17 Jan 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-38

Asalam aleykum wasomaji wapendwa.

Katika makala yangu moja ya hivi karibuni nilibashiri kuwa Rais George W Bush na Chama chake cha Republican wangepewa hukumu yao stahili katika uchaguzi wa katikati ya muhula ulofanyika hivi karibuni,na hukumu hiyo ingeelemea zaidi kwenye suala la vita ya Irak.Na ndivyo ilivyokuwa.Japo miaka kadhaa nilishawahi kuwa “mtabiri wa nyota” kwenye magazeti ya Komesha na Kasheshe (unazikumbuka nyota za Ustaadh Bonge?),hili la Bush na Republicans kusulubishwa halikuhitaji elimu ya unajimu.Wapiga kura wengi walibaini kuwa serikali ya Bush ilikuwa imewaghilibu kuhusu baadhi ya sababu za kuivamia Irak na pia kulikuwa na plani mbovu za nini kifanyike baada ya vita (post-war plans).Yaani kwa kifupi ni kwamba walikosea mahesabu tangu mwanzo.Inatarajiwa kuwa Bush ambaye amebakiwa na takriban miaka miwili kabla hajamaliza kipindi chake cha urais atakuwa na wakati mgumu kupitisha kirahisi maamuzi yake bila kukumbana na upinzani kutoka kwa chama cha Democrat.Na baada ya kugundua hasira za Wamarekani wengi,lugha na kauli za Bush baada ya uchaguzi huo zimekuwa zikiashira kukubali ukweli kwamba kuna makosa yalifanyika.Katika kukwepa kelele zaidi akaamua “kumtosa” hata swahiba wake wa karibu na miongoni mwa waasisi wakuu wa vita vya Irak,aliyekuwa Waziri wa Ulinzi,Donald Rumsfield.

Pengine CCM nayo inaweza kujifunza kitu flani kutokana na uchaguzi huo wa kati ya muhula (mid-term election) wa huko Marekani.Natambua kuwa huo haukuwa uchaguzi wa Rais lakini kwa namna flani umetoa mwanga kuhusu upepo wa kisiasa unavyoweza kuvuma kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2008.Kwa mantiki hiyo,sintakosea sana nikilinganisha uchaguzi huo ulopita majuzi na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 huko nyumbani.Naizungumzia CCM kwa vile ndio chama tawala na ndicho chenye serekali iliyo madarakani.Vilevile nashindwa kuvizungumzia vyama vya upinzani kwa vile licha ya kutokuwa kwenye utawala,vingi vyao vinaonekana kupata uhai pale tu unapojiri wakati wa uchaguzi (ukiondoa Chadema na CUF na kidogo NCCR na TLP).

Ushindi wa Tsunami kwa CCM katika uchaguzi uliopita ulimaanisha kuwa wananchi bado wana imani na chama hicho kikongwe.Pengine imani hiyo ilitokana na mazowea.Pengine kwa vile wapo walioogopa kufanya majaribio ya kukiweka madarakani chama cha upinzani (yale mambo ya zimwi likujualo halikuli likakwisha…kwa maana kuwa angalau CCM ilishaonekana ilichofanya ikiwa madarakani kuliko hao ambao haijulikani nini wangefanya pindi wangeingia madarakani).Au pengine imani hiyo ni matokeo ya CCM kuitumia vizuri falsafa isiyo rasmi ya siasa za Afrika kwamba chama tawala hakipaswi kushindwa uchaguzi labda kiwe kimechoka kukaa madarakani.Wahubiri wa falsafa hiyo (ambayo nimeshasema siyo rasmi) wanataja dalili za chama tawala kuchoka madaraka kuwa ni pamoja na kuwa na makundi ndani yake (yaani kwa mfano kuwe na CCM-Mtandao na CCM-Asili.Huo ni mfano tu).Na kimsingi makundi hayo huwa yanakuwa na nguvu kana kwamba hayako ndani ya chama kimoja bali yenyewe ni kama vyama tofauti.Zipo dalili nyingine ambazo nitazijadili sku nyingine.

Kwa vile wapiga kura waliipa fadhila CCM kuwa kuipa kura nyingi dhidi ya vyama vingine ni dhahiri kwamba chama hicho kina deni la fadhila kwa hao waliokiweka madarakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano.Japo deni hilo halina muda maalum wa kulipwa,ni matarajio ya wengi kwamba malipo yangeanza mara baada ya kuundwa kwa serikali mpya.Na serikali ilipoundwa zikatolewa ahadi zaidi ya zile za wakati wa kampeni huku msisitizo ukiwa ni kubadilisha maisha ya Mtanzania.CCM ilijua na inajua kuwa kwa kiasi kikubwa Tanzania haipaswi kuwa kwenye umasikini ilionao hivi sasa.Pia inafahamu vizuri sana kwamba zipo njia kadhaa zinazowezekana na kumkomboa Mtanzania kutoka katika lindi la umasikini.Soma Ilani ya Uchaguzi ya CCM ujue ni namna gani chama hicho kilivyo na majibu ya matatizo yanayoikabili nchi yetu.

Hata hivyo,naomba niwe mkweli na sidhani kama ukweli wangu utamuudhi mtu anayeitakia mema nchi yetu.Serikali inapaswa kutumia uungwana kuwaeleza walioiweka madarakani kuhusu utata unaoendelea kuhusu tatizo la umeme.Na hapa nazungumzia mkataba na kampuni ya Richmond.Mengi yamesemwa na yanaendelea kusemwa,nisingependa kuyarudia hapa.Lakini hivi tuseme kwamba viongozi wetu hawasikii hayo yanayozungumzwa mtaani kuhusu mkataba huo?Yaani hakuna kabisa aliyesikia madai kuwa “mradi huo” unawahusisha vigogo flani na watoto wao?Kama tetesi hizo hazijasikika basi itakuwa ni kwa makusudi au zinapuuzwa tu.Mtaani kwetu kwa sie tulio huku ughaibuni ni kwenye mtandao (internet) hasa kwenye saiti za Watanzania.Huko yanasemwa mengi sana,na naamini kuwa wahusika wanayasikia. “Wazushi” flani eti wanadai kuwa mitambo iliyoletwa ni ya injini chakavu za Boeing,wengine wanamhusisha mzalendo flani mkarimu aliyetoa alichonacho kusaidia kampeni na hatimaye amerejeshewa fadhila.Yanasemwa mengi sana,na yayumkinika kuamini kuwa wahusika wanayasikia kwa vile serikali ina “masikio marefu ya kusikia kila kisemwacho na pua ndefu za kunusa kila harufu.”

Kikao kilichopita cha Bunge kimemalizika na sikusikia lolote kuhusu huu mkataba wenye utata.Sasa kwanini kiongozi mmoja asijitokeze na kuueleza umma kwamba mambo yako namna hii.Majuzi nimesoma kwenye gazeti flani kiongozi mmoja wa TANESCO akielezea kuhusu mkataba huo,na kwa nilivyoelewa mimi iliashiria kuwa maamuzi ya kuingia mkataba huo yalifanywa kwenye wizara husika.Je ni nani hasa aliyesaini mkataba huo?Yuko wapi huyo muungwana atueleze ni lini hiyo mitambo iliyoletwa kwa mbwembwe na hao jamaa itaanza uzalishaji wa umeme?Nani anaeweza kuwaeleza Watanzania kuwa lini hasa tatizo hili la umeme litakwisha?Au ndio lishageuka kuwa kama rushwa ambayo baadhi ya watu wameshaizowea kama majina yao,kwa vile piga ua inaendelea kuwepo?

Kuitangaza nchi yetu huko nje na kuwaita wawekezaji ni wazo zuri sana lakini kama Mramba anasema Warusi na Wajapani wanashindwa kuja kwa wingi kuwekeza Tanzania kwa vile tu hapo Bongo hakuna vyakula vya Kirusi au Kijapani,je mlevi gani atakaekuja kuwekeza kwenye giza?Je hao wanaoombwa sasa kuja kusaidia kutatua tatizo la umeme walikuwa hawajazaliwa wakati tunaingia mkataba wa mabilioni na watu ambao haijulikani lini watatekeleza ahadi wanazojiwekea wao wenyewe?Jamani,hivi hakuna sheria ya kuibana kampuni inayoshindwa kutekeleza ahadi yake katika muda unaostahili?Wanasheria wa serikali wameenda likizo au suala hili ni “no-go area”?

Oke,tujaribu kuamini kuwa serikali haijasikia yanayonong’onwa huko mitaani kuhusu mkataba huo na suala zima la mgao wa umeme.Je waheshimiwa wabunge nanyi hamjawasikia mnaowawakilisha wakiulizia kulikoni?Tulionyeshwa mapicha kibao ya mitambo ikiwasili,na magazeti mengine (sio hili) yakaenda mbali zaidi hadi kutoa maelezo kuhusu aina ya ndege zilizoleta mitambo hiyo.Jamani,hivi hamuwezi kwenda kuwauliza hao jamaa ni lini hasa watatekeleza ahadi walizojiwekea wenyewe?Kuleta sufuria na kuziweka jikoni ilhali watu wanaendela kupiga miayo huku tayari wamekaa mkao wa kula majamvini na pilau halionekani ni jambo linalokera,na katika mazingira hayo ni shurti kwa mwenye shughuli kutoa tamko kulikoni.Na hapa mwenye shughuli ni aidha serikali au hao jamaa wa Richmond.Kiongozi mmoja (wa ngazi yoyote ile) awafanyie uungwana Watanzania kwa kuwaambia ukweli.

Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.