18 Oct 2007

Nadhani sio wazo baya kuja na makala mbili kwa mpigo.Usichoke kusoma,au kama namna gani vipi soma moja halafu nyingine iweke kiporo uisome baadae.

KULIKONI UGHAIBUNI-82

Asalam aleykum,

Siasa za kimataifa zina vituko vyake,na pengine hakuna mahala pazuri vya kushuhudia vituko hivyo zaidi ya kuangalia baadhi ya siasa za nadani na za nje za Marekani.Hivi karibuni kumeibuka mgawanyiko baina ya pande mbili za siasa za nchi hiyo,yaani chama cha Democrats na kile cha Republicans,kuhusu unyama uliofanywa na Uturuki kwa Waarmenia mwaka 1915 ambapo inakadiriwa zaidi ya watu milioni moja walipoteza maisha.Democrats wanataka Marekani itamke bayana kuwa unyama huo uliosababisha maafa makubwa ni sawa na “genocide”,yaani mauaji ya halaiki kama yale ya Rwanda au yale ya Manazi dhidi ya Wayahudi.Lakini Republicans wanasema kuwa kwa kufanya hivyo Marekani itajiweka pabaya katika vita yake dhidi ya ugaidi ambapo Uturuki ni mshirika wake wa karibu.Democrats wanaoona kwamba siasa za kuwapendeza marafiki walioshiriki kwenye vitendo vya kukiuka haki za binadamu sio wazo la busara pengine kwa imani kwamba pasipo Marekani kuweka bayana msimamo wake katika suala hilo itapelekea kuchafua taswira yake kama taifa linalopigania usawa katika kila kona ya dunia (kwa mujibu wa imani ya nchi hiyo).Tayari Uturuki imeanza kutunisha misuli yake kwa kumtaka balozi wake huko Marekani kurejea nchini kwake “kwa majadiliano” (hiyo ni lugha ya kidiplomasia ya kuonyesha kutoridhishwa na mambo flani) na pia kumekuwa na maandamano ya kulaani jitihada zinazoendelea nchini Marekani kuutangaza unyama huo kuwa ni “genocide”.

Kimsingi,Marekani inategemea sana maelewano yake na Uturuki hasa kwa vile nchi hiyo inaweza kuvamia kaskazini mwa Iraki wakati wowote ule kuwadhibiti Wakurd ambao kwa Uturuki wanaonekana kama magaidi wa namna flani.Ni dhahiri kwamba kwa namna hali ya usalama nchini Iraki ilivyo legelege,uvamizi wa Uturuki kwa Wakurd utaleta mparaganyiko mkubwa zaidi ya uliopo sasa.Pia Uturuki inafuatilia kwa karibu sana mwenendo wa mambo huko Irak hasa inapojitokeza hoja ya kuwa sera ya majimbo (yaani Wakurd kaskazini,na waumini wa madhehebu ya Sunni na Shia katika maeneo yaliyosailia). Wapo wanaodhani suluhu ya kudumu nchini Irak itapatikana tu pale nchi hiyo itapogawanywa kwa misingi ya kidini/ukabila,pengine kwa vile jitihada za kuwaunganisha Wairak zinaelekea kuwa ngumu kuliko kuchanganya maji na mafuta.Hofu ya Uturuki ni kwamba iwapo Wakurd watapata “uhuru” wa namna hiyo basi kuna uwezekano wakajaribu kuvuruga amani nchini Uturuki.Hivi sasa nchi hiyo inasubiri idhini ya bunge la nchi hiyo kabla haijaanza “kuwashughulikia” inaowaita magaidi wa Kikurd kaskazini mwa Irak.Uhasama kati ya Waturuki na Wakurd ni wa muda mrefu sana,na kuelezea kwa undani kutahitaji makala nzima.Pamoja na vurugu zinazoendelea nchini Irak,eneo la kaskazini mwa nchi hiyo linalokaliwa na Wakurd limetulia kwa kiasi kikubwa,na iwapo Uturuki itavamia eneo hilo basi ni dhahiri kwamba jiographia nzima ya vita ya Irak itabadilika.

Hebu tuangalie mambo huko nyumbani kwenye anga za soka,hususan ubabaishaji usioisha wa wakongwe wetu wa soka Simba na Yanga.Hivi ni lini vilabu hivi vitatambua kwamba ni rahisi zaidi kupata damu kutoka kwenye jiwe kuliko kupata kocha mahiri wa kigeni kuingia mkataba wa muda mrefu na vilabu hivyo?Nionavyo mie,suala la makocha wa kigeni limekuwa ni la ushabiki zaidi kuliko mantiki.Utasikia moja ya vilabu hivyo ikidai kuwa na orodha ya makocha kadhaa wa kimataifa ambao wameonyesha nia ya kuja kufundisha.Well,sisemi kwamba hilo haliwezekani lakini cha msingi hapa sio kuwa na makocha kadhaa “wachovu” bali wataaluma wa soka ambao wataleta mapinduzi ya kweli kwenye vilabu hivyo.Hivi kuna mtu mwenye busara yake ambaye yuko tayari kuacha shughuli zake huko aliko na kwenda kubahatisha maisha nchi nyingine kwenye timu ambazo uhai wa uongozi ulio madarakani ni wa kusuasua kuliko wa joto la mgonjwa wenye homa ya vipindi.

Na japo nafahamu kuwa sio dhambi kutafuta makocha ya nje ya nchi,swali la msingi wanalopaswa kuulizwa Simba na Yanga ni hili:kama mara kadhaa wanashindwa kumudu gharama za makocha wa ndani ambao wanalipwa kwa sarafu ya Tanzania,watawezaje kumudu mshahara unaopaswa kulipwa kwa dola ya Kimarekani.Kocha yeyote mzuri hawezi kuvumilia ubabaishaji unaopelekea kocha huyo aonekane hafai.Ni kama Jose Maurinho alivyoamua kuachana na klabu ya Chelsea baada ya kutofautiana na bilionea mmiliki wa timu hiyo Abrahmovic.Ili timu ifanye vizuri inahitaji uongozi imara,uongozi ambao utamudu kutekeleza matakwa ya kocha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba programu yake ya maendeleo ya timu inafuatwa vizuri,uongozi ambao hautakuwa “ukimsomesha” kila kukicha kocha kuhusu stahili zake.Kigumu zaidi kwa wakongwe hawa wa soka kumudu kuleta makocha wa kigeni ni huo utegemezi wao kwa wafadhili.

Kuna wakati huwa najiuliza iwapo baadhi ya viongozi wa vilabu hawa wanafahamu kuwa timu zao ziko Tanzania,na sio katika nchi ya Magharibi ambako kuna siku mabilionea huwa “wanawashwa” na utajiri wao na kuamua kumwaga fedha kana kwamba wamepagawa.Lakini hata mabilionea hao huwa hawapati “kichaa” hicho kwa mwaka mzima,na kwa maana hiyo wanakuwa makini sana na fedha wanazotoa kama msaada.Sasa nani anatarajia tajiri mmoja awe anamwaga fedha zake kwa klabu ambayo si ajabu wakati mwenendo wake kwenye ligi unasuasua huku wachezaji wakilalama njaa (japo mfadhili anatoa fedha za mishahara),viongozi wanazidi kunawiri.Kwenye somo la sosholojia kuna “kanuni ya kupeana” (exchange theory) ambapo inaaminika kwamba kila anayetoa kitu anategemea kupata kitu flani.Mfano mwepesi ni pale unapotoa senti zako kwa ombaomba barabarani.Iwapo atanyoosha mikono juu kukuombea dua kwa ulichompatia basi kuna uwezekano kesho yake utampatia tena msaada kwa vile siku iliyopita alikurudishia fadhila kwa njia ya “dua” (kuonyesha shukrani zake).Kadhalika,mfadhili anapojitokeza kudhamini timu anatarajia kupata kitu flani,kama sio faida kwa kuitangaza kampuni au bidhaa zake basi angalau matokeo ya timu husika yawe ya kuridhisha (hapo anachorudishiwa ni liwazo la moyo,au tuite “kutarazika” kwa Kiswahili cha pwani).Hata kama atajitokeza tajiri ambaye anageuza mchanga kuwa fedha ni dhahiri atachemsha tu akijiingiza kwenye udhamini wa vilabu hivi kwani mara nyingi harufu ya fedha kwa waungwana hawa ni kama nuksi inayosababishwa na bahati ya utajiri wa raslimali katika baadhi ya nchi za dunia ya tatu.

