18 Dec 2014

Desemba 9, ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa. Niliadhimisha sikukuu hiyo kwa sala, kumshukuru Mungu kwa kunijaalia kuongeza mwaka mwingine katika umri wangu sambamba na kuomba baraka zaidi.
Kadhalika, kama zilivyokuwa sikukuu zangu za kuzaliwa huko nyuma, niliadhimisha siku hiyo kwa kufanya tafakuri ya nilipotoka, nilipo na niendako.
Siku ya kuzaliwa ina pande mbili, moja ya furaha kwa maana ya kutimiza mwaka mwingine katika maisha, na ya pili ni kutambua kwamba umri unakwenda mbele, na hivyo kupitia malengo mbalimbali kuona kama yametimia, na kwa kiwango gani, na wapi panahitaji jitihada zaidi, sambamba na kuweka malengo mapya inapobidi.
Kadhalika, wakati kwa vijana wenye umri mdogo, sikukuu ya siku ya kuzaliwa ni furaha tupu, ambapo kwa mfano, sheria mbalimbali zinatoa ruhusa fulani kwa kutimiza umri fulani, kwa wenye umri mkubwa, sikukuu hiyo huambatana na ukweli mchungu kuwa ‘dakika zinayoyoma.’
Kwa kijana wa miaka 17, kutimiza miaka 18 kunamaanisha fursa ya kupiga kura, kwa mfano. Kwa hapa Uingereza, kutimiza miaka 18 kunamaanisha ruhusa kisheria kutumia kilevi.
Lengo la makala hii si kuzungumzia sikukuu yangu ya kuzaliwa. Ukweli kwamba sikukuu yangu ya kuzaliwa inalingana na sikukuu ya kusherehekea uhuru wa Tanganyika huzua tafakuri nyingine mpya kuhusu nchi yetu.
Wakati sikukuu ya kuzaliwa kwangu ni suala langu binafsi, sikukuu ya uhuru wa Tanganyika ni suala linalomgusa kila mmoja wetu.
Japo hujiskia fahari kuchangia sikukuu ya kuzaliwa na Tanganyika, ukweli mchungu ni kwamba ninalazimika pia kujiuliza nchi yangu imetoka wapi, ipo wapi, na inaelekea wapi, na mara nyingi tafakuri hiyo huvuruga kabisa sikukuu yangu ya kuzaliwa.
Kama nilivyotimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe, jana Tanganyika yetu imetimiza miaka 53 tangu ipate Uhuru. Wakati binafsi ninaweza kuhitimisha kuwa angalau nimepiga hatua fulani kimaisha, huku malengo kadhaa niliyojiwekea huko nyuma yakitimia au yakielekea kutimia, kwa mwenzangu Tanganyika hali si nzuri.
Tumefika mahala, baadhi ya Watanganyika wamefikia hatua ya kutamani mkoloni asingeondoka.
Nitakuwa mwenye roho mbaya iwapo nitazungumzia mabaya tu yaliyoiandama na yanayoendelea kuiandama nchi. Lakini kwa vile tafakuri katika siku muhimu kama hiyo inalenga zaidi kuangalia maeneo yanayoifanya isiwe timilifu, basi inakuwa vigumu kutoyapa uzito matatizo badala ya mafanikio.
Kadhalika, siku hiyo ni ya kupima mzani wa mafanikio na kufeli, na pindi mzani ukielemea upande wa kufeli, basi lazima taa ya tahadhari iwashwe kwani hali hiyo yaweza kuashiria matatizo zaidi huko mbele.
Kati ya sababu za kudai Uhuru kutoka kwa mkoloni ni kutaka kujitawala wenyewe, sambamba na kuondokana na mfumo wa kibaguzi uliotufanya tuwe mithili ya wageni katika nchi yetu wenyewe.
Miaka kadhaa baada ya Uhuru, jitihada zilizoongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, zilionyesha matunda ya uhuru na si tu tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga jamii yenye usawa lakini pia tulimudu kujitegemea wenyewe.
Matatizo yalianza kujichomoza baada ya Mwalimu kuondoka madarakani na hatimaye kufariki kwake. Kimsingi, nchi yetu ilikuwa kama ipo mikononi mwa Nyerere, na ilikuwa inasubiri aondoke tu ili irejee mahala pabaya pengine zaidi ya ilivyokuwa kabla ya Uhuru.
Ieleweke kwamba wakati mkoloni alikuwa na ‘excuse’ (japo isiyokubalika) ya kuiba raslimali zetu kwa ajili ya matumizi ya viwanda vyao huku Ulaya, wakoloni weusi kwa maana ya Watanganyika wenzetu waliosomeshwa na Watanganyika wenzao waliojinyima ili wapate viongozi, hawana sababu moja hata ya kutusaliti.
Yaani angalau mkoloni angeweza kujitetea kwamba acha niibe kwa sababu hii nchi si yangu. Lakini kwa wakoloni weusi, Watangayika wenzetu wanaoendekeza ufisadi hawawezi kudiriki kujitetea kwa namna yoyote ile, hasa ikizingatiwa kwamba kihistoria, takriban sote ni ndugu kwa kuzingatia asili yetu.
Kwa maana hiyo, kiongozi anayekabidhiwa dhamana kisha akafanya ufisadi, anajiathiri yeye mwenyewe pia kwa sababu mahala fulani, kuna mtu wake wa karibu atakayekuwa mhanga wa ufisadi huo.
Tusiende mbali. Angalia skandali ya ufisadi wa hivi karibuni wa Tegeta Escrow. Baadhi ya wabunge walikuwa wakitokwa na mapovu kutetea kuwa fedha fedha hizo si za umma ilhali nao ni sehemu ya umma wanaoukana. Takriban wote waliojivika kilemba cha itikadi, mdudu anayeiangamiza Tanganyika yetu kwa kasi kubwa.
Si kwamba watu hawa wamekunywa maji ya bendera kiasi cha kutoelewa kitu kingine chochote zaidi ya maslahi ya chama chao bali itikadi yatumika tu kama kilemba cha kufika nia zao mbaya.
Lakini pia suala la Tegeta Escrow limeibua tena tatizo moja linalotukwaza kama Taifa. Hili ni utegemezi wetu kwa wanasiasa na taasisi kama vyama vya siasa na watu, kwa maana ya wanasiasa.
Ukiweka kando kelele ndogo kwenye mitandao ya kijamii kudai wananchi watendewe haki kwa kurejeshewa fedha zilizokwapuliwa katika akaunti ya Tegeta Escrow na wahusika wawajibishwe, kwa kiasi kikubwa suala hilo liliachwa mikononi mwa wanasiasa.
Katika hili, ninaweza kumlaumu Mwalimu Nyerere kidogo. Pengine kwa vile tulikuwa tukihangaika kujenga Taifa lenye kujali usawa wa binadamu, na hivyo kuleta umuhimu wa wateule wachache wa kusimamia mambo, zama hizo zilikuwa za viongozi kama miungu-watu.
Mfumo wa siasa enzi hizo uliwapa madaraka wateule wachache ambao kila walichosema kilikuwa sahihi hata kama si sahihi, na ukaribu wao na watawaliwa ulikuwa mdogo mno.
Miongoni mwa madhara ya mfumo huo ndio hii hali tuliyonayo sasa ambapo wananchi wamekuwa wategemezi wa kupindukia kwa taasisi kama serikali au vyama vya siasa, na watu, hususan, wanasiasa.
Sasa angalau katika zama hizo za Mwalimu, kwa kiasi kikubwa sote tulikuwa na maslahi yanayolingana, yaani ujenzi wa Taifa kwa faida ya wote. Hivi sasa tuna wahuni wengi tu waliojiingiza kwenye siasa kwa maslahi yao binafsi. Na kama nilivyotanabahisha awali, maslahi ya chama yamekuwa kama kitu cha kuficha tu maslahi binafsi.
Ni muhimu kutambua udhaifu wa taasisi zetu na wanasiasa wetu. Lakini hata taasisi hizo zingekuwa timilifu na wanasiasa wetu kuwa imara, ukweli unabaki kuwa wao ni sehemu ya tabaka tawala, na kwa kiasi kikubwa wanatetea maslahi ya tabaka hilo, ilhali wananchi wengi wapo tabaka la chini.
Na kwa vile hatuna tabaka la kati la kueleweka, utegemezi kwa vyama vya siasa/ serikali au wanasiasa utaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi.
Wakati jana Tanganyika yetu imetimiza miaka 53, hivi kuna anayeweza angalau kubashiri hali itakuwaje miaka 20 kutoka sasa?
Kwa kasi hii ya mafisadi kushindana kuifilisi nchi, Tanganyika ya mwaka 2050, kwa mfano, itakuwa na tembo hata mmoja? Je, madini tuliyonayo ambayo yanawanufaisha zaidi wawekezaji na watawala wetu yatadumu kwa muda gani? Na hata hayo mafuta na gesi ambayo tunanyimwa haki ya kuona mikataba yake, yatakuwa neema au laana  kwetu?
Hadi wakati ninaandika makala hii, maazimio ya Bunge kuhusu skandali ya Tegeta Escrow hayajajibiwa. Ukimya wa Rais Jakaya Kikwete unaanza kuwafanya baadhi ya wananchi kuhisi kuwa tumeliwa.
Wananchi wanaishia kuonyesha masikitiko tu pasipo dalili ya kushinikiza wapatiwe haki yao kwa njia za amani.
Tumeona nguvu ya umma inavyoweza kuzaa matunda. Watanzania walihamasishana hadi msanii Diamond akashinda tuzo tatu kwenye Tuzo za Video za Kituo cha Televisheni cha Channel O (CHOAMVA). Tumeshuhudia pia nguvu ya umma ilivyomwezesha mwakilishi wa Tanzania katika Big Brother 2014 kuwa mshindi na kujinyakulia dola za Kimarekani 300,000. Kwanini basi nguvu hiyohiyo isitumike kushinikiza sio tu maazimio ya bunge kuhusu Tegeta Escrow yafanyiwe kazi bali pia kudai mabilioni yetu yaliyoibiwa na kufichwa katika mabenki nchi Uswisi yarejeshwe?
Nihitimishe makala hii kwa kumtakia mwenzangu Tanganyika heri na baraka ya kutimiza miaka 53. Lakini ninaomba pia kutumia fursa hiyo kumkumbusha (kwa maana ya wananchi wenzangu) kuwa tulipotoka kulikuwa na matumaini, tulipo si kuzuri na tuendako hakueleweki.
Ni wajibu wetu kubadili mwelekeo huu. Hili si suala la hiari bali la lazima iwapo twataka kuiona Tanganyika yetu ikiishi maisha marefu ya furaha na amani.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.