30 Apr 2015



“KAKA, kinachotokea hapa kilitarajiwa...na ilikuwa suala la ‘when’ na sio if”, hii ni kauli ya rafiki yangu mmoja Mwafrika Kusini baada ya kumuuliza kuhusu vurugu dhidi ya wahamiaji katika nchi hiyo ambazo zimesababisha vifo, majeruhi, wahamiaji kuhifadhiwa katika kambi kama wakimbizi na wengine kadhaa kuondoka nchini humo.
Ni suala la kusikitisha sana kuona taifa lililoweka historia duniani kwa kukabiliana na makaburu na mfumo wao wa ubaguzi wa rangi (Apartheid) na hatimaye kuushinda, linageuka kuwa taifa hatari dhidi ya wahamiaji kutoka nchi nyingine za Afrika.
Lakini kama alivyotanabaisha rafiki yangu niliyemnukuu hapo mwanzoni, matarajio makubwa waliyokuwa nayo Waafrika weusi nchini Afrika Kusini baada ya kumalizika kwa mfumo wa kibaguzi wa makaburu yameendelea kuwa ndoto tu kwa wengi wao. Uzoefu unaonyesha kuwa katika jamii yoyote ile kwa kadiri inavyokabiliwa na matarajio makubwa ambayo ni magumu kufikiwa, moja ya waathirika wa hali hiyo ni wahamiaji.
Pengine mfano mzuri ni huku nchi za Magharibi ambapo baada ya kuyumba kwa uchumi wa dunia, hali ya maisha imekuwa ngumu, na kauli za upinzani dhidi ya wahamiaji- kutoka kwa wanasiasa na hata raia wa kawaida- zimesambaa.
Kwa hapa Uingereza ambapo tunatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu Mei 7, mwaka huu, moja ya mada kubwa kwa wanasiasa imekuwa suala la uhamiaji. Wanasiasa wanalazimika aidha kukabiliana na wanasiasa wenzao wanaolaumu kuwa wahamiaji wanachangia hali mbaya ya uchumi au kuonekana wanajali vilio vya wananchi wenye malalamiko ya aina hiyo.
Ni kwa sababu hiyo, chama cha kibaguzi cha UKIP kinachoongozwa na Nigel Farage kimetokea kujipatia umaarufu mkubwa hasa kwa vile kinabainisha waziwazi ‘chuki’ yake dhidi ya wahamiaji. Huko Ufaransa, chama cha kibaguzi cha National Front nacho kimekuwa maarufu kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya wahamiaji. Hali ipo hivyo pia nchini Italia na Udachi, huku Ujerumani ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wahamiaji. Kimsingi, katika nchi nyingi za Magharibi, kuyumba kwa uchumi wa dunia kumeambatana na kuimarika kwa vyama vya mrengo mkali wa kulia (far right) ambavyo kimsingi ni vya kibaguzi na vinapinga vikali wahamiaji. Vile vile, sauti za wananchi wa kawaida kuzitaka serikali zao kudhibiti ujio wa wahamiaji zimekuwa zikiimarika na kuongezeka.
Tukirejea kinachojiri Afrika Kusini, ni rahisi kuwashutumu wenzetu hao kwa vitendo vya ubaguzi dhidi ya wahamiaji hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya waathirika wa vurugu dhidi ya wahamiaji ni raia wa nchi zilizoisaidia Afrika Kusini kwa kiwango kikubwa katika mapambano dhidi ya mfumo wa kibaguzi wa Makaburu. Ni rahisi pia kuwalaumu kwa sababu hata kama ingekuwa kweli kuwa wahamiaji wanasababisha ukosefu wa ajira kwa ‘wazawa’ bado haikubaliki kuwafanyia vurugu, kuwajeruhi na hata kuwauwa. Hilo halikubaliki hata chembe.
Hata hivyo, busara kidogo tu zapaswa kutukumbusha kuwa ni vigumu ‘kuingiza akili’ kichwani mwa mtu mwenye njaa (masikini). Tumbo lina tabia moja: mara nyingi, linapohitaji chakula halina subira, au busara. Linachohitaji ni chakula tu, na mara nyingi halijali chakula hicho kinapatikana kwa njia zinazokubalika au la. Ushuhuda wa hili ni katika msimu wa uchaguzi huko nyumbani ambapo mara kadhaa tunashuhudia watu wazima na akili zao wakifungiwa sehemu au kusafirishwa kama magunia kutoka sehemu moja au nyingine ili ‘kulinda kura za mgombea’ kama si kumhakikishia ushindi. Wanaodhalilishwa hawafanyi hivyo kwa mahaba ya kisiasa bali njaa zao.
Mie ni miongoni mwa waumini wa kanuni isiyo rasmi kuhusu uhusiano kati ya umasikini na fursa za uongozi wa kisiasa. Kwamba, watawala hawafanyi bidii kukabiliana vya kutosha na umasikini kwa sababu umasikini unawapa fursa ya kuwahadaa wapiga kura na hatimaye kuwanunua kwa urahisi. Umasikini wa wapigakura ni mtaji mzuri kwa wanasiasa wenye fedha za kununua kura.
Ni vigumu kumkumbusha mpiga kura kuwa ‘ah huyu mbunge alitoa ahadi kadhaa katika uchaguzi uliopita lakini wala hatujamsikia akisema lolote huko bungeni. Hatujawahi japo kuona picha zake akiwa bungeni,’ pale mwanasiasa husika ana rundo la fedha za kutuliza njaa za wapigakura.
Doti za khanga, pishi za mchele, kilo za sukari na ‘takrima’ kama hizo humlainisha mpigakura mwenye njaa asahau kabisa kuhusu miaka mitano ijayo ya utapeli wa kisiasa kama ilivyotokea miaka mitano iliyopita. Njaa yahitaji mlo, hayo madhara yatajulikana mbele ya safari. “Kwani akiwa mbunge tena nitakufa?” Wanajipa moyo wapigakura wenye njaa wanaosubiri kwa hamu ‘fadhila’ za mgombea.
Kwa Afrika Kusini, sababu kubwa ya chuki dhidi ya wahamiaji ni matatizo mbalimbali yanayowakabili Weusi nchini humo ambayo yanakinzana na matarajio makubwa waliyonayo kutoka kwa utawala wa ‘Waafrika wenzao’ baada ya ‘kuwapora madaraka’ makaburu.
Lakini kibaya zaidi, ni mchanyato wa umasikini, ukosefu wa elimu na ‘dozi’ ya uchochezi. Moja ya vichocheo vya vurugu dhidi ya wahamiaji nchini humo ni kauli iliyotolewa na Chifu wa Wazulu, Goodwill Zwelithini, dhidi ya kufurika kwa wahamiaji nchini humo. Kana kwamba hiyo haitoshi, mtoto wa Rais Jacob Zuma, Edward, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wahamiaji wafukuzwe nchini humo akidai wanachangia uhalifu na hali ngumu ya uchumi. Kadhalika, wanasiasa kadhaa Weusi pia wamekuwa wakitoa kauli za kuchochea chuki dhidi ya wahamiaji.

Chambuzi mbalimbali zilizofanyika kabla na baada ya vurugu hizo dhidi ya wahamiaji zimeonyesha kuwa sio tu idadi ya wahamiaji ni ndogo mno kuathiri uchumi wa Afrika Kusini bali pia kinachofanya soko la ajira nchini humo kuvutia na kuvuta wafanyakazi kutoka nchi nyingine ni ukweli kuwa ‘ni rahisi kwa mzawa kuishi bila kazi kwa vile anapatiwa msaada na serikali’ ilhali kwa mhamiaji ni lazima afanye kazi au biashara ili aweze kumudu gharama za maisha.
Lakini pia, huko nyuma, Rais Jacob Zuma aliwahi kunukuliwa akiwalaumu Waafrika Kusini weusi kwa ‘uvivu,’ kutegemea serikali iwapatie kila kitu badala ya kujishughulisha wenyewe. Sasa kwa vile takribani katika kila nchi inayomudu kuwasaidia raia wake wasio na kazi, msaada wa serikali huwa ni wa kujikimu tu, haishangazi kuona ‘wazawa’ wakiwachukia wahamiaji wanaojituma kwa biashara na ajira na kujipatia kipato cha zaidi ya kujikimu tu
Kwa mtazamo mpana, na hili ni funzo kwa nchi nyingine za Afrika ikiwa pamoja na Tanzania yetu, ni ukweli kwamba umasikini ni bomu linalosubiri muda wa kulipuka. Kwa nchi yetu, hali si nzuri. Sio tu kwamba umasikini unazidi kushamiri na kuongezeka, vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watawala wetu vinakuwa kama ‘kuchoma kisu kwenye jeraha bichi.’ Haiingii akilini kwa mlalahoi ambaye hana uhakika wa mlo ujao kusikia viongozi fulani wamekwapua mabilioni ya shilingi huko Benki Kuu.
Na wakati faraja ya masikini inaweza kupatikana katika neno la Mungu, mtu fukara anaposikia habari kuwa Askofu wake kuzawadiwa mamilioni ya ufisadi, anaweza kushawishika kutumia vibaya msemo wa ‘mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe,’ hasa ikizingatiwa kuwa nguvu anazotumia shambani zinaishia kunenepesha kitambi cha viongozi wa vyama vya ushirika na kuongeza idadi ya ‘nyumba ndogo’ zao. Kwanini asishawishike kuzitumia nguvu hizo kwenye uhalifu?
Tofauti na Afrika Kusini ambapo ‘adui’ anaonekana mhamiaji ‘anayepora ajira za wazawa,’ adui wa fukara wa Tanzania ni Mtanzania mwenzie anayetumia madaraka yake kufanya ufisadi, na hivyo kuongeza ufukara kwa mlalahoi huyo.
Tunaweza kujidanganya kuwa ‘Tanzania ni kisiwa cha amani’ lakini tusisahau kuwa ‘mwenye njaa hana amani.’ Amani yetu ni ya kufikirika zaidi kuliko uhalisia. Amani si ukosefu wa mapigano tu bali pia kuridhika nafsini, tumbo lililoshiba, mfuko wenye hela ya matumizi, jitihada za kujipatia kipato halali zinapozaa matokeo tarajiwa. Kimsingi, ukosefu wa amani usioambatana na vurugu ni kichocheo kikubwa cha vurugu zinazopelekea kuvunja amani waziwazi. Na hicho ndicho kinachojiri nchini Afrika Kusini. Sio sahihi lakini nenda kamwambie mwenye njaa kuhusu ‘wewe kuwa na njaa ilhali mie ninakula hadi kusaza ni kitu sahihi’ kama atakuelewa. Wanasema ‘njaa haina akili,’ na mwenye njaa yupo tayari kwa lolote ili kutuliza njaa yake.
Nimalizie makala hii kwa kutoa rai kwa wanasiasa wetu, hasa wakati huu tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, kuweka kipaumbele katika kupambana na umasikini sambamba na kukabiliana na ufisadi ambao kwa kiasi kikubwa unachangia mno kushamiri na kukua kwa umasikini.
TUZIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.