Zamani nikuwa nafuatilia ratiba ya ligi kujua lini itakuwa siku ya siku ya mtanange kati ya watani wa jadi.Siku hizi sina muda mbovu namna hiyo kwani raha ya enzi hizo ilikuwa kushinda mechi zote,na droo ilikuwa ni sawa na kupoteza mechi.Sasa hata Simba wakiifunga Yanga ilhali wameshatandikwa na Coastal Union na Prisons,na pengine kuishia kuukosa ubingwa,huo ushindi dhidi ya watani wao unakuwa na maana gani.Niite “Sultani njozi” lakini kwangu umuhimu pekee wa mechi ya watani hao wa jadi ni kwamba yeyote atakayefungwa atakuwa amefungulia kifuniko kinachozuia (kwa muda) migogoro ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa inanyemelea klabu zote mbili.Mie sio muumini wa kulaumu pasipo kutoa ushauri lakini pia yayumkinika kusema kwamba kuzishauri Simba na Yanga zifanye mambo yake katika namna inavyopaswa kuwa ni sawa na kujaribu kumtafuta paka mweusi kwenye chumba chenye giza ilhali paka huyo hayupo kabisa chumbani humo.Ni kupoteza muda.

Alamsiki
$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$

KULIKONI UGHAIBUNI-81

Asalam aleykum,

Kwanza inabidi niwatake radhi wasomaji wapendwa wa safu hii baada ya kupotea kwangu wiki mbili zilizopita.Haikuwa nia yangu kutojumuika nanyi katika safu hii bali ni kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.Napenda kuwahakikishia kuwa nitakuwa nanyi kama hapo awali.

Miongoni mwa matukio ya muhimu yanayojiri hapa Uingereza kwa sasa ni pamoja na kesi inayoendelea dhidi ya polisi kuhusiana na kifo cha raia wa Brazil (aliyekuwa na makazi jijini London) Jean Charles de Menezes,aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi waliomfananisha na gaidi waliyekuwa wakimwinda.Tukio hilo lilitokea mwaka juzi siku chache baada ya mashambulizi ya kigaidi kwenye mfumo wa usafiri wa jiji la London ambapo vijana watatu walijilipua mabomu ya kujitoa mhanga kwenye treni za chini ya ardhi na mmoja alijilipua kwenye “daladala”,mashambulizi yaliyochukua uhai wa zaidi ya watu 50 huku wengine kadhaa wakiachwa na majeraha ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu.M-Brazil huyo alikumbana na mauti yake katika namna ya kusikitisha.Polisi walikuwa wakimwinda gaidi flani aliyekuwa akaishi kwenye ghorofa moja na alilokuwa akaishi de Menezes,na kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikana baadaye,polisi hao walishasisitizwa kwamba gaidi huyo “adhibitiwe kwa gharama yoyote ile”.Kwa bahati mbaya au pengine kwa uzembe (mahakama ndio itaamua) de Menezes alipotoka kwenye makazi yake,alidhaniwa kuwa ndie huyo gaidi aliyekuwa akiwindwa,na polisi walimfuatilia hadi alipoingia kwenye treni kabla ya kumdhibiti na hatimaye kummwagia risasi kadhaa zilizochukua uhai wake hapohapo.Haikuchukua muda mrefu kubainika kuwa aliyeuawa alikuwa raia asiye na hatia,lakini hiyo sio kabla ya baadhi ya magazeti kuibuka na stori kuwa “big boss” wa mashambulizi ya kigaidi ameuawa,wakidhania kuwa M-Brazil huyo alikuwa ndiye hasa anayesakwa na polisi.

Kwa kawaida ya hapa,pindi polisi wakiua,kamisheni huru inayofuatilia utendaji wa polisi (IPCC) hujitosa mara moja kuendesha uchunguzi wake.Na hivyo ndivyo ilivyokuwa baada ya kifo cha M-Brazil huyo.Matokeo ya uchunguzi wa IPCC yalionyesha kuwa polisi walikuwa na makosa yaliyosababishwa na mkanganyiko baina ya viongozi wa mkakati wa kumnasa gaidi aliyekuwa akiwindwa,askari waliokuwa wakimfuatilia gaidi huyo na askari wa kitengo cha SO19 ambacho ni wataalamu wa silaha.Hata hivyo,IPCC haikupendekeza hatua zozote za kisheria dhidi ya wahusika kwa madai kwamba lengo la operesheni hiyo lilikuwa ni kwa ajili ya maslahi ya usalama wa umma lakini uzembe uliojitokeza ulipekea kifo cha mtu asiye na hatia.Badala yake,suala hilo lilielekezwa kuwa kinyume na sheria ya Afya na Usalama (health and safety act),ambapo kimsingi ilipunguza uzito wa kosa zima.Kwahiyo,hivi sasa kesi hiyo inaendelea kuunguruma huku mashahidi mbalimbali wakielezea namna de Menezes alivyokutana na mauti yake.Pamoja na kukiri makosa yao,polisi wameendelea na msimamo kuwa nia yao ilikuwa nzuri,yaani kumdhibiti gadi waliyekuwa wakimfuatilia,na mkanganyiko wa kumfananisha de Menezes na gaidi huyo inaweza kuwa matokeo ya presha iliyokuwa ikivikabili vyombo vya usalama katika kipindi hicho cha mashambulizi ya ugaidi jijini London.

Kimsingi,utendaji kazi wa polisi (na vyombo vingine vya usalama) hapa Uingereza ni kama mtihani wa namna flani.Kwa upande mmoja wanategemewa kuhakikisha raia wako salama muda wote,lakini kwa upande mwingine wanatakiwa wasiminye haki za raia kwa kisingizio cha kuwalinda raia hao.Na hapo ndipo siasa za ndani za Uingereza zinapokinzana sana na za Marekani.Baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11,2001,usalama wa raia nchini Marekani ulichukua umuhimu wa juu zaidi kuliko haki za kiraia,tofauti na hapa ambapo watengeneza sheria wameendelea kusisitiza kwamba kusalimisha uhuru wa raia (civil liberty) katika jina la kuilinda jamii dhidi ya magaidi ni sawa na kuwazawadia magaidi hao ushindi wa mezani.

Mamlaka husika zinajitahidi kuwaandaa polisi wafanye kazi kwa ufanisi lakini bila kunyanyasa raia.Japokuwa polisi wamekuwa wakilaumiwa sana kwa ubaguzi (yaani namna wanavyodili na raia weupe na wale wasio weupe) ukweli unabaki kwamba mamlaka husika zinajitahidi ipasavyo katika kutekeleza wajibu wake.Lakini hata baada ya kutekeleza wajibu huo kwa kuweka wazi taratibu zinazotakiwa kufuatwa na polisi,kuwapo kwa taasisi huru kama IPCC kunasaidia kuwafanya polisi wawajibike ipasavyo zaidi.Yayumkinika kusema kwamba askari polisi hapa hufikiria kwa makini sana kabla hajafikia uamuzi wa kutumia nguvu ya ziada au silaha aliyonayo.

Nimeona habari moja ya kusikitisha kwenye gazeti flani la huko nyumbani ambapo inadaiwa kwamba mkazi mmoja wa Wilaya ya Kilombero aliuawa kutokana na mateso aliyopewa na polisi.Kwa mujibu wa habari hiyo,marehemu alikutana na mauti yake baada ya kifikishwa “Kalvari” ya polisi hao (Kalvari ni mahala aliposulubiwa Yesu Kristo).Hili limekuja miezi michache baada ya kifo cha mfugaji mmoja wilayani humo ambaye kifo chake kilizua maswali kutokana na tofauti za maelezo kati ya polisi wilayani Kilombero (yaliyoungwa mkono na daktari mmoja wa hospitali ya Mtakatifu Francis ya Ifakara) na matokeo ya uchunguzi wa maiti katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.Binafsi sijasikia matokeo ya uchunguzi wa kifo cha mfugaji,lakini naamini sheria itachukua mkondo wake.Siongelei matukio ya wilayani Kilombero kwa vile ni maeneo ya nyumbani,bali nashawishika kutoa changamoto kwa polisi wetu kutambua uhumimu wa usawa katika utekelezaji wa majukumu yao na haki za kiraia walizonazo wananchi wa kawaida.

Nadhani wapo watakubaliana nami kwamba kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu utendaji wa polisi wetu hususan linapokuja suala la kuthamini haki za raia.Utakuta askari trafiki anasimamisha daladala pengine kwa nia nzuri tu lakini pasipo kujali kuwa kuna abiria wanaowahi shughuli zao mbalimbali.Katika mazingira kama hayo,namna pekee ya kuonyesha kujali haki za abiria hao ni kumpatia dereva maelekezo mafupi (kwa mfano kujisalimisha mwenyewe kituo cha polisi baada ya kukamilisha ruti yake) au kuwasihi abiria watafute usafiri mwingine badala ya kuwagandisha muda mrefu katika mazingira yanayoweza kuzusha hisia kwamba trafiki “anadai kitu kidogo”.Kuna wakati flani nilijikuta nikiwa “mwenyeji” kwenye kituo flani cha polisi wilayani Kinondoni baada ya kuingizwa mjini na vibaka walionikwapulia kiselula changu.Ziara zangu za mara kwa mara kituoni hapo zilinipa picha ambayo sio ya kupendeza sana.Ifahamike kuwa sio kila anayekamatwa na polisi ana makosa,huyo ni mtuhumiwa,na ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kuthibitisha (au kukanusha) tuhuma dhidi ya mtuhumiwa.Yayumkinika kusema kuwa baadhi ya polisi wanajiona kama wako juu ya sheria na maneno “haki za binadamu” au “uhuru wa raia” ni mithili ya misamiati mipya vichwani mwao.Ifahamike kuwa silizungumzii jeshi zima la polisi bali baadhi ya watendaji wa jeshi hilo ambao licha ya kuchafua jina la taasisi hiyo muhimu,wanaikwamisha pia katika utendaji kazi wake hasa katika maeneo ya “uswahilini” ,wilayani na vijijini ambako baadhi ya polisi hugeuka Miungu-watu.Na watu wanawaogopa kweli hasa kwa vile wanafahamu kuwa wanaweza kumzulia mtu kesi na kama hana uwezo wa kupata wakili mzuri basi ataozea jela.

Nafahamu kuwa kuna kitu kinachoitwa tume ya haki za binadamu na utawala bora (sina uhakika sana na jina hilo,pengine kwa vile taasisi hiyo haisikiki sana) lakini yayumkinika kusema kwamba kuwa na taasisi pekee haimaanishi kwamba mambo yatakwenda vema bali kuwa na taasisi ambazo zinaonekana zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.Iwapo polisi huwa wanasihi wananchi mara kwa mara kuepuka kujichukulia sheria mikononi (mob justice) je wananchi wajifunze nini pindi mtuhumiwa anapofia mikononi mwa polisi (“police justice”?!!!).Huku nikiamini kuwa tukio hilo la mauaji ya “Kalvari” wilayani Kilombero litafanyiwa kazi,nimefarijika kusikia agizo la serikali kupiga marufuku kuwaweka watuhumiwa kituo cha polisi zaidi ya masaa 24 (japo hayo masaa 24 ni mithili ya karne nzima kutokana na mazingira ya kutisha kwenye selo hizo).


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube