24 Nov 2016


KAMA nilivyoahidi katika toleo lililopita la gazeti hili, wiki hii ninaendelea na uchambuzi kuhusu uchaguzi wa Rais wa Marekani uliofanyika wiki mbili zilizopita na kushuhudia mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, akiibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake mkuu, Hillary Clinton wa Democrat.

Makala yangu katika toleo la wiki iliyopita ilibeba swali ‘je Trump atabadilika?” Swali hilo lilitokana na ukweli kwamba kauli za Trump na tabia yake kwa ujumla, kabla ya kuwa mgombea, akiwa katika mchakato wa chama chake kupata mgombea, na wakati wa kampeni kama mgombea wa chama chake, zilisheheni kasoro lukuki; ubaguzi dhahiri wa kidini, unyanyasaji wa wanawake na dhihaka kwa walemavu, kupandikiza chuki dhidi ya Wamarekani wasio weupe, chuki dhidi ya wageni, na mengineyo mengi yaliyoibua wachambuzi wa siasa kutodhani kuwa Trump angeweza kushinda katika uchaguzi huo.
Lakini tatizo halikuwa kwa Trump pekee bali pia watu waliomzunguka na baadhi ya makundi ya wafuasi wake. Moja ya kundi muhimu kwa ushindi wa bilionea huyo ni lile linalofahamika kama ‘alt-right’ (kifupi cha ‘alternative right’ yaani mbadala wa wahafidhina/wenye mrengo wa kulia). Kundi hili limekuwa ‘mwiba’ sio kwa waliberali pekee bali pia hata wahafidhina wenye msimamo wa wastani.
Na kundi hilo hatari ndilo analotoka mmoja wa wateule wa awali kabisa wa Trump, Steve Bannon, aliyeteuliwa kuwa mkuu wa mikakati wa Trump. Bannon alikuwa mmoja wa viongozi wa kampeni ya bilionea huyo na kabla ya hapo alikuwa mwenyekiti wa gazeti ‘hatari’ la mtandaoni, Breitbart. Gazeti hatari kwa sababu lengo lake kuu ni kuamsha hisia za makundi fulani kwa kubeza, kulaani na hata kutukana makundi kama vile Wamarekani weusi (gazeti hilo lilidai kuwa kiasili ni wahalifu), Walatino, wahamiaji, Waislam (gazeti hilo limewaita kila jina baya), watetezi wa haki za wanawake ikiwa pamoja na waathirika wa vitendo vya kubakwa, na takriban kila baya usilotarajia kuliona kwenye gazeti maarufu ambalo mwezi uliopita pekee, tovuti yake ilitembelewa na wasomaji zaidi ya milioni 19.
Kwa kumteua Bannon, ni wazi kuwa Trump ameamua kukumbatia makundi yaliyomuunga mkono hata kama yanajenga taswira isiyopendeza kwa urais wake. Tayari makundi mbalimbali ya utetezi wa haki za kiraia Marekani yanamtaka Trump kutengua uteuzi wa Bannon, mtu mwenye ajenda za kibaguzi na muumini wa ‘ukuu wa watu weupe’ (white supremacist).
Lakini taswira ya kuogofya kuhusu aina ya watu ambao Trump atawakumbatia katika urais wake haijaishia kwa Bannon pekee bali pia hata chaguo lake la mshauri wake wa masuala ya usalama wa taifa, Luteni Jenerali (mstaafu) Michael Flynn na Mwanasheria Mkuu, Seneta Jeff Sessions. Wakati Jenerali Flynn alitimuliwa na utawala wa Rais Barack Obama kutokana na kile kinachoelezwa kuwa kasoro za kiuongozi, Sessions ana tuhuma za ubaguzi wa rangi. Kadhalika, msimamo wa Jenerali huyo kuhusu masuala ya ugaidi wa kimataifa unaotajwa kuwa unaweza kuikosanisha Marekani na mataifa ya kiislamu kwa vile anaamini kuwa tatizo la ugaidi linachangiwa na Uislamu na sio magaidi kutumia kisingizio cha Uislamu kuhalalisha unyama wao.
Mteule mwingine wa Trump kushika nafasi ya ukuu wa shirika la ujasusi la nchi hiyo, CIA, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mike Pompeo, naye anatazamwa kama mtu anayeweza kulirejesha shirika hilo katika zama zake za hatari kabisa, hasa kutokana na msimamo wake mkali kupindukia kwenye masuala ya intelijensia na usalama. Ikumbukwe kuwa katika zama zake hatari, CIA ilishiriki katika operesheni chafu kama vile mauaji ya Rais wa zamani iliyokuwa Zaire, Patrice Lumumba.
Tukiweka kando dalili za awali za mwelekeo wa serikali ya Trump, tugeukie kwanza swali muhimu: “..kwa nini Hillary Clinton alishindwa na Trump.” Sababu zinaweza kuwa nyingi, lakini za muhimu zaidi ni pamoja na ukweli kwamba Hillary alikuwa mmoja wa wanasiasa wanaochukiwa mno Marekani, japo chuki dhidi yake ilikuwa pungufu kidogo kulinganisha na Trump.
Kadhalika, kasoro kubwa iliyomwandama Hillary ni kuonekana kama sio mwaminifu hususan kutokana na skandali iliyomwandama muda wote wa kampeni yake kuhusu matumizi ya ‘server’ binafsi kwa mawasiliano ya barua-pepe alipokuwa ‘Waziri wa Mambo ya Nje.’
Vile vile, Hillary alishindwa kuwa na kauli mbiu yenye kueleweka kirahisi, kulinganisha na mpinzani wake, Trump, ya ‘Ifanye Marekani jabali tena’ (Make America Great Again). Sambamba na hilo ni ukweli kwamba ilikuwa vigumu mno kwa Democrat kuendelea kuwa Ikulu baada ya miaka minane ya urais wa Barack Obama. Kwa Marekani, ni ngumu sana kwa chama kilichokuwa madarakani kwa mihula miwili mfululizo kushinda muhula wa tatu.
Kingine kilichomwangusha Hillary ni kuzidiwa kwa kura na Trump miongoni mwa Wamarekani weupe, hususan wale ambao hawana elimu ya chuo. Kuongeza majeraha zaidi, ngome zake kuu, yaani wanawake, Wamarekani weusi na Walatino hawakumpigia kura nyingi kama ilivyotarajiwa huku Trump naye akifanikiwa kupata kura za kutosha katika makundi hayo yaliyotarajiwa kumwangusha.
Pengine kubwa zaidi ni kilichotukumba sote tuliokuwa tunafuatilia kwa karibu uchaguzi huo. Ilionekana kama jambo lisilowezekana kwa Trump kushinda urais. Kauli zake zilikuwa chafu kupita maelezo, hasa ile aliyorekodiwa akiwatusi wanawake na kujigamba kuwa ‘ukiwa mtu maarufu wanawake wanakupapatikia,’ kashfa dhidi ya walemavu, wanawake, Waislamu na Walatino (aliowaita wabakaji), na kila neno chafu ambalo mgombea japo wa ukiranja shule ya msingi, achilia mbali urais wa Marekani, hakupaswa kuropoka.
Ni kwamba, katika mazingira ya kawaida, na kwa kuamini kuwa Wamarekani wana akili timamu, isingewezekana Trump kushinda uchaguzi huo. Na katika kutupatia matumaini zaidi, takriban kura zote za maoni (opinion polls) zilionyesha Hillary akiongoza kati ya asilimia mbili na 14. Japokuwa kulikuwa na tahadhari kuwa kura hizo za maoni zilikuwa na walakini, wengi wetu tuliamini kuwa suala sio iwapo Hillary angeshinda bali angeshinda kwa kiasi gani.
Na hii inaleta swali, kwa nini takriban kura zote za maoni ziliashiria kuwa Hillary angeshinda lakini ikawa kinyume chake? Hali kama hiyo ilitokea kwenye uchaguzi mkuu wa Uingereza, Mei mwaka jana na ikajirudia kwenye kura kuhusu Uingereza kubaki au kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya. Katika kura zote hizo, matokeo yalikuwa tofauti kabisa na ubashiri wa kura za maoni.
Moja ya maelezo kuhusu ‘ubashiri fyongo’ wa kura za maoni, sio kwenye uchaguzi huo wa Marekani tu bali pia kwenye uchaguzi mkuu wa UK mwaka jana na kwenye kura ya ‘Brexit’ Juni mwaka huu, ni kile ambacho Profesa Timur Kuran wa Chuo Kikuu cha Harvard huko Marekani amekieleza katika kitabu chake ‘ukweli faraghani, uongo hadharani’ (Private Truths, Public Lies), katika kanuni (theory) yake inayojulikana kama ‘preference falsification.’ Kwa kifupi, kanuni hiyo inaeleza kuwa baadhi ya watu wanaohojiwa kwenye kura za maoni kuhusu masuala yanayogusa hisia za jamii hutoa majibu wanayoona yanaendana na ‘mtazamo wa jamii’ japo misimamo yao ni kinyume.
Kwa mfano, katika suala la Brexit, kwa kuzingatia kanuni ya Profesa, kulikuwa na hisia kuwa wanaotaka Uingereza ijitoe Umoja wa Ulaya ni wabaguzi wa rangi (racists). Kadhalika, kwa vile Trump alishatoa kauli kadhaa za kibaguzi na makundi mbalimbali ya kibaguzi kama vile KKK yalitangaza kumuunga mkono, ilijengeka picha kuwa ‘wafuasi wa Trump ni wabaguzi.’ Kwa hiyo, baadhi ya waliohojiwa kwa minajili ya opinion pools za Brexit na Trump ‘walibaki na ukweli wao faraghani na kuongea uongo hadharani,’ na katika mazingira hayo, uungwaji mkubwa kutaka UK ijitoe EU na hiyo ya Trmp miongoni mwa wapigakura haikuweza kuonekana kwa waendesha kura za maoni (pollsters).
Kwa upande mwingine, Hillary alikuwa mwathirika wa zama mpya za ‘siasa za uongo,’ wenyewe wanaita ‘post-truth politics,’ ambapo vitu muhimu kwenye mijadala na kampeni za kisiasa, kama vile ukweli na hoja za kitaalamu, vinazidiwa nguvu na kauli za uongo lakini za kugusa hisia na imani za watu. Kampeni ya Brexit hapa Uingereza ilitawaliwa na ‘post-truth politics’ na ikawezesha kambi iliyotaka Uingereza ijitoe ishinde kwenye kura ya maoni, na kwa mara nyingine tena imemwezesha Trump kushinda huko Marekani.
Kama nilivyoandika katika makala yangu kwenye toleo lililopita, tatizo la ‘post-truth politicis’ ni ‘waumini’ wa aina hiyo ya siasa. Takriban wote, angalau kwa kuangalia aina ya watu na vikundi vyao, ni waumini pia wa siasa za kibaguzi za mrengo mkali wa kulia.
Ndio, ‘post-truth politics, ni matokeo ya tabaka tawala, tabaka la wanasiasa, tabaka la wasomi na mfumo wa siasa, uchumi na jamii kushindwa kusikiliza vilio vya wananchi wa kawaida, lakini kwa bahati mbaya au makusudi, viongozi wa siasa hizo ni watu hatari zaidi ya viongozi waliopo kwenye mfumo tulionao sasa, angalau kwa nchi za Magharibi.
Je ‘post-truth politics,’ na ufanisi wake kwa Brexit na ushindi wa Trump ni vitu vinavyoweza kuenea kwa upana zaidi? Hilo ni suala la muda. Kipimo cha kwanza ni uchaguzi mkuu nchini Ufaransa Aprili hadi Juni mwakani, na kura ya maoni/chaguzi nchini Italia, Austria na Ujerumani.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanadai kuwa ‘siasa za umaarufu’ (populist politics) kama hizo za ‘post-truth’ zina ‘uhai’ (life-span) wa kati ya miaka mitano hadi saba tu. Kwa hiyo wanabashiri kuwa hazitodumu kwa muda mrefu, na pengine hiyo itazifanya zisisambae sehemu kubwa ya dunia.
Kwa huko nyumbani, na pengine Afrika kwa ujumla, ‘siasa za hadaa/uongo’ zimekuwa sehemu muhimu ya siasa zetu za kila siku. Tofauti na kinachojiri huku nchi za Magharibi ni kwamba siasa za uongo zinatumiwa na watu wanaotaka kuondoa mfumo uliopo madarakani ilhali kwa akina ‘siye’ siasa za aina hiyo ndio zimeweka mfumo uliopo madarakani.
Je ‘siasa za hadaa/uongo’ zinaweza kuung’oa mfumo uliowekwa madarakani kwa hadaa/uongo? Mwamuzi ni muda. Hata hivyo, ukweli kuwa kuna vuguvugu la kushinikiza mapinduzi dhidi ya mfumo ulioshindwa kuutumiakia umma unaweza kuwa chachu kwa nchi kama zetu kuwahamasisha kuwa ‘imetosha.’ Na kama Trump licha ya kasoro zake zote ameweza kushinda urais kwa kisingizio cha ‘kupigania haki za wanyonge dhidi ya mfumo uliowatelekeza,’ basi yayumkinika kuhisi kuwa hata akina sie tunaweza kukumbwa na hali hiyo, japo binafsi naona uwezekano huo ni mdogo kwa sasa.
Na pengine ‘post-truth politics’ na wimbi la kudai mapinduzi dhidi ya mfumo ulioshindwa kuhudumia umma vinaweza visiwe na matokeo bora kwa nchi zetu za Afrika kutokana na kushamiri rushwa, siasa za kujuana na uwezo wa mfumo uliopo madarakani kutumia kila aina ya nguvu kusambaratisha jitihada zozote za kuupinga.
Mwisho, moja ya athari tarajiwa za Trump – kama akiendelea na msimamo wake wa kibaguzi – ni pamoja na bara la Afrika kutokuwa kipaumbele cha sera za nje za Marekani, kama ambavyo yawezekana uadui kati ya Marekani na nchi za kiislamu kuzorota maradufu, hususan kutokana na imani fyongo ya Trump na baadhi ya wasaidizi wake kuuhusisha Uislam na ugaidi.
Nihitimishe makala hii kwa upande mmoja kuikumbusha CCM kuwa wimbo wa upinzani dhidi ya mfumo unaoonekana kuwapuuza wananchi wa kawaida unapamba moto, na kwa vile CCM ni sehemu ya mfumo ambao baadhi ya Watanzania wanaona umewatelekeza, basi ni muhimu kujirekebisha. Kwa upande mwingine, Brexit na urais wa Trump ni funzo kwa vyama vya upinzani kuwa kusimama upande wa waliochoshwa na mfumo unaowapuuza kunaweza kusaidia kuleta ushindi kwa chama/mfumo mbadala.
Nimalizie makala hii kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika toleo lijalo, kwa kuangalia athari za urais wa Trump duniani kwa ujumla hususan barani Afrika, kwa nini Hillary ameshindwa na kwa nini kura za maoni zilibashiri matokeo ya uchaguzi huo “ndivyo sivyo” na nini tunaweza kujifunza kutokana na uchaguzi huo

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.