13 Mar 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-52


Asalam aleykum,

Kwa siku kadhaa sasa duru za siasa za kimataifa zimeshuhudia Joji Bushi na neococonservatives wenzake wakihaha kujenga mazingira ya kuwasha moto mwingine huko Ghuba ambapo safari hii mlengwa ni Iran.Huko nyuma nilitumia takriban makala nzima kuelezea kundi la watu wanaotengeneza sera za Bushi na Marekani kwa ujumla.Neoconservatives au neocons kwa kifupi,ni kundi la wahafidhina ambao licha ya mapenzi yao yaliyokithiri kwa taifa la Israel,wanaamini kuwa Marekani kama taifa lenye nguvu zaidi ya yote duniani lina haki isiyo na kikomo ya kutetea maslahi yake mahala popote pale katika sayari hii.Kundi hilo ambalo limefanikiwa kutoa wasaidizi kadhaa wa karibu wa Rais Bush ikiwa ni pamoja na Makamu wa Rais Dick Cheney na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Donald Rumsfield,limekuwa mstari wa mbele katika kusukuma wanachokiita “vita dhidi ya ugaidi” itekelezwe katika kila kona.Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanawaona wahafidhina hawa wenye mitizamo ambayo wakati mwingine ina utata kuwa ni watu hatari zaidi hasa kwa vile wanaonekana kupenda sana vita.

Siku chache zilizopita,Marekani ilitoa ilichokiita ushahidi kwamba Iran imekuwa ikivisaidia vikundi vinavyoendeleza mapigano nchini Irak baada ya kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein.Baadhi ya watu hata huko Marekani kwenyewe wanauona “ushahidi” huo kama ni kisingizio tu cha kuanzisha “kimbembe” kingine huko Iran.Na katika kuonyesha kuwa huenda vita nyingine iko njiani,Makamu wa Rais Cheney alinukuliwa akiwa ziarani nchini Australia akisema kwamba “lolote linawezekana” kuhusu Iran,kauli iliyotafsiriwa kuwa inaelekea kuna moto mwingine unaotarajiwa kuwashwa hivi karibuni.Hakuna anayeweza kubashiri nini kitatokea iwapo Marekani itaivamia Iran lakini inapaswa kufahamika kuwa Iran nayo ni nchi ambayo imejitosheleza kijeshi.Pia silaha kubwa zaidi inayoipa jeuri nchi hiyo hadi kufikia hatua ya kuita Maazimio ya Umoja wa Mataifa kuwa ni “vipande vya makaratasi tu visivyo na nguvu za kisheria” ni utajiri wake wa “dhahabu ya maji” yaani mafuta,au “wese” kama wanavyoitwa watoto wa mjini.Uvamizi dhidi ya nchi hiyo utakuwa na athari kubwa sana katika uchumi wa dunia hasa kwa vile hadi sasa bei ya mafuta bado iko juu sana.

Lakini ukiangalia sana sera za kibabe za Marekani hutashindwa kubaini mapungufu kadhaa.Kwa mfano,baadhi ya wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaamini kwamba adui namba moja wa taifa hilo alikuwa Osama bin Laden na kundi lake la Al-Qaeda,na wala si Saddam.Baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11,2001 jeshi la Marekani lilipelekwa Afghanistan kumsaka Osama na Al-Qaeda yake.Hadi leo si tu kwamba Osama bado “anapeta” huko aliko,na Al-Qaeda imefanikiwa kujitanua takriban kila kona ya dunia,kikundi cha Taleban ambacho mwanzoni kilipokea kipigo kikali kutoka kwa Marekani kwa madai kuwa kilikuwa kinamhifadhi Osama na Al-Qaeda,kinaelekea kujikusanya kwa nguvu pengine zaidi ya ilivyokuwa kabla ya uvamizi huo.Wiki hii wamemkosakosa Makamu wa Rais Cheney alipokwenda Afghanistan kukutana na Rais Hamid Karzai kujadili tishio la Taliban.

Kimsingi,Marekani na washirika wake ilipaswa kutilia mkazo zaidi kwenye jitihada zake Afghanistan kabla ya kufikiria kuivamia Irak ,ambayo nayo imegeuka kuwa “gonjwa lisilotibika” kutokana na vurugu zinazotishia kuimegamega nchi hiyo katika misingi ya kidini.Ofkoz,Saddam alikuwa dikteta na alistahili kudhibitiwa lakini ni ukweli usiopingika kuwa uvamizi wa Marekani na washirika wake haujaonyesha matunda yoyote mazuri katika kuleta amani kwenye nchi hiyo.Wapo wanaodiriki kusema kwamba japo Saddam alikuwa dikteta lakini wakati wa utawala wake watu walikuwa wakiweza kwenda makazini,mashuleni na kwingineko bila hofu ya kulipuliwa na mabomu ya kujitoa mhanga.Na hadi sasa hali ya miundombinu nchini humo ni mbaya kupita kiasi.Kibaya zaidi ni kwamba kabla ya uvamizi huo Irak haikuwa na vikundi vinavyojihusisha na mashambulizi ya kigaidi,na kimsingi hoja kwamba Saddam alikuwa anashirikiana na Osama ilithibitka mapema kuwa ilikuwa feki,lakini sasa inafahamika bayana kuwa Al-Qaeda wameweka kambi ya kudumu nchini humo.

Huko Marekani kuna mpasuko mkubwa kati ya vyama vikuu vya siasa vya Democrat na Republican ambapo wengi wa Democrats (na Republicans kadhaa) wanadhani kuwa vita vya Irak haina mwelekeo na ushindi ni ndoto ya mchana kwa hiyo ni bora Marekani iondoe majeshi yake katika nchi hiyo.Tayari zaidi ya askari 3000 wa Marekani wameshapoteza maisha yao na idadi ya Wairaki walikufa ni ya kutisha japokuwa takwimu za taasisi za kimataifa zimekuwa zikipingana na zile zinazotolewa na serikali ya Joji Bushi.Wapo wanaodhani kuwa hili wazo jipya la kutaka kuivamia Iran ni sawa ni kile watoto wa mjini wanachokiita “kuua soo” yaani kupata sababu ya kuficha uso kwa aibu baada ya kufeli katika sera nzima ya Bushi kuhusu Irak.

Taarifa nilizozipata wakati naandaa makala hii zinasema kwamba hatimaye Marekani imekubali kukutana na Iran na Syria kujadili hali ya usalama huko Irak.Haya ni sawa kabisa na mabadiliko ya rangi za kinyonga kwa vile licha ya kushauriwa hivi karibuni na tume huru ya (Waziri wa zamani) James Baker kwamba hakuna ubaya kwa nchi hiyo kukaa kitako na “adui” zake wa Syria na Iran kujadiliana kuhusu hatma ya Irak,Bushi na wapambe wake walitamka bayana kuwa hawana muda wa kukutana na maadui zao.Pengine habari hizi kwamba kutakuwa na mkutano kati ya nchi hizo tatu zinaweza kuwa dalili mojawapo ya busara kwamba zipo njia nzuri zaidi za kupata amani kuliko mtutu wa bunduki,hasa ikizingatiwa kuwa risasi za moto zimeonyesha kutofua dafu kwa hao jamaa wanaotumia silaha ya kujilipua wenyewe katika mashambulizi ya kujitoa mhanga.

Baada ya kuangalia siasa za kimataifa,naona nigusie mambo mawili matatu yanayohusu huko nyumbani.La kwanza ni kuhusu ziara ya timu ya Real Madrid ya Hispania kuja Bongo kufungua uwanja wetu mpya.Naamini nia ya kuwaleta ni nzuri lakini gharama zao ni kubwa kupita kiasi.Na pengine tukilinganisha gharama hizo na faida tunazotarajia kuzipata tunaweza kuishia kupata hasara zaidi kuliko faida.Hao jamaa watakuja kama watalii,sasa tangu lini mtalii akagharamiwa na nchi yenye vivutio vya utalii?Tungeweza kuafikiana nao kwamba hatutawatoza fedha yoyote watakapotembelea vivutio vyetu vya utalii lakini sharti ni kwamba wajigharamie huduma zote au baadhi ya huduma hizo.Na hapa nadhani gharama kubwa zaidi itakuwa ya posho za hao waungwana.Hawa ni watu wanaolipwa mamilioni ya shilingi kwa wiki,sasa itakuwa ni kujiumiza kama tutachukua jukumu la kupoteza hela yetu ya ngama kwa ajili ya watalii hawa.Kama Kanisa la Anglikana halikutupa masharti yoyote walipoamua kufanya mkutano wao mkuu hapo nyumbani (ambao ukiondoa mjadala wa ushoga umesaidia kwa kiasi flani kuitangaza nchi yetu) iweje hawa jamaa wa Real Madrid watuwekee masharti magumu namna hiyo.

Mwisho, ni taarifa moja ya kushtuka niliyosoma hivi punde kwamba mengi ya maduka ya madawa (pharmacies) jijini Dar yanaendesha shughuli zake kiujanjaujanja-aidha hayajahakikiwa na mamlaka husika,hayajasajiliwa,watendaji wake ni vihiyo au madawa wanayouza yana walakini.Ni taarifa ya kutisha kwa vile katika mwaka wangu wa mwisho pale Mlimani (UDSM) nilifanya utafiti flani kuhusu athari za sera ya uchangiaji gharama za huduma ya afya,ambapo miongoni mwa matokeo ya utafiti huo ni kwamba wananchi wengi hasa wale wa vipato vya kati na chini hupendelea kujinunulia dawa kwanza kabla ya kufikiria kwenda hospitali.Kwa mantiki hiyo,maduka ya madawa ni kama hospitali zisizo rasmi huko mitaani na kwa kiasi kikubwa ndizo tegemeo la kwanza la huduma ya afya.Dawa ni sumu zisipotolewa kulingana na kanuni zake,na kwa vile afya ya mtu si sawa na gari ambalo likichakaa utanunua jingine,basi ni vema mamlaka husika zikaongeza jitihada za kuwabana wababaishaji wote waliojichomeka kwenye eneo hilo nyeti.


Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube