17 Nov 2016

JUMANNE iliyopita inaweza kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu mbaya kutokana na uchaguzi mkuu nchini Marekani ambao mshindi alikuwa mgombea wa chama cha kihafidhina cha Republican, Donald Trump.
Trump – mwongo wa waziwazi, mnyanyasaji wa wanawake, mzinzi, mbaguzi wa rangi, mbaguzi wa kidini na mwasisi wa harakati za kibaguzi dhidi ya uraia wa Rais wa sasa wa nchini hiyo, Barack Obama, alifanikiwa kumshinda mpinzani wake mkuu, mgombea wa chama cha Democrat, Hillary Clinton.
Kibaya zaidi ni kwamba mfumo fyongo wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ulimwezesha Trump kuwa mshindi licha ya kupata kura pungufu (60,350,241) dhidi ya mpinzani wake Hillary (aliyepata kura 60, 981, 118). Kura hizo zilizopigwa siku ya uchaguzi hujulikana kama popular vote, lakini kura muhimu zaidi na zinazoamua mshindi wa uchaguzi ni zinazofahamika kama electoral votes. Mshindi hutakiwa kupata kura hizi 270 au zaidi.
Inabidi kuelezea kwa kifupi kuhusu mfumo huo unaokanganya. Kimsingi, Wamarekani hawamchagui Rais wao moja kwa moja, badala yake kila jimbo lina watu wanaofahamika kama electors (wachaguzi) ambao hukutana mwezi Desemba mara baada ya kura zilizopigwa na kila aliyejiandikisha kupiga kura Novemba 8 ya mwaka wa uchaguzi.
Kama tulivyoona kwenye matangazo ya runinga, kila jimbo lina idadi yake ya "wachaguzi." Na jumla ya wachaguzi hao kutoka majimbo yote 51 ya Marekani ni 538.
"Wachaguzi" hao nao huchaguliwa na vyama vyao. Kila chama kina kanuni zake za uchaguzi wa "wachaguzi" hao. Uchaguzi wao hufanyika kwa hatua mbili. Kwanza, chama huchagua orodha ya "wachaguzi watarajiwa" na pili, "wachaguzi halisi" huchaguliwa na wapigakura siku ya uchaguzi. Majina ya wanaogombea kuwa “wachaguzi" yanaweza kuonekana katika karatasi ya kura au yasionekane, kutegemea kanuni husika.
Hakuna sheria inayowabana "wachaguzi" kumpigia kura mgombea aliyeshinda popular vote. Na ni katika mazingira haya ndio maana kumekuwa na jitihada za kuwashawishi "wachaguzi" hao kutompigia kura Trump, ili kumkwamisha na hatimaye kumwezesha Hillary achaguliwe. Hata hivyo, uwezekano wa hilo kutokea ni mdogo. Kihistoria, asilimia 99 ya "wachaguzi" hupiga kura kwa mshindi wa "popular vote."
Kila jimbo lina "ikulu" yake (state capitol), na hapo ndipo "wachaguzi" kutoka kila jimbo hukutana Desemba kupiga kura zao. Masanduku ya kura walizopiga hufunguliwa mwezi Januari katika kikao cha "Baraza la Wawakilishi".
Iwapo katika matokeo kutakuwa hakuna mgombea mwenye kura nyingi, au wagombea wawili watakuwa na kura sawa, Baraza la Wawakilishi litamchagua Rais miongoni mwa wagombea watano wenye kura nyingi zaidi.
Kila jimbo hupewa "kura za wachaguzi" (electoral votes) kulingana na jumla ya maseneta na wawakilishi. Kiwango cha chini kwa kila jimbo ni kura tatu. Majimbo makubwa huwa na kura nyingi kwa vile uwakikishi katika Baraza la Wawakilishi hutegemea idadi ya wakazi katika jimbo husika.
Tukirejea kwenye matokeo ya uchaguzi, Trump alipata kura za “wachaguzi” 290 huku Hillary akiambulia 228. “Wachaguzi” katika kila jimbo watakutana Desemba 17 kupiga kura zao, huku matarajio makubwa yakiwa wataheshimu jinsi wingi wa kura za “wachaguzi” alizoshinda Trump.
Kwa hiyo japo kinadharia kuna uwezekano wa “wachaguzi” hao kuamua kumnyima kura Trump na badala yake kumpa kura hizo Hillary, hali itakayosababisha matokeo ya uchaguzi huo kubadilika, uwezekano huo kiuhalisi ni mdogo mno.
