13 Nov 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-30:

Asalam aleykum,

Mwaka jana wanamuziki mbalimbali maarufu duniani walifanya matamasha makubwa nchini Uingereza,Marekani,Japan,Italia,Ufaransa,Canada na Afrika Kusini kwa lengo la kukusanya fedha za kupambana na umasikini barani Afrika.Miaka 10 kabla ya hapo kulifanyika matamasha kama hayo kwa lengo hilohilo.Matamasha hayo yalizua mjadala mmoja mkubwa kuhusu iwapo kweli nia nzuri ya kupambana na umasikini barani Afrika inaweza kufikiwa bila kuwaelimisha viongozi wa Kiafrika juu ya umuhimu wa kuthamini maisha ya wanaowatawala.Wapo waliosema kuwa hakuna haja ya kuchanga mamilioni ya fedha ambayo yataishia mifukoni mwa viongozi wabadhirifu,lakini wengine wakasema itakuwa sio vema kuwatelekeza mamilioni ya Waafrika wanaoteseka kwa umasikini kwa vile tu wana viongozi wanaothamini matumbo yao kuliko ya wale wanaowaongoza.Matamasha yalifanyika,fedha zikapatikana na sijui kama ziliwafikia walengwa au la.

Siwalaumu wazungu wanaotushangaa sie masikini wa kutupwa ambao maisha ya kifahari ya baadhi ya viongozi wetu hayalingani hata na yale ya mabilionea wa huku Ughaibuni.Pengine kabla ya kuendelea na hoja hiyo nieleze wasiwasi wangu kuhusu hali ya mambo ilivyo huko nyumbani.Baada ya Rais Kikwete kutangaza baraza lake la mawaziri ulizuka mjadala kuhusu ukubwa wa baraza hilo.Mimi nilikuwa miongoni mwa waliodhani baraza hilo ni kubwa sana kwa nchi masikini kama yetu.Hofu yangu ilimalizwa kwa kiasi flani na kauli aliyotoa Rais kwamba ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kwa kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya,ni muhimu kuwa na timu kubwa ya kutekeleza jukumu hilo zito.Wasiwasi kidogo niliobaki nao ulikuwa kwenye baadhi ya sura zilizokuwamo kwenye baraza hilo.Inafahamika kuwa baadhi ya walioteuliwa walikuwa mawaziri kwenye awamu iliyotangulia,na baadhi yao walikuwa kero kwa wananchi.Sihitaji kuwataja majina kwani sote tunawajua.

Siku za hivi karibuni Waziri wa Miundombinu Basil Mramba amekaririwa akisema kwamba serikali ina mpango wa kununua ndege nyingine ya Rais.Nisichokielewa ni aidha hiyo inayotumika sasa ni mbovu au kuna fedha za kutosha kuwa na ndege mbili za Rais.Kama ni mbovu mbona bado inatumika.Kama imechakaa mbona barabara zetu nazo zimechakaa na bado tunazitumia,mabehewa ya TRC yamechakaa lakini bado yanabeba abiria.Au Mramba anataka kutuambia kuwa maisha ya kiongozi wetu ni bora zaid kuliko ya mamilioni anaowaongoza?Naomba niseme kuwa haya ni maoni yangu binafsi na sio ya gazeti hili,na kama yataamuudhi Mheshimiwa Waziri anivumilie tu kwa vile nami ni mlipa kodi na nina haki ya kuhoji matumizi ya kodi nayokatwa.Nitamke bayana kuwa kauli za Mramba zimekuwa za jeuri kama vile fedha anazopanga kununulia hiyo ndege zinatoka mfukoni mwake.Na sijui jeuri hiyo anaipata wapi!Badala ya kuzungumzia mipango gani aliyonayo kuhusu kuboresha barabara zetu anaturudisha kwenye suala ambalo nina hakika anajua kabisa linawakera Watanzania.Kwanini asielekeze nguvu zake katika kufufua au hata kuanzisha shirika la ndege la Tanzania ambalo pamoja na mambo mengine linaweza kumpatia usafiri Rais wetu?Mbona Tony Blair kuna wakati anatumia ndege za British Airways?Nakubali kwamba Rais wetu hawezi kusafiri kwa kutumia daladala au kwenda ziarani kwenye treni za TRC zilizochoka vibaya.Anahitaji usafiri unaoendana na hadhi yake.Lakini kwa sasa si anao usafiri huo?Kuna haja gani ya kuzungumzia vitu ambavyo hatuvihitaji kwa muda huu?Kwanini,kama fedha za kununulia ndege nyingine zipo,zisielekezwe katika kurejesha uhai wa Shirika la Reli,kwa mfano?Mramba anataka watu waanze kumchukia Kikwete bila sababu ya msingi kwa sababu wakati anazungumzia kununua ndege nyingine ya Rais maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanataabika kwa kusafiri kwenye mabehewa chakavu na barabara mbovu kupindukia na baadhi zikiwa na madaraja ambayo yanahitaji dua kadhaa kuyapita kwa usalama.Huyu Mramba anatoka Tanzania hii masikini wa kupindukia au jimbo la matajiri la Texas huko Marekani?

Na ndio maana nilisema hapo mwanzo kuwa nilipatwa na hofu na ukubwa wa baraza la mawaziri la Kikwete,sambamba na baadhi ya sura zilizomo kwenye baraza hilo.Pengine ukubwa wa baraza sio tatizo lakini pia inawezekana ukubwa huo unawapatia nafasi ya kujificha bila kubainika wale wasioendana na falsafa za “maisha bora kwa kila Mtanzania” na “kasi,nguvu na ari mpya”.Nakumbuka nilipokuwa huko nyumbani,mwalimu wangu wa zamani pale UDSM (Mlimani),Dokta Mwami wa Idara ya Sosholojia,aliniambia kuwa baadhi ya nyakati anatoa mihadhara (lectures) kwenye madarasa yalilofurika wanafunzi kiasi kwamba inakuwa vigumu kwa namna flani kumjua kila mwanafunzi aliyemo darasani.Pengine waziri mdhaifu anaweza kupata mwanya wa kujificha kwenye baraza la mawaziri lililo kubwa.Hata hivyo hata kama baraza lingekuwa na mawaziri 100 lakini wote ni wawajibikaji sidhani kama kungekuwa na manung’uniko.Watanzania wanataka maendeleo na hawajali kama yataletwa na kundi la watu watano au mia mbili.

Nakumbuka Rais Kikwete alishonya kuwa watu wasitafsiri sura yake iliyojaa tabasamu kuwa ni dalili ya upole na kuwaachia viongozi wazembe.Kauli zake zimeonyesha kuwa anaweza kumpa mtu kibano huku anatabasamu.Adhabu ni adhabu tu,hata kama anayeitoa anafanya hivyo huku anacheka.Tunafahamu viongozi waliokuwa wakitoa hotuba za ukali huku wamekunja uso na ungedhani kwamba dakika tano baada ya kumaliza hotuba hizo wala rushwa wangejipeleka wenyewe TAKURU au wazembe wangejiondoa wenyewe madarakani,lakini wapi!Sasa,Jakaya aanze kufanya kweli kwa hawa watendaji wake ambao kwa hakika hawaonekani kuelewa lugha anayoongea.Watanzania hawawezi kupata usingizi bora,acha hayo maisha bora,kama kila kukicha wakisikia kauli za kibabe zilizojaa dharau kuhusu matumizi ambayo kwa muda huu si ya dharura ukilinganisha na hali mbaya ya miundombinu yetu.Jakaya anapaswa kuwaonyesha wananchi wake wanaompenda kupindukia kuwa suala la ndege ni kimbelembele tu cha mtendaji wake mmoja,na kwamba ndege anayoitumia kwa sasa inamtosha,na fedha zinazozongumziwa kununulia ndege hiyo zitaelekezwa kwenye mahitaji ya haraka ya miundombinu yetu iliyo hoi bin taabani.Akimwachia Mramba aendelee kutoa kauli zake zisizoeleweka watu wanaweza kudhani kuwa Waziri huyo anatekeleza tu matakwa ya bosi wake (Rais),jambo ambalo naamini litawaumiza Watanzania wenye matumaini makubwa na Rais wao kipenzi.

Hata kama Waheshimiwa wabunge watakasirika lakini naomba niwaambie kuwa nawalaumu kwa kuwaacha watu kama waziri Mramba wamalize kikao cha bunge la bajeti huko Dodoma bila kutambua mahitaji halisi ya waajiri wa wabunge hao (wananchi wanaowawakilisha).Na pengine Mheshimiwa Lowassa asingemkwamua Mramba ili bajeti yake ipite tusingemsikia akitufanya wajinga kuamini kuwa hivi sasa ndege nyingine ya Rais ni muhimu kuliko mahitaji mengine lukuki katika wizara yake.Ni matumaini yangu kuwa kama alivyomkalia kooni Sauper na Darwin’s Nightmare yake kwa vile inachafua jina la Tanzania basi Jakaya atamkumbusha Mramba kuwa kuzungumzia ununuzi wa ndege muda huu ni sawa na kumchafulia jina yeye (Kikwete) kwa sababu anafahamu sana nini wananchi wanataka kusikia kutoka kwa mawaziri wake.

Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube