31 Oct 2008


HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI TAREHE 31 OKTOBA, 2008

Ndugu Wananchi;

Tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia rehema zake tunapata fursa ya kuzungumza mwisho wa mwezi huu Oktoba kwa mujibu wa utaratibu wetu mzuri. Mwisho wa mwezi uliopita sikuweza kuzungumza nanyi kwa sababu ya kuwa New York, Marekani kwa shughuli za kila mwaka za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kwanza suala la OIC,
Pili Uchumi wa Dunia,
Tatu mauaji ya wenzetu Albino, 
Nne Madai ya Walimu
Na tano suala la Mfuko wa Madeni ya Nje yaani EPA.

Suala la OIC

Ndugu Wananchi;

Hivi karibuni kumekuwepo na mjadala usiofurahisha kuhusu suala la Jumuiya ya Kiislamu (OIC) kufuatia taarifa iliyotolewa Bungeni na kwenye vyombo vya habari na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe. 

Nasema isiyofurahisha kwa sababu mjadala huo unaelekea kuchukua sura ya malumbano baina ya waumini wa dini zetu kuu na kupandikiza chuki baina ya serikali na wafuasi wa dini hizo. Ni mjadala unaosikitisha sana jambo ambalo napenda kuwasihi Watanzania wenzangu tusiuendeleze na wala tusiuendekeze. Unaweza kulipeleka taifa
letu mahali pabaya.

Napenda kukumbusha kuwa mwaka 1993 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitakiwa kujiondoa kutoka kwenye jumuiya ya OIC baada ya kujiunga kwa hoja kwamba hilo ni shirika la kimataifa ambalo wanachama wake ni mataifa, hivyo kwa hapa nchini kama kungekuwepo na kujiunga iliyostahili kufanya hivyo ni Serikali ya Muungano. Hayo ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo basi Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ilijiondoa kwenye OIC na kuiachia Serikali ya Muungano kushughulikia jambo hilo na kuamua ipasavyo. 

Tangu wakati huo Zanzibar wamekuwa wanasubiri uamuzi wa Serikali ya Muungano. Kila wakati wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekuwa wanaliuzia suala hilo. Hivi sasa jambo hilo limekuwa mojawapo ya kero kubwa za Muungano zinazoshughulikiwa na Kamati ya pamoja ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi. Kwa mujibu wa muundo wa Serikali ya Muungano kila kero ya Muungano ina Wizara yake inayohusika nayo
kushughulikia. Kwa suala hili ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ndiyo inahusika. Wizara imeamua kufanya utafiti wa jambo lenyewe na wakishakamilisha utafiti huo watoe ushauri kwa Serikali zetu mbili kwa uamuzi. 

Ndugu Wananchi;

Nijuavyo mimi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa haijakamilisha kazi yake ya utafiti na hivyo haijawasilisha Serikalini matokeo ya utafiti wao pamoja na mapendekezo yao kwa ajili ya kutafakariwa na kuamuliwa ipasavyo. Kwa sababu hiyo basi Serikali haijafanya uamuzi wowote kuhusu suala la OIC kwa vile hatujapokea mapendekezo yoyote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa. Wizara haijamaliza kazi yake. Katika hali hii, nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na subira. Tuwaache Wizira ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wafanya kazi yao kwa utulivu ili waishauri Serikali kwa hekima na busara.


Aidha, napenda kuwaomba pia hapo Wizira itakapokamilisha kazi yake (sijui lini) na kuyafikisha mapendekezo yake Serikalini, tuiache Serikali yetu nayo itafakari kwa utulivu ili ifanye uamuzi ya hekima utakaojenga na kulihakikishia taifa letu umoja, amani, utulivu na upendo miongoni mwa raia wa nchi yetu.

Ndugu zangu;

Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa siku zote mimi na wenzangu wote Serikalini tunatambua unyeti wa suala la OIC. Aidha, tunatