2 Mar 2017


MWAKA 1990 nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kuliibuka mgomo mkubwa uliodumu kwa siku kadhaa. Kwangu, mgomo huo ulikuwa ni mtihani mkubwa, kwani sikuwa ‘mwanafunzi’ wa kawaida, bali nilikuwa kamanda wa wanafunzi au chifu.
Shule hiyo, pamoja na Sekondari ya Wasichana Tabora, zilikuwa shule pekee nchini zilizokuwa na mchepuo wa kijeshi. Hata sare zetu zilikuwa ‘magwanda,’ na baadhi ya walimu wetu wakiwa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Huo wadhifa wa kuwa chifu ulikuwa ni ukiranja mkuu. Kwa hiyo mgomo huo ulitokea wakati nikiwa kiranja mkuu katika shule hiyo yenye historia ya kipekee. Chanzo kikuu cha mgomo huo kilikuwa madai ya wanafunzi kuwa chakula kilikuwa duni.
Nimesema kuwa mgomo huo ulikuwa mtihani kwangu kwa sababu kwa upande mmoja nilikuwa mwanafunzi kama wenzangu waliogoma, na upande mwingine, nilikuwa sehemu ya uongozi wa shule hiyo. Na kwa hakika, nilikuwa kiungo kati ya utawala na wanafunzi.
Hatimaye mgomo huo ulimalizika na kwa vile sikuwa nimeelemea upande wowote wakati wa mgomo huo, kumalizika kwake kuliniacha nikiwa ‘sijauudhi’ upande wowote – wa utawala wa shule na wa wanafunzi wenzangu. Na nyenzo yangu muhimu ilikuwa kusimamia kwenye kanuni na sheria, sambamba na kushawishi matumizi ya busara ili kufikia mwafaka. Mara nyingi huwa vigumu kuziridhisha pande zote za mgogoro husika.
Nimelikumbuka tukio hilo muhimu baada ya kutupia jicho baadhi ya mambo yanayoendelea kwenye Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli. Ni kwamba, kwa kiasi kikubwa, baadhi ya mawaziri wameonyesha bayana kuwa aidha hawaendani na kasi ya Dk. Magufuli au wanamhujumu kwa makusudi.
Baadhi yetu tunaofuatilia siasa za Tanzania tulikwishahisi mapema kuwa uamuzi wa Dk. Magufuli kuzileta baadhi ya sura zile zile ambazo zilikuwa mzigo kwa taifa huko nyuma, ungeweza kusababisha matatizo mbele ya safari.
Kwa kurejea tukio la mgomo nililolielezea hapo juu, Rais anajikuta kwenye ‘mtihani’ kwa sababu kwa upande mmoja anapaswa kuwa upande wa watendaji wake aliowateua kwa umakini mkubwa (ndio maana ilichukua wiki kadhaa kabla Rais hajatangaza Baraza lake la Mawaziri) na kwa upande mwingine yeye sio rais wa mawaziri wake pekee bali Watanzania wote.
Sakata la vita dhidi ya dawa za kulevya lililoibuliwa upya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, limechangia kwa kiasi kikubwa kuonyesha kukosekana ‘visheni’ ya pamoja miongoni mwa mawaziri katika Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli.
Kwa mtazamo wangu, pengine ingekuwa vema kama Rais alipounda Baraza lake la Mawaziri angeepuka kuwaingiza makada wengi wa chama chake kwenye baraza hilo. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba chama hicho tawala kimeshika hatamu za uongozi wa taifa na ukada unawapa jeuri baadhi ya watendaji wa serikali. Na si kosa lao kwa sababu ukada umekuwa nyenzo muhimu katika uongozi wa Tanzania huku baadhi ya wakosaji wakiepuka adhabu kwa vile tu ni makada muhimu.
Wakati wa sakata la dawa za kulevya lililoibuliwa na RC Makonda, angalau waziri mmoja alijitokeza waziwazi kupingana na uamuzi wa kutangaza majina ya watuhumiwa, akidai hatua hiyo ingeathiri chapa (brands) za wasanii waliotajwa katika orodha ya watumiaji au wauzaji wa dawa za kulevya.
Kanuni muhimu ya uongozi ni uwajibikaji wa pamoja, na pindi mtendaji mmoja akikosea, basi kuna fursa ya kuongea tofauti za kimtazamo faragha badala ya kuitisha mikutano na waandishi wa habari kuonyesha mpasuko.
Naomba ieleweke kuwa sio ninakemea uhuru wa kujieleza miongoni mwa watendaji wa serikali, ikiwa pamoja na mawaziri, lakini uhuru huo sharti uzingatie kanuni.
Hata tukiweka kando hali tata iliyotokana na sakata hilo la dawa za kulevya, haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za nchi yetu kutambua kuwa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli ni mzigo kwake. Ni mzigo kwa vile aidha hawaendani na kasi yake au wanafanya makusudi kwa minajili ya kumkwamisha.
Ndio maana, picha inayopatikana mtaani ni kwamba mara kadhaa ni mpaka rais aingilie kati ndio hiki au kile kifanyike. Swali linalojitokeza ni je, rais haoni hali hiyo? Je, washauri wake (kwa mfano ndugu zetu wa Idara ya Usalama wa Taifa) nao hawaoni hali hiyo?
Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Dk. Magufuli kuwa pengine imefika wakati mwafaka kufanya utumbuaji kwa watu baadhi ya aliowakabidhi dhamana ya uwaziri kwenye kabineti yake. Asipochukua hatua mapema, inaweza kugharimu urais wake.
Nitaendelea na makala hii wakati mwingine kujadili kile Waingereza wanaita ‘power struggles’ zinazoendelea ndani ya CCM na ambazo kwa kiasi fulani zinachangia utendaji duni wa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli (kwa maana ya utendaji duni kama mkakati wa makusudi).

Baruapepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @chahali

3 comments:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.