24 Oct 2008


SERIKALI ipo katika hatua za mwisho za kuingia ubia na Kampuni ya Sonangol kutoka nchini China kwa ajili ya kuendesha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Nia hiyo ya serikali ilitangazwa jana kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mohamed Misanga, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa ATCL.

Alisema ATCL, hivi sasa ipo katika hali mbaya kiuchumi kutokana na kuelemewa na madeni sambamba na kutokuwa na mtaji ambao utawezesha kuingia katika soko la ushindani.

Alisema awali serikali ilipozindua upya kampuni hiyo iliahidi kuchukua madeni yote na kutoa mtaji kwa kampuni hiyo, ili iweze kufanya biashara ya ushindani, lakini imeshindwa kutekeleza ahadi yake.

“Hali ya kiuchumi kwa ATCL ni mbaya, serikali imeamua kuinusuru kwa kuingia ubia na Kampuni ya Sonangol International ambayo wakati wowote kuanzia sasa watasaini mkataba,” alisema Misanga.

Alisema wabunge wameionya serikali kuwa makini na mwekezaji huyo, ili ubia huo usije ukawa kama wa kampuni ya SAA ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo iliyosababisha ATCL iwe hoi na kuidai madeni makubwa.

Alisema lengo la wabunge ni kuona serikali haiingi tena katika uingiaji mikataba mibovu ambayo imekuwa isainiwe na wataalamu wa serikali kila kukicha,” alisema Misanga.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuwa hivi sasa ATCL imekuwa ikinunua mafuta kwa siku kila ndege inapotaka kufanya safari badala ya kununua mafuta ya muda wa miezi mitatu au minne.

Aliongeza kuwa shirika hilo halikopesheki na kila kinachopatikana hutumika kwa madeni na shughuli za uendeshaji, jambo ambalo hulidhoofisha shirika hilo kununua na kukodisha ndege.

Alibainisha kuwa Serikali tayari imeamua kuiandikia barua Kampuni ya SAA kuitaka iache kuidai ATCL na badala yake iidai serikali ambayo ndiyo iliyoyachukua madeni.

Aidha, alisema ATCL ipo katika mchakato wa kuuza ndege yake aina ya Boeing 737-200 ambayo inadaiwa kutumia mafuta mengi sambamba na kupitwa na wakati.

“Uamuzi huu utasaidia kupunguza gharama zisizo za lazima kwa shirika lakini pia itasidia kupatikana kwa fedha kidogo zitakazotumika kwa mambo mengine,” alisema Misanga.

Aidha, alikanusha kuwa ATCL hakuna ndege mbovu zilizoletwa hivi sasa kwani kuna Mamlaka mbalimbali ambazo huzithibitisha ndege hizo kabla ya kuanza kazi.

CHANZO: Tanzania Daima

Hivi hatuwezi kuwauliza wenzetu Wakenya au Waethiopia kwanini wao wameweza lakini sie tunashindwa?Well,pengine Kenya na Ethiopia ni mbali,if so kwanini tusiwadadisi wazalendo wenzetu wa Precision Air?

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2020

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Nisapoti

Podcast

Chaneli Ya YouTube