29 Jan 2016

KATIKA tasnia ya ushushushu kuna kitu kinachoitwa Moscow Rules (yaani Kanuni za Moscow). Hizi ni kanuni za zama za Vita Baridi ambazo majasusi waliopangiwa kazi nchini Urusi walipaswa kuzizingatia, kwa sababu nchi hiyo ilikuwa nguli wa kukabiliana na majasusi. Moja ya kanuni hizo inasema; “Once is an accident. Twice is a coincidence. Three times is an enemy action.” Kwa tafsiri isiyo rasmi; kitu kinachojiri mara moja ni ajali; kikijiri mara ya pili ulinganifu wa bahati mbaya, sio makusudi; kikijiri mara ya tatu ni kitendo cha adui.”

Nimeanza makala hii na angalizo hilo kwani ndio wazo lililoniingia kichwani mara baada ya kusoma kauli za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe.

Wiki iliyopita, Membe alinukuliwa na vyombo vya habari akimkosoa Rais Dk. John Magufuli, angalau katika maeneo matatu. Kwanza, Membe alidai kuwa kiuhalisi, Dk. Magufuli hajapunguza idadi ya wizara kama alivyoahidi bali amepunguza idadi ya mifuko, na kutanabaisha kuwa Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na sio wizara.

Alichofanya ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema waziri huyo wa zamani ambaye pia alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliowania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.

Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa utakuwa hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai,”aliongeza Membe.

Membe alidai kwamba Magufuli ameendeleza wizara zile zile lakini kaamua kuzikusanya pamoja, na kuona kuwa mfumo huo mpya wa wizara unaweza kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa vile mawaziri sasa watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Hilo tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Tuone kama bajeti itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki vile vile maana yake hakuna kilichofanyika,”alitahadharisha.

Eneo la pili ambalo Membe alimkosoa Magufuli ni udhibiti wa safari za nje, akidai kuwa Tanzania si kisiwa. Membe, aliyekuwa mtetezi mkuu wa safari mfululizo za Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete nje ya nchi, alisema kuwa safari za nje zina manufaa kwa taifa, na kusisitiza kuwa lazima Rais Magufuli asafiri kwenda nje ya nchi.

Tanzania si kisiwa, hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako,” alisema Membe, na kutahadharisha kuwa nchi yetu inaweza kuwa kama Zimbabwe kwani ukijitenga, utatengwa.
Alisema nchi ina mabalozi 36 tu duniani kote kati ya nchi 194 zinazohitaji uwakilishi huo na kibaya zaidi, mabalozi hawaruhusiwi kuingia kwenye baadhi ya vikao, na hata wakiingia wakifika kwenye hatua ya uamuzi watazuiwa kushiriki.

Eneo la tatu ambalo japo hakumtaja Magufuli wala kukosoa moja kwa moja lakini linaloweza kutafsiriwa kama kuikosoa serikali kuhusu wafanyabiashara, ambapo alitahadharisha serikali kutowachezea.

Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Mtama (CCM) alipongeza kasi ya Magufuli katika vita dhidi ya ufisadi na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi lakini akatahadharisha kuhusu haja ya kuwa mwangalifu katika kuwashughulikia wafanyabiashara. Alidai kuwa wafanyabiashara wana masikitiko makubwa dhidi ya serikali, na anaona suala hilo litaibuka kwa kishindo bungeni.

Licha ya maeneo hayo matatu, Membe alizungumzia kauli ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, aliyedai wafanyabiashara waliomuunga mkono wananyanyaswa. Alieleza kuwa si dhambi kwa wafanyabiashara kufadhili vyama vya siasa wakati wa uchaguzi, na kwamba serikali ya chama kilichoshinda uchaguzi inapaswa kuwakusanya wafanyabiashara wote na kufanya nao kazi na sio kuwaburuza.

Kadhalika, mwanasiasa huyo alizungumzia kuhusu “timua timua” ya watumishi wa umma wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi.

Ni rahisi kumshughulikia mtu usiyemfahamu lakini siyo rahisi kumshughulikia mtu unayemfahamu,” alidai Membe, na kuongeza kuwa haitokuwa shida kwa Magufuli kuwashughulikia watendaji aliowakuta serikalini ambao kimsingi hakuwateua, na hawafahamu. Alihoji iwapo Rais ataweza kuwatimua aliowateua mwenyewe.

Kauli hizo za Membe zimezua mjadala mkubwa, hususan kwenye mitandao ya kijamii. Japo kabla yake, aliyekuwa Naibu wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga, alimkosoa Magufuli kuhusu ukubwa wa kabineti yake, ukweli kwamba Membe bado ni kiongozi wa juu wa CCM ilhali Mahanga alihamia upinzani, unaashiria mengi.

Lakini binafsi sikushangazwa na kauli hizo za Membe, hasa kwa vile awali, katika kitabu nilichokichapisha hivi karibuni kuhusu safari ya urais wa Magufuli, mafanikio na changamoto katika urais wake, nilibainisha kuwa moja ya changamoto zinazoweza kumkabili Rais huyo wa Awamu ya Tano ni maadui wa ndani ya chama chake.

Kimsingi, hoja zote za Membe hazina mashiko. Kuhusu anachoita ukubwa wa baraza la mawaziri, la muhimu kwa Watanzania si ukubwa au udogo bali uchapakazi. Ni bora kuwa na mawaziri, manaibu na makatibu wakuu hata 1,000 wachapakazi, kuliko kuwa na serikali ndogo inayokumbatia mafisadi.
Pia Membe alipaswa kufahamu kuwa utendaji kazi wa viongozi wa serikali unategemea sana utendaji kazi na msimamo wa bosi wao, yaani Rais aliyewateua. Ni dhahiri kuwa Membe anatambua kuwa Magufuli si mtu wa porojo, mtoa ahadi anazoshindwa kuzitekeleza mwenyewe (rejea kauli ya “ninawajua wala rushwa kwa majina” ya Kikwete), na kimsingi Watanzania na dunia nzima wanafahamu kuwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ya Magufuli ni tofauti na zama za nchi kujiendesha yenyewe (on autopilot).

Kuhusu safari za nje, Membe amepotoka mno, pengine kwa sababu kwa wadhifa wake wakati huo, alikuwa mmoja wa wasafiri nje ya nchi mara kwa mara. Kwanza, Rais Magufuli hajawahi kutamka kuwa hatosafiri. Kwa hiyo, kauli ya Membe kuwa lazima atasafiri ni fyongo.

Pili, zuio la safari za nje sio ‘blanket ban’ bali ni kwa safari zisizo na tija. Lakini kwa nini tushangazwe na kauli hiyo ya Membe ilhali tunafahamu misafara ya serikali iliyopita ilivyosheheni wajumbe kwa kutumia fedha za umma? Ni mtu mwenye matatizo tu anayeweza kutetea safari zenye manufaa zinazoligharimu taifa matrilioni ya shilingi huku faida tarajiwa zikiwa pungufu ya gharama husika.

Mwanadiplomasia msomi kama Membe alipaswa kuangalia hapo jirani tu kwa Rais Paul Kagame, kulinganisha idadi ya safari zake nje na zile za Kikwete kisha kuangalia hali ya uchumi kati ya nchi hizo mbili.

Vilevile ni rahisi kwa Membe kuzungumzia mafanikio ya safari hizo kwa vile ni Watanzania wachache wanaofahamu vituko vilivyoambatana na safari hizo. Ni mara ngapi safari hizo za ‘manufaa’ zilijumuisha shopping, kuhudhuria birthday parties, na matukio mengine yasiyo na tija kwa serikali?

Kuhusu wafanyabiashara, ni upuuzi wa hali ya juu kuhisi tu kuwa kuna uonevu dhidi ya mfanyabiashara yeyote. Kama kuwabana wafanyabiashara wakwepa kodi ni uonevu basi Magufuli aongeze dozi, maana hizi sio zama za Tanzania kuwa shamba la bibi.

Membe anadai wafanyabiashara wana masikitiko na suala hilo linaweza kuibuka bungeni. Anamaanisha Bunge limejaa wafanyabiashara au? Na kama masikitiko yao ni kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuwabana ili wasikwepe kodi na kwamba masikitiko hayo yanaweza kusababisha kupoteza wawekezaji, basi na waondoke hata kesho. Hatuhitaji wakwepa kodi nchini. Kimsingi, wanaolalamika wala hawastahili kuitwa wafanyabiashara bali wahujumu wa uchumi wetu.

Na hoja yake kuhusu ‘timua timua’ haishangazi kwani moja ya udhaifu wa serikali ambayo Membe alikuwa waziri ilikuwa ni kuwaonea aibu wanaoboronga, na matokeo yake hali hiyo ilivutia waborongaji wapya kwani walishabaini kuwa hakuna wa kuwachukulia hatua. Hivi Membe anaweza kutuambia lolote kuhusu ahadi ya Riais Kikwete aliyoitoa Februari 2006 kwamba anawafahamu wala rushwa kwa majina na anawapa muda wajirekebishe? Sawa, Magufuli alipoingia Ikulu alikuta orodha hiyo ya wala rushwa aliowajua Kikwete na kuamua kuifanyia kazi?

Nimeeleza awali kuwa nimelizungumzia suala hilo kwa kirefu kitabuni. Sitaki kabisa kuamini kuwa kauli za Membe ni zake peke yake. Hisia zinanituma kuamini kuwa huu ni moshi tu unaoashiria moto unaowaka ndani kwa ndani ya CCM kati ya makundi makuu mawili: la Hapa Kazi Tu la Magufuli linalotaka kuiondoa Tanzania katika lindi la ufisadi unaoifanya nchi yetu kuzidi kuwa masikini, na kundi la wanufaika wa ufisadi linalomwona Magufuli kama mtu anayewaziba pumzi. Naam, ufisadi ni ‘lifeline’ ya watu walioigeuza nchi yetu Shamba la Bibi, wakivuna wasichopanda.

Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa makada wa CCM, ambao wengi wao wanaimba Hapa Kazi Tu, lakini wakisikia madhambi yaliyofanywa na mwana-CCM fulani wanakimbilia kuwanyooshea vidole wapinzani. Wapinzani wakuu wa Magufuli hawapo Chadema au nje ya nchi bali wapo ndani ya chama hicho tawala. Na njia pekee ya kupambana nao ni kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kutanguliza umoja na mshikamano wa chama. Kuna usemi mchawi akimaliza kuroga mtaa hugeukia familia yake. Majipu yaliyomo ndani ya CCM yasipotumbuliwa mapema yatamkwaza Magufuli na nchi yetu kwa ujumla.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.