19 Jan 2017

WAKATI Marekani ikijiandaa kwa sherehe ya kuapishwa kwa Rais Mteule Donald Trump hapo keshokutwa, rais huyo mteule amejikuta kwenye ‘kitimoto’ baada ya kumshambulia mjumbe wa Congress (bunge ‘dogo’ la nchi hiyo),mmoja wa wanasiasa wakongwe na mpinzani wa muda mrefu wa ubaguzi wa rangi, John Lewis.
Kama ilivyozoeleka, Trump alitumia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter kufanya mashambulizi hayo baada ya Lewis, ambaye anaheshimika mno nchini humo kwa kushirikiana na nguli wa haki za watu weusi, marehemu Dk. Martin Luther King, Junior, kueleza bayana kuwa hamwoni Trump kama rais halali wa Marekani. Pia alieleza kuwa itakuwa sio sahihi kukalia kimya ‘mambo yasiyopendeza’ ya Trump.
Kadhalika, Lewis alieleza bayana kuwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 hatohudhuria sherehe za kumwapisha rais mpya, na anasusia kuapishwa kwa Trump kama njia ya kuonyesha upinzani wake kwa rais huyo mpya.
Trump alimshambulia Lewis katika ‘tweets’ zake ambapo alidai kuwa mwana Congress huyo anapaswa kutumia muda mwingi zaidi kushughulikia eneo analoliwakilisha, ambalo kwa mujibu wa Trump, lipo katika hali mbaya na limegubikwa na uhalifu.
Tweets za Trump dhidi ya Lewis zilizosababisha watumiaji kadhaa wa mtandao huo wa kijamii kumlaani rais huyo mtarajiwa, hasa kwa vile wikiendi iliyopita ilikuwa ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Dk. King, siku yenye umuhimu mkubwa kwa Wamarekani weusi.
Hayo yamejiri siku chache tu baada ya Trump kuwa katika ‘vita kubwa ya maneno’ dhidi ya ‘jumuiya ya ushushushu’ (intelligence community), taasisi 16 za ushushushu za nchi hiyo. Sababu kuu ya ‘ugomvi’ kati ya Trump na mashushushu hao ni taarifa iliyowasilishwa kwa Rais Barack Obama, na Trump mwenyewe, kuhusu hujuma za Urusi kwenye uchaguzi mkuu uliopita nchini Marekani.
Taarifa hivyo, ilitanabaisha kuwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin ndiye aliyetoa maagizo ya ‘kumsaidia Trump’ na ‘kumuumbua Hillary Cinton, aliyekuwa mpinzani mkuu wa Trump.
Lengo la makala hii sio kujadili siasa za Marekani au vituko vya Trump, bali kutumia matukio hayo kuelezea hali ilivyo sasa huko nyumbani – Tanzania, ambapo kwa kiasi kikubwa suala la uwepo au kutokuwepo kwa baa la njaa linazidi kutawala duru za habari.
Kuna masuala kadhaa yanatokea kwa wakati mmoja. Kubwa zaidi ni kauli ya Rais Dk. John Magufuli sio tu kukanusha taarifa za uwepo wa baa la njaa bali pia kusisitiza kuwa ‘serikali haina shamba’ la kuiwezesha kuwapatia chakula wananchi wanaolalamikia njaa.
Jingine ni tishio kali kutoka kwa Rais Magufuli dhidi ya ‘magazeti mawili’ aliyodai yanaandika habari za uchochezi. Pia aliyashutumu kuwa yamenunuliwa na mfanyabiashara mmoja wa nafaka ili yaandike kuhusu taarifa za uwepo wa baa la njaa, kwa minajili ya mfanyabiashara huyo kuuza nafaka zake.
Binafsi sijashangazwa na tishio la Rais kwa magazeti. Uamuzi wake wa kukaa mwaka mzima bila kuongea na wanahabari ulipaswa kutufahamisha mtazamo wake kwa vyombo vya habari. Ikumbukwe kuwa hata wakati wa kampeni zake za urais mwaka 2015 hakufanya mahojiano na vyombo vingine vya habari, pengine ni kwa bahati tu, alifanya mahojiano na gazeti hili la Raia Mwema tu.
Na hii si mara ya kwanza kwa Rais kuvitupia lawama vyombo vya habari, wiki chache zilizopita alivishutumu kwa kumchonganisha na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Japo haikuwekwa wazi, lawama hizo zilitokana na habari zilizoandikwa na baadhi ya magazeti kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa na mpango wa kupiga mnada mizigo ya taasisi ya WAMA iliyo chini ya mama Salma Kikwete. Kusema magazeti yalizusha habari hiyo ni kuyaonea kwa sababu chanzo cha habari kilikuwa taasisi ya serikali, TRA.
Binafsi nabaki najiuliza, hivi kweli kama kuna magazeti yanalipwa kufanya uchochezi, yangekuwepo huru hadi kufikia hatua ya Rais ‘kuyananga’ bila kuyataja jina? Je, Idara Habari (MAELEZO) na wizara yenye dhamana ya vyombo vya habari, na waziri husika (Nape Nnauye) wamelala usingizi mzito kutojua hayo hadi Rais aliposhtuka na kuweka suala hilo hadharani?
Kwa mtazamo wangu, nadhani tishio la Rais limelenga kutisha vyombo vyote vya habari na sio magazeti hayo mawili tu. Kwamba wanahabari wasiandike kitu kisichompendeza Rais.
Rais hataki kusikia habari kuhusu tishio la baa la njaa. Hata wito wa viongozi wa kidini Wakristo na Waislam kuwataka waumini wao wafanye sala/dua kuombea mvua na kuepushwa na baa la njaa haujamfanya Rais kubadili msimamo wake.
Na muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii nimeona video ya mkutano wa Rais huko Magu, ambapo wakati akihutubia, baadhi ya wananchi walisikika wakisema “njaa baba,” na Rais akawajibu “njaa… unataka nikakupikie mimi chakula?”
Binafsi sidhani kama Rais anahitaji ‘kisingizio’ cha kufungia magazeti, yawe mawili au yote. Lakini pia Rais asiwe mkosefu wa shukrani kwa mchango wa magazeti katika kumfikisha Ikulu, kwa kufikisha ujumbe wake binafsi na chama chake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Lakini ni muhimu pia Rais atambue kuwa hizi sio zama za Radio Tanzania, Uhuru na Mzalendo, na Daily News na Sunday News pekee. Huu ni mwaka 2017, tupo katika zama za digitali ambapo upashanaji wa habari una njia lukuki, kuanzia Whatsapp hadi mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook, Instagram, nk. Katika zama hizi, kufungia chombo cha habari hakuzui usambazaji wa habari muhimu miongoni mwa wananchi.
Nihitimishe makala hii kwa wito huu kwa Rais wangu, mara kadhaa amekuwa akituomba sisi wananchi tumsaidie katika uongozi wake. Na moja ya misaada ambayo watu wengi wamekuwa wakimpatia ni kumsihi apunguze ukali, ajaribu kutumia lugha ya kidiplomasia, na asiogope kukosolewa.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.