15 Sept 2016


NIANZE makala hii kwa kutoa salamu za rambirambi na pole kutokana na vifo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi iliyopita huko Bukoba. Hadi wakati ninaandika makala hii jumla ya watu 16 walikuwa wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya 200 wakiwa wamejeruhiwa.
Jinsi janga hilo lilivyochukuliwa kwa kiasi kikubwa ‘kama tukio la kawaida’ huku baadhi ya wenzetu wakiendelea na tamasha la muziki wakati tunapaswa kuwa katika maombolezo ya kitaifa, imenifanya nijikute katika tafakuri kuhusu uhusiano kati yetu na nchi yetu.
Ukiacha ‘mbwembwe’ za hapa na pale, huku nyingi zikiwa za kinafiki, Watanzania wengi wanaielezea vibaya nchi yao. Si jambo la kushangaza kusikia mtu akidai ni bora kuzaliwa paka Ulaya kuliko kuzaliwa binadamu Tanzania. Kadhalika, siku hizi imezoeleka kusikia baadhi ya wenzetu wakidai bora nchi yetu ilipokuwa chini ya utawala wa mkoloni kuliko hali ilivyo sasa.
Na kwa akina sisi tulio nje ya nchi tukijaribu kuchangia japo kwa mawazo tu kuhusu mustakabali wa tafa letu, tunaishia kuambiwa tunajipendekeza…tunataka ukuu wa wilaya na vitu vya kukatisha tamaa kama hivyo.
Tofauti za kiitikadi zimechangia kuimarisha ‘chuki dhidi ya Tanzania,’ ambapo kwa upande mmoja, wengi wa wafuasi wa chama tawala CCM wamekuwa wakijaribu kujenga picha kuwa wafuasi wa vyama vya upinzani ‘sio Watanzania kamili,’ huku kwa upande mwingine, wafuasi wengi wa vyama vya upinzani wakijaribu kujenga picha ya Tanzania kama nchi mbaya kabisa duniani kutokana na utawala wa CCM.
Kuna kitu kinafahamika kama ‘national psyche’ au saikolojia ya taifa – kwa maana nyepesi, sisi kama Watanzania tunajionaje? Na sisi kama Watanzania tunalichukuliaje taifa letu?  Tukiweka kando ‘mabaya’ kama rushwa, ufisadi na umasikini wetu, je kuna lolote tunalojivunia kuhusu nchi yetu? Tunapoona yanayojiri nchi kama Burundi, Somalia na Sudan ya Kusini, tunatambua thamani ya tulichonacho ambacho baadhi ya wenzetu hawana?
Hii saikolojia ya taifa inaweza kuwa muhimu sana katika kuelezea kwanini uzalendo umekuwa ukiporomoka kwa kasi. Tunapowaona wenzetu wamejipaka rangi za bendera za nchi zao katika mechi za kimataifa au matukio muhimu yanayohusu mataifa yao sio suala la ushabiki tu bali mapenzi waliyonayo kwa nchi zao.
Kwa hapa Uingereza bendera yao ya ‘Union Jack’ inagusa na kuvuta hisia kali kwa Waingereza wengi kama ilivyo bendera ya Marekani, ‘Stars and Stripes.’ Lakini sio bendera tu, hata alama za kitaifa kama vile sanamu ya Kristo Mkombozi (Christ the Redeemer), jijini Rio, Brazil; Mnara wa Eiffel, Paris, Ufaransa; Mapiramidi ya Giza, Misri; Ukuta Mkuu wa China, Mnara wa Uhuru (Statue of Liberty), New York, Marekani, na ‘Jicho la London’ (London Eye) na Big Ben, jijini London, hapa Uingereza.
Sisi licha ya vivutio lukuki tulivyonavyo, mpaka leo ‘tunasuasua’ kuwa na utambulisho wa taifa letu. Kama ni Mlima Kilimanjaro, basi huo unafahamika zaidi kuwa upo Kenya kuliko Tanzania, na kama ni madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana nchi kwetu pekee, ni India na Kenya ndizo zinazoongoza kwa mauzo ya madini hayo. Mchakato wa kusaka vazi la taifa umejifia kifo cha asili. Hii inatosha kueleza sie ni watu wa aina gani.
Lakini kinachokera zaidi ni kuona taifa limekumbwa na janga la tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi iliyopita huko Bukoba, na kusababisha vifo 16 na majeruhi zaidi ya 200 (hadi wakati ninaandika makala hii) lakini tukio hilo linaonekana kuwagusa zaidi watu walio nje ya Tanzania kuliko sisi Watanzania wenyewe.
Hivi inaingia akilini kweli kuona tamasha la burudani la Fiesta likifanyika Jumapili huko Singida katika kipindi cha majonzi ambapo Watanzania walikuwa wakiendelea kupata habari za kusikitisha (zaidi kupitia vyombo vya habari vya kimataifa) za kuongezeka idadi ya vifo na majeruhi? Katika hili lawama zinapaswa kwenda kwa waandaaji wa tamasha hilo, wasanii walioshiriki na wahudhuriaji. Hawa wote ni Watanzania na walipaswa ‘kuwa na mshipa wa aibu’ kuwafahamisha kuwa maombolezo ni muhimu zaidi ya burudani
Jumapili hiyo tena kulijitokeza mkanganyiko ambapo awali taarifa iliyotolewa na Ikulu ilieleza kuwa Rais Dk John Magufuli angesafiri kwenda Zambia kwenye sherehe ya kuapishwa Rais mteule wa nchi hiyo Edgard Lungu. Hivi kweli kabla ya kutolewa taarifa hiyo, wahusika walikuwa hawafahamu kuhusu kilichojiri huko Bukoba kiasi cha ‘kuamini’ kuwa Rais angeweza tu kusafiri?
Japo baadaye iliripotiwa kuwa Rais hatosafiri na badala yake atawakilishwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu, baadhi yetu tulibaki na ‘sintofahamu’ kuhusu kilichopelekea mkanganyiko huo.
Hadi wakati ninaandika makala hii, mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, blogu kadhaa za Tanzania na vyombo vya habari vya kimataifa ndio vimekuwa vikitoa ripoti za takriban kila saa kuhusu tukio hilo, ilhali vyombo vingi vya habari ‘vikiburudika na mapumziko ya mwisho wa wiki.’
Kitaifa, hakuna tamko la maombolezo ya kitaifa wala bendera kupepea nusu mlingoti. Tumezowea sana majanga, kama vile ajali mfululizo zinazogharimu maisha ya Watanzania lukuki, kiasi kwamba hatujali ‘kihivyo’ kilichotokea huko Bukoba?
Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa Rais Magufuli kuangalia uwezekano wa kufanyika mjadala wa kitaifa kuhusu uhusiano wetu na Tanzania yetu, kushuka kwa kasi kwa uzalendo, na saikolojia ya taifa letu kwa ujumla. Kadhalika, ninamwomba Mungu awapumzishe mahali pema peponi Watanzania wenzetu waliouawa na tetemeko hilo la ardhi, sambamba na kumwomba awajalie ustahimilivu wafiwa, na uponyaji wa haraka kwa majeruhi wa janga hilo la kitaifa.
Baruapepe: [email protected] Blogu:www.chahali.com Twitter: @chahali  

1 comment:

  1. Ukweli mtupu. Lakini sina imani kama watapita huku, natamani kama ungemwandikia moja kwa moja mh raisi wetu.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.