13 Mar 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-53


Asalam aleykum,

Wiki hii imeshuhudia pigo la namna flani kwa Rais Joji Bushi wa Marekani.Pigo hilo limekuja baada ya mahakama moja nchini humo kumwona mmoja wa washirika wa karibu wa Bushi,Lewis Libby,kuwa ana hatia ya kuzuia sheria kuchukua mkondo wake.Libby ambaye alikuwa msaidizi wa Makamu wa Rais Dick Cheney,alikuwa akikabiliwa na shtaka la kulidanganya Shirika la Upelelezi la Marekani(FBI) na mahakama kuhusu taarifa za kuvujisha jina la shushushu wa Shirika la Ujasusi la nchi hiyo (CIA).Skandali hiyo ilianza baada ya kuvuja taarifa kwamba mwanamama aitwaye Valerie Palme ni shushushu wa CIA.Inaaminika kuwa jina la mwanamama huyo lilivujishwa kwa makusudi kwa nia ya kumharibia utendaji wake wa kazi,na pia ilikuwa ni sawa na kisasi kutokana na mume wa shushushu huyo,Balozi Joseph Wilson kuweka hadharani upinzani wake dhidi ya plani za Bushi na washirika wake za kuivamia Iraki.Mwaka 2002 Balozi Wilson alikwenda nchini Niger kuchunguza madai kwamba serikali ya Rais wa zamani wa Irak,Saddam Hussein,ilikuwa inataka kununua kemikali za kinyuklia kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi.Mwaka mmoja baadaye,Balozi huyo alitamka hadharani kuwa madai hayo yalikuwa sio ya kweli.Baadaye ilikuja kufahamika kuwa baadhi ya data alizokuwa nazo Wilson zilipatikana kutoka kwa mkewe,ambaye hadi muda huo hakuwa akijulikana hadharani kama ni shushushu.Kwa kifupi,kuvujisha habari kuwa Valerie ni shushushu ilikuwa ni sawa na kuwakomoa wanandoa hao.

Sasa kinachosubiriwa ni hukumu dhidi ya Libby na inawezekana akaenda jela kwa miaka kadhaa.Hukumu hiyo imetafsiriwa kama pigo kwa Bushi na washirika wake hasa kwa vile kwa namna flani imefichua jinsi “wapenda vita” hao walivyo tayari kufanya lolote kuhakikisha wanatimiza azma zao.Na hilo limetokea wakati ambapo siasa za Marekani zimetawaliwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu maendeleo ya vita huko Irak huku wengi wakiamini kuwa vita hiyo inaelekea kubaya japo Bushi ameendelea kupiga debe kwamba mambo yanaendelea vizuri na ushindi ni lazima.

Ikulu ya Marekani haikupendezwa hata kidogo na hukumu hiyo kwa vile ni fedheha kwa mtu aliyekuwa na madaraka makubwa kama Libby kudanganya kwa mamlaka za kisheria za nchi hiyo.Na hapo ndipo nikajikuta naliangalia upya suala la mbunge mmoja wa huko nyumbani ambaye hivi majuzi ameumbuliwa hadharani kuwa ni kihiyo.Jeshi la polisi lilitamka bayana kuwa mbunge huyo aliwadanganya wapiga kura kuhusu elimu yake.Kwa maana nyingine,Mheshimiwa huyo alifanikiwa kupata ubunge kwa kutumia taaluma feki.Sijui nini kitafuata lakini nadhani mtu mwenye furaha zaidi baada ya kusikia habari hizo ni mpinzani wa mbunge huyo ambaye tangu mwanzoni alionekana kushtukia elimu ya mbunge huyo.Sintashangaa iwapo atakwenda mahakamani kutaka matokeo ya ubunge huo yatenguliwe.

Kilichonishangaza zaidi ni kauli ya jeshi la polisi kuwa haliwezi kumchukulia hatua yoyote mbunge huyo.Ibara ya 68 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka waziwazi kwamba mbunge atatakiwa kula “kiapo cha uaminifu” mbele ya Spika…sasa kabla hatujaenda mbele,japo kiapo cha uaminifu hakihusiani na elimu ya mbunge anayeapishwa,UAMINIFU wa huyo Mheshimiwa aliyekumbwa na kashfa ya elimu una utata.Nasema una utata kwa vile si tu alidanganya kwa chama chake na Tume ya Uchaguzi kuhusu elimu yake bali pia aliwadanganya wapiga kura wake ambao ndio anaowatumikia hivi sasa.Bila kupunguza hadhi ya Spika,yayumkinika kusema kuwa mtu ambaye anaweza kuwadanganya maelfu ya wapiga kura kuhusu elimu yake,ataaminika vipi anapoahidi uaminifu kwa mtu mmoja,yaani Spika?Hivi jeshi la polisi linaposema kuwa haliwezi kuchukua hatua yoyote wanamaanisha kuwa siku hizi ni “poa tu” kuwasilisha vyeti feki kujipatia madaraka ya kutumikia umma?Kama walikuwa wanajua hilo sasa kulikuwa na umuhimu gani wa kufanyia uchunguzi suala hilo?Upeo wangu mdogo wa kisheria unaniambia kuwa kugushi cheti ni kosa kisheria,sasa sijui imekuwaje jeshi hilo litupe mzigo huo kwa CCM na wapiga kura wa jimbo analotoka Mheshimiwa huyo.Na kama “kumfagilia” vile,wanasema kuwa wapiga kura jimboni kwa Mheshimiwa huyo wana uhuru wa kumchagua tena iwapo watajiskia kufanya hivyo!Nasema hivi,fedha za walipakodi zilizotumika kufanyia uchunguzi huo zitakuwa zimepotea bure iwapo jeshi hilo litaishia kutoa kauli tu bila kuchukua hatua zinazostahili.

Lakini kichekesho kingine ni kauli ya Mheshimiwa mwenyewe kutamba kuwa “atatesa” kwa miaka 20 ijayo licha ya kashfa hiyo ya ukihiyo.Hii ni sawa na kuwadharau wapiga kura wake.Suala hapa sio kama watu wanampenda au la,bali la muhimu hap ni ukweli kwamba AMEWADANGANYA KUHUSU ELIMU YAKE.Nani angependwa kuwakilishwa na mtu aliyeomba kura huku akijua bayana kuwa elimu yake ni ndogo kuliko hiyo alikuwa akiitangaza?Nadhani Mheshimiwa huyo amesahau kuwa Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi,na kwa vile ili kuwa mkulima hulazimiki kuwa na elimu ya kiwango flani,basi angeweza kuwaomba wananchi wamchague kwa elimu yake ya kweli alikuwa nayo kuliko kuwazuga na elimu ambayo sio yake.

Anapodai kuwa suala la kudanganya kuhusu elimu yake halioani na wadhifa wake kama mwakilishi wa wananchi anamaanisha nini?Kama lilikuwa halioani kwanini basi aliamua kudanganya?Kwa lugha nyingine,ambayo kimsingi ndio hali halisi,kila mwananchi bila kujali kiwango cha elimu yake (alimradi anajua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza) ana haki ya kugombea ubunge.Sote tunafahamu kuwa si lazima uhitimu elimu ya kidato cha sita nje ya nchi ili uweze kujua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza.Siku hizi kuna watoto kibao huko chekechea ambao wanatwanga “ung’eng’e” utadhani wamezaliwa London.Lakini pia tunafahamu kuwa kutokana na mambo ya utandawazi kwenye sekta ya elimu wapo wahitimu kadhaa ambao licha ya kusomea nje ya nchi,suala la “lugha” ni mgogoro.Mantiki zote hizi zinaonyesha kuwa Mheshimiwa huyo hakuwa na haja ya kudanganya kuhusu elimu yake ili aukwae ubunge.Na badala ya kutamba kuwa ataendelea kukalia kiti hicho,ni vema angetumia nafasi aliyonayo sasa kuwaomba msamaha wapiga kura wake,Tume ya Uchaguzi na chama chake kilichompitisha kupata tiketi ya ubunge huo.

Kuendelea kuhalalisha makosa sio uungwana,hata kama jeshi la polisi limeamua “kulichunia” suala hilo.Waingereza wana msemo “to err is human but to rectify is greatness” yaani kwa lugha ya Taifa ni kwamba “kukosea ni ubinadamu lakini kujirekebisha ni kujijengea heshima.”Pia kuna msemo kuwa kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa ni kosa.Sasa vyovyote ilivyo,kudanganya kuhusu elimu ni kosa,lakini kurudia kosa kwa kudai kuwa suala la elimu halihusiani na ubunge ni zaidi ya kosa la mwanzo.Napenda kusisitiza kuwa huu ni mtizamo wangu binafsi na hauwakilishi mawazo ya gazeti hili.Vilevile,kama navyosema siku zote,lengo la makala hii sio kutiana vidole machoni au kutishia ulaji wa mtu bali ni kurekebishana pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo.

Alamsiki



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.