
WIKI
iliyopita, watumiaji kadhaa wa mtandao wa kijamii wa Twitter nchini Kenya
waliishambulia vikali Serikali ya Tanzania, na Rais Dk. John Magufuli, kutokana
na kuanza kwa operesheni ya kudhibiti wahamiaji haramu inayoendelea huko
nyumbani (Tanzania).
Aliyeanzisha
chokochoko hiyo ni bloga mmoja maarufu nchini humo ambaye awali alimtaka Rais
Uhuru Kenyatta kuchukua hatua dhidi ya alichokiita ubaguzi dhidi ya raia wa
Kenya wanaoishi nchini Tanzania.’
Bloga huyo si
mgeni kwa uchochezi. Ninaita uchochezi kwa sababu madai hayo ya ubaguzi
hayakuwa na ukweli wowote. Lakini kwa tunaomfahamu, hatukushangazwa sana na
madai hayo, kwa sababu hata huko nchini Kenya, bloga huyo ameshakumbana na
misukosuko kadhaa kutokana na kauli zake tata.
Tweets zake
kuhusu suala hilo zilisababisha Wakenya kadhaa mtandaoni kuzungumzia uonevu huo
huku wakitumia hashtag #OperesheniTimua. Sina hakika kama hilo ndilo jina
halisi la operesheni hiyo.
Binafsi
niliona shutuma hizo dhidi ya Serikali ya Magufuli kama kichekesho fulani, hasa
ikizingatiwa kuwa ni hivi majuzi tu, Wakenya lukuki walikuwa wakimsifu Rais
wetu huyo kwa hatua zake mbalimbali za kudhibiti mapato na matumizi, sambamba
na kupambana na rushwa, huku wakiilaumu Serikali ya Rais Uhuru.
Majirani zetu
hao walikuwa mstari wa mbele katika kuipaisha ‘hashtag’ #WhatWouldMagufuliDo
ambayo kimsingi ilikuwa ikionyesha jinsi watu mbalimbali duniani
walivyoridhishwa na hatua hizo za Magufuli.
Sasa,
tukiafikiana tu kuwa Magufuli amedhamiria kwa dhati kupambana na kila uozo
uliopo, basi ni wazi kuwa ilikuwa suala la muda tu kabla serikali yake
haijaanza kuvalia njuga suala la uhamiaji haramu. Na ninaamini kuwa majirani
zetu wa Kenya hawakutarajia serikali yetu kuwafumbia macho wahamiaji haramu
kutoka nchi yoyote ile hata kama ni jirani yetu Kilichonikera zaidi ni kuona
tweet ya Naibu Rais wa Kenya William Rutto akifuata mkumbo wa kukemea
#OperesheniTimua pasi kujiridhisha vya kutosha kuhusu tuhuma zilizotolewa na
bloga husika.
Nilipotafakari
kwa undani kuhusu suala hilo nikapatwa na hisia kuwa Tanzania legelege yenye
sheria zisizofanya kazi ilikuwa ni habari njema kwa wasioitakia mema nchi yetu.
Sio siri kwamba, uzembe mkubwa katika Idara ya Uhamiaji umechangia sana
kushamiri kwa tatizo la wahamiaji haramu. Na sio siri pia kuwa majirani zetu, ikiwa
ni pamoja na Kenya, walinufaika sana kutokana na uzembe huo.
Lakini zama
hizo za raia wa kigeni kununua haki ya makazi nchini mwetu zaelekea kufikia
ukingoni, na hiyo si habari njema kwa wanufaika. Lakini hata kama hatua hiyo
inawakera basi angalau wangekuwa na ustaarabu katika kulizungumzia suala hilo
kuliko kuzusha tuhuma za uongo. Japo ni kweli kwamba kuna raia wengi wa Kenya
nchini Tanzania, operesheni hiyo ya kupambana na wahamiaji haramu haiwalengi
raia wa kigeni – iwe ni kutoka Kenya au kwingineko – ambao wapo nchini Tanzania
kihalali. Iwapo waathirika wengi wa operesheni hiyo ni Wakenya basi labda iwe
kutokana na wengi wao kutokuwa nchini mwetu kihalali (nasisitiza labda kwa vile
sina takwimu sahihi).
Baadhi ya
majirani zetu hao waliochangia mjadala mkali kuhusu mada hiyo walifika mbali na
kudai kuwa Tanzania itadhoofika kwa kuwafukuza Wakenya kwa vile inawategemea
mno. Binafsi nadhani kauli za aina hii zina madhara zaidi kwa Wakenya wanaoishi
kihalali nchini mwetu kuliko madhara kwa serikali na nchi yetu.
Wanaopandikiza
chuki hiyo hawapo Tanzania, na endapo kauli zao zitaibua chuki dhidi ya raia wa
nchi hiyo, hao wapiga kelele hawatoathirika moja kwa moja bali ndugu zao
waliopo nchini mwetu. Lakini si jambo la kushangaza kuona mazuri ya Magufuli yakianza
kukera baadhi ya watu. Walishazowea kuiona nchi yetu kama kituko. Na
walinufaika na ulegelege uliokuwepo, ikiwa ni pamoja na upungufu katika
udhibiti dhidi ya wahamiaji haramu.
Na katika hilo
la kukerwa na utendaji unaotia moyo wa Magufuli si majirani zetu hao tu, majuzi
nilisikia mahojiano ya kiongozi wa Chadema, Tundu Lissu, akitoa mtizamo wake
kuhusu mwenendo wa Magufuli na serikali yake. Lugha yake haikuwa tofauti na
inayosikika kwa wengi wa wafuasi wa vyama vya upinzani. Kwao, kufanikiwa kwa Magufuli
ni kama kudidimia kwa vyama vyao.
Na hilo sio
gumu kulielewa, kwa sababu kwa kiasi kikubwa kushamiri kwa upinzani nchini
Tanzania ni matokeo ya udhaifu wa CCM, uliowapa wapinzani nafasi ya kusema
chochote, kuliko uimara wa wapinzani binafsi. Kwa maana hiyo, hatua za Magufuli
na serikali yake kupambana na mengi yaliyokuwa kero kwa Watanzania kunawanyima
wapinzani fursa ya kuongea.
Lawama na
shutuma za wapinzani zimevuka mipaka hadi kutugusa baadhi yetu ambao baada ya
muda mrefu wa kukosoa mwenendo wa mambo katika nchi yetu, sasa tumepata ahueni
kutokana na kazi nzuri ya Magufuli, na tunapata kila sababu ya kupongeza na
kuinadi nchi yetu.
Binafsi,
nimekuwa miongoni mwa waathirika wa shutuma hizo baada ya kuchapishwa kitabu
kinachozungumzia safari ya urais wa Dk. Magufuli, mafanikio na changamoto kwa
urais wake. Kuna wanaodai ni mapema mno kuzungumzia mafanikio ya kiongozi huyo,
lakini bila kubainisha wakati gani ni mwafaka kuzungumzia mafanikio yake.
Kuna
waliokwenda mbali zaidi na kudai kitabu hicho ni jitihada zangu binafsi
kutafuta ukuu wa wilaya. Kwa uelewa wangu, shutuma hizo ni matokeo ya hadaa
kubwa iliyofanyika kwa wafuasi wengi wa vyama vya upinzani kuwa vyovyote
ambavyo ingekuwa, mgombea wao wa kiti cha urais, Edward Lowassa, lazima
angeshinda kiti hicho.
Kuishi kinyume
cha matarajio hewa si kitu rahisi, na huenda itachukua muda mrefu kwa wapinzani
wa Magufuli kubaini kuwa kila zuri analofanya ni kwa maslahi ya Watanzania wote
bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Tanzania ya neema si tu kwa waliompigia
kura Magufuli bali kila Mtanzania, hata aliyemnyima kura.
Wakati
tunaweza kuwaelewa majirani zetu wanaokerwa kuona Tanzania imeamka, haingii
akilini kuona baadhi ya Watanzania wenzetu wakijifanya vipofu wasioona
mabadiliko makubwa na ya kasi yanayoletwa na Magufuli na serikali yake.
Walihadaiwa kuhusu mabadiliko, sasa wanaletewa mabadiliko halisi wanaanza
kulalamikia.
Katika
mahojiano yake niliyoyataja awali, Lissu anamlinganisha Magufuli na Waziri Mkuu
wa zamani, Edward Sokoine, lakini si kwa uchapakazi wake na chuki yake kubwa
dhidi ya wahujumu uchumi bali kile ambacho mwanasheria huyo anadai ni
kutoheshimu sheria.
Pia
alimfananisha Magufuli na Naibu Waziri Mkuu wa zamani, na sasa Mwenyekiti wa
taifa wa TLP, Agustino Mrema, kuwa ni kiongozi anayefanya kazi ili aandikwe na
vyombo vya habari. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Hivi kweli mazuri
haya mengi yaliyojiri tangu Magufuli aingie madarakani ni kwa minajili ya
kupata vichwa vya habari?
Nimalizie
makala hii kwa kukumbusha kuwa kinyume na mabadiliko yaliyoahidiwa na Lowassa
ambayo yalitarajiwa kutokea kama miujiza pasipo mipango madhubuti,
tunachoshuhudia kwa Magufuli ni mabadiliko ya dhati yaliyobainishwa katika
mikutano yake mbalimbali ya kampeni za uchaguzi, na kufafanuliwa kwa kirefu katika
hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge jipya.
Ushauri wangu kwa Watanzania wenzangu ni
kupuuzia wote wanaokerwa na mwenendo wa kutia matumaini wa Magufuli na serikali
yake. Wanasema ukirusha jiwe kizani kisha ukasikia kelele, basi ujue limempiga
mtu. Hizi kelele, kebehi au shutuma dhidi yake ni matokeo ya jitihada zake za
kizalendo za kuathiri waliokuwa wakinufaika na mwenendo fyongo wa nchi yetu
katika maeneo mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment