10 Jun 2007

Asalam aleykum,

Pengine hii ni tetesi ambayo ungependa kuisikia.Kuna habari kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye anastaafu rasmi mwezi huu ana mpango wa “kubadili dhehebu.”Blair ni muumini wa Kanisa la England (Church of England) wakati mkewe,Cherie,ni Mkatoliki.Inasemekana kuwa miongoni mwa ziara za mwisho za Blair akiwa Waziri Mkuu ni kwenda Vatican kukutana na Papa Benedikti,na “wambea” wanadai katika ziara hiyo Blair atajiunga rasmi na Kanisa Katoliki.Taarifa zaidi zinadai kuwa licha ya kujiunga na Kanisa hilo,Blair pia anataka kuwa deacon (kwa mujibu wa tafsiri kwenye kamusi ya English-Swahili neno hilo linamaanisha shemasi,japo upeo wangu mdogo wa Ukatoliki unaniambia kuwa ushemasi ni hatua moja kabla ya upadre).Enewei,ni vizuri kwa Blair kumrejea Bwana kwa namna yoyote ile inayofaa hasa baada ya kuboronga kwenye sera yake ya Iraki ambapo wengi wetu tunafahamu matokeo yake.

Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mchakato wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya “chama dume” CCM.Watu wanapigana vikumbo kuhakikisha wanaibuka videdea kwenye kinyang’anyiro hicho.Na wale wanaojua kutumia midomo yao kutengeneza fedha,basi huu ni wakati wa kuchuma hasa.Nadhani wapo wanaoombea kuwa tuwe na chaguzi kubwa kila wiki maana sio siri kwamba chaguzi zinawanufaisha wengi.Ita rushwa,takrima au ukarimu lakini hilo sio nalotaka kulizungumzia kwani linahitaji makala nzima.Unajua wakati mwingine ni vigumu sana kutofautisha rushwa na ukarimu.Hivi kijana anapotoa ofa za chipsi kuku na bia kwa mrembo anayemtamani anakuwa anatoa rushwa akubaliwe kimapenzi au anafanya ukarimu ili “somo lieleweke”?Na mgombea anapotumia “ukarimu wa kisiasa” kuwakamatisha mafedha wapiga kura wake ili apate uongozi anakuwa anatoa rushwa au anakuwa mkarimu kwa wapiga kura hao?Tutalijadili hilo siku zijazo kwani kama nilivyosema awali mjadala huo unahitaji muda na nafasi ya kutosha.

Kumekuwa na maneno ya chinichini na ya waziwazi kuhusu hofu ya “watoto wa vigogo” kuiteka CCM hasa baada ya baadhi ya watoto wa wanasiasa wetu kuchukua fomu za kugombea uongozi kwenye nafasi mbalimbali za chama hicho tawala.Mmoja ambaye nadhani ametajwa sana ni Ridhiwani Kikwete.Kwa wafuatiliaji wa makala zangu watakumbuka kuwa nilishawahi kuelezea huko nyuma “mkutano” wangu na kijana huyo kwenye hafla moja ya Watanzania mjini Manchester,hapa Uingereza.Katika makala hiyo nilielezea namna nilivyovutiwa na namna Ridhiwani alivyo,yaani kama si kufanana na baba yake,JK,isingekuwa rahisi kuhisi kuwa kijana huyo ni mtoto wa Rais.Yaani tofauti na mazowea yetu ambapo tumezowea kuona watoto wa vigogo wakijifanya tofauti na sie tunaotoka familia za kawaida,mtoto huyo wa JK alionekana kuwa “down-to-earth” kweli kweli.Tulipokutana nilimfahamisha kuwa kwa hakika anatoa picha nzuri sana sio kwa familia yake tu bali pia hata kwa familia za viongozi wengine.Nakumbuka alinieleza kwamba tangu utotoni amekuwa akiamini kwenye jitihada zake binafsi na wala sio nafasi ya mzazi au familia yake.

Sasa wapo waungwana ambao wanadhani kuwa kijana huyo anaweza kutumia jina la baba yake ili kukwaa madaraka.Kwanza binafsi sioni kosa kwa mtoto wa kiongozi kugombea uongozi wa aina yoyote ile kwani hiyo ni haki yake ya kidemokrasia na kikatiba.Iwapo wapiga kura watashawishika kumpa kura kwa vile ni mtoto wa Rais,haitakuwa kosa kwani naamini kuwa kwenye kampeni zake ananadi sera zake na wala sio mahusiano yake na JK.Joji Bush,rais wa sasa wa Marekani ni mtoto wa rais aliyepita wa nchi hiyo,na hakuna anayelalamika kwani Bush mtoto aliingia madarakani kwa jitihada zake binafsi ikiwa ni pamoja na kuuza sera zake vizuri dhidi ya wagombea wengine.Nadhani hofu kwamba madaraka yanazunguka miongoni mwa familia flani haina uzito sana kwani la muhimu kwa kiongozi sio familia anayotaka bali uwajibikaji wake.Naomba nisisitize kuwa simpigii debe Ridhiwani au mtoto yoyote yule wa kigogo kwani hata kama ningetaka kufanya hivyo mie sio mpiga kura kwenye mikutano ya chaguzi za CCM.

Nilipokuwa Mlimani (UDSM) mwalimu wangu wa Sosholojia Padre John Sivalon aliwahi kutueleza darasani kwamba suala la watu wa familia au ukoo mmoja kushika au kupeana madaraka ni kitu cha kawaida huko Marekani,alimradi hakuna sheria iliyokiukwa.Alisema labda tofauti kati ya huko Marekani na Afrika ni ukweli kwamba kwa wenzetu huko mtu anapopata nafasi kwa vile ni ndugu ya mtu flani basi anajitahidi kuhakikisha hamuangushi huyo nduguye.Unajua kwa wenzetu sifa ya familia au ukoo ni jambo muhimu sana.Sasa kama mtoto wa kiongozi atapata nafasi kwa vile baba yake ni flani,anahakikisha kuwa anawajibika kwa nguvu ili kulinda heshima ya baba yake huyo pamoja na familia na ukoo kwa ujumla.Na kikubwa wanachoangalia wenzetu ni uwezo wa mtu na wala sio familia au ukoo anaotoka.Pia ikumbukwe kuwa kwa mgombea kuwa mtoto wa kiongozi haimaanishi kuwa atajipigia kura mwenyewe bali hilo ni jukumu la wapiga kura ambao ili wamchague ni lazima waridhishwe na uwezo wa mgombea huyo

Pia yatupasa tukumbuke kuwa kuna familia au koo ambazo siasa iko damuni.Na ipi ni njia bora ya kuendeleza utamaduni wa familia au ukoo kama sio kushiriki kwenye mazoezi halali ya kidemokrasia kama chaguzi?Inawezekana ukoo wa akina Kikwete una damu ya siasa,na kama msemo wa Kiswahili usemavyo kuwa maji hufuata mkondo,naamini kuwa mtoto wa JK kufuata hatua ya baba yake kwenye fani ya uongozi wa kisiasa ni jambo zuri.Wenzetu huku Ughaibuni wanapenda kuangalia vipaji vya watoto wao na mchango wa vipaji hivyo katika familia au ukoo,na hatimaye kuviendeleza vipaji hivyo

Jingine ambalo naamini litanifanya nitofautiane na wenzangu wengi ni kuhusu marupurupu ya wabunge ambayo imefahamika kuwa yataongezeka katika mwaka ujao wa fedha.Awali mie nilikuwa miongoni mwa wale wanaoamini kuwa wabunge wanalipwa fedha nyingi zaidi ya wanazostahili.Mawazo hayo yalibadilika baada ya kuongea na Mheshimiwa flani mmoja ambaye alifanikiwa kuingia bungeni mwaka jana kwa tiketi ya CCM (naomba nisimtaje jina).Mheshimiwa huyo ambaye ni rafiki yangu wa karibu alinieleza mambo ambayo niliyashuhidia kwa macho yangu binafsi.Alinimabia kuwa ubunge ni jukumu linalohitaji moyo hasa kwa wale ambao majimbo yao yanakabiliwa na matatizo mbalimbali.Nilishuhudia kwa macho yangu namna wapiga kura walivyokuwa wakimiminika nyumbani kwa Mheshimiwa huyo kuomba misaada mbalimbali hususan ya kifedha.Aliniambia,(na mwenyewe nilishuhudia) Chahali watu wanalalamika wanaposikia sie wabunge tunaomba tuboreshewe maslahi yetu lakini hawajui namna gani “familia zetu zinavyotanuka” baada ya kupata ubunge.Wapiga kura wanakuwa sehemu ya familia kwani inamwia vigumu mbunge kuwatelekeza watu wanaodamka asubuhi kuja nyumbani au ofisini kwa mbunge huyo wakiomba msaada mmoja au mwingine.Akiwatosa atakuwa anajichimbia kaburi la kisiasa katika uchaguzi ujao lakini licha ya hilo,kwa mila na desturi zetu za Kitanzania inafahamika kuwa tunawajibika kuwasaidia wale wasiojiweza hata kama kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajiathiri sie wenyewe.Nafahamu kuwa wapo wabunge ambao inawezekana hawatoi misaada kwa wapiga kura wao lakini hapa nazungumzia kila nilichokiona kwa macho yangu mwenyewe.Na kwa vile ubunge sio kazi ya kuhubiri injili ambayo mshahara wake ni peponi bali ni jukumu ambalo kwa mwajibikaji halisi linamaanisha “kuufutua” ukoo (kuongezeka idadi ya wanaokutegemea) basi nadhani uamuzi wa serikali kuboresha maslahi ya waheshimiwa wabunge ni sahihi.

Mwisho,nadhani uamuzi wa Katibu wa Bunge kuwapiga stop wanahabari kuhudhuria vikao vya kamati za bunge sio wa busara.Hao ni wawakilishi wetu,na tunapaswa kujua namna wanavyojadili masuala mbalimbali yanayotuhusu.Kwani kuna siri gani ambazo zinaathiriwa na kuwepo kwa waandishi wa habari wakati wa vikao vya kamati za bunge?Natumaini kuwa hatua hiyo itakuwa ya muda tu,na pia nataraji wabunge wetu wataikemea kwani nao wanavihitaji sana vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alamsiki


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.