1 Jan 2019

Image result for happy new year 2019

Heri ya mwaka mpya 2019.

Kila mwaka mpya, blogu hii huwaletea ubashiri kuhusu masuala mbalimbal yanayotarajiwa kutokea nchini Tanzania katika mwaka husika. 

Hata hivyo, ni muhimu kutanabaisha mapema kuwa ubashiri huu sio exact science. Unatokana tu na ufahamu mkubwa wa mwandishi kuhusu siasa za Tanzania sambamba na mwenendo wa mabo ulivyokuwa mwaka jana 2018.

Moja ya matukio yanayotarajia kutikisha Tanzania ni jaribio la kumpindua Rais Magufuli. Jaribio hilo ni mwendelezo wa lile lililoshindikana mwezi Novemba mwaka jana na mwandishi alikuwa mtu pekee aliyeliweka hadharani.

Iwapo jaribio hilo litafanikiwa au la ni nje ya uwezo wa blogu hii kubaini hilo, lakini wahusika ni kundi lilelile lililojaribu kumdhuru Magufuli Novemba mwaka jana, kundi linalohusisha baadhi ya viongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Haitokuwa jambo la kushangaza endapo baadhi ya wahusika "wakadhibitiwa mapema" japo blogu hii haiwezi kueleza kwa hakika "kudhibitiwa" huku kutahusisha hatua gani. 

Sambamba na hilo ni ubashiri wa mabadiliko makubwa ya uongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Tukiweka hilo kando, inabashiriwa kuwa uhusiano kati ya Tanzania na nchi wahisani/jumuiya za kimataifa utakuwa mbaya zaidi ya ilivyokuwa mwaka jana, japo hatimaye Magufuli atafyata mkia na kuwaangukia wahisani hao kufuatia hali mbaya ya fedha serikalini.

Kadhalika, sokomoko la korosho sio tu litaendelea kupelekea watendaji kadhaa wa serikali kupoteza madaraka - sio kutokana na kufeli kwao bali kufanywa mbuzi wa kafara - lakini pia litajitokeza kwenye mazao mengine/sekta nyingine pia. 

Hata hivyo kama ambavyo tayari serikali imeanza "kubadili gia angani" katika suala la korosho, huko kwenye mazao mengine/sekta nyingine nako hatimaye serikali itaufyata lakini sio kabla ya kusababisha mkanganyiko mkubwa.

Inabashiriwa kuwa "hama hama" ya wabunge na madiwani wa upinzani kwenda CCM itarejea kwa kasi kubwa, hatua itakayolenga zaidi kudhoofisha jitihada za wapinzani kushikamana na kupambana na Magufuli.

Inabashiriwa pia kuwa baadhi ya miradi mikubwa inayopigiwa chapuo na serikali ya Magufuli itakwama kutokana na hali mbaya ya kifedha. 

Kadhalika kuna uwezekano wa ATC kuanzisha safari za kimataifa lakini itakuwa kwa muda mfupi tu baada ya ndege kuzuiwa nje ya nchi kutokana na madeni ya serikali nje ya nchi.

Vilevile, inabashiriwa kuibuka upya na kushamiri kwa "kelele" za kutaka muhula wa urais uongezwe kutoka miaka mitano ya sasa hadi miaka saba au zaidi. 

Inabashiriwa pia kuwa muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa utapita licha ya upinzani mkali kutoka kwa vyama vya upinzani. 

Sambamba na tukio hilo ni uwezekano kwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na mbunge wake Esther Matiko kuhukumiwa kifungo katika kipindi cha vuguvugu la kupitishwa sheria hiyo kandamizi.

Kadhalika, inabashiriwa kuwa kunaweza kufanyika jaribio la kumdhuru Mbunge wa Chadema Tundu Lissu kabla hajarejea nyumbani baada ya kuwa nje ya nchi kitambo kwa matibabu kufuatia jaribio la kutaka kumuua. Inabashiriwa kuwa kutakuwa na jitihada za makusudi za kumzuwia mbunge huyo machachari kurudi nyumbani.

Inabashiriwa pia kuwa baadhi ya wanachama maarufu wa CCM watavuliwa uanachama katika jitihada za Magufuli kutunisha misuli yake katika uongozi wa chama hicho. Walengwa ni wana-CCM ambao majina yao yanatajwa kama potential candidates katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Maamuzi ya kiuendawazimu ya Wakuu wa Mikoa/Wilaya yataendelea kutawala mwaka huu, wahusika wakuu wakiwa walewale waliovuma kwa maamuzi ya hovyo mwaka jana.

Habari njema kwa Watanzania wengi ni anguko la Daudi Albert Bashite na mpambe wake Musiba. 

Habari nyingine njema ni jinsi utawala wa Magufuli sio tu utawaleta viongozi mbalimbali wa upinzani karibu zaidi lakini pia kuna uwezekano wa viongozi hao kupata ujasiri na kushawishi wafuasi wao kuingia mtaani kudai haki kwa nguvu.

Kwa upande mwingine, hali ya uchumi itazidi kuwa ngumu kutokana na sababu za ndani na nje ya nchi.Ndani ya nchi ni pamoja na ukweli kwamba serikali ya Magufuli imeingia mwaka huu 2019 ikiwa na hali mbaya kifedha japo kumekuwa na jitihada kubwa za kutoa takwimu feki kuashiria kuwa uchumi uko vizuri. Kwa nje ni uwezekano wa mtikisiko wa kiuchumi kama ule wa mwaka 2008 ambao utatikisa sekta ya fedha/uchumi kimataifa.

Mwisho, kuna uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi - halisi au la kutengenzwa. Halisi ni kutokana na tishio linaloendelea huko Msumbiji ambako sio tu kuna "magaidi" kutoka Tanzania wanaosumbua huko bali pia kuna vikosi vya JWTZ vinavyosaidiana na jeshi la nchi hiyo kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi nchi humo.

Uwezekano wa kutengenezwa tishio la ugaidi ni mbinu inayoweza kutumiwa katika kipindi ambapo serikali ya Magufuli itakuwa inaandamwa na suala linaloipelekesha.

Nimalizie makala hii kwa kutakia heria ya mwaka mpya 2019 na kusisitiza tena kuwa ubashiri huu sio exact science. 





0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.