Tathmini ya uchaguzi huo inahitaji zaidi ya makala moja, na katika makala hii nitagusia mambo muhimu kwa kifupi tu kwa matarajio ya kuendeleza mada hii katika makala zijazo.
Ushindi wa Trump umetokana na nini? Nchi za Magharibi zinapitia zama mpya ya siasa inayofahamika kama “post-truth politics.” Hii ni aina ya siasa inayotawaliwa na hisia na ushawishi kuliko ukweli au hoja za kitaalamu. Aina hii mpya ya siasa ilikuwa na ufanisi sana hapa Uingereza, katika kampeni za kura ya kuamua iwapo nchi hii iendelee kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) au ijitoe. Wanasiasa wa kambi iliyotaka Uingereza ijitoe walishutumiwa mara kadhaa kwa kutumia takwimu za uongo na kujenga hoja za chuki dhidi ya wageni na EU kwa ujumla, huku wakipinga kwa nguvu zote takwimu za kitaalam zilizoonyesha bayana madhara ya nchi hii kujitoa EU.
Tulipopiga kura Juni 23 mwaka huu, kambi hiyo iliyotumia hadaa na hoja za chuki ndiyo iliyoibuka mshindi, japo tayari nchi hii inashuhudia kipindi kigumu kiuchumi kama ambavyo wataalamu mbalimbali walivyoonya wakati wa kampeni.
Ukweli (facts) una sehemu tukufu katika siasa za kidemokrasia za Magharibi. Kila wakati demokrasia ilipokwenda mrama, kila ilipotokea wapigakura kufanyiwa ulaghai au wanasiasa kukwepa maswali, tulikimbilia kwenye ukweli kama mkombozi.
Lakini kwa sasa, ukweli unaonekana kupoteza nafasi yake katika kujenga mwafaka. Tovuti ya kutofautisha ukweli na uongo ya PolitiFact ilibaini kuwa takriban asilimia 70 ya hoja za Donald Trump ziliangukia makundi ya “karibu na uongo” “uongo” and “uongo kabisa." Lakini hiyo haikumzuia kushinda urais wa Marekani
Kadiri siasa zinavyozidi kuwa za uhasama na kutawaliwa na ufanisi wa wahusika kwenye nyenzo za teknolojia kama vile runinga na mitandao ya kijamii, "afya" ya ukweli (facts) kwenye mijadala na midahalo inakuwa tete. Matarajio ya wasikilizaji, watazamaji na wasomaji yanaelemea zaidi kwenye ushawishi wa mtoa hoja hata kama hoja hizo ni za uongo wa waziwazi.
Taratibu, nafasi ya wajuzi, wasomi, wazoefu na makundi mengine tuliyozoea kuyaamini kutupatia mwongozo sahihi inazidi kudidimia na mbadala wake ni hoja za kugusa hisia za watu hata kama zinapanda mbegu za mfarakano, kutumia uongo hata pale unapoonekana waziwazi ilimradi tu unaweza kuvutia kuungwa mkono na sehemu ya hadhira, kupandikiza hasira ili kuipa nguvu hadhira kuchukua hatua hata kama zinapanda athari na kwa ujumla, kutotoa fursa kwa ukweli (facts).
Aina hii mpya ya siasa ni hatari, sio tu kwa sababu unafanya ukweli kuwa uongo na uongo kuwa ukweli, bali pia kwa vile imetokea kuwa chaguo mwafaka la wanasiasa waumini wa siasa za mrengo mkali wa kulia; wabaguzi wa rangi, wabaguzi wa kidini; na viumbe hatari kama hao.
Nitazungumzia zaidi mada hii siku nyingine.
Kwa upande mwingine, ushindi wa kambi iliyotaka Uingereza ijitoe EU (licha ya hoja zao za uongo na kupandikiza chuki) na ushindi wa Trump huko Marekani ni ujio wa mapinduzi ya kimfumo; upinzani wa umma dhidi ya tabaka la wanasiasa, wasomi na taasisi za kisiasa na uchumi. Hii ingepaswa kuwa habari njema lakini tatizo ni kwamba wanaoendesha kampeni ya mapinduzi haya ni wanasiasa hatari kabisa katika nchi zao na kimataifa.
Ushindi wa Trump umepokelewa kwa shangwe kubwa na viongozi wa vyama vya kisiasa vya kibaguzi na vyenye mrengo mkali wa kulia, kama Marine LePen wa Ufaransa, Victor Orban wa Hungary, Frauke Petry wa Ujerumani, Heinz-Christian Strache wa Austria na Geert Wilders wa Uholanzi. Na kwa hapa Uingereza, mwasisi wa harakati za nchi hii kujitoa EU, Nigel Farage, amekuwa mwanasiasa wa kwanza wa nchi hii kukutana na Rais-Mteule, Donald Trump.
Kwa hali ilivyo Marekani hivi sasa ambapo kuna maandamano mbalimbali ya kupinga ushindi wa Trump, mustakabali utategemea zaidi jinsi kiongozi huyo atakavyomudu kubadilika na kuwa kiongozi wa Wamarekani wote na sio kundi la Wamarekani weupe wasio na elimu ya chuo, Wakristo wenye msimamo mkali, na magenge ya wabaguzi wa rangi kama vile kundi la Klu Klux Klan (KKK) pekee.
Je, Trump atabadilika? Kwa jinsi ambavyo kila kitu kuhusu Trump ni vigumu kukibashiri kwa ufasaha (mwenyewe anasema kutotabirika ni siri ya mafanikio), jibu fupi ni kwamba; “…hakuna ajuaye isipokuwa Trump mwenyewe.” Jibu refu ni kwamba awali kauli zake kuwa atachukua mazuri na kuacha mabaya ya mpango wa bima ya afya ya jamii ujulikanao kama Obamacare (ambao Trump aliahidi kuufuta mara moja wakati wa kampeni) ziliashiria dalili za mabadiliko.
Pia taarifa kuwa amezitoa hofu nchi za Japan na Korea Kusini kuhusu msaada wa kijeshi wa Marekani kwa nchi hizo, zilileta dalili ya matumaini kwamba huenda ameanza kubadilika. Japan inakabiliwa na tishio kutoka China, na Korea Kusini inakabiliwa na tishio kutoka Korea Kaskazini, na Jeshi la Marekani ni ngao muhimu kwa mataifa hayo.
Vile vile, tovuti ya kampeni za uchaguzi ya Trump iliondoa tamko lake la kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo pindi akishinda urais. Hatua hiyo Ilitafsiriwa kuwa ni dalili za ‘msema ovyo’ huyo kulegeza msimamo.
Hata hivyo, tayari Trump ameeleza kuwa ataanza utekelezaji wa dhamira yake ya kuwatimua wahamiaji haramu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 11 nchini humo, ambapo ametangaza kuwa ataanza kuwatimua ‘wageni haramu’ milioni tatu mara tu baada ya kuapishwa.
Nihitimishe makala hii kwa kugusia vitu viwili. Kwanza, kushamiri kwa wimbi la “post-truth politics” na “mapinduzi dhidi ya tabaka la wanasiasa, wataalam au taasisi za siasa na uchumi” hasa kwa vile mwezi ujao, Italia itakuwa na kura ya maoni kuhusu katiba za nchi hiyo na Austria itakuwa na uchaguzi mkuu, Uholanzi itakuwa na uchaguzi wa bunge mwezi Machi mwakani, Ufaransa itakuwa na uchaguzi mkuu Aprili hadi Juni mwakani, na Ujerumani itakuwa na uchaguzi wa wabunge mwezi Septemba mwakani. Mataifa yote hayo yanakabiliwa na vuguvugu kubwa la upinzani dhidi ya Umoja wa Ulaya na chuki dhidi ya wageni, pamoja na “post-truth politics.”
Pili, moja ya makundi yaliyomsaidia sana Trump kushinda urais ni linalofahamika kama ‘alt-right.’ Kwa lugha rahisi, hawa ni zaidi ya wahafidhina. Ni wabaguzi wa rangi na dini, wapinzani wa harakati za wanawake na wanaosherehesha unyanyasaji wa wanawake, na kwa kifupi, “watu waliofanikiwa kuhamasisha kuwahadaa watafiti wa kura za maoni kuhusu nafasi ya Trump katika uchaguzi wa rais Marekani.”
Nimalizie makala hii kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika toleo lijalo, kwa kuangalia athari za urais wa Trump duniani kwa ujumla hususan barani Afrika, kwa nini Hillary ameshindwa na kwa nini kura za maoni zilibashiri matokeo ya uchaguzi huo “ndivyo sivyo” na nini tunaweza kujifunza kutokana na uchaguzi huo.
ITAENDELEA TOLEO LIJALO


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.