Ninaipenda siasa...kama stadi (study, yaani kuisoma), lakini kwa hakika ninapata shida sana na jinsi mengi ya ninayosoma katika stadi za siasa (political studies) yanavyogeuka inapokuja kwenye matendo au shughuli za kisiasa an zinazohusiana na siasa.
Stori kidogo. Fani niliyotamani sana kuisoma na pengine kubobea ni utabibu. Nilitamani mno kuwa daktari. Lakini ndoto yangu ya udaktari ilipata kikwazo baada ya kupata matokeo ya mtihani wa kumaliza kidato cha nne. Japo nilipata A kwenye Kemia na C kwenye Baiolojia, niliambulia D kwenye Hisabati na kufeli kabisa Fizikia ambapo nilipata F. Na japo nilipata Division One, uwezekano wa kuchukua 'combination ya udaktari' yaani PCB (Fizikia, Kemia na Baiolojia) kidato cha tano uliathiriwa na hiyo F ya Fizikia. Uwezekano pekee ulibaki kwenye kujaribu combination ya CBG (Fizikia, Kemia na Jiografia) ambayo ingeniwezesha kuikwepa Fizikia.
Nilipojiunga na kidato cha tano katika sekondari ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys') nikakumbana na vikwazo vingine. Kwanza, Kemia ya kidato cha kwanza mpaka cha nne ni tofauti kwa kiasi kikubwa na ile ya kidato cha tano na cha sita. Kuna kitu inaitwa Physical Chemistry ambayo kimsingi ni kama mchanganyiko wa Kemia, Hisabati na Fizikia. Sasa kama nilivyotanabaisha hapo awali, udhaifu wangu katika Fizikia na Hisabati ulimaanisha kuwa nisingeweza kuimudu Kemia ya High School.
Pili, shule yetu ilikuwa haina mwalimu ya Jiografia, na ilibidi tuwe tunakwenda shule ya jirani ya Tabora Girls' kuhudhuria vipindi vya somo hilo. Angalau Baiolojia haikuwa tatizo japo kiukweli ilihitaji uwezo mkubwa wa kukariri na kuelewa majina ya sampuli za viumbe ambayo mengi yana asili ya Kilatini au Kigiriki. Kwahiyo kwa kifupi, dhamira yangu ya kusoma combination ya CBG ilikufa kifo cha asili.
Hivyo nikaamua kusoma combination yenye masomo ya Historia, Jiografia na Kiingereza. Hii ilikuwa mteremko kwa kiasi kikubwa, lakini ndoto yangu ya kuwa daktari ndio ikayeyuka. Lakini wanasema kile unachotaka sio lazima ndio unachopata (what you wish for is not always what you get).
Sukuma miaka kadhaa baadaye, nikajiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam na hapo nikajikuta nina uchaguzi wa ama kuzamia kwenye sayansi za siasa na utawala wa umma (pilitical science and public administration au sosholijia, elimu inayohusu masuala yya jamii. Mwaka wa pili, nikafanya uamuzi wa kuchukua hiyo choice ya pili, yaani Sosholojia. Kwa hakika niliipenda sana sosholojia. Yaani ilinisaidia mno kuielewa jamii. Miongoni mwa masomo ya kupendeza sana yalikuwa lile lilifundisha kuhusu uhusiano wa jamii, utamaduni na afya; somo la jinsia na uhusiano wa kijinsia, na zaidi ya yote ni sosholojia ya dini ambapo pamoja na mambo mengine tulifundishwa kuhusu Ukristo, Uislamu na Imani za Asili.
Sukuma miaka kadhaa zaidi mbele, nikapata skolashipu ya kuja hapa Uingereza kusoma Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Politics and International Relations), mkazo ukiwa kwenye masuala ya usalama. Kwa vile skolashipu ni kama zawadi, mwanafunzi anakuwa hana uchaguzi. Nilitamani sana kuendelea na Sosholojia lakini sikupewa fursa ya kuchagua. Na hivyo ndivyo nilivyojikuta nikiingia kwenye stadi za siasa. Tuishie hapo/
Kwanini nimeelezea stori hiyo? Ni kwa sababu kama nilivyosema awali, ninaipenda siasa kama stadi. Yaani baada ya kutokuwa na choice ya kusoma sosholojia, na 'kulazimishwa' kusoma Siasa, ikabidi niipende tu. Niliipenda pia kwa sababu siasa za kimataifa zina 'raha' yake kuzielewa, ukichanganya na maeneo kama diplomasia, amani na 'ugomvi' (peace and conflicts) na masuala ya usalama wa kimataifa (international security).
Lakini tatizo la siasa kama stadi ni ukweli mchungu kwamba kile unachosoma darasani mara nyingi hakiakisi hali halisi mtaani. Siasa kama fani au stadi sio mbaya, ina mafunzo mengi, inafundisha miongozo mingi na kanuni nyingit muhimu kwa maisha ya mwandamu, lakini mtaani hali ni tofauti. Sihitaji kuelezea kwa undani kwanini watu wengi wanaichukia siasa. Lakini mfano mwepesi ni kwenye kampeni za uchaguzi ambapo utasikia chama kikitanabaisha sera nzuri kabisa lakini baada ya kuingia madarakani kikaishia kufanya kinyume kabisa na kilichoyaahidi. Na kwa Tanzania yetu tuna mfano hai wa jinsi sera tamu za CCM zinavyoishia kuwanufaisha matajiri na mafisadi huku zikiwadidimiza walalahoi.
Na mfano mchungu zaidi, uliopelekea niandike makala hii, ni jinsi Chadema katika mwavuli wa UKAWA inavyoelekea kuwasaliti mamilioni ya Watanzania kwa uwezekano wa kumpokea fisadi Edward Lowassa kuwa mgombea wa urais.
Jana niliumia mno nilipoona picha kadhaa zinazomwonyesha Lowassa akiwa na viongozi wa UKAWA. Baadaye, mwenyekiti wa NCCR, moja ya vyama vinavyounda UKAWA pamoja na Chadema, CUF na NLD, alitamka bayana kuwa wanamkaribisha Lowassa kujiunga nao.
Lakini baadaye kidogo nikapata ahueni baada ya kupatikana taarifa zilizothibitishwa na akaunti ya Twitter ya Chadema Media kuwa picha zilizokuwa zinamwonyesha Lowassa na viongozi wa UKAWA ni feki, yaani zilikuwa photoshopped. Hata hivyo furaha hiyo haikudumu muda mrefu baada ya Mbatia na wenzake kutangaza bayana kuwa wanamkaribisha Lowassa . Na kuna uwezekano leo Jumanne, aidha UKAWA wakamtangaza Lowassa kuwa mgombea wao wa Urais au Lowassa mwenyewe akatangaza kujiunga nao.
Huu ni usaliti mkubwa mno hasa upande wa Chadema, chama kilichojidhihirisha kuwa kinauchukia ufisadi kwa dhati. Sote twakumbuka jinsi Chadema ilivyojipatia umaarufu kwa kupambana na ufisadi, hasa baada ya kutangaza hadharani 'orodha ya aibu' (list of shame) pale Mwembeyanga jijini Dar ambapo walitaja orodha ya mafisadi akiwemo Lowassa. Kadhalika Chadema ilifanya jitihada kubwa kuibua ufisadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na skandali ya Richmond iliyopelekea Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu. Vilevile chama hicho kilitufumbua macho kuhusu ufisadi wa EPA, Meremeta, Dowans, Buzwagi, TanGold, Kiwira, nk. Kwa kifupi, ilikuwa haiwezekani kuzungumzia mapambano ya ufisadi Tanzania bila kuitaja Chadema.
Na katika harakati zake za kupambana na ufisadi, kuna Watanzania wenzetu waliopoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa vibaya na kuachiwa ulemavu kwa kukiunga mkono chama hicho.
Na kwa kuonyesha kuwa Chadema ilikuwa mwarobaini kwa CCM na mafisadi kwa ujumla, chama hicho kilifanyiwa kila aina ya hujuma. Mara kiliitwa chama cha kidini, baadaye kikaitwa cha kikabila, na hadi hivi majuzi kiliitwa chama cha kigaidi. Lakini taratibu Watanzania walifumbuka macho na kubaini kuwa sababu kubwa ya CCM na serikali yake kuiandama Chadema ni kwa vile chama hicho cha upinzani kilichofanya vizuri tu katika uchaguzi mkuu uliopita kinasimamia maslahi ya wanyonge ilhali CCM inatetea mafisadi na ufisadi.
Japo mie binafsi sikuwa mwanachama wa Chadema, nilikiunga mkono kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi kulingana na msimamo wangu kwenye suala hilo. Nilikuwa nina imani kuwa laiti Chadema ikifanikiwa kuingia Ikulu basi kwa hakika safari ya kuipeleka Tanzania yetu mahali inapostahili kuwa inawezekana.
Sasa hili la kumpokea Lowassa ni pigo kubwa mno na ni usaliti wa hali ya juu kabisa. Ndio, Lowassa anaweza kuwasaidia Chadema na UKAWA kuingia Ikulu. Lakini kwa kuangalia tu maswahiba wa Lowassa utaweza kujua tutakuwa na serikali ya aina gani. Sipati shida kubashiri kuwa tutaishia kuikumbuka CCM.
Na huo ndio ubaya wa siasa katika vitendo, tofauti na ilivyo nzuri na mwafaka katika stadi. Kwamba kistadi za siasa, Chadema ilijijenga na kupata umaarufu kwa kuzingatia kanuni ilizojiwekea na ikajitambulisha kama chama kilichopo kwa maslahi ya wanyonge, tofauti na CCM iliyokimbia kanuni zake na kuwakumbatia matajiri na mafisadi. Lakini ghafla bin vup, Chadema inaelekea kwenda kulekule ilipo CCM.
Nimalizie makala hii kwa kuahidi kufanya uchambuzi wa kina kuhusu suala hili katika makala yangu ya wiki ijayo katika gazeti la Raia Mwema. Spoiler alert, wiki hii katika toleo litakalokuwa mtaani kesho ninamjadili Magufuli.
Asanteni kwa kuchukua muda wenu kunisoma.