Showing posts with label KILIMO TANZANIA. Show all posts
Showing posts with label KILIMO TANZANIA. Show all posts

30 Jul 2016


Kwa rafiki zangu huko Facebook, nadhani mwakumbuka stori moja niliyowasimulia kitambo kuhusu rafiki yangu mmoja, Mtanzania, ambaye kitaalua ni mfamasia, lakini ameamua kuweka kando taaluma hiyo na kujikita katika kilimo.

Baadhi ya marafiki zangu waliomba mawasiliano nae, na takriban wote walinipa mrejesho kuwa wamevutiwa sana na jitihada za @d33dat, ambaye binafsi ninamchukulia kuwa ndio mwasisi wa falsafa ya "Kilimo kama Ajira."

Angalia mahojiano mafupi kati yake na kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC Swahili yaliyofanyika jana Ijumaa Julai 29, 2016.



9 Oct 2011



Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete,

Kwanza naomba kukupa salamu za heri kwa siku yako ya kuzaliwa uliyoadhimisha jana.Mungu akuzidishie uhai,afya njema na nguvu ya kuendelea kututumikia Watanzania wenzako.

Baada ya salamu hizo,naomba niende kwenye mjadala usio rasmi ulioanzia juzi huko Twitter.Katika majibu yako kwa swali langu tunawezaje kuuelezea umasikini unaowakabili wakazi wa wilaya Kilombero (ambapo ulizuru majuzi) licha ya utajiri mkubwa wa raslimali-hususan ardhi yenye rutuba ambayo imelifanya eneo hilo kuwa maarufu kwa kilimo cha mpunga na nafaka ya mchele-ulieleza, naomba nikunukuu, "In Kilombero we've extension officers,SACCOS,market facilitation and mechanization initiatives.Some are using these opportunities" (kwa Kiswahili,Kilombero tuna maafisa ugani,vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa,uwezeshaji masoko,jitihada za matumizi ya mashine.Baadhi ya watu wanatumia fursa hizi."

Labda nikuulize,Mheshimiwa Rais,je uliona umasikini usiofichika unaowagubika wakazi wengi wa wilaya ya Kilombero?Ninatumai uliouna japo watendaji wengi wana tabia ya kuificha taswira zisizopendeza ili waonekane wanatekeleza wajibu wao ipasavyo.Hapa ninamaanisha si ajabu iwapo watendaji wa serikali wilayani Kilombero wangeamua kukupa picha ya "kila kitu ni shwari" ili uridhishwe na utendaji kazi wao.

Tuje kwenye jibu lako with an assumption kwamba uliona umasikini unaowakabili "matajiri" wa Kilombero (in the sense of kuwa wakazi kwenye sehemu yenye utajiri lukuki).Mheshimiwa Rais,tatizo la Tanzainia yetu halipo kwenye uwepo wa maafisa wenye majukumu fulani bali ni iwapo maafisa hao wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.Mara kadhaa,Mheshimiwa Rais,umelazimika kutumia madaraka yako kuwasaidia wananchi licha ya uwepo wa waziri husika,naibu wake,katibu mkuu,naibu katibu mkuu,mkurugenzi wa idara husika,mkuu wa mkoa,mkuu wa wilaya na pengine diwani kama si mwenyekiti wa serikali ya mtaa.

Mheshimiwa Rais,kama ilivyo kwenye sheria zetu nzuri na ambazo kwa hakika zingesimamiwa ipasavyo tungemedu kukabiliana na matatizo kama ufisadi kwa ufanisi (kwa mfano kwa kiutumia ipasavyo Sheria ya Uhujumu Uchumi) ni wazi pia kuwa laiti wengi wa watendaji unaoamini kuwa wanaweza kuwasaidia wananchi kufikia malengo yao ya kimaendeleo wangetimiza wajibu wao ipasavyo basi tusingeendelea kuwa moja ya nchi masikini kabisa duniani licha ya utajiri lukuki wa raslimali tulionao.

Ni wazi,Mheshimiwa Rais,kuwa laiti maofisa ugani unaowazungumzia huko Kilombero wangekuwa wanatimiza wajibu wao ipasavyo sio tu baadhi ya wakazi au wazawa wa neo hilo kama mie tusingekuwa na cha kulalamikia bali pia eneo hilo lingeweza kabisa kuwa mithili ya Saudi Arabia ya Tanzania (kwa kulinganisha uzalishaji mafuta wa Saudi na mchele wa wilaya ya Kilombero).Wnachofanya maofisa ugani unaosifia uwepo wao ni kukupatia ripoti nzuri zenye kutia matumaini lakini kimsingi wao ni miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya eneo hilo.

Mheshimiwa Rais,ninaomba kuafikiana nawe kuwa uwepo wa SACCOs umelta ukombozi mkubwa kwa wananchi hususan wa vijijini.Masikini hawa ambao hawana amana za kuwawezesha kukupa benki wamepata ukombozi mkubwa kupitia SACCOs.Hata hivyo,nyingi ya taasisi hizo zimekuwa zikikabiliwa na na tatizo sugu la mtaji mdogo ambao unapelekea kuhudumia wananchi wachache kuliko ilivyopaswa.

Mhehimiwa Rais,utakumbuka jinsi wajanja (polite word for mafisadi) walivyo-misuse "Mamilioni ya Kikwete" na sehemu ya fedha hizo kuishia mifukoni mwao badala ya kuwafikia walengwa.Moja ya taasisi ambazo zingenufaika sana na mpango huo ni SACCOs mbalimbali nchini.

Lakini pia,Mheshimiwa Rais,katika kuonyesha namna serikali yako isivyotoa kipaumbele cha kutosha kwa wakulima waodogo wadogo,fedha za stimulus package zilielekezwa zaidi kwa viwanda na kampuni (ikiwa pamoja na zilizo hewa) badala ya kuwatupia macho wakulima hawa.

Kwa hakika inapendeza kumwona mwekezaji wa kigeni akiwekeza katika kilimo cha mpunga.Lakini ni wazi,Mheshimiwa Rais,ingependeza zaidi iwapo uwekezaji huo ungefanywa na wakulima hao masikini.Sio tu uwekezaji huo ungeinua hali za maisha za walalahoi hawa lakini pia ungeweza kutoa ajira za kutosha na kusaidia harakati za maendeleo ya eneo hilo na nchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Rais,kuhusu kuwezesha upatikanaji wa soko,ninaamini kuwa laiti ungepeata wasaa wa kusikia kilio cha wakazi wa eneo hilo (na pengine maeneo mengine ya uzalishaji) ungebaini kuwa licha ya utajiri wa mpunga/mchele,wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na tatizo sugu la masoko.Kimbilio kubwa limekuwa kwa walanguzi ambao hujazana huko kila unapojiri msimu wa mavuno.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba wakati tunaadhimisha mika 50 ya uhuru wetu,baadhi ya wakazi wa Kilombero hullazimika kurejea njia za kale za uuzaji wa mazao yao ambapo barter trade hutumika kuwawezesha baadhi ya wakulima kumudu kupata bidhaa kama mitumba ya nguo,sukari na hata chumvi.Hivi Waziri husika ana mpango gani mahsusi ya kusaidia wakulima wa aina hii?Tumesikia kuhusu Kilimo Kwanza na Mapinduzi ya Kijani lakini kama ilivyokuwa katika zama za Ujamaa na Kujitegemea kauli mbiu hizo zimesihia kuwa matamko tu yenye malengo mazuri lakini utekelezaji sio wa kuridhisha.

Kuhusu sapoti katika matumizi ya teknolojia kwa maana ya mashine za kilimo,laiti Mheshimiwa Rais ungeongea na wananchi wa eneo hilo wangekufahamisha kuwa wanakabiliwa na tatizo sugu la uhaba wa matrekta.Machache yaliyopo ni mabovu na gharama zake ni kubwa mno kiasi kwamba wakulima wanalazimika kutegemea jembe la kono.Miaka 50 ya uhuru lakini mkulima wa Kitanzania bado anategemea zaidi jembe la mkono badala ya mashine za kisasa.

Mheshimiwa Rais,moja ya sababu zilizowashawishi Watanzania kukupa kura nyingi mwaka 2005 (na baadaye mwaka 2010) ni dhamira uliyoonyesha mwanzoni kuwa unataka kupunguza (kama si kumaliza kabisa) matatiao yanayowakabili Watanzania.Kihistoria,unafahamika kama miongoni mwa viongozi wachache walio karibu sana na wananchi (hata kabla hujaingia Ikulu).Uelewa wako kuhusu matatizo ya Watanzania ulitarajiwa kutoa suluhisho la tatizo la umasikini wa kutupa unaowakabili Watanzania wengi.

Binafsi siamini kuwa wewe binafsi ndio pekee wa kulaumiwa bali baadhi ya watendaji wako.Sasa,Mheshimiwa Rais,mwaka 2006 ulionya watendaji wabovu wasitafsiri vibaya upole wako kwani usingesita kuwawajibisha.Lakini ukweli ni kwamba wengi wa watendaji wako hao wameendela kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Rais,mwezi huu wa Oktoba utakuwa unatimiza mwaka mmoja mzima tangu uingie madarakani kwa awamu nyingine ya Urais.Lakini kama unakumbuka vyema,nyingi ya hadi ulizotoa mwaka 2005 hazijatekelezwa,na ukichanganya na za mwaka 2010 utaona kuwa una kazi ya ziada kumaliza utekelezaji wa ahadi hizo kabla hujang;atuka rasmi mwaka 2015.

Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa ili tuendelee tunahitaji WATU,ARDHI,SIASA SAFI na UONGOZI BORA.Sasa Mheshimiwa Rais,sio tu kwamba watu wapo bali pia   wana nia na kiu ya maendekleo yao binafsi na ya jamii zao.Ardhi ipo ya kutosha ikama ulivyoona huko Kilombero.Nadhani kinachokosekana na SIASA SAFI na UONGOZI BORA.

Mheshimiwa Rais,umebakiwa na miaka minne tu kabla hujamaliza muda wako kwa mujibu wa sheria.Hivi  ungependa umalize muda wako ukiwa na legacy isiyopendeza kuhusu masikini wa kutupa ambao hawana mbele wala nyuma.

Mwaka 2005 uliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania lakini baadhi yetu sasa tumekuwa tukitafsiri kama Mauisha Bora kwa kila fisadi.Ninaamini kabisa,Mheshimiwa Rais uliota ahadi hizo ukiamini kuwa zinatekelezeka.Lakini kwa bahati mbaya-au makusudi- hali yetu ni mbaya sana.Maendeleo tunayodaiwa kuyafikia yameendelea kubaki ndoto ya mbali.

Sasa Mheshimiwa kwa vile umebakiwa na miaka minne tu na rundo la ahadi zinazosubiri utekelezaji basi ninaomba utumie muda huu ulisailia kufanya jtihada za makusudi kuhakikisha unakumbukwa kwa jambo moja au jingine la msingi.

Basi Mheshimiwa Rais naomba nisikuchoshe sana na makala hii ndefu.Ninaamini una kila SABABU,na UWEZO lakini kiachokosekana ni NIA ya kuifikisha Tanzania mahala inapostahili kuwepo kimaendeleo.Kama Rwanda wamemudu kupiga hatua licha ya mauaji ya kimbari huko nyuma kuathri umoja wao kitaifa,na kama Botswana na Sychelles zinamudu kuwa majabali ya uchumi barani japo tunaweza kuwa na utajiri mkubwa wa raslimali kuliko nchi hizo,hivi tuna sababu gani ya kuendelea kusuasua kiuchumi na kimaendeleo kiujumla?

UKIAMUA,INAWEZEKANA

26 Jun 2009

Ifakara katika picha niliyopiga mwezi Mei mwaka jana.

Mji una neema ya ardhi yenye rutuba inayokubali kilimo cha mpunga,mahindi,na mazao mengine lukuki.Ungetegemea mapinduzi ya kijani yaanzie sehemu kama hizi lakini kama kawaida ya wanasiasa wetu,maneno meeengi huku vitendo vikiishia kwenye michakato,mikakati,vipaumbele,semina elekezi na ubabaishaji mwingine kama huo.Habari hii hapo chini licha ya kunigusa kutokana na ukweli kwamba wilaya ya Kilombero ndio nyumbani,pia inawakilisha matatizo yanayowakabili mamilioni ya Watanzania wanaotegemea kilimo kama njia pekee ya kuwawezesha kuishi.Isome kwanza:

Kilombero, Ulanga wahofia njaa

na Joseph Malembeka, Kilombero

BAADHI ya
wananchi wanaoishi katika wilaya za Kilombero na Ulanga mkoani Morogoro wameiomba serikali kuingilia kati ununuzi holela wa mazao ya chakula unaofanywa na walanguzi sasa.

Ombi hilo limekuja kutokana na ongezeko kubwa la wafanyabiashara kuingia wilayani humo na kununua kwa kasi mpunga ukiwemo uliovunwa na uliopo mashambani.

Wakizungumza na Tanzania Daima juzi, John Lyapi na Selemani Kinana walisema kama serikaliikifumbia macho suala hilo kuna hatari ya wakazi wengi wa wilaya hizo kupata baa la njaa mwaka huu.

Lyapi alisema kwa sasa walanguzi hao wamevamia zaidi katika tarafa za Malinyi na Mtimbira na kuwarubuni wananchi kuwauziampunga wao kwa sh 5,000 kwa debe na huku wakiwafuatilia hadi mashambani.

Alisema kutokana na wengi wa wakulima kwa kipindi hiki wanatokea mashambani inawawia vigumu kukataa kupokea fedha hizo, kwani wengi wao huwa kama wanaanzamaisha mapya majumbani baada ya kuhamia mashambani kwa muda mrefu.

Naye Kinana mkazi wa Kilombero alisema kila kukicha bei ya mazao ya chakulaimekuwa inapanda na kushuka kutegemeana na kuongezeka kwa walanguzi hususanwakubwa.

Alisema endapo serikali itakabiliana kikamilifu na walanguzi haoitasaidia kuondoshwa chakula kingi wilayani humo na kunusuru janga la njaa.

Kwa mujibu wa wakuu wa wilaya hizo Evarist Ndikilo (Kilombero) na DkRajabu Rutengwe (Ulanga) kwa nyakati tofauti walisema tayari halmashauri zimeagizwa kuwatangazia wananchi kuacha mtindo huo.

Walisema mbali na kupiga marufuku kwa wananchi kuuza vyakula pia wanakusudia kuweka sheria itakayowasaidia, iliwaweze kujikwamua na janga la njaa kwa kutouza vyakula hivyo.

CHANZO: Tanzania Daima

Mkuu wa wilaya ya Kilombero anaweza hata kuamuru jeshi la polisi likamate wanaouza chakula,lakini haitokuwa ufumbuzi wa tatizo hilo.Bottom line is,watu wanauza akiba ya chakula chao ili kukabiliana na ugumu wa maisha.Unadhani kuna mkulima anayependa kula mbegu?

Hivi kwanini hizo trilioni moja na ushee zilizotengwa kukabailiana na msukosuko wa uchumi zisiangalie walalahoi kama hawa?Katika mpango huo ambao bado nina wasiwasi unaweza kuishia kuwa-bailout mafisadi kama si kuzua EPA nyingine,wakulima wa kawaida wamepewa kisogo licha ya hadithi za KILIMO KWANZA.

Ukitembelea Ifakara katika kipindi hiki cha mavuno utapata picha moja ya kusikitisha.Wakulima wa mji huo wanatumia takriban robo tatu ya mwaka kulima mpunga (na kilimo cha mpunga kiko very demanding huku kikitegemea kudra za Mungu kwenye hali ya hewa).Baada ya mavuno,mji huo unafurika wanunuzi wa mpunga na mchele,huku wengine wakiufuata hukohuko mashambani.Kwa vile muda huu wengi wa wakulima huwa hoi kiuchumi,bei ya mpunga na mchele huwa ni karibu na bure.Pia baadhi ya wakulima wenye mahitaji mengine muhimu kama vile nguo,sukari,nk huamua kupokea bidhaa hizo badala ya fedha (barter trade) alimradi siku ziende mbele.Na muda si muda,wakulima hao hujikuta wameuza hadi mbegu na kurejea mahala palepale walipoanzia: hawana hela,hawana chakula.

Tuna wizara ya wajibu wa kushukulikia kilimo,na tuna wizara yenye wajibu wa kuwasaidia wakulima kupata masoko ya kuaminika ya mazao yao.Pia tuna wizara inayowajibika na masuala ya ushirika.Kwa makusudi,wizara hizi zimebaki majina tu japo utasikia zinatengewa mamilioni kama sio mabilioni,sio tu kwa ajili ya "kuleta ufanisi" bali pia huduma za ukarimu-chai,chakula,nk.

Tuna takriban Watanzania wenzetu 50 wenye wadhifa wa uwaziri au unaibu waziri.Sehemu kubwa tu ya fedha za walipa kodi inatumika kuwahudumia waheshimiwa hawa.Lakini ni ukweli usiopingika kuwa utendaji kazi wao ni chini ya kiwango.Walikabidhiwa dhamana ya kutekeleza kaulimbiu ya MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA lakini yayumkinika kuhitimisha kuwa sanasana wamefanikiwa kujitengenezea maisha bora wao wenyewe na "wafadhili wao wa kisiasa".


Kwa mmiliki wa makazi hayo pichani juu,habari za Maisha Bora kwa Kila Mtanzania ni kama utani mbaya kwake.Japo amezungukwa na ardhi kijani yenye rutuba,hajui jioni itakuwaje let alone hiyo kesho au msimu ujao wa kilimo na mavuno.Ukimwambia kuwa kuna kaulimbiu mpya ya
KILIMO KWANZA anaweza kukushushia ngumi!

17 Oct 2008

Picha kwa Hisani ya MichuziJr
Pinda ataja sababu za kilimo kuwa duni
IMEELEZWA kuwa kilimo cha Tanzania bado kiko duni, kutokana na wakulima wengi kulima bila ya kutekeleza kanuni za kilimo bora na hivyo kuchangia kushuka kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini. 

Hayo yamesemwa jana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda katika ukumbi wa Bz mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kuhamasisha kilimo, uliohusisha mikoa ya Kigoma, Mbeya , Ruvuma , Rukwa , Iringa na Morogoro . 

Waziri Pinda alisema kuwa kilimo cha Tanzania bado duni kutokna na eneo linalolimwa ni kidogo na tija ni ndogo, ambapo alisema inakadiliwa kuwa eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta milioni 44 na eneo linalotumika ni sawa na asilimia 24 ya eneo hilo. 

Alisema kuwa kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji lina hekta milioni 29.4 hata hivyo eneo linalotumika ni sawa na hekta 290,000 sawa na asilimia moja . 

“Ni vyema tukaangalia kuongeza maeneo ya kulima kama kweli tumedhamiria kuongeza tija katika sekta ya kilimo," alisema Waziri Pinda . 

Aidha waziri Pinda aliongeza kuwa mbali na changamoto hiyo katika sekta ya kilimo bado huduma za ugani ni duni na kudai uzoefu unaonesha kuwa wakulima wengi wanalima bila ya kufuata kanuni za kilimo bora . 

Alisema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha kilimo chao kushuka na kutokuwa na tija na mavuno yao kuwa kidogo, hali ambayo wizara inatakiwa kujiuliza ina maofisa ugani wangapi mikoani na vitendea kazi kiasi gani viko katika ofisi zao, ikiwa pamoja na kujiwekea mipango ya kazi. 

Waziri Pinda alisema kuwa sababu nyingine zinazochangia hali hiyo ni matumizi duni ya teknolojia za kilimo cha kisasa hasa matumizi ya jembe la mkono, badala ya matrekta. 

Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 70 ya wakulima nchini hutumia jembe la mkono na asilimia 20 hutumia plau wakati asilimia 10 hutumia matrekta takwimu ambayo ni ndogo katika kufikia malengo ya uzalishaji na kuboresha sekta ya kilimo nchini.


CHANZO: Majira

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.