24 Jan 2017

Mazingira yote yalikuwa 'yameiva' kwa vyama vya upinzani kufanya vizuri kwenye chaguzi za madiwani. Angalau kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Zanzibar, vyama vya upinzani 'vya Bara' (Chadema, ACT- Wazalendo, nk, isipokuwa CUF) vinaweza kuwa na 'kisingizio' kuwa upinzani huko, kwa maana ya CUF pekee, umepaganyika mno na isingekuwa rahisi kuchukua jimbo la Dimani. 

Lakini vyama vyetu vya upinzani haviwezi kuwa na excuse ya maana kutokana na matokeo mabaya kabisa waliyopata katika chaguzi hizo. 

Mwaka juzi, wakati Tanzania yetu inakwenda kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, uchaguzi ambao mie binafsi nililazimika kumpigia debe mgombea wa CCM, Dkt John Magufuli, baada ya 'Chadema kutusaliti' kwa kumpokea aliyekuwa kada maarufu wa CCM, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, niliwakumbusha mara kwa mara ndugu zangu wa UKAWA kwamba, kwanza, ni ukosefu wa busara kutegemea vyama vya upinzani kufanya vema katika mazingira yaleyale yaliyowafanya wafanye vibaya katika chaguzi zilizotangulia.

Vyama vya upizani vilivyoshiriki katika chaguzi hizo za madiwani viliingia vikiwa katika mazingira yaleyale yaliyovifanywa vibwagwe na CCM katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Kibaya zaidi, hadi leo, si Chadema, NCCR Mageuzi, CUF au ACT-Wazalendo waliofanya 'post-mortem' (taarifa ya uchunguzi inayoeleza chanzo cha kifo) ya kwanini vyama husika vilifeli. Badala ya kufanya tathmini ya kina kuhusu sababu zilizovikwamisha vyama hivyo mwaka 2015, kumekuwa na mwendelezo wa porojo kuwa "njia ya Ikulu 2020 ni nyeupe."

save image


Kama kuna chama ambacho kinapaswa 'kusikia maumivu zaidi' kutokana na matokeo ya chaguzi hizo basi ni Chadema, kwa sababu wafuasi wa chama hicho - na kidogo ACT-Wazalendo - ndio pekee miongoni mwa vyma vyote vya upinzani nchini Tanzania, kuendeleza harakati za siasa, licha ya zuwio la serikali ya Rais Magufuli.

Kwamba, zuio hilo halijaathiri wafuasi wa Chadema kutumia teknolojia ya  mitandao ya kijamii, kuanzia Twitter, Whatsapp, Facebook, Jamii Forums, nk kuiban a mfululizoCCM na serikali yake. 

Lakini hapohapo kuna walakini. Ndio, ni wajibu wa vyama vya upinzani kuikosoa CCM na serikali yake. Hata hivyo, kukosoa tu hakutoshi hasa pale ambapo panapohitajika ufumbuzi.

Mifano ni mingi, lakini tuchukulie tishio la baa la njaa. Wakati serikali ya Rais Magufuli na CCM wakisisitiza kuwa hakuna tishio hilo, vyama vya upinzani vikiongozwa na Chadema vimekuwa mstari wa mbele kuonyesha kuwa tatizo hilo lipo.

Lakini kuonyesha tatizo tu bila kujaribu kutafuta ufumbuzi sio busara sana. Na baadhi yetu tulipomsikia Lowassa akisema, namnukuu "Serikali imesema haitoi chakula, mimi nimejadiliana na chama changu tumeona tufanye mpango wa kuwatafutia chakula Watanzania.”

Hicho chakula kiko wapi? Kuwapa wananchi matumaini kisha kutotekeleza ahadi husika ni hadaa. Lakini kuna wanaoshangaa eti "mbona licha ya 'kiburi cha serikali ya CCM kuhusu tishio la njaa' badi chama hicho kimeibuka kidedea kwenye chaguzi za madiwani?"

Jibu jepesi ni kwamba CCM "is the devil they know," kwamba pamoja na mapungufu yake, inaweza kutoa mifano hai ya ilivyowahi kuwasaidia wananchi siku za nyuma. Na hata kama inafanya 'kiburi' kuhusu tishio la njaa, angalau "haijatoa ahadi hewa" kama hiyo ya Bwana Lowassa.

Hebu pata picha: siku chache kabla ya chaguzi hizo, CCM 'yajipiga bao yenyewe' kwa kushikilia msimamo kuwa hakuna njaa na hata ikiwepo hakutokuwa na chakula cha msaada. Chadema kwa kushushiwa bahati hiyo, wanachangamka, wanakusanya misaada ya chakula, na kufanya harambee ya kuwasaidia watu wenye uhaba wa chakula. Naam, pengine serikali ingetaka kuingilia, lakini ninaamini nguvu ya umma ingekuwa upande mmoja na Chadema katika dhamira yao hiyo nzuri. Kwa bahati mbaya imebaki kuwa nzuri tu, na haijatekelezwa.

Kutekelezwa kwa ahadi hiyo kungeweza kutafsiriwa na CCM kama rushwa kwa wapigakura lakini mwenye njaa anachojali ni mkono kwenda kinywani na wala sio amepewa chakula kama msaada au rushwa. Ninaamini kabisa kuwa laiti ahadi ya Lowassa na Chadema yake kuhusu kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na baa la njaa ingetimizwa, basi pengine muda huu chama hicho kingekuwa kinachelekea ushindi.

Tukiweka kando suala hilo, ndugu zangu wa Upinzani, hususan Chadema wameendelea kuwa na imani fyongo kuwa "CCM inachukiwa mno," na "chuki hiyo dhidi ya CCM itapelekea kura kwa Wapinzani." Wanachopuuza ndugu zangu hawa ni ukweli kwamba udhaifu wa CCM sio uimara wa Upinzani. 

Ikumbukwe kuwa wakati CCM inaweza kusubiri hadi mwaka 2020 ili ianze kampeni za kubaki madarakani, Wapinzani wanapaswa kutumia muda huu kuwaonyesha Watanzania kuwa wao wanaweza kuwa mbadala wa kweli wa CCM. Lakini tunachoshuhudia ni Upinzani kuwa 'bize zaidi' kuiongelea CCM badala ya kutenda vitu vitakavyowapa matumaini Watanzania kuwa vyama hivyo ni mbadala sawia.

Ndugu zangu wa Chadema wana mtihani mkubwa zaidi. Pengo lililoachwa na Dokta Slaa limeshindwa kuzibika. Katibu Mkuu aliyepo madarakani anaweza kukisaidia sana chama hicho akiamua kuachia ngazi kwa hiari yake mwenyewe. Ninaamini mtu kama Godlisten Malisa, kada mwenye uwezo mkubwa, anaweza kushika wadhifa huo na akaibadili Chadema. 

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa chama hicho Bwana Freeman Mbowe, yupo kwenye wakati mgumu mno pengine kuliko muda wowote ule wa maisha yake ya kisiasa. Mbowe anaandamwa na madeni yanayoweza kuathiri mno biashara zake. Japo deni sio jinai, kiongozi wa upinzani kuandamwa na madeni au kutolipa kodi kwa miaka kadhaa ni kitu kinachotoa taswira mbaya kwa wananchi.

Kuna lawama kadhaa zinazorushwa kwa Rais Magufuli kuwa anazitumia taasisi za serikali kama  vile TRA na NHC "kumwandama" Mbowe, lakini ukweli ni kwamba dawa ya deni ni kulipa. Na Chadema inaweza kuingia matatani ikitetea "ukwepaji kodi wa Mbowe" kwa sababu sote twajua kuwa hilo ni kosa (japo si la jinai).

Halafu kuna hizi 'drama' zinazoweza kuwavunja moyo watu wasio na chama lakini wanatafuta chama cha kukiunga mkono. Suala la 'kupotea' kwa kada wa Chadema, Ben Saanane, limeacha doa kubwa kwa chama hicho. Kwa upande mmoja, ilichukua wiki tatu tangu kada huyo adaiwe kupotea kabla ya uongozi wa chama hicho kutoa tamko rasmi. Lawama zaidi zaweza kwenda kwa Mbowe kwa vile Ben alikuwa msaidizi wake binafsi. 

Na Chadema walipotoa tamko rasmi kukfuatiwa na mkanganyiko mkubwa zaidi: huku Mbowe anadai Ben katekwa, kule Tundu Lissu anadai vyombo vya dola vinajua kada huyo yuko wapi, na pale, gazeti la Mwanahalisi la mbunge wa chama hicho Saed Kubenea likaeleza kuwa "Ben yupo, amekuwa akionekana kwenye vijiwe vya chama hicho." Na baada ya jithada fupi mtandaoni zilizoambatana na alama ya reli #BringBenBackAlive na kuchapishwa fulana, suala hilo limekufa kifo cha asili. Huu ni uhuni wa kisiasa maana hatutegemea chama makini kinachojitanabaisha kuwa mbadala wa CCM kuendesha mambo yake kienyeji hivyo.

Kuna tatizo jingine ambalo Chadema wamekataa katakata kulishughulikia. Kabla ya kumpokea Lowassa, ajenda kuu ya Chadema ilikuwa vita dhidi ya ufisadi. Ujio wa Waziri Mkuu huyo wa zamani ulikilazimisha chama hicho kuachana na ajenda hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa sana ndio iliyokiwezesha chama hicho kuwa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Na kwa vile Rais Magufuli amejaribu kuifanya vita dhidi ya ufisadi kuwa moja ya ajenda zake kuu, Chadema kwa muda huu haina ajenda kuu yenye mvuto kwa wananchi. Chama hicho kimegeuka kuwa cha kusubiri matukio kisha kuyadandia. Sawa, ni kazi ya vyama vya upinzani kukikosoa chama tawala/kuikosoa serikali, lakini hiyo sio kazi pekee. Na kwa kusubiri matukio, Chadema inakuwa kama "inaendeshwa na CCM."

Niliandika kwa kirefu katika vitabu vyangu viwili kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kimoja kabla ya uchaguzi huo na kingine baada, kwamba asilimia kubwa ya wapigakura nchini Tanzania sio wanachama wa CCM au vyama vya upinzani. Kwamba mtaji  mkubwa kwa chama chochote kinachotaka kushinda uchaguzi ni ku-win hearts and minds za hao wasio na chama chochote. Kundi hili ndilo lililompa ushindi Magufuli mwaka 2015.

Katika hilo, tatizo kubwa la vyama vyetu vya upinzani ni 'kudanganganyana wao kwa wao kuhusu mshikamano, umoja na wingi wao.' Badala ya kufanya jtihada za ku-reach out kudni la watu wasio na vyama, wao wapo bize kuhamasishana wenyewe kwa wenyewe. Basi angalau kuhamasishana huko kungeendana na kuwavuta watu wasio na vyama, ambao ni turufu muhimu kwenye chaguzi zetu.

Nilwahi kuandika huko Facebook, kuwa 'hasira sio mkakati (wa kisiasa)' kwa kimombo "anger is not a strategy.' Sio siri kuwa wafuasi wa upinzani wana hasira, ni hii sio dhambi wala kosa, lakini wanakosea kudhani kuwa hasira hiyo itawaletea mafaniko ya kisiasa. Hawataki kujifunza kwenye mifano hai ya hasira ambazo zimebaki kuwa hasira tu: hasira dhidi ya Tanesko zimeshindwa kuifanya taasisi hiyo iache uhuni wa mgao wa umeme wa milele; hasira dhidi ya huduma mbovu zinazotolewa na baadhi ya makampuni ya simu hazijaziathiri kwa namna yoyote ile; hasira dhidi ya TFF haijaweza kuifanya Taifa Stars iache kuwa kichwa cha mwendawazimu.

Hasira ili iwe na manufaa shurti iambatane na programu makini ya kuleta mabadiliko kusudiwa. Na hili liliusiwa na Dkt Slaa, kwamba mabadiliko ya kweli yatapatikana tu kwa kuwa na programu makini zitakazohusisha watu makini.

Pengine wapinzani watajitetea kuwa zuio la Dkt Magufuli linalokataza mikutano na maandamano ya vyama vya siasa (isipokuwa CCM) limewaathiri kwa kiasi kikubwa katika kujitengenezes mazingira bora ya ushindi kwenye chaguzi hizo. Mie siafikia kabisa zuio hilo la Rasi Magufuli, lakini wapinzani wangeweza kulitumia 'kumpiga bao yeye na CCM' kwa kulitekeleza kwa kuelekeza nguvu zao 'mtaani,' kuwatumikia wananchi zaidi ya 'wanavyoangushwa na CCM/Serikali.'

Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kwa vyama vya upinzani kukaa chini na kufanya post-mortem ya chaguzi za madiwani, na kutengeneza programu makini (sio hizo operesheni zisizo na kichwa wala miguu) zitakazosimamiwa na kutekelezwa na watu makini. Na wafuasi wa vyama hivyo waache kupoteza muda mwingi kwenye kukosoa tu CCM na serikali huku wakikwepa kuelekea focus yao kwenye vyama vyao. Ni hivi, kama vyama vya upinzani vimeweza kumng'oa moja wa madikteta hatari duniani huko Gambia, Yahya Jammeh, basi hakuna sehemu ambapo upinzani hauwezi kukiong'oa chama tawala madarakani. Lakini hilo halitotokea kwa kujidanganya kuwa "CCM inachukiwa sana." Kuchukiwa kwa CCM sio kupendwa kwa Chadema, au Cuf, au chama kingine cha upinzani. 

ANGALIZO: Mada husika ilikuwa kwa ajili ya makala kwenye gazeti la Raia Mwema lakini nimechukua mapumziko ya uandishi wa makala kwenye gazeti hilo wakati nikisubiri marekebisho flani kutoka kwao.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.