17 Jan 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-44

Asalam aleykum,

Heri nyingine ya Mwaka Mpya 2007.Nimesema “nyingine” kwa vile nilishatoa salamu kama hizo kwenye makala ilopita.Naona mwaka mpya umeanza kwa kasi nzuri sana huko nyumbani.Hatimaye TANESCO wametangaza kuwa mwaka huu hakutakuwa na mgao wa umeme,na kama utatokea basi sababu itakuwa ni matatizo ya kiufundi au hujuma. Nadhani hujuma hizo ni pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma…mafuta ambayo inadaiwa hutumiwa na baadhi ya wakaanga chipsi wasio waadilifu ambao “katika kupunguza gharama za uzalishaji” huyamiksi na mafuta halisi ya kula kukaangia chipsi kuku. Hivi tumwiteje mtu anayemlisha mteja wake kitu kisichostahili? Muuaji au anabana matumizi? Enewei, tuachane na hilo, naamini TANESCO watawadhibiti wezi hao wa mafuta ili sio tu kuzuia hititlafu kwenye transfoma ambazo zinaweza kuleta tena mgao bali pia kuwaokoa walaji wanaoweza kujikuta wanalishwa chipsi kuku zilizokaangwa kwa kutumia mafuta hayo ya transfoma. Ila hivi kweli kuna vibaka wenye jeuri ya kupanda kwenye transfoma na kunyonya mafuta kirahisi namna hiyo? Au ni vibaka wenye kile Waingereza wanakiita “inside knowledge” (kuwa na habari nyeti au ujuzi kuhusu hila au jambo linalofanyika)?

Pia mwaka umeanza vizuri kwa sababu mvua zimekuwa “za kumwaga” na tayari mabwawa yanayozalisha umeme yamepata maji ya kutosha kiasi cha kuipa jeuri TANESCO kusema hakutakuwa na mgao mwaka huu. Pia mvua hizo zimeleta neema nyingine kwa jamaa wa Richmond.Duh, kweli kila maajabu yanawezekana huko nyumbani. Hawa watu walitetewa wee na sasa tunaambiwa eti wameuza mkataba! Hivi inawezekana TANESCO waliposaini mkataba wenye vipengele vinavyoruhusu mkataba huu kuuzwa kwingine walishawasiliana na mnajimu flani aliyewaeleza kuwa baada ya miezi michache jamaa wa Richmond watachemsha! Nasema mvua zimewakomboa hawa wababaishaji kwa kuwa navyowajua Watanzania, hawajali kama umeme unazalishwa na TANESCO, IPTL au Richmond, wanachotaka wao ni umeme tu. Pia hawajali kama umeme huo ni matokeo ya mitambo ya Richmond kufanikiwa kuingiza megawati zake ishirini na kitu kwenye gridi ya Taifa, au kwa vile mabwawa yamepata maji ya kutosha kusukuma mitambo ya umeme, au hatimaye Mungu ametuhurumia na kusitisha mitihani yake. Kuna falsafa moja ya mtaani inadai kuwa ukishafanikiwa kupata kitu basi namna ulivyokipata inakuwa sio muhimu sana. Umeme umerudi, kwa hiyo jinsi ulivyorudi sio muhimu sana. Nani alisema ukweli, nani aliongopa sio muhimu sana kama kurejea kwenye kanuni za jiographia ya nchi za tropiki kama Tanzania ambapo mchana unapaswa kuwa na urefu sawa na usiku, takriban masaa 12 ya giza na 12 ya mwanga, na sio kama wakati wa mgao ambapo muda wa giza ulifanywa kuwa mrefu kuliko ule wa mwanga.

Lakini neema ya mvua ambayo imesaidia kumaliza tatizo la mgao, ndugu zetu wa TANESCO wataendelea kulipa mamilioni ya shilingi kwa IPTL kwa sababu kuna waungwana flani walisaini mkataba wa muda mrefu unaoibana TANESCO kuendelea kuilipa IPTL hata kama TANESCO haihitaji kununua umeme kutoka kwa IPTL, kama ilivyo katika kipindi hiki ambacho mabwawa yanaipa uwezo TANESCO kuzalisha umeme bila kuhitaji “tafu” ya kampuni nyingine. Nimesoma kwenye gazeti flani kwamba mkataba kati ya makampuni hayo mawili ni wa miaka ishirini. Kwa maana hiyo mvua inyeshe, mabwawa yajae mpaka yatapike, na Richmond nao watoe zawadi ya mwaka mpya kwa kuamua kuipatia TANESCO megawati 1000 (sio 100 zilizowatoa jasho hadi kuuza mkataba) bado TANESCO wataendelea kukuhoa mamilioni ya shilingi kwa IPTL kila mwezi. Hii ndio mikataba kama ile ya Karl Peters na wale machifu wetu ambao angalau wao wangeweza kujitetea kuwa hawakuwa na shule ya kutosha. Lakini tusilaumu sana, pengine hao walisaini mkataba huo na mingine ya aina hiyo ni wale ambao wanalipenda sana Taifa letu kiasi kwamba wanachukua tahadhari za muda mrefu, yaani hata kama waliosaini mikataba hiyo watakuwa wamestaafu (au wako jela?) bado wajukuu zao “wataendelea kulihudumia Taifa.”

Pia mwaka umeanza vizuri kwa vile BAKWATA imetangaza jihad dhidi ya wale wanaojihusisha na madawa ya kulevya. Nawapongeza sana kwa uamuzi huo ambao binafsi naona unaendana na kile nilichokiandika wiki iliyopita kuhusu “mapambano ya kiroho” (moral crusade). Ila kwanini BAKWATA wasitanue vita hiyo na kuwajumuisha wala rushwa pia? Kwa sababu navyoona mie itakuwa ni kazi ngumu kuwabana wauza unga ilhali upenyo wa kuingiza unga huo unaendelea kuachwa wazi. Na upenyo huo ni rushwa, yaani ile inayomfanya mtu mwenye dhamana ya kupekua mizigo airport au bandarini kutofanya hivyo kwa vile kishapewa mgao wake. Tamko la BAKWATA linanikumbusha hoja wa mwalimu wangu wa zamani wa Sosholojia ya Dini pale Mlimani, Dokta Fadha John Sivalon, ambaye alisema kuwa taasisi za kidini ni nguvu muhimu sana katika kuleta mabadiliko kwenye jamii. Naamini ikitangazwa jihad dhidi ya wala rushwa tunaweza kuona baadhi ya wahusika wakianza kufikira mara mbilimbili kabla ya kuomba au kupokea teni pasenti. Na huenda ikasaidia kupunguza marudio ya mikataba kama ile ya enzi za Karl Peters na machifu wetu.

Kuna vingi vizuri katika mwaka mpya huu ikiwa ni pamoja na Simba kuwa chini ya uongozi mpya. Kama msomaji wangu mpendwa ni mshabiki wa wana-Jangwani basi naomba “nikuudhi kidogo” kwa kutamka bayana kuwa mie ni mpenzi wa “wekundu wa Msimbazi” japo mapenzi yangu yameathiriwa sana na hii migogoro ya nenda rudi kila kukicha. Hatimaye Simba-Taliban wamefanikiwa kuingiza viongozi madarakani.Ila tayari kuna ubabaishaji umeshaanza kujitokeza mapema kweupe. Kwa mfano, kuna hili suala la kocha kutoka Brazil ambalo nadhani viongozi wa Simba wanapaswa kuwa wakweli kwa wapenzi wao. Kuendelea kusema kuwa kocha huyo bado yuko na klabu hiyo wakati alishatamka bayana kuwa alipoondoka ndio “imetoka jumla” ni sawa na “kuwazuga” wana “lunyasi” kama mimi.Vilevile kuna suala la uendeshaji mzima wa klabu.Angalau enzi za akina Azim Dewji na Mohammed Enterprises ilikuwa inajulikana nani ni mfadhili “rasmi”.Siku hizi naona imekuwa suala la kutegemea fadhila za wenye nazo.Uongozi wenye mwelekeo unatakiwa kuhakikisha klabu inajitegema kimapato au inakuwa na mfadhili anayeeleweka bayana. Pia nionavyo mie, suala la mchezaji Athumani Iddi ni kama linakuzwa tu. Kama hataki kuichezea Simba na tayari ameshaanza mazoezi na Yanga basi bora aachwe. Na kama kinachombana ni huo mkataba wa miaka matatu basi suala hilo linaweza kumalizwa kisheria kwa namna ambayo mtu akivunja mkataba halali anavyoshughulikiwa. Au kama namna gani vipi, basi mkataba huo uuzwe kwa Yanga kwa namna ileile ambavyo Richmond wameuza mkataba wao kwa kampeni ya Dowans .

Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube