7 Oct 2007

MTANZANIA UGHAIBUNI-2

Asalam aleykum,

Niseme bayana kwamba napenda sana kuangalia runinga kila nafasi inaporuhusu. Na kwa mazoea hayo, napenda kutamka bayana kwamba mara nyingi huwa nafahamu mengi ya yanayojiri katika sayari yetu hii. Lakini pia ni vema nikisema kwamba “mahaba” yangu kwa runinga huwa mara kadhaa yananiacha na maswali mengi kuliko ajibu, na kuna nyakati huwa nabaki na majonzi napoona namna wanadamu wenzetu wanavyosumbuka na kuteseka katika sehemu flani za dunia yetu. Ni mengi, lakini linalovuma sana kwa sasa hivi katika “channels” mbalimbali za ni namna utawala wa kidikteta huko Burma unavyoendesha kampeni zao za kimyama dhidi ya watu wasio na hatia ambao wamechoshwa na miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi. Inatia uchungu kuona picha za miili ya watawa wa Kibudha (Buddhist monks) iliyotelekezwa mitaani au inayoelea kwenye maji yote yakiwa ni matokeo ya mtangange kati ya vyombo vya dola vya nchi hiyo dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakidai demokrasia na kupinga udikteta. Inaumiza zaidi kuona kauli “za kisanii” za Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya au Marekani zinazodai kuwa “duni inaona unyama huo na haitavumilia” ilhali hakuna mikakati yoyote thabiti ya kuwapa matumaini watu wanaoteseka huko Burma kwamba siku moja wataamka wakiwa na amani ya kudumu. Ni hadithi zisizotofautiana sana na zile walizosikia wenzetu wa Rwanda wakati wa mauaji ya halaiki,au zile zinazoleta matumaini “hewa” kila kukicha huko Darfur au Somalia.Hili dude linalooitwa “Jumuiya ya Kimataifa” limezidi kuthibitisha kuwa ni la kufikirika zaidi kuliko lenye ufanisi kwani laiti lingetafsiri kauli zake katika vitendo basi kwa hakika dunia ingekuwa ni mahala salama sana.

Hivi runinga zingeendelea kutuonyesha picha hizi za kusikitisha sembuse nchi kama Marekani ingeamua kwa dhati kukomesha mateso yanayoendelea sehemu mbalimbali duniani?Hivi mamilioni ya waliokata tamaa na maisha ingeendelea iwapo tamaa ya mafuta katika seheu kama Iraki ingekuwa ajenda ndogo kuliko kapata haki halisi za binadamu katika sehemu zilizogubikwa na mateso duniani?Kwa hakika dunia ingeweza kabisa kuwa sehemu mwafaka ya kuishi kwa kila binadamu iwapo wale wenye uwezo wa kukomesha mateso hayo wangedhamiria kwa dhati kuhakikisha kwamba hakuna nafasi kwa madikteta kunyanyasa wale wasio na hatia.Nakubali kwaba ugaidi ni tishio kubwa kwa amani ya dunia yetu lakini kuna matishio mengine ambayo yanawaathiri wanadamu kila kukicha kuliko huo ugaidi,matishio hayo yakiwa ni pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu na rushwa zinazodumaza maendeleo ya nchi nyingi za dunia ya tatu licha ya misaada lukuki inayomwagwa kuzikwamua nchi hizo.

Mimi naamini kuwa nchi tajiri na zenye nguvu za kuamua namna gani sie maskini tuishi zina uwezo wa kukomesha uonevu huu.Hivi mabenki makubwa katika nchi hizo yangeamua kwa dhati kuwabana wale ambao wanawekeza mabilioni ya dola kwenye akaunti katika mabenki hayo (ilhali maelfu kwa maelfu ya wanaowaongoza ni maskini wakutupwa ) kwa kuwauliza tu swali jepesi la “mmepata wapi fedha hizi” isingesaidia kuwafanya wabadhirifu,wala rushwa na wezi wa raslimali kujiuliza mara mbilimbili kabla ya kuiba?Mjuzi mmoja wa wizi wa raslimali za baadhi ya nchi za dunia ya tatu alinieleza kwamba kwa kuhofia kutaifishwa raslimali zao,wezi wengi katika nchi hizo hupendelea kuweka fedha zao katika mabenki ya nje kwa vile huko ndiko salama zaidi.Mjuzi huyo alidai pia kwamba nchi na mashirika wahisani hawajali sana kuhusu vilio vya wanaoibiwa au kuwa na uchungu na misaada wanayotoa kwa vile wanafahamu fika kuwa fedha hizo haramu zitarudi mikononi mwao (wahisani) kupitia akaunti za siri za wezi hao.

Siku moja niliwahi kuulizwa na rafiki yangu mmoja Mkenya kwamba kwanini Tanzania ina amani zaidi kulinganisha na jirani zake.Nikamweleza kwamba pamoja na sababu nyingine ikiwa ni pamoja na hekima na busara za Baba wa Taifa za kuwaunganisha Watanzania na mchango wa lugha ya Kiswahili,sababu muhimu ni kwamba Watanzania licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120 ni kama watu wa ukoo mmoja.Sensa zetu huwa hazichanganui mwingiliano wa makabila huko nyumbani,lakini ni dhahiri kuwa zoezi hilo likijaribiwa litakuwa gumu sana kwa vile kuna mwingiliano mkubwa mno.Nikiangalia kwenye ukoo wetu nakuta kuna ninaowaita ndugu zangu ambao kimsingi asili yao ni makabila tofauti na asili ya ukoo wetu.Na hata hiyo asili yenyewe ya ukoo wetu inaweza kuwa ni ya jumlajumla tu (general) kwani historia inaonyesha kuwa mengi ya makabila ya kibantu yaliyopo huko nyumbani yapo yalipo sasa baada ya mtawanyiko wa Wanguni walioingia nchini kutokea sehemu nyingine.Mama yangu ni M-bena lakini makazi ya Wabena hawa ni Malinyi wilayani Ulanga.Na kuna Wabena wengine huko Iringa ambao kuna madai ya kihistoria kuwa hawa ni watu wa asili moja na hao Wabena wa Malinyi.Ngoja “nisichanganye madawa” (nisikoroge mambo) hapa.Hoja nayotaka kuitengeneza hapa ni kwamba mtu anaweza kufanya ubadhirifu akidhani anainufaisha familia yake pekee kumbe wakati huohuo anawaathiri ndugu zake wengine ambao kwa sababu za kihistoria wako katika makabila mengine.Laiti sote tungeangaliana kama Watanzania wenye asili zinazoshabihiana basi yayumkinika kusema kwamba baadhi ya wala rushwa na wabadhirifu wangeweza kuwa na huruma kwa ndugu zao.Lakini hata tusipoiangalia hoja hii ya umoja katika tofauti zetu (yaani kuwa katika makabila tofauti japo asili zetu zinashabihiana) kuna ukweli usiopingika kwamba kukwaza maendeleo katika kipindi hiki ni sawa na kuvichimbia makaburi vijukuu vitakavyokuwa vinahitaji baadhi ya huduma ambazo baadhi ya wabadhirifu wanazibinafsisha kuwa zao binafsi badala ya kujenga misingi ya vizazi vijavyo.Kuna wakati huwa nashindwa kupata majibu naposikia mtu amekwiba fedha za ujenzi wa mradi flani wa maendeleo japo ana watoto kadhaa katika familia yake na wengine kadhaa zaidi nje ya ndoa.Laiti mtu huyu angekuwa na akili basi ni dhahiri angetambua kuwa watoto wake lukuki aliokuwa nao sasa watamletea wajukuu baadae ambao nao wataleta watoto na wajukuu zaidi,na kwa maana hiyo kitendo chochote cha kukwaza maendeleo hivi sasa kitaathiri vizazi vyake vijavyo.Napenda kuamini kabisa kuwa yeyote yule mwenye upendo wa dhati na vizazi vyake vijavyo,achilia mbali vile vya wenzie,atafanya kila liwezekanalo kuitumikia nchi yetu kwa namna ambayo vizazi hivyo vijavyo havitapatwa na hasira za kubomoa makaburi yetu miaka 20 au 50 ijayo kwa hasira za kutengenezewa msingi mbaya wa maisha.Na kwa wale wanaoamini kuwa kuna moto wa kiyama baada ya kifo basi naamini watafanya kila wawezalo kukata tamaa zao za kidunia kwani bila kufanya hivyo watageuzwa kuwa kuni kwenye moto wa ahera.

Nimalizie kwa kuzungumzia kituko kimoja nilichokisoma katika gazeti flani la wiki iliyopita.Kituko hicho kinahusu kesi ya Profesa Mahalu,ambapo kwa mujibu wa gazeti hilo,wanasheria wa serikali wamekiri kuwa kesi hiyo “haina mwenyewe”.Nachojiuliza ni hiki,kama kesi haina mwenyewe sasa wao wanakwenda mahakamani hapo kumwakilisha nani!Hivi zile kesi za Jamhuri dhidi ya flani zimekufa siku hizi?Ningeelewa walichosema wanasheria hao wa serikali kama wangekuwa wametoka taasisi zinazotoa msaada wa kisheria,ambazo kimsingi zinaweza kudakia kesi yoyote ile kwa minajili ya kutaka haki itendeke.Mie sio mwanasheria,lakini pamoja na umbumbumbu wangu katika taaluma hiyo nadhani hawa waungwana wangeweza kabisa kuitaja Jamhuri kuwa ndio yenye kesi dhidi ya mwanadiplomasia huyo,hasa kwa vile wao ni waajiriwa wa Jamhuri na sio magazeti yaliyoibua madai hayo.Na iwapo walikuwa wakiamini kwamba chanzo za kesi hiyo ni hayo magazeti basi pengine ingeleta maana zaidi iwapo wangeyashawishi magazeti hayo kufungua kesi halafu wao wayasaidie katika kesi hiyo.Lakini pia kama wanadhani hakuna mlalamikaji katika kesi hiyo basi ni bora waachane nayo tu kwa vile kwa namna “wanavyowajibika” ni dhahiri kuwa huko mbele tutasikia vituko vikubwa zaidi ya hiki nachokielezea hapa.Kama dada yangu Freda anavyopenda kusema,hii ni kaaazi kweli kweli.

Alamiski


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube