Africa Confidential Toleo la 28 Machi 2018
27 Machi 2018
Hatua
za kidikteta za Magufuli zinakumbana na upinzani unaoongezeka lakini ndio
Ameshika uelekeo huo na anatishia wanaomkosoa
Katikati
ya muhula wake wa kwanza, Rais John Magufuli anakabiliwa na shinikizo. Huku
akikabiliwa na tishio kubwa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
vikundi vya kiraia, viongozi wa kanisa, na sasa vijana kwenye mitandao ya
kijamii, anaonekana kufurahia mapambano hayo. Dola pia inatishiwa na makundi
yenye silaha yaliyokuwa viongozi wa serikali na chama mkoani Pwani (MKIRU).
Majibu ya serikali kukabiliana na changamoto hizo yametawaliwa na ukatili ambao
haujawahi kuonekana kamwe, na kupelekea kulaaniwa kutoka kila upande.
Kuongezeka
kwa vurugu za kisiasa, hasa wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni,
kulipelekea lawama dhidi ya utawala wa mabavu wa Magufuli. Ubalozi wa Marekani
ulitaka kufanyike uchunguzi kuhusu utekaji na mauaji ya kiongozi wa upinzani
jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni. Umoja wa Ulaya baadaye ulionyesha
wasiwasi wake kuhusu "mwenendo wa hivi karibuni unaotishia kanuni za
demokrasia" baada ya polisi kutumia risasi katika maandamano ya Chadema
katika mkesha wa siku ya kupiga kura Februari 17, hali iliyopelekea majeruhi
watatu na kuuawa kwa mpita njia.
Wiki
mbili baada ya matamko hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ilijibu kwa taarifa yenye
kurasa tatu na nusu ikiyahusisha matukio ya huko MKIRU na "vikundi vya
ndani na nje ya nchi vinavyochukizwa na jitihada za Magufuli kuondoa ufisadi,
biashara ya mihadarati, ujangili, ukwepaji kodi na kujenga uwajibikaji."
Vikundi
hivyo vyenye silaha, ambapo baadhi vinadaiwa kuwa na mahusiano na Al-Shabaab ya
Somalia, vimewauwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na baadhi ya watendaji wa
serikali. Tatizo hilo lilianza tangu mwaka 2014 lakini likafikia kilele mwaka
2017 baada ya operesheni ya kikatili ya vyombo vya dola kushambulia. Serikali
inajaribu kuushawishi umma kwamba maandamano ya amani dhidi ya haki za kiraia
na mauaji hayo ya MKIRU ni pande mbili za kitu kimoja. Ni watu wachache tu
wanaoshawishika kuamini.
Katika
ujumbe wao kwa msimu wa Kwaresma, maaskofu wa Katoliki walionya kwamba kuendelea
kwa ukandamizaji wa kisiasa kutapelekea migawanyiko itakayohatarisha misingi ya
kitaifa ya umoja na mshikamano. Walieleza kwamba kuzuwia shughuli za kisiasa
sio halali na kunakiuka katiba. Kituo ch Demokrasia (TCD), ambacho huvileta
pamoja vyama vya siasa kilitoa tamko la pamoja na viongozi wa Kikristo na
Kiislamu kudai mapitio ya Katiba. Hii ilifuatiwa na kauli ya kuunga mkono ya
vikundi zaidi ya 100 vya kiraia.
Jumapili
ya Majivu Machi 25 ilishuhudia maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (ELCT) wakitoa tamko kali wakiilaani utekaji watu, utesaji watu,
upoteaji watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya wanasiasa, mauaji yanayotokana
na itikadi za kisiasa, vitisho, kesi za kubambikizwa, na unyanyaswaji wa raia
unaofanywa na vyombo vya dola. Pia walitaka katiba mpya iwepo kabla ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2020. "Taifa huongozwa na katiba ambayo ndio msingi wa
sheria zote", walisema. "Haiongozwi na ilani za vyama."
Pia
kuna changamoto za kisheria. Mahakama Kuu inatarajiwa kusikia kesi mbili za
kikatiba zilizoletwa na watetezi wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Chama
cha Wanasheria TLS, Umoja wa Watetezi wa Haki za Binadamu (the Tanzania Human
Rights Defenders Coalition), na Taasisi ya sheria na haki za binadamu (the
Legal and Human Rights Centre). Kesi zote zinaongozwa na Fatma Karume wa
kampuni ya uwakili ya IMMA, ambayo ofisi zake zilichomwa moto Agosti mwaka
jana. Akiwa anatoka kwenye familia yenye nguvu ya Karume, amekuwa mwiba kwa
utawala uliopo madarakani. TLS inaongizwa na mmoja wa wateja wake, kiongozi wa
Chadema Tundu Lissu, ambaye bado yupo Ubelgiji anakopata matibabu ya majeraha
ya risasi kufuatia jaribio la kumuuwa.
Kumekuwa
na ukosoaji ndani ya CCM pia. Nape Nnauye, mbunge aliyetimuliwa uwaziri mwaka jana,
ametoa wito wa kuifanyia marekebisho Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) akieleza
"kwa macho makavu" kuwa kama ambavyo taasisi hiyo imekuwa ikifanya
kazi kwa manufaa ya dola, pia imekuwa ikiitumikia CCM, inaendeshwa kisiasa.
Mbunge
mwingine wa CCM, Hussein Bashe, ambaye awali hakufahamika kuwa na mtazamo huru,
na aliongoza kampeni ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwania urais,
naye ametokea kuwa mtetezi wa uhuru wa kujieleza na mawazo mbadala.
Haya
na matamko mengine yanaashiria demokrasia ya Tanzania ipo katika kipindi
kigumu. Akiongea kwenye shughuli ya TCD ambayo ilipelekea wito wa katiba mpya,
Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kilutheri alitanabaisha kuwa kamwe hajawahi
kuona polisi wakitumia risasi dhidi ya waandamanaji. "Nini
kimebadilika?" aliulizwa.
Moja
ya majibu kwa swali lake hilo ni "hakuna kikubwa (kilichobadilika)." Kunapokuwa
na upinzani mkali kwenye chaguzi zilizopita, dola na chama tawala vimekuwa
vikikimbilia kwenye ukatili. Kufanya vema kwa Chadema katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010 kulipelekea angalau miaka miwili ya ukatili. Ilianza Januari 2011
ambapo polisi walitumia risasi dhidi ya maandamano ya wafuasi wa Chadema
Arusha.
Februari
2012, wanaharakati 16 wa haki za binadamu walikamatwa kwa kuunga mkono mgomo wa
madaktari. Agosti mwaka huohuo, polisi walimuua kwa risasi muuza magazeti huko
Morogoro wakati wa maandamano ya Chadema. Mwezi uliofuata, mwandishi wa habari
Daudi Mwangosi aliuawa na polisi kufuatia kupigwa na bomu la kutoa machozi huku
akiwa amekandamizwa chini na polisi. Katika mwezi huohuo, kiongozi wa
maandamano ya madaktari, Steven Ulimboka alitekwa, akateswa na kuachwa ajifie
mwenyewe kwenye msitu nje ya jiji la Dar es Salaam, tukio linalodhaniwa kufanywa
na maafisa wa TISS. Baadaye mwaka huo huo, na pia Mei 2013, njia za kikatili zilitumika
kukabiliana na maandamano yaliyoambana na wimbi kubwa la machafuko katika
historia ya Tanzania.
CCM
inakabiliwa na changamoto kubwa kudumisha utawala wake. Kwa kutoongelea suala
la ufisadi mkubwa (katika kampeni zake za uchaguzi mkuu wa) mwaka 2015, ilitoa
fursa kwa Chadema kupata mafanikio (ya kuridhisha) katika uchaguzi huo. Wimbo
la ukandamizaji linaloendelea hivi sasa, linailenga Chadema, na pia
linachangiwa na hofu kuhusu vikundi vyenye msimamo mkali vyenye silaha (kama
ilivyokuwa huko MKIRU).
Sintofahaumu
hiyo inaweza kueleza ukatili mkubwa uliotumika kukabiliana na kilichokuwa kikijiri
katika mkoa wa Pwani. Miili kadhaa iliyofungwa kwenye 'viroba' iliyokutwa
inaelea maeneo ya (Msasani) Peninsula jijini Dar es Salaam inaashiria jinsi
hali ilivyokuwa.
Wizara
ya Mambo ya Nje ilitoa tamko masaa tu baada ya tovuti ya African Arguments ya
Royal African Society kuchapisha habari iliyoeleza kuhusu matumizi ya silaha za
moto dhidi ya waandamanaji huko wilayani Rufiji katika ofisi za halmashauri ya
mji.
Kwa
kuunganisha vitendo vya vikundi hivyo vilivyokuwa vinavyotumia silaha (huko
MKIRU) na upinzani dhidi ya mageuzi yanayofanywa na Magufuli, inatoa kisingizio
kwa dola kutumia nguvu dhidi ya makundi yote mawili (vikundi vya MKIRU na
upinzani dhidi ya Magufuli).
Mkuu
wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo aliwataka Watanzania kuwa wazalendo dhidi ya
tishio kwa amani, umoja, uhuru na mshikamano. Kichekesho ni kwamba aliyasema
hayo katika maadhimisho ya viongozi waliopambana na utawala wa mkoloni mwaka
1907 katika Vita ya Maji Maji. Jinsi dola inavyopambana na vurugu na upinzani inarejesha
kumbukumbu za jinsi serikali ya mkoloni ilivyopambana na upinzani dhidi yake.
Mafanikio
yoyote ya kuelezea kuhusu tishio linaloukabili demokrasia nchini Tanzania yatategemea
zaidi makundi mbalimbali ndani ya CCM na tabaka tawala. Wanaoonekana kama
wapinzani ndani ya CCM kama Nape na Bashe watabaki ndani ya chama hicho kwa
gharama yoyote, wakicheza mchezo mrefu wa subira hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025
ambapo inatarajiwa Magufuli atamaliza muda wake.
Viongozi
wa dini – Magufuli anajitambulisha kama Mkatoliki mcha Mungu – wanaweza kufanikiwa
kumshawishi kupunguza matumizi ya vyombo vya dola dhidi ya upinzani. Lakini
wanaharakati na wanasiasa wa upinzani wanafahamu fika kuwa kudhibitiwa kwa
asilimia 100.
MHALAKI (SOCIALITE) AONGOZA MAPAMBANO KUPITIA MTANDAO
WA KIJAMII WA INSTAGRAM
Mashtaka
yanayofunguliwa na taasisi za kiraia na matamko ya viongozi wa dini ni kitu
kimoja, lakini wito wa kufanyika maandamano unaotolewa na bloga mwenye makazi
yake Los Angeles (Marekani), Mange Kimambi, ni changamoto tofauti kabisa kwa
Magufuli. Kimambi amekuwa sura ya hadharani ya wito wa maandamano ya nchi nzima
tarehe 26 Aprili dhidi ya Magufuli.
Akifahamika
zaidi kwa masuala ya fasheni na habari zinazohusu watu maarufu, akaunti ya Instagram
ya Kimambi imekuwa ikihamasisha na kuyapa umaarufu maandamano hayo,
yanayotarajiwa kufanyika siku ya Muungano, ambayo ni kumbukumbu ya Muungano
kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Kimambi
anayedhaniwa kuwa anashirikiana na wanaharakati nchini Tanzania, anachukuliwa
kwa uzito mkubwa na mamlaka za nchi hiyo. Akiongea kwenye tukio moja Machi 9
kijijini kwake Chato, Magufuli alisema "tusubiri na tuone wakiandamana, na
watanitambua." Siku chache kabla, Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba
aliwatuhumu waandaaji wa maandamano hayo kuwa wanapanga kuuwa watu na kisha
kuvitupia lawama vyombo vya dola. Maonyo mengine yametolewa na angalau makamanda
wa polisi wa mikoa saba. Inafahamika kuwa viongozi wa serikali na chama
(tawala) wameelekezwa kuhamasisha upinzani dhidi ya maandamano hayo na tayari
watu kadhaa wameshakamatwa.
Kimambi
ni mwanaharakati ambaye haingekuwa rahisi zamani kumtarajia. Alipata umaarufu
mwaka 2009 kupitia blogu yake ya 'U-Turn' ambayo ilikuwa ikisimulia kuhusu
maisha yake kama mhalaki huko Dubai. Baadaye alihamia katika makazi yake ya
sasa, Los Angeles, kabla ya kuanza kuiteka Instagram mwaka 2015, ambapo alimpigia
Magufuli kampeni yenye ufanisi, licha ya yeye kushindwa kuteuliwa kugombea
ubunge jimbo la Kinondoni.
Alimgeuka
Magufuli takriban Mei 2016 ambapo alipinga vikali kusitishwa kwa matangazo ya
moja kwa moja ya vikao vya bunge. Anachanganya upinzani wa kisiasa na nguvu yake
kama mhalaki anayeweza kumjenga au kumbomoa mtu kwa kutumia mitandao ya
kijamii. Awali ilikuwa kuhusu picha zake binafsi na "selfies" lakini
baadaye mabadiliko yakajitokeza. Kufikia mwishoni mwa mwaka 2016, akaunti yake
ikawa sehemu kuu ya harakati za mtandaoni za upinzani dhidi ya serikali, na sehemu
ya kuona nyaraka mbalimbali zilizovuja.
Akaunti
yake imechukua nafasi ya Jamii Forums, jukwaa la maoni mtandaoni lililokuwa
kitovu cha upinzani mtandaoni, na ambalo waanzilishi wake wanakabiliwa na kesi
mahakamani na wamekuwa wakisumbuliwa na mamlaka kwa muda mrefu.
Huku
akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 1.4* kwenye Instagram, uwezo wa Kimambi
kuwafikia watu unawazidi wanasiasa wote wa Tanzania, japo kuna shaka kuhusu
maandamano ya April 26. Kujitokeza kwa watu wengi kwenye maandamano hayo
kutategemea uwezo wa waandaaji wake wa maandamano hayo nchini Tanzania, ambao wanaokabiliana
na utawala usio na huruma – polisi watamwaga risasi kwa ajili ya kuuwa, kama ambavyo
wamefanya huko nyuma.
Haitojalisha
hata kama hakuna mtu atayejitokeza kuandamana Aprili 26. Kutoka umbali wa
kilomita 26,000, Kimambi tayari ameweza kufanya zaidi ya kutikisa mkia wa chui
kwa kutumia simu ya mkononi tu. Na laiti ikitokea asalimisha yeye mwenyewe, mara
moja kukamatwa kwake kutakuwa tukio kubwa kabisa litakaloiweka Tanzania kwenye
macho na masikio ya dunia nzima.
MAELEZO
YANGU: Makala hii ni tafsiri ya neno kwa neno ya makala ya gazeti maarufu la duniani
la habari za kuchunguza kuhusu bara la Afrika la AFRICA CONFIDENTIAL Toleo laMachi 28, 2018 lililokuwa na kichwa cha habari "Enemies Without And Within."
Nimejitahidi
kadri nilivyoweza kufanya tafsiri ya karibu kabisa kutoka Kiingereza kwenda
Kiswahili. Ni vigumu kufanya tafsiri timilifu kwa asilimia 100 hasa pale
mwandishi na mtafsiri ni watu wanaoongea lugha mbili tofauti. Ni rahisi kwa mtu
aliyeandika mwenyewe kufanya tafsiri ya alichoandika kuliko kazi hiyo kufanywa
na mtu mwingine.
*
Idadi ya "followers" kwenye akaunti ya Mange kwa sasa ni watu milioni
1.8.