17 Oct 2008

Picha kwa Hisani ya MichuziJr
Pinda ataja sababu za kilimo kuwa duni
IMEELEZWA kuwa kilimo cha Tanzania bado kiko duni, kutokana na wakulima wengi kulima bila ya kutekeleza kanuni za kilimo bora na hivyo kuchangia kushuka kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini. 

Hayo yamesemwa jana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda katika ukumbi wa Bz mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kuhamasisha kilimo, uliohusisha mikoa ya Kigoma, Mbeya , Ruvuma , Rukwa , Iringa na Morogoro . 

Waziri Pinda alisema kuwa kilimo cha Tanzania bado duni kutokna na eneo linalolimwa ni kidogo na tija ni ndogo, ambapo alisema inakadiliwa kuwa eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta milioni 44 na eneo linalotumika ni sawa na asilimia 24 ya eneo hilo. 

Alisema kuwa kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji lina hekta milioni 29.4 hata hivyo eneo linalotumika ni sawa na hekta 290,000 sawa na asilimia moja . 

“Ni vyema tukaangalia kuongeza maeneo ya kulima kama kweli tumedhamiria kuongeza tija katika sekta ya kilimo," alisema Waziri Pinda . 

Aidha waziri Pinda aliongeza kuwa mbali na changamoto hiyo katika sekta ya kilimo bado huduma za ugani ni duni na kudai uzoefu unaonesha kuwa wakulima wengi wanalima bila ya kufuata kanuni za kilimo bora . 

Alisema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha kilimo chao kushuka na kutokuwa na tija na mavuno yao kuwa kidogo, hali ambayo wizara inatakiwa kujiuliza ina maofisa ugani wangapi mikoani na vitendea kazi kiasi gani viko katika ofisi zao, ikiwa pamoja na kujiwekea mipango ya kazi. 

Waziri Pinda alisema kuwa sababu nyingine zinazochangia hali hiyo ni matumizi duni ya teknolojia za kilimo cha kisasa hasa matumizi ya jembe la mkono, badala ya matrekta. 

Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 70 ya wakulima nchini hutumia jembe la mkono na asilimia 20 hutumia plau wakati asilimia 10 hutumia matrekta takwimu ambayo ni ndogo katika kufikia malengo ya uzalishaji na kuboresha sekta ya kilimo nchini.


CHANZO: Majira

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.