13 Jan 2016


WIKI iliyopita, watumiaji kadhaa wa mtandao wa kijamii wa Twitter nchini Kenya waliishambulia vikali Serikali ya Tanzania, na Rais Dk. John Magufuli, kutokana na kuanza kwa operesheni ya kudhibiti wahamiaji haramu inayoendelea huko nyumbani (Tanzania).
Aliyeanzisha chokochoko hiyo ni bloga mmoja maarufu nchini humo ambaye awali alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatua dhidi ya alichokiita ubaguzi dhidi ya raia wa Kenya wanaoishi nchini Tanzania.’

Bloga huyo si mgeni kwa uchochezi. Ninaita uchochezi kwa sababu madai hayo ya ubaguzi hayakuwa na ukweli wowote. Lakini kwa tunaomfahamu, hatukushangazwa sana na madai hayo, kwa sababu hata huko nchini Kenya, bloga huyo ameshakumbana na misukosuko kadhaa kutokana na kauli zake tata.

Tweets zake kuhusu suala hilo zilisababisha Wakenya kadhaa mtandaoni kuzungumzia uonevu huo huku wakitumia hashtag #OperesheniTimua. Sina hakika kama hilo ndilo jina halisi la operesheni hiyo.

Binafsi niliona shutuma hizo dhidi ya Serikali ya Magufuli kama kichekesho fulani, hasa ikizingatiwa kuwa ni hivi majuzi tu, Wakenya lukuki walikuwa wakimsifu Rais wetu huyo kwa hatua zake mbalimbali za kudhibiti mapato na matumizi, sambamba na kupambana na rushwa, huku wakiilaumu Serikali ya Rais Uhuru.

Majirani zetu hao walikuwa mstari wa mbele katika kuipaisha ‘hashtag’ #WhatWouldMagufuliDo ambayo kimsingi ilikuwa ikionyesha jinsi watu mbalimbali duniani walivyoridhishwa na hatua hizo za Magufuli.

Sasa, tukiafikiana tu kuwa Magufuli amedhamiria kwa dhati kupambana na kila uozo uliopo, basi ni wazi kuwa ilikuwa suala la muda tu kabla serikali yake haijaanza kuvalia njuga suala la uhamiaji haramu. Na ninaamini kuwa majirani zetu wa Kenya hawakutarajia serikali yetu kuwafumbia macho wahamiaji haramu kutoka nchi yoyote ile hata kama ni jirani yetu Kilichonikera zaidi ni kuona tweet ya Naibu Rais wa Kenya William Rutto akifuata mkumbo wa kukemea #OperesheniTimua pasi kujiridhisha vya kutosha kuhusu tuhuma zilizotolewa na bloga husika.
Nilipotafakari kwa undani kuhusu suala hilo nikapatwa na hisia kuwa Tanzania legelege yenye sheria zisizofanya kazi ilikuwa ni habari njema kwa wasioitakia mema nchi yetu. Sio siri kwamba, uzembe mkubwa katika Idara ya Uhamiaji umechangia sana kushamiri kwa tatizo la wahamiaji haramu. Na sio siri pia kuwa majirani zetu, ikiwa ni pamoja na Kenya, walinufaika sana kutokana na uzembe huo.

Lakini zama hizo za raia wa kigeni kununua haki ya makazi nchini mwetu zaelekea kufikia ukingoni, na hiyo si habari njema kwa wanufaika. Lakini hata kama hatua hiyo inawakera basi angalau wangekuwa na ustaarabu katika kulizungumzia suala hilo kuliko kuzusha tuhuma za uongo. Japo ni kweli kwamba kuna raia wengi wa Kenya nchini Tanzania, operesheni hiyo ya kupambana na wahamiaji haramu haiwalengi raia wa kigeni – iwe ni kutoka Kenya au kwingineko – ambao wapo nchini Tanzania kihalali. Iwapo waathirika wengi wa operesheni hiyo ni Wakenya basi labda iwe kutokana na wengi wao kutokuwa nchini mwetu kihalali (nasisitiza labda kwa vile sina takwimu sahihi).

Baadhi ya majirani zetu hao waliochangia mjadala mkali kuhusu mada hiyo walifika mbali na kudai kuwa Tanzania itadhoofika kwa kuwafukuza Wakenya kwa vile inawategemea mno. Binafsi nadhani kauli za aina hii zina madhara zaidi kwa Wakenya wanaoishi kihalali nchini mwetu kuliko madhara kwa serikali na nchi yetu.

Wanaopandikiza chuki hiyo hawapo Tanzania, na endapo kauli zao zitaibua chuki dhidi ya raia wa nchi hiyo, hao wapiga kelele hawatoathirika moja kwa moja bali ndugu zao waliopo nchini mwetu. Lakini si jambo la kushangaza kuona mazuri ya Magufuli yakianza kukera baadhi ya watu. Walishazowea kuiona nchi yetu kama kituko. Na walinufaika na ulegelege uliokuwepo, ikiwa ni pamoja na upungufu katika udhibiti dhidi ya wahamiaji haramu.

Na katika hilo la kukerwa na utendaji unaotia moyo wa Magufuli si majirani zetu hao tu, majuzi nilisikia mahojiano ya kiongozi wa Chadema, Tundu Lissu, akitoa mtizamo wake kuhusu mwenendo wa Magufuli na serikali yake. Lugha yake haikuwa tofauti na inayosikika kwa wengi wa wafuasi wa vyama vya upinzani. Kwao, kufanikiwa kwa Magufuli ni kama kudidimia kwa vyama vyao.

Na hilo sio gumu kulielewa, kwa sababu kwa kiasi kikubwa kushamiri kwa upinzani nchini Tanzania ni matokeo ya udhaifu wa CCM, uliowapa wapinzani nafasi ya kusema chochote, kuliko uimara wa wapinzani binafsi. Kwa maana hiyo, hatua za Magufuli na serikali yake kupambana na mengi yaliyokuwa kero kwa Watanzania kunawanyima wapinzani fursa ya kuongea.

Lawama na shutuma za wapinzani zimevuka mipaka hadi kutugusa baadhi yetu ambao baada ya muda mrefu wa kukosoa mwenendo wa mambo katika nchi yetu, sasa tumepata ahueni kutokana na kazi nzuri ya Magufuli, na tunapata kila sababu ya kupongeza na kuinadi nchi yetu.

Binafsi, nimekuwa miongoni mwa waathirika wa shutuma hizo baada ya kuchapishwa kitabu kinachozungumzia safari ya urais wa Dk. Magufuli, mafanikio na changamoto kwa urais wake. Kuna wanaodai ni mapema mno kuzungumzia mafanikio ya kiongozi huyo, lakini bila kubainisha wakati gani ni mwafaka kuzungumzia mafanikio yake.

Kuna waliokwenda mbali zaidi na kudai kitabu hicho ni jitihada zangu binafsi kutafuta ukuu wa wilaya. Kwa uelewa wangu, shutuma hizo ni matokeo ya hadaa kubwa iliyofanyika kwa wafuasi wengi wa vyama vya upinzani kuwa vyovyote ambavyo ingekuwa, mgombea wao wa kiti cha urais, Edward Lowassa, lazima angeshinda kiti hicho.

Kuishi kinyume cha matarajio hewa si kitu rahisi, na huenda itachukua muda mrefu kwa wapinzani wa Magufuli kubaini kuwa kila zuri analofanya ni kwa maslahi ya Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Tanzania ya neema si tu kwa waliompigia kura Magufuli bali kila Mtanzania, hata aliyemnyima kura.

Wakati tunaweza kuwaelewa majirani zetu wanaokerwa kuona Tanzania imeamka, haingii akilini kuona baadhi ya Watanzania wenzetu wakijifanya vipofu wasioona mabadiliko makubwa na ya kasi yanayoletwa na Magufuli na serikali yake. Walihadaiwa kuhusu mabadiliko, sasa wanaletewa mabadiliko halisi wanaanza kulalamikia.

Katika mahojiano yake niliyoyataja awali, Lissu anamlinganisha Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, lakini si kwa uchapakazi wake na chuki yake kubwa dhidi ya wahujumu uchumi bali kile ambacho mwanasheria huyo anadai ni kutoheshimu sheria.

Pia alimfananisha Magufuli na Naibu Waziri Mkuu wa zamani, na sasa Mwenyekiti wa taifa wa TLP, Agustino Mrema, kuwa ni kiongozi anayefanya kazi ili aandikwe na vyombo vya habari. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Hivi kweli mazuri haya mengi yaliyojiri tangu Magufuli aingie madarakani ni kwa minajili ya kupata vichwa vya habari?

Nimalizie makala hii kwa kukumbusha kuwa kinyume na mabadiliko yaliyoahidiwa na Lowassa ambayo yalitarajiwa kutokea kama miujiza pasipo mipango madhubuti, tunachoshuhudia kwa Magufuli ni mabadiliko ya dhati yaliyobainishwa katika mikutano yake mbalimbali ya kampeni za uchaguzi, na kufafanuliwa kwa kirefu katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge jipya.


 Ushauri wangu kwa Watanzania wenzangu ni kupuuzia wote wanaokerwa na mwenendo wa kutia matumaini wa Magufuli na serikali yake. Wanasema ukirusha jiwe kizani kisha ukasikia kelele, basi ujue limempiga mtu. Hizi kelele, kebehi au shutuma dhidi yake ni matokeo ya jitihada zake za kizalendo za kuathiri waliokuwa wakinufaika na mwenendo fyongo wa nchi yetu katika maeneo mbalimbali. 

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.