ulishamalizika mwaka jana. Tumeshampata Rais na serikali yake. Ninaiangalia Tanzania kama nchi na si kwa ‘lensi’ ya u-CCM au u-Chadema. Uchambuzi huu mfupi unafanyika katika mantiki hiyo, kwamba Tanzania yetu ni muhimu zaidi kuliko vyama vya siasa, na maslahi ya taifa ni muhimu zaidi ya maslahi ya kiitikadi.
Baada ya angalizo hilo, nina hoja kuu mbili ambazo ndio mtazamo wangu rasmi kuhusu ‘Magufuli ni dikteta/si dikteta.’
Hoja ya kwanza ni kwamba sidhani kuwa uamuzi wa kuzuia shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani ni la busara. Katiba inaviruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli hizo alimradi zinazingatia sheria na hazisababishi uvunjifu wa amani.
Kwa kuazima busara za Kighoma Malima, “haki haitolewi kama zawadi. Haki hudaiwa, wakati mwingine kwa nguvu,”. Wapinzani wanaona ni sawia kwao kutumia nguvu kudai haki yao.
Hivi, vyama vya upinzani vikiachwa kufanya mikutano yao (kwa kuzingatia sheria za nchi) kutakuwa na madhara gani hasa? Katika hili, naona kama Rais Magufuli anashauriwa vibaya, hasa ikizingatiwa kuwa kwa kiasi kikubwa kabisa, amemudu kumiliki takriban hoja zote za muhimu za vyama vya upinzani, hususan, vita dhidi ya ufisadi. Binafsi, ninaona zuio hilo la shughuli za kisiasa za wapinzani ni sawa na “kuwapa wapinzani kitu cha kuongea.”
Hoja yangu ya pili ni kwamba ifike mahala vyama vya upinzani vitambue kuwa mikutano na maandamano si shughuli pekee za vyama vya siasa. Kuna masuala mengine mbalimbali yanayoweza kufanywa na vyama hivyo badala ya mikutano na maandamano tu.
Ndiyo, mikutano na maandamano ni haki ya vyama vya siasa, lakini si kipaumbele kikubwa cha Watanzania, hasa katika kipindi hiki ambacho Rais Magufuli anafanya kila jitihada kuiondoa Tanzania yetu kutoka katika lindi la ufisadi ambao kwa kiasi kikubwa umechangia umasikini unaoikabili nchi yetu.
Nimalizie makala hii kwa kukumbushia kuwa huko nyuma, takriban sote – ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani – tuliafikiana kuwa “ili Tanzania yetu iendelee, twahitaji Rais dikteta.” Na yayumkinika kuhisi kuwa kama udikteta wawezesha kuongeza pato la taifa, kuwaibua watumishi hewa, kuwadhibiti ‘wauza unga,’ na kurejesha nidhamu ya ‘asiyefanya kazi na asile,’ basi Dk. Magufuli aendelee tu kuwa ‘dikteta.’