Leo Machi 18, 2019 ni siku ambayo lazima iingie kwenye
vitabu vya kumbukumbu kwa sababu kuu tatu, ambazo zote zinamhusu mwanasiasa
mkongwe Seif Sharif Hamad na Chama cha Wananchi (CUF)
Sababu ya kwanza, leo ni siku ambayo mwanasiasa huyo, maarufu
kwa jina la Maalim Seif, "ametimuliwa" rasmi kutoka chama
alichoshiriki kukiasisi (CUF).
Kibaya zaidi, "kutimuliwa" huko kumekuwa na
baraka kisheria, baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa
mwenyekiti halali wa chama hicho.
Ikumbukwe tu Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti
kwa sababu anazozijua yeye kabla ya kuamua kurejea kwenye wadhifa huo "kwa
mabavu." Kwa bahati mbaya – au pengine makusudi – sheria na kanuni za CUF
zilikuwa zinatoa mwanya kwa Lipumba (au mwanasiasa mwingine yeyote yule)
kufanya "uhuni" kama huo.
Sababu ya pili, ni kwamba leo CUF imekabidhiwa rasmi
kwa Lipumba. Kisheria. Mahakama imetenda haki kwake kwa sababu japo alichofanya
ni uhuni, kisheria uhuni huo ulihalalishwa na CUF yenyewe.
Hili la Lipumba kukabidhiwa chama si jambo dogo. Kuna
mawili hapa. Moja, hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Lipumba kukijenga chama
hicho na hatimaye kukirejesha kwenye nafasi ya kuaminika kama "mbadala wa
CCM."
Lakini la pili, na hili ndilo ninahisi litatokea, ni
mwanzo wa mwisho wa CUF. Sio siri kuwa Lipumba amesaidiwa sana na CCM kuipora
CUF kutoka mikononi mwa Maalim Seif. CCM hawajafanya hayo kwa vile wanampenda
Lipumba.Hapana. Wanamtumia tu kumdhibiti Maalim Seif ambaye licha ya kila hujuma
zilizokuwa zikifanywa na CCM na taasisi zake, ameendelea kuwa mwanasiasa maarufu
zaidi kuliko wote katika siasa za Zanzibar.
Sasa, baada ya Lipumba kutumika "kummaliza Seif ndani
ya CUF," kuna uwezekano wa aina mbili tu. Wa kwanza ni kwa mwanasiasa huyo
msomi kukubali kuendelea kutumika kama kibaraka wa CCM huku CUF ikigeuka kuwa
CCM-B, na wa pili, ni kujaribu kusimama kama chama halisi cha upinzani na
hapohapo "kumwagiwa radhi na CCM" na hatimaye kupelekea kifo cha
chama hicho.
Uwezekano mkubwa zaidi ni huo wa kwanza - ukibaraka.
Kwamba CUF haitokufa. CUF itaendelea kushiriki chaguzi mbalimbali. CUF itajenga
taswira ya chama kamili cha upinzani. Lakini uwepo huo wa CUF hautokuwa kwa
manufaa ya chama hicho au siasa za upinzani bali kwa manufaa ya CCM.
Kuna kila dalili kuwa CCM itaisaidia CUF kujitanua
nchi nzima kwa sababu moja kuu: uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa mbovu
kuliko chaguzi zote zilizowahi kutokea Tanzania. Kuna uwezekano mkubwa tu kwa
baadhi ya vyama vikuu vya upinzani kutishia kususia uchaguzi huo. Na hapo ndipo
CUF ya Lipumba itakapotumika kuhalalisha "ushindi wa Magufuli/CCM."
CCM itaisaidia CUF kuweza kusimamisha wagombea takriban
kila jimbo kwa upande wa Tanzania Bara. Lakini pia CCM itaisaidia CUF kuendelea
kuwa chama imara cha upinzani huko Zanzibar, ambako uimara wake utasaidia
kugawa kura dhidi ya CCM na wagombea wake.
Hata hivyo, "laana ya kutumika" itaikumba
CUF baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kama isipoishia kusambaratika basi
itabaki "chama jina" kama TLP ya Mrema.
Kuhusu uamuzi wa Maalim Seif kuhamia ACT- Wazalendo,
japo hatua hiyo inaweza kuwashangaza baadhi ya watu, ukweli mchungu baada ya
Mahakama Kuu kuhalalisha "uhuni" wa Lipumba, sambamba na "uhuni"
wake mwingine majuzi ambapo "alijitangaza" kuwa Mwenyekiti kupitia
"uchaguzi mkuu hewa" ambao pia "ulimtimua Maalim Seif" kwa
kuteua mtu mwingine kushika wadhifa wa Katibu Mkuu.
Kwa kuzingatia muda mfupi uliosalia kabbla ya uchaguzi
mkuu wa mwakani, Maalim Seif kuendelea kutafuta haki yake mahakamani kungeweza
kumkuta akiwa bado kwenye korido za mahakama wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu
ujao. Ni vigumu mno kwa chama cha siasa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi
mkuu huku kikiwa kinakabiliwa na mpasuko katika uongozi wake wa juu.
Kwahiyo, kimkakati, uamuzi huo wa Maalim Seif
unaeleweka, na unaweza kuwa ni mbinu muhimu kwake kuendelea kuwa relevant
kisiasa.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa aina mbili kuhusu
mustakabali wa Maalim Seif na wa chama chake kipya cha ACT- Wazalendo.
Uwezekano wa kwanza ni kwa chama hicho kuibuka kuwa
tishio katika siasa za Tanzania. ACT – Wazalendo ni chama kizuri lakini ambacho
hakikui. Kimeendelea kuwa "chama cha mtu mmoja" chini ya uongozi wa
Zitto Kabwe. Kwa muda mwingine, chama hicho kimekuwa cha kiharakati zaidi
kuliko cha kisiasa.
Mapungufu hayo yanaweza kubadilika kwa njia kuu tatu.
Kwanza, Maalim Seif hajawahi kupata fursa nzuri ya kunadi mvuto wake kwenye
majukwaa ya siasa za Tanzania Bara. ACT-Wazalendo wanaweza kuwa Jukwaa muhimu
katika hilo.
Pili, Zitto hajawahi kupata jukwaa mwafaka kunadi mvuto
wake wa kisiasa huko Zanzibar. Kwa kuungana na Maalim Seif, hii inaweza kuwa
ndio fursa mwafaka kwake.
Tatu, ACT-Wazalendo kama chama inaweza kupata fursa
mwafaja kabisa ya kuwa chama cha kitaifa badala ya kuwa "chama cha
Kigoma."
Haya yote yatawezekana tu endapo kutakuwa na
"kujitoa mhanga" kati ya mwenyeji Zitto na mgeni Maalim Seif. Kwa
mara ya kwanza, Zitto atajikuta akiongoza chama ambacho ndani yake kuna
mwanasiasa maarufu zaidi yake. Naam, Maalim Seif ni mkongwe zaidi kisiasa
kuliko Zitto. Endapo Zitto "atajitoa mhanga" (make a sacrifice) na kukubali
"kumezwa" na umaarufu wa Maalim Seif, basi chama hicho kitakuwa na
fursa kubwa ya kupanuka zaidi na hata kuja kuwa chama kikuu cha upinzani katika
pande zote za Muungano.
Lakini endapo kutakuwa na mgongano wa ego kati ya
wanasiasa hao, basi mustakabali wa chama hicho utakuwa mashakani. Lakini
pengine uwezekano wa hili kutokea ni mdogo kutokana na ukweli kwamba suala la
Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo sio limetokea tu ghafla. Ni dhahiri kuwa
kulikuwa na majadiliano ya muda mrefu na yayumkinika kuhisi kwamba tofauti kati
ya wanasiasa hao wawili (Maalim Seif na Zitto) zilifanyiwa kazi wakati wa
majadiliano hayo.
Suala jingine ambalo linaweza kuijenga ACT-Wazalendo
"mpya" (ya Zitto na Maalim Seif) au kuibomoa ni mtihani ulioikumba
Chadema mwaka 2015.
Kwa mwelekeo ulivyo ndani ya CCM ambapo Magufuli hafanyi
siri kuwa anataka chama hicho kiwe chini ya uongozi wa watu wake (wengi wao
wakiwa wana-Kanda ya Ziwa wenzake), kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka wimbi
kubwa tu la wanasiasa wenye majina watakaotaka kuhamia Upinzani. Na endapo
Zitto na Maalim Seif watakuwa "dream team" ya kuaminika, basi
ACT-Wazalendo inaweza kuwa na mvuto zaidi kwa "wakimbizi kutoka CCM" kuliko
Chadema.
Si ajabu kwa wanasiasa kama Nape Nnauye, Mwigulu
Nchemba, Bernard Membe kujiunga na ACT-Wazalendo endapo chama hicho kitaonekana
kuwa kinaweza kutoa ushindani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani.
Sasa, wakati kupokea "majina makubwa" kutoka
CCM husaidia kuongeaza umaarufu wa chama, uzoefu umeonyesha kuwa wengi wao
wenye majina hayo makubwa ni wanafiki wanaokwenda upinzani kwa sababu zao
binafsi na sio kwa maslahi ya vyama husika vya upinzani.
Kibaya zaidi, kila ujio wa "wahamiaji" hao
ni fursa mwafaka kwa CCM kupandikiza "mamluki" wake kama ilivyotokea
kwa Chadema ilipompokea Lowassa mwaka 2015.
Je ACT-Wazalendo "mpya" inaweza kutoa
upinzani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani? Jibu fupi ni "muda ndio utaongea"
(time will tell). Jibu pana zaidi ni kwamba japo uwezekano huo upo lakini
sidhani kama muda unatosha kukitanua chama hicho nchi nzima hususan katika
kipindi hiki ambacho chama pekee cha siasa kinachoruhusiwa kufanya shughuli za
siasa ni CCM tu.
Ni hivi, kundi muhimu kabisa la wapigakura katika
uchaguzi mkuu wowote ule nchini Tanzania ni "Watanzania wasio na
vyama." Kwamba, hakuna chama cha upinzani kinachohitaji kupoteza muda wake
kuwashawishi wafuasi wa CCM wakipigia kura, kama ambavyo CCM haina muda na
wafuasi wa upinzani kuwashawishi waipigie kura. Vilevile, si CCM wala vyama vya
upinzani vinavyohitaji kuwashawishi wanachama/wafuasi wao wapigie kura vyama
vyao. Watu wanaohitaji kushawishiwa ni hao wasio na vyama. Na habari njema ni
kwamba kundi hilo ndilo lwenye idadi kubwa zaidi ya wapiga kura.
Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi, CCM ina takriban
wanachama milioni 8 ilhali wapinzani wana wanachama takriban milioni 5. Kwa makadirio,
takriban Watanzania milioni 25 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015. Kwahiyo, milioni 8 wa CCM jumlisha milioni 5 wa upinzani jumla
inakuwa milioni 13. Ukichukua milioni 25 kutoa miloni 13 unabakiwa na milioni
12. Kwa makadirio, hawa ni "wapigakura wasio na vyama." Na kimahesabu,
hata nusu tu ya kundi hili likielemea upande mmoja, upande huo unaweza kabisa
kushinda uchaguzi husika. Of course, hapo tunaweka kando hujuma za kawaida za
kuibeba CCM kwenye takriban kila uchaguzi mkuu.
Nimalizie kwa kukumbusha kuwa uchambuzi huu sio exact
science. Umeelemea kwenye uelewa wa kutosha wa mchambuzi kuhusu siasa za
Tanzania.
Kadhalika, uchambuzi huu ni endelevu. Utafanyiwa
marejeo mara kwa mra kila kutakapokuwa na umuhimu wa kufanya hivyo
0 comments:
Post a Comment