1 Feb 2008

Makala yangu hii ilitoka katika toleo la jana la gazeti la Mtanzania

Miongoni mwa adha za kumiliki runinga hapa Uingereza ni kuilipia ada ya leseni (TV Licence Fee).Ada hiyo kwa kiasi kikubwa hutumika kuendesha BBC ambalo ni shirika la utangazaji la nchi hii.Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kwamba baadhi ya vipindi vya BBC havina ladha inayoweza kuhalalisha shirika hilo kuendelea kupewa ruzuku inayotokana na ada ya leseni za runinga.Hata hivyo,BBC imeendelea kuwa shirika la habari maarufu na lenye mtandao mkubwa sio tu ndani ya Uingereza bali duniani kwa ujumla.Na miongoni mwa vipindi maarufu vya shirika hilo la habari ni Newsnight,kipindi kinachoonyeshwa siku za wiki kuanzia saa 4.30 usiku.

Kipindi hicho huchambua habari muhimu zilizojitokeza katika siku husika ndani na nje ya nchi hii.Hivi karibuni,Newsnight ilizungumzia machafuko yanayoendelea nchini Kenya.Kwa hakika ilikuwa inatia uchungu kuona namna watu wanavyotaabika nchini humo.Moja kati ya mambo yaliyolinisikitisha zaidi ni mahojiano mafupi kati ya mtangazaji wa BBC aliyeko nchini Kenya na mwanamama mmoja ambaye wakati wa mahojiano hayo alikuwa kamanda wa polisi wa eneo flani (jina la afande huyo na mahala alipokuwa anaongoza vimenitoka kidogo).

Kamanda huyo alianza mahojiano hayo kwa kukanusha madai kwamba jeshi la polisi la Kenya limekuwa likiuwa raia wasio na hatia katika kutekeleza sera ya “piga risasi kuua” (shoot-to-kill policy).Alidai kuwa wanachofanya wanausalama ni kudhibiti machafuko na uhalifu.Mwishoni mwa mahojiano,afande huyo alieleza uchungu alionao kuona nchi yake ikiteketea.Alisema kwamba ameshatembelea sehemu nyingi duniani na kuona watu wa nchi hizo wakiwa na fahari na nchi zao,jambo ambalo lilimwongezea mapenzi kwa nchi yake.Aliwalaumu wanasiasa wa Kenya kwa kuzorotesha jitihada za kuleta amani.

Cha kusikitisha ni kwamba kamanda huyo aliyeonekana kuguswa sana na madhila yanayowakumba Wakenya wenzie aliondolewa kwenye usimamizi wa operesheni za mitaani na kukabidhiwa majukumu ya kiofisi (desk job).Yaani aliadhibiwa kwa kusema ukweli wa moyoni mwake kuhusu namna wanasiasa wanavyoendekeza maslahi yao kuliko ya nchi na wananchi.Naamini mwanamama huyo ni mmoja tu kati ya askari wengi ambao wanalazimika kupiga na hata kuua Wakenya wenzao katika kutekeleza amri “halali” za serikali.

Ilielezwa katika kipindi hicho cha Newsnight kwamba licha ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwezi Desemba mwaka jana kuwa chanzo kikuu cha machafuko hayo yasiyoonyesha dalili ya kupungua,msingi wa matatizo ulijengwa miaka kadhaa iliyopita.Kwa mujibu wa uchambuzi wa wajuzi wa siasa za Kenya,kwa muda mrefu kumekuwa na manung’uniko miongoni mwa baadhi ya makabila kuhusu umiliki wa njia za uchumi ambapo inadaiwa Wakikuyu wamekuwa na upendeleo zaidi.

Tofauti za kikabila na kidini ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya machafuko sehemu mbalimbali duniani hususan barani Afrika.Lakini tofauti hizo hustawi vizuri zaidi mahala ambapo kuna manung’uniko kuhusu haki na usawa hasa katika uchumi.Ni rahisi kumshauri fukara aingie mtaani “kujikomboa” kuliko kumshawishi mtu afunge biashara zake akashiriki maandamano.Pia ni vigumu kwa watu wa makabila au dini tofauti wanaoshirikiana katika ajira na utoaji au upokeaji huduma kuanzisha vurugu ambazo kwa vyovyote zitapelekea kuathiri mahusiano yao (kwa mfano, mahusiano kati ya mfanyabiashara na mteja au mwajiri na mwajiriwa).

Tofauti na nchi kama Uingereza ambapo mvuto wa kisiasa miongoni mwa wapiga kura uko chini hasa kwa vijana,wengi wetu tulishuhudia namna kampeni za uchaguzi nchini Kenya zilivyogusa karibu kila sehemu ya maisha ya Wakenya,kama ambavyo chaguzi zetu huko nyumbani zinavyokuwa na mvuto mkubwa.Ni dhahiri kwamba amani ingeshapatikana iwapo nguvu nyingi zilizotumiwa na wanasiasa wa Kenya na vyama vyao kushawishi wapiga kura zingeelekezwa pia kwenye kutafuta mwafaka katika vurugu zinazoendelea.

Ni vigumu kubashiri namna gani vurugu hizo zitadhibitiwa na kumalizwa kwa vile Kibaki na Raila wanaonekana kutokubaliana katika njia sahihi za kuleta amani.Yayumkinika kusema kwamba hakuna uwezekano wa Kibaki na serikali yake kukubali mapungufu yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo kwa vile kwa kufanya hivyo watakuwa wameongeza nguvu kwenye hoja za Raila na wafuasi wake kwamba matokeo ya uchaguzi huo ni feki.

Kwa upande mwingine,Raila anafahamu gharama kubwa ya maisha na mali wanayoipata wafuasi wake kwa kupinga matokeo ya uchaguzi huo,na kukubali kushirikiana na Kibaki pasipo makubaliano ya kutengua ushindi wa rais itakuwa ni sawa na usaliti wa daraja la kwanza.Historia nayo haitoi matumaini ya amani kwa jirani zetu wa Kenya kwani hakuna rais yeyote (hasa barani Afrika) anayeamini alishinda uchaguzi kwa njia halali aliye tayari kukubali uchaguzi urejewe kwa minajili tu ya kuridhisha wapinzani wake au kutuliza machafuko nchini mwake.

Madhara ya muda mrefu ya kinachoendelea nchini Kenya ni kuzaliwa kwa kizazi chenye kinyongo.Ni kipi kinachoweza kufuta kinyongo cha mtoto aliyepoteza wazazi wake katika machafuko hayo?Kibaya zaidi ni kwamba kadri machafuko yanavyoendelea ndivyo kizazi hicho cha kinyongo kinavyozidi kuongezeka.

Miezi michache iliyopita Watanzania walitoa maoni kuhusu wazo la kuunda muungano wa nchi za Afrika Mashariki,na wengi wao walipinga uharakishaji wa muungano huo.Ni kama walifahamu kwamba kelele za kuwa na muungano zilikuwa za kisiasa zaidi kuliko kuzingatia hali halisi ndani ya nchi husika. “Mikoa” ambayo ingeunda “nchi” hiyo (yaani sie na Uganda,na pengine Burundi na Rwanda) imeshindwa kuwa na mchango wa maana wakati “mkoa mwingine” (Kenya) unazidi kuteketea.Sijui ingekuwaje iwapo haya yangekuwa yanatokea ndani ya muungano huo!

Baadhi ya wapinzani wa muungano huo walieleza bayana kwamba japo wanafahamu umuhimu wa ushirikiano,au hata kuungana kisiasa,ukweli unabaki kwamba nchi husika zina matatizo yake lukuki ambayo yanapaswa kushughulikiwa kwanza kabla ya kuyakuza kwa kuunda “nchi” kubwa zaidi iliyojaa vipande vyenye matatizo binafsi.

Jeuri za wanasiasa wa Kenya kutosikiliza vilio vya wananchi wao na kupuuza jitihada mbalimbali zinazofanywa na wasio Wakenya ni onyo muhimu kwa wenye ndoto za ya muungano wa Afrika Mashariki kwamba kama wanashindwa kuweka mbele maslahi ya nchi yao na wananchi wao watajali vipi maslahi ya Watanzania au Waganda.

Kubwa la kujifunza katika sakata hili ni jinsi ilivyo amani iliyojengwa kwa miaka miongo kadhaa inavyoweza kuyeyuka ndani ya kipindi kifupi kabisa.Harakati za kumfukuza mkoloni nchini Kenya zilichukua miaka mingi na kugharimu maisha mengi.Wakenya walikuwa bado wako katika harakati za kupata uhuru wa kweli hadi wakati machafuko yanaanza nchini humo.Kinachoendelea sasa ni sawa na kusigina jitihada na damu za mashujaa waliopigania uhuru wa nchi hiyo.

Kwa Watanzania,wakati tunaendelea kuwaombea jirani zetu amani (yaelekea hakuna la ziada tunaloweza kufanya zaidi ya hilo) ni muhimu kutambua kwamba amani na utulivu tulionao unaweza kudumu milele iwapo tu jitihada za makusudi zitafanyika kuondoa umasikini,kuhakikisha pato la taifa linatumika kwa maslahi ya wote na “haki” kuwa haki ya kweli kwa kila Mtanzania bila kuangalia tabaka.Kelele dhidi ya ufisadi na mafisadi ni sehemu muhimu ya harakati za kuhakikisha amani na utulivu nchini inadumu milele.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.