9 Mar 2017


KATIKA hitimisho la makala yangu katika safu hii wiki iliyopita niliahidi kuwaletea uchambuzi kuhusu mivutano ya kugombea madaraka (power struggles) ndani ya chama tawala CCM.Kwa bahati nzuri, kati ya makala hiyo na hii, kumejitokeza tukio ambalo linaweza kuhusishwa na mada hiyo ninayoiongelea katika makala hii.
Wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli alimteua Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.Uteuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti, na kuzua mjadala unaoendelea hadi wakati ninaandika makala hii.
Kwa upande mmoja, inaonekana kama kuna mwafaka wa kutosha kwamba Rais ametumia madaraka yake kikatiba kufanya uteuzi huo.
Kwa upande mwingine, pengine kutokana na ukweli kuwa hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais kumteua mke wa mtangulizi wake kuwa mbunge, kuna hisia za hapa na pale kwamba uteuzi huo hauleti picha nzuri.
Kwamba, labda kwa vile Salma alikwishakaa Ikulu kwa miaka 10 kama mke wa Rais basi pengine nafasi hiyo ya ubunge wa kuteuliwa ingeenda kwa mtu mwingine.
Hata hivyo, licha ya kuwa Rais ameshaeleza kwa nini alifanya uteuzi huo, ukweli unabaki kuwa Katiba inamruhusu kufanya hivyo, na Salma Kikwete kama Mtanzania mwingine ana haki ya kuteuliwa kushika wadhifa wowote ule bila kujali historia yake kama mke wa rais mstaafu.
Lakini licha ya kuruhusiwa na Katiba kufanya uteuzi, kwa sisi tunaofuatilia kwa karibu siasa za Tanzania, tunauona uteuzi huo kama wa kimkakati, kwa maana ya Dk. Magufuli kujipanga vyema kwa ajili ya mitihani miwili ya kisiasa inayomkabili:  uchaguzi mkuu wa CCM baadaye mwaka huu, na kubwa zaidi, kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Ni hivi, katika nchi zetu zinazoendeshwa kwa mazoea, ni dhahiri kuwa kiongozi wa aina ya Magufuli hawezi kuwa maarufu miongoni mwa waliozoea kuona mambo yakiendeshwa sio yanavyopaswa kuwa, au kwa njia sahihi, bali kwa mazoea, hata kama mazoea hayo yana matokeo hasi.
Viongozi wa aina ya Magufuli wanaominya mianya ya ulaji, wanaozuia safari za ‘matanuzi’ ughaibuni, na wanaojaribu kuwa upande wa wananchi wanyonge badala ya kuendelea kutetea masilahi ya tabaka tawala, hawawezi kuwa na marafiki wengi.
Na ukweli kuhusu Dk. Magufuli ni kwamba kwa muda mfupi aliokaa madarakani ametengeneza maadui wengi tu serikalini na ndani ya chama chake. Kwa serikalini, maadui hao sio tishio kwake kwa sababu mfumo wa utawala sio tu unamwezesha kuwadhibiti kirahisi maadui hao bali pia hata kufahamu dhamira zao ovu mapema.
Changamoto kubwa zaidi kwake ipo ndani ya chama chake. Sio siri kwamba CCM aliyoirithi Magufuli imekuwa, kwa muda mrefu, kichaka cha mafisadi, sehemu ambayo watu waliohitaji kinga dhidi ya mkono mrefu wa sheria walikimbilia huko. Hii haimaanishi kuwa CCM nzima imesheheni watu wa aina hiyo.
Kwa vile licha ya kuwa Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho tawala, Magufuli ni kama mgeni kwenye medani za uongozi wa juu wa chama hicho, maadui zake ndani ya chama wanaweza kutumia fursa walizonazo – kama vile ushawishi wao au kukubalika kwao – kumhujumu kiongozi huyo.
Lakini kama ilivyo serikalini, Magufuli ametengeneza maadui ndani ya chama chake kwa sababu ile ile ya kuanzisha zama mpya za kuachana na siasa za/uongozi wa mazoea.
Katika ngazi mbalimbali za uongozi wa chama hicho, kuna viongozi waliozoea kujiona kama wanaendesha kampuni binafsi, huku wakitumia fursa zao kufanya ufisadi. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kuiona alama ya jembe na nyundo kwenye bendera ya CCM ikigeuka kuwa umma na bunduki kuashiria ulaji.
Uadui mkubwa ni kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo, kuna jitihada za chinichini ndani ya chama hicho tawala kuangalia uwezekano wa kumfanya Magufuli awe rais wa awamu moja.
Angalau hadi muda huu hakuna dalili kuwa uchaguzi mkuu wa CCM unaweza kuwa na athari zozote katika uenyekiti wa Magufuli japo ni wazi maadui zake watatumia kujipanga kwa ajili ya kinyang’anyiro cha mwaka 2020.
Kwa kumteua Salma Kikwete, Magufuli amemleta karibu mtu muhimu katika siasa za CCM, na pengine kujenga ngome imara ya kumwezesha sio tu kushinda uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya CCM bali pia kumrahisishia kazi ngumu ya kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho tawala.
Nimalizie kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika makala zijazo
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.