28 Apr 2016

MIONGONI mwa wahadhiri walionifundisha nilipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni Mmarekani mmoja aliyependa sana kufundisha kwa kutumia mifano halisi. Moja ya mada ambazo zilizonigusa sana ni kuhusu ‘undugunaizesheni.’ Alieleza kuwa hata Marekani kuna tabia hiyo, ambapo mara nyingi watu wenye nyadhifa muhimu hupenda kufanya kazi na watu wanaowafahamu au hata ndugu zao. 

Na kwa vile mfumo wa serikali nchini humo sio kama wetu wa ‘ili mtu ateuliwe kuwa waziri sharti awe mbunge – awe wa kupigiwa kura na wananchi jimboni, wa viti maalumu au wa kuteuliwa na rais. Kwa wenzetu huko, rais anaweza kumteua mtu yeyote kuwa kwenye “kabineti” yake japo baadhi ya nyadhifa zinahusisha mteuliwa kuidhinishwa na mabunge ya nchi hiyo. 

Mhadhiri huyo Mmarekani alitanabaisha kuwa baadhi ya viongozi ‘huwavuta’ ndugu zao wa karibu, jamaa au marafiki sio tu kwa vile ni watu wao wa karibu bali pia kulingana na sifa walizonazo. Lakini la muhimu zaidi ni matarajio kuwa ndugu, jamaa au rafiki anaweza kuwa mtiifu sana kwa aliyemteua, hasa ikizingatiwa kuwa ‘akimwangusha, anajiangusha naye pia.’

Kwa hiyo, si kwamba suala la undugunaizesheni – kufanya upendeleo kwenye maeneo kama vile teuzi za nafasi za uongozi, halipo Afrika, au huko nyumbani pekee bali hata huku kwa hawa wenzetu wanaojigamba kwa kuzingatia taratibu na kanuni. 

Kimsingi, kumteua mtu unayemjua, alimradi ana sifa stahili, sio kuvunja taratibu na kanuni, hususan kama mchanganuo wa kumteua mtu huyo haukuwanyima watu wengine fursa ya kuteuliwa. 

Suala la ‘undugunaizesheni’ limekuwa likinijia akilini kila ninapokutana na habari kuhusu sakata la Lugumi. Lakini pengine kabla ya kuingia kwa undani kujadili sakata hilo ni vema nikaweka bayana msimamo wangu maana ‘wenye nchi’ wamekuwa wakali kweli, ukikosoa kidogo tu unaonekana kuwa wewe ni jipu au mtetezi wa majipu.

Ni kwamba namuunga mkono Rais Dk. John Magufuli, katika jitihada zake kubwa za kutumbua majipu. Hata hivyo, mara kadhaa amekuwa akitusihi Watanzania tumsaidie katika jitihada zake hizo. Na miongoni mwa njia za kumsaidia mtu ni kumshauri au hata kumkosoa pale inapobidi. Binafsi, ninaamini kuwa mtu pekee anayeweza kumaliza sakata la Lugumi ni Rais Magufuli tu, hakuna cha Bunge wala Takukuru. Ni hivi, si mfanyabiashara yeyote tu anayeweza kupewa zabuni nyeti ya kuweka mashine za kuchukua alama za vidole katika mamia ya vituo vya polisi nchini. Mtu anayepewa dhamana kubwa namna hiyo lazima awe ‘mtu fulani.’ 

Mengi yanayozungumzwa kuhusu mmiliki wa kampuni hiyo ya Lugumi yamebaki kuwa tetesi tu, lakini moja linalisikika zaidi ni madai kuwa alikuwa ‘karibu na watawala’ katika Serikali ya Awamu ya Nne. Na kwa jinsi tunavyoelewa nchi yetu ilivyokuwa inajiendesha yenyewe (on autopilot) katika awamu hiyo, hakuna miujiza hapa wala hakuna la ajabu ambalo lisingewezekana. Tuwe wakweli, nchi ilikuwa inaendeshwa kimzaha. 

Tetesi pia zinadai kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, ambaye sio tu ndiye mwenye dhamana ya kufuatilia kuhusu sakata hilo kwa vile linaihusu wizara yake, lakini pia ni mmoja wa wanaotajwa kuhusika na ufisadi huo kupitia umiliki wa kampuni yake ya Infosys. 

‘Mazingaombwe’ yanayolizunguka sakata hili yanazidi kuendelea. Awali, ilielezwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi aliikwepa Kamati husika ya Bunge alipotakiwa kutoa maelezo kuhusu sakata hilo. Baadaye, tukasikia Bunge likitoa taarifa za kujikanganya, ikiwa na pamoja na kituko cha kudai kuwa kamati husika haikuomba mkataba husika bali maelezo tu (kana kwamba kuomba mkataba huo ni kuvunja sheria za nchi). 

Siku chache baadaye, ikaibuka video inayomwonyesha mtendaji mmoja wa kampuni ya Infosys akieleza kuwa Waziri Kitwanga sio mmiliki wa kampuni hiyo, na kwamba aliachana nayo kabla haijaingia mkataba huo wenye utata. 

Baadaye tena, Waziri Kitwanga mwenyewe akajitokeza kuzungumzia suala hilo akidai kuwa wakati suala hilo linatokea, yeye hakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, na ndio maana hapendi wala hataki kuzungumzia suala hilo. 

Kauli hii inatoka kwa waziri ambaye Jeshi la Polisi lipo chini ya wizara yake. Sawa, hakuwa waziri wakati suala hilo linatokea, lakini sasa ni waziri. Kwa nini basi asipende wala kutaka kuongelea suala ambalo sio tu linaitia doa wizara yake na jeshi la polisi bali pia linaweza kuathiri usalama wa taifa letu? 

Kwa nini kama Waziri Kitwanga anajua vema majukumu yake hakushughulikia suala hilo kabla ya kuibuliwa na Kamati ya Bunge? Na hapo tunaweza kujiuliza, kwa nini Rais Magufuli hakuchukua hatua stahili dhidi ya mtendaji wake huyo, kwa staili ya kutumbua majipu? 

Sarakasi za sakata la Lugumi zimeendelea kwa Bunge kuunda timu maalumu ya kuchunguza suala hilo. Nilidhani kuwa Takukuru wangeweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi kwa vile sidhani kama wabunge walioteuliwa ni wataalamu wa uchunguzi wa masuala yenye dalili za ufisadi. Labda tuwape muda, huenda wanajua wanachofanya. 

Kichekesho zaidi kimeibuka muda mfupi kabla sijaandaa makala hii, ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu ameibuka na kudai kuwa kampuni ya Lugumi ilitekeleza mkataba husika, na kukanusha madai ya Kamati husika ya Bunge, na taarifa zilizosambaa mtandaoni na kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni hiyo ilishindwa kufunga mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo 108 kama ilivyotamkwa kwenye mkataba. 

IGP Mangu alidai kushangazwa na habari hizo na kueleza kuwa kampuni ya Lugumi ilitekeleza mkataba husika kama ilivyokubaliana na serikali. 

“Siyo kweli, watu wana ugomvi wao, lakini nakueleza wazi kwamba, tembelea vituo vyote tulivyokubaliana, utakuta mashine zipo. Inawezekana zingine hazifanyi kazi kwa sababu ya kukosekana kwa intaneti,” alisema mkuu huyo wa jeshi la polisi. 

Ni akina nani hao “wenye ugomvi wao” ambao jeshi la polisi linashindwa sio tu kuwachukulia hatua bali hata kuwataja majina hasa ikizingatiwa kuwa kashfa hiyo inachafua taswira ya taasisi hiyo ya dola? 

Na kama huo ndio ukweli, kwa nini basi IGP Mangu hakujitokeza kwenye kikao cha Kamati ya Bunge iliyokutana kufuatilia suala hilo? Si angeenda tu na kuwaeleza kama anavyosema sasa kuwa suala hilo linatokana na “ugomvi” wa watu fulani? 

Lakini utetezi wake ungekuwa na maana tu kama angeweza kubainisha ni vituo vingapi na vipi ambavyo mashine hizo zilifungwa, na vingapi na vipi ambavyo mashine zinafanya kazi au hazifanyi kazi. 

Na kuhusu uwezekano wa kuwepo mashine zisizofanya kazi kutokana na kutokuwepo kwa Intaneti, basi ni uzembe wa wazi wa IGP na Waziri wake Kitwanga kwa sababu hilo ni jipu lililopaswa kutambuliwa mapema kabla ya kuibuliwa na kamati ya Bunge. Je, huduma ya Intaneti ilikatwa kwa kutolipiwa kwa vile Jeshi la Polisi lilinyimwa fungu husika au ni habari zile zile wa ‘watumishi hewa’? 

Nilianza makala hii kwa kuzungumzia suala la undugunaizesheni. Kuna hisia kuwa uteuzi wa Waziri Kitwanga ulitokana na ukaribu alionao na Rais Magufuli. Hilo sio kosa. Lakini ni jukumu la mteuliwa kuhakikisha hamwangushi aliyemteua. Na katika sakata hili la Lugumi, yayumkinika kuhisi kuwa Waziri Kitwanga anamwangusha Rais Magufuli. 

Wengi tuna imani na Dk. Magufuli, lakini ni ukweli usiofichika kuwa moja ya mitihani mikubwa inayomkabili ni pamoja na uwezekano wa kuangushwa na ‘maswahiba zake,’ watu anaowaamini lakini wasioitendea haki imani hiyo, shinikizo ndani ya chama chake CCM, na kubwa zaidi, ‘madudu’ yaliyofanyika katika awamu iliyopita hususan yale ambayo akiyagusa tu, nchi itatikisika (rejea kauli ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyowahi kuitoa bungeni kuhusu sakata moja la ufisadi ambapo aliwaambia bayana wabunge wamsulubu tu lakini asingeweza kuongelea suala husika). 

Nimalizie makala hii kwa kumsihi Rais Magufuli kuwa uungwaji mkono anaohitaji zaidi ni kutoka kwa Watanzania wa kawaida, waliompigia kura na hata waliomnyima kura. Hawa hawatomwangusha kwa sababu wanamhitaji, na hadi sasa amewathibitishia hivyo. Baadhi ya watendaji wake wapo kwa maslahi yao binafsi, na hawa watamwangusha asipokuwa makini. Ni muhimu kwa Rais wetu kukumbuka kuwa utumbuaji majipu halisi unamtengenezea maadui lukuki, ambao wanaweza kuunganisha nguvu na kumyooshea kidole pale yanapojitokeza mambo kama haya ya kina Lugumi. 


Mpendwa Rais Magufuli, chukua hatua moja tu na sakata hili la Lugumi litamalizika (kwa maslahi ya Watanzania) 

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.