29 Apr 2015

Inasikitisha, inaumiza, inashangaza, na inaacha maswali mengi kuliko majibu kila tunaposikia “ajali yauwa...ajali yajeruhi...” Ndio, matukio ya ajali huko nyumbani yamekuwa kama jambo la kawaida kutokana na mfululizo wake, lakini hali ilivyo sasa ni ya kutisha.
Huko nyuma niliandika takriban makala mbili kuhusu suala hili la ajali, sio tu kwa vile tukio lolote linalopelekea kupotea kwa uhai wa wenzetu linaumiza nafsi bali pia kutokana na ukweli kwamba kwa hapa Uingereza ajali ndogo tu ni tukio linalokamata hisia za takriban nchi nzima, kinyume na ilivyozoeleka huko nyumbani.

Wakati ajali zinaendelea kuteketeza maisha ya Watanzania wenzetu, angalau kwa mara ya kwanza Taifa linaonekana kuguswa, na tayari zimeanza harakati za uhamasishaji dhidi ya ajali katika mitandao mbalimbali ya kijamii. Hata hivyo, ukweli mchungu unabaki kuwa ajali bado zinaonekana kama matukio ya kawaida tu.
Sijui lini taifa limeonyesha kuguswa na vifo vilivyotokana na ajali kiasi cha angalau bendera kupepea nusu mlingoti. Sijui sababu ni kwamba ajali zimezoeleka mno, au kwa vile ‘ajali haina kinga,’ au kwa sababu wahanga wengi wa ajali za barabarani ni ‘watu wa kawaida.’
Kabla sijaanza kuandika makala hii nilisoma habari kuhusu vurugu zilizotokea huko Korea ya Kusini katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu itokee ajali mbaya ya feri iliyosababisha vifo takriban 300. Hakuna anayefahamu kinachojiri baada ya kifo, lakini yayumkinika kuamini kuwa marehemu wasingependa kukumbukwa kwa vurugu. Lakini vurugu zilizotokea huko Korea ya Kusini ni ishara ya wananchi kukerwa na jinsi serikali yao ilivyoshughulikia janga hilo, hata kama haikuisababisha.
Hapa simaanishi kwamba Watanzania nao waingie mtaani na kufanya vurugu kuisukuma serikali ichukue hatua stahili dhidi ya ajali. Hata hivyo, ni muhimu angalau kuiamsha serikali kwa kuifahamisha kuwa hatuwezi kuangalia tu maisha ya Watanzania yakiteketea kama hayana thamani kutokana na mfululizo wa ajali. Busara kwamba ‘ajali haina kinga’ hai-apply katika nyingi ya ajali zinazotokea huko nyumbani.
Kwa mtizamo wangu, chanzo kikubwa cha ajali ni rushwa. Rushwa inayowezesha madereva wasio na sifa kuwa barabarani huku wakihatarisha uhai wa abiria wao. Rushwa inayoruhusu magari mabovu yabebe abiria na kuweka rehani uhai wa abiria. Rushwa inayofumbia macho makosa ya madereva barabarani na hivyo kuwapa imani kuwa hakuna kitu kiitwacho ‘kosa kinyume cha sheria za usalama barabarani’ alimradi dereva ana uwezo wa ‘kumpoza’ askari wa usalama barabarani.
Wanasema ‘rushwa huuwa.’ Na katika janga hili la mfululizo wa ajali, rushwa inauwa kweli kweli, na inaendelea kugharimu maisha ya Watanzania wenzetu kila kukicha.
Rushwa imekuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya Mtanzania, na sintoshangaa iwapo baadhi ya wasomaji ‘wataniona mtu wa ajabu’ kwa kuhitimisha kuwa rushwa ni chanzo kikuu cha ajali huko nyumbani. Kwa wengi, rushwa ni tukio la muda mfupi tu linalorahisisha au kuwezesha upatikanaji wa huduma au bidhaa. Hata hivyo, ukweli mchungu ni kwamba rushwa ni kama kansa, inaitafuna jamii taratibu, na siku ya siku, madhara yake makubwa hujitokeza hadharani.
Mfano mmoja kuhusu athari za rushwa ni suala la ugaidi nchini Kenya. Wachambuzi wa masuala ya usalama wanahitimisha kuwa kwa kiasi kikubwa tu, rushwa katika vyombo vya dola nchini Kenya imewarahisishia magaidi wa Al-Shabaab kutimiza malengo yao kuishambulia nchi hiyo.
Kwa huko nyumbani tumeshuhudia matatizo mengine ya kijamii yanavyorutubishwa na rushwa. Mfano rahisi ni kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya. Tanzania yetu sasa ni miongoni mwa vituo vikuu vya biashara hiyo duniani, na kilichotufikisha katika nafasi hiyo isiyopendeza hata kidogo ni urahisi wa kuingiza na kutoa madawa ya kulevya nchini mwetu. Niwe mkweli, kila ninaposikia polisi wamekamata kiasi fulani cha madawa ya kulevya, hisia yangu ya kwanza ni madawa hayo yaliyokamatwa yataishia kumnufaisha mtendaji fulani wa taasisi zenye wajibu wa kuyadhibiti.
Takriban kila dereva na abiria anafahamu jinsi askari wa usalama barabarani walivyogeuza rushwa kuwa haki yao. Kibaya zaidi, madereva wengi nao wamejenga fikra kuwa kutoa rushwa kwa askari wa usalama barabarani ni wajibu wao. Hili ni janga: rushwa kama haki wa wapokeaji na wajibu kwa watoaji.
Wakati mmoja nikiwa safarini huko nyumbani, basi nililopanda lilisimamishwa na askari wa usalama barabarani, na baada ya dakika kadhaa, baadhi ya abiria walisikika wakimhasisha dereva ‘amalizane na trafiki’ (ampe rushwa) ili safari iendelee. Hivi ndivyo rushwa ilivyoota mizizi katika Tanzania yetu.
Kwa upande mwingine, janga la ajali kuonekana kama jambo la kawaida tu ni mwendelezo wa kasumba inayolikwamisha mno taifa letu: kuzowea matatizo. Angalia tatizo la mgao wa umeme lilivyodumu miaka nenda miaka rudi pasipo Watanzania kutumia nguvu ya umma kuilazimisha serikali na Tanesco yake imalize tatizo hilo. Mgao wa umeme umekuwa stahili ya Watanzania, na kikubwa wanachoweza kufanya ni kuitukana Tanesco matusi yasiyoandikika hapa, kana kwamba matusi hayo yatamaliza tatizo hilo la miaka nenda miaka rudi.
Kwenye sekta ya huduma, hali ni hivyohivyo. Ukifuatilia kwenye mitandao ya jamii, idadi ya matusi yanayoelekezwa kwa makampuni ya huduma mbalimbali, kwa mfano makampuni ya simu, ni kubwa na inakua kila siku, lakini ‘mashujaa hao wa matusi’ hawataki kabisa kujifunza kuwa matusi yao hayabadili chochote, na ndio maana kila kukicha inawalazimu waje na matusi mapya kama si kuyarudia yale ya zamani.
Lakini kwa hali ilivyo sasa kuhusu janga la ajali, ‘usugu’ huo wa kuyazowea matatizo inabidi ifikie kikomo. Taifa lolote linalojali mustakabali wake lazima liamke inapofikia hatua ya watu 969 kupoteza maisha kutokana na ajali katika kipindi cha takriban miezi mitatu tu. Naam, tangu mwaka huu uanze, tumepoteza wenzetu takriban 300 kila mwezi kutokana na ajali, kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana wiki iliyopita.
Katika sehemu kubwa ya makala hii nimezungumzia rushwa kama chanzo kikuu cha janga la ajali. Hata hivyo, kwa mtizamo wangu, kingine kinachochangia baadhi ya ajali ni ‘uzembe’ wa wengi wa abiria: kukaa kimya pale madereva wanapohatarisha maisha ya abiria kwa uendeshaji usiozingatia sheria za usalama barabarani. Na pengine cha kukera zaidi ni tabia iliyojengeka miongoni mwa abiria wengi kuwasifia madereva wanaodhani ni kosa la jinai kuendesha motokaa taratibu hata kwenye eneo hatari.
Inasikitisha na kuchukiza kusikia abiria wakimshangilia dereva anayeendesha basi kwa kasi au ku-overtake gari jingine pasi kuona kama kuna gari jingine linakuja kwa mbele au la. Dereva anayeshangiliwa kwa uendeshaji gari wa hatari anajenga imani kwamba huo ndio udereva stahili, vinginevyo abiria wangemkemea.
Ifike mahali Watanzania tuache kukubali kilicho pungufu (not settling for less). Ukinunua tiketi kwa ajili ya safari umenunua pia haki na stahili zako ambazo kamwe hupaswi kumruhusu dereva azichezee. Ni wazi kuwa umoja na mshikamano wa abiria kukemea madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani unaweza kusaidia kupunguza baadhi ya ajali zinazoepukika.
Nimalizie makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali mfululizo.
Pia ninaomba kufikisha ujumbe huu kwa askari wa usalama barabarani: kila shilingi mnayodai kama rushwa ili kufumbia macho ukiukwaji wa sheria za barabarani inachangia ajali na vifo vya Watanzania wenzetu. Mikono ya kila askari aliyepokea rushwa na kisha gari husika likapata ajali ina damu ya waliokufa katika ajali husika.
Kadhalika, ninatoa wito kwa madereva, hususan wa magari ya abiria, kuthamini uhai wa abiria wao, kwa kuepusha ushindani hatari barabarani, mwendo kasi na kuheshimu sheria za usalama barabarani.
Lakini kubwa zaidi kwa Watanzania wote ni kupambana na kansa hii ya rushwa ambayo sasa inalitafuna taifa kwa kuchangia ajali hizi mfululizo, kama inavyosababisha madhara mengine makubwa katika nyanja mbalimbali za maisha.

ANGALIZO: Makala hii ilichapishwa katika toleo la tarehe 22.04.15 lakini iliwekwa mtandaoni juzi. Samahani kwa kuchelewesha kui-post.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube