4 Jun 2007

Asalam aleykum,

Miongoni mwa mambo niliyozungumzia katika makala iliyopita ni namna “ugonjwa” wa “reality television” ulivyoenea huku ughaibuni.Kwa waliosahau, “reality tv” ni vipindi kwenye televisheni ambavyo hujaribu kuonyesha maisha ya mshiriki/washiriki kwenye kipindi hicho katika hali halisi.Hivi ni vipindi ambavyo kwa mfano hufuatilia maisha ya mwanamke mjamzito kwa miezi kadhaa hadi pale anapojifungua.Au wakati mwingine huonyesha maisha ya kundi flani likiwa limefungiwa sehemu flani huku kamera zikifatilia masaa 24 (mfano vipindi vya Big Brother).Nilieleza pia kuhusu mpango wa kampuni ya Endemol ya Uholanzi (ambayo hutengeneza vipindi vya runinga) kuandaa kipindi cha “Big Donor” ambapo washiriki wangeshindana kupata figo la mwanamama mmoja anayesubiri kufa kwa kansa.Endemol sasa wameibuka na kudai kuwa mpango wa kuwa kipindi hicho ulikuwa “hewa” (feki).Wanadai kuwa nia ya kuitangaza plani hiyo ilikuwa kutoa changamoto kwa wananchi kuhusu kuchangia viungo kwa wale wenye kuvihitaji.Wanajua wao kama hiyo ni kweli au porojo tu.

Pamoja na ukweli kwamba baadhi ya watu wanaviona vipindi vya “reality” kama vyenye nia ya kuwatumia washiriki wa vipindi hivyo kwa manufaa ya waaandaaji,vipo vipindi kadhaa vya “reality” ambavyo vinatoa mafundisho kwa jamii.Hapa ntazungumzia vipindi vitatu vyenye mantiki inayofanana.Kuna wakati flani,Michael Portillo,mmoja wa wanasiasa maarufu hapa UK aliamua kushiriki kwenye kipindi ambacho mama mwenye nyumba alimwachia mwanasiasa huyo jukumu la kutunza watoto kwa siku kadhaa.Ulikuwa ni mtihani kweli kwa Portilo ambaye pia ni mbunge katika chama cha kihafidhina cha Conservatives.Kuna wakati mtazamaji angejikuta anamwonea huruma mbunge huyo jinsi alivyokuwa “akipelekeshwa” katika jukumu la kutunza watoto hao.Lakini kipindi hicho kilipoisha,Portillo alieleza kuwa amejifunza mambo mengi sana katika muda aliokaa na watoto hao ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa kwa mama siku moja ya ulezi wa watoto ni zaidi ya majukumu ya ofisini.

Pia kuna kipindi kingine kinaitwa “wife swap.”Kipindi hicho huonyesha familia mbili zikibadilishana wake (mamsapu) na waume,ambapo mara nyingi familia hizo huwa zinatoka katika “backgrounds” tofauti kabisa (kwa mfano,familia inayoamini katika kuishi “fast life”-kinywaji,sigareti,muziki mkubwa,nk-na familia ya kilokole,au kwa mfano wa huko nyumbani,familia kutoka “ushuani” Oysterbay na nyingine kutoka Kimbiji).Katika kipindi hicho mke kutoka familia “iliyozowea raha” au inayoishi kwa kufuata “sheria kali” anaonjeshwa joto ya jiwe kwenye upande mwingine wa maisha,huku mume nae akienda kuonja ladha ya maisha ambayo ni tofauti kabisa na yale aliyozowea.Hebu fikiri mume aliyezowea kushinda baa akila kinywaji na kuvuta sigara moja baada ya nyingine anakwenda kuishi kwenye familia ya kilokole ambayo pombe na sigara ni dhambi kubwa pengine zaidi ya kuua.Au pale mke aliyezowea kufanyiwa kila kitu na hauzigeli anajikuta anawajibika kupika chakula,kulaza watoto na kufanya majukumu mengine ya ndani ambayo kwake ni sawa na ndoto ya mchana.Japo kuna wakati “swap” (mbadilishano) huo hupelekea kuleta songombingo za hali ya juu,mwishoni washiriki hukiri kuwa wamejifunza vitu vingi kwa kuishi maisha ambayo wamekuwa wakiyasikia au kuyaona kwenye runinga tu.
Kipindi cha tatu ambacho kilinivutia sana ni kile cha “Young Black Farmers” kilichoshirikisha kundi la vijana weusi “watukuku” tisa kutoka South London (hilo ni eneo la jiji hilo ambalo ni lazima uwe “ngangari” ili umudu maisha).Vijana hao ambao miongoni mwao kulikuwa na wauza unga, “mateja” (wabwia unga),makahaba,vibaka na matapeli,walipelekwa kwenda kuishi kwenye ranchi ya Wilfred Emmanuel-Jones,Mwingereza Mweusi ambaye alikuwa anaendesha shughuli za kilimo na ufugaji wa kibiashara kwenye eneo lililojaa watu weupe la Devon.South London imejaa watu weusi,na kwa vijana wengi wa maeneo hayo wazo la “kujichanganya” na watu weupe ni la mbali sana labda iwe kwenye usafiri,shuleni au ofisini.Sasa wazo la kuishi Devon ambako wengi wa wakazi wake hawajawahi kuwa na rafiki Mweusi,lilikuwa ni kama ndoto isiyoweza kuwa kweli.Vijana hao walitakiwa kutekeleza majukumu kadhaa hapo Devon na mshindi angeibuka na skolashipu ya kujifunza mambo ya kilimo na ufugaji hapo kwenye ranchi.Kwa lugha nyingine,ushindi katika zoezi hilo ulimaanisha kuepuka maisha waliyozowea vijana hao huko South London ya kukimbizana na polisi,kukwepa vita vya magenge na adha nyingine za maisha ya “kigetogeto.”Wapo walioachia ngazi siku za mwanzo tu,lakini wengine waliamua kupambana na ugumu wa kumkubalisha mtu mweupe aamini kuwa hata kijana Mweusi anayeamka kwa brekifasti ya “kokeni” anaweza kuwa mtu bora mwenye kujua majukumu yake katika jamii.Mwishoni mwa kipindi alipatikana mshindi mmoja ambaye nadhani alikuwa kibaka kabla ya kwenda hapo kwenye ranchi.Kwa wengine,licha ya kushindwa wote walikubali kuwa maisha ya kijijini hapo yamewapa fundisho kubwa sana maishani mwao.Na japo takriban wote walionyesha kukata tamaa siku walipowasili kijijini hapo kwa mara ya kwanza,siku ya kuondoka ilikuwa ni majonzi makubwa kwao kwani ilikuwa ni kama wameonjeshwa pepo na sasa wanarudi tena ahera.

Ningekuwa na uwezo ningeandaa kipindi kama hicho huko nyumbani.Ningemchomoa kigogo mmoja kutoka kwenye shangingi lake lenye kiyoyozi masaa 24 halafu ningempeleka Manzese Kwa Mfuga Mbwa akaone shida ya maji huko,asome kwa koroboi kwa vile kama ilivyo sehemu nyingi za uswahilini Tanesko huwa wanajiamulia tu kukata umeme bila taarifa,na asubuhi ashuhudie namna gani ilivyo vigumu kubanana kwenye daladala (kama atafanikiwa kupanda,na iwapo kitambi chake kitastahimili m-banano huo),halafu nimtembeze kwenye mitaa aone namna watu wanavyopigwa “roba za mbao” kirahisi,ningempitisha Uwanja wa Fisi aone vibinti vidogo kabisa vinavyotumikishwa kama makahaba.Na pengine ningemchomoa bimkubwa mmoja kutoka ushuani Masaki halafu nimpeleke Sofi Majiji (tafuta kwenye ramani ya nchi yetu ufahamu nazungumzia sehemu gani).Ningemtaka aende na watoto wake kisha watoto hao wa “kishua” waende ziara ya angalau wiki moja kwenye “shule halisi za msingi vijijini”,wamsikilize mwalimu wakiwa wamekalia matofali huku mama yao akiwa ameenda porini kutafuta kuni na akirudi aende kisimani kuchota maji.Ningetaka mama na watoto hao waonje ladha ya namna ya kubalansi maisha kwa shilingi mia tano kwa siku na kula ugali na matembele yasiyo na chumvi wala hayajaungwa kwa vile shilingi alfu haitoshi.Halafu wakishaumwa na mbu waende zahanati ya kijiji,wapange foleni masaa kadhaa kisha “watolewe upepo” kupimwa maleria,halafu waandikiwe dawa ambazo hazipo hapo kwenye zahanati.Pia ningemkurupusha kigogo mmoja wa NGO ya UKIMWI nimpeleke akaishi na waathirika “halisi” wa ugonjwa huo (na sio wale “walengwa” kwenye ripoti za mwaka),akaone maana halisi ya unyanyapaa,aone namna gani madawa ya kuongeza maisha (ARVs) yalivyo adimu,na pengine aangalie kama kweli akirejea ofisini NGO yake iendelee kudai kuwa ipo kwa ajili ya kuhudumia waathirika wa UKIMWI au ipo kwa ajili ya kuhudumia “kifriji” chake na nyumba ndogo yake.Nadhani vipindi hivyo vingetoa fundisho kubwa sana.

Mwisho,nimechekeshwa na habari moja kwamba wana-CCM huko Ulanga na Kilombero wanataka kuwashtaki wabunge wao eti kwa vile wameshindwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.Nimecheka kwa vile wanaolalamika ndio haohao waliowapa ubunge walalamikiwa.Hivi wanaolalamika walijiuliza vya kutosha kabla ya kupiga kura kuwa wanayoahidiwa na walalamikiwa yatatekelezwa au yanatekelezeka?Hivi waliusikia vizuri ule wimbo wa “ndio mzee” wa Joseph Haule (Profesa Jay wa Mitulinga) ambapo mgombea ubunge anaahidi kutatua matatizo ya usafiri kwa kuleta helikopta?Nadhani wapiga kura wana tatizo la kuamini neno “NITAFANYA…” badala ya “NILIFANYA…”Yaani kigezo cha kumchagua mtu kisiwe atafanya nini bali ameshafanya nini.Mmoja wa walalamikiwa hao amenukuliwa akisema kuwa kazi ya kuleta maendeleo si ya mbunge pekee.Angalau ameongea kistaarabu kuliko Mheshimiwa mmoja (mbunge wa zamani jimbo moja la Dar) ambaye aliposikia wapiga kura wanamlalamikia aliwapa kitu “laivu” kwamba walimchagua kwa hela zake alizowapa wakati wa kampeni,sasa wanapolalamika wakati wameshakula hela hizo wanamtaka yeye afanye nini!

Alamsiki

1 comment:

  1. Duh!Mzee kwelitupu!Vipo vipindi ambavyo vinaelimisha. Kama ulivyo vitaja hapo juu.Ni kweli mara nyingi ni vigumu kuelewa maisha ya watu wengine bila kujaribu kuishi kama wao. Lakini nahisi pia siku inakuja ambayo inabidi TZ tuwe na vipindi vingi vielimishavyo ambavyo tunajitengenezea wenyewe. Hicho kipindi cha young black farmers sijawahi kukiona. Lakini baada ya dondoo uliyoweka nimejiuliza tu kuwa hao walioonjeswa maisha mengine halafu wakarudi kulekule sijui kwamuda gani wataweza kutumia walicho jifunza. Kwa sababu mara nyingi mazingira unayojivinjari yanaweza kukusababisha ushindwe kuacha katabia fulani. Hapa na maana kuwa, kama wewe mtumiaji madawa ya kulevya halafu unaishi na watumia madawa ya kulevya ni vigumu kuacha hata kama unajua unatakiwa uache.Kwa sababu kuna baadhi ya programs ambazo zinaelimisha watu lakini haziwajengi kujikwamua kutoka katika tatizo.Ningependa Tanzania tukianza kufanya haya maswala uwepo vilevile katika mpango jinsi ya kuwa saidia hata walioshindwa baada ya proguramu.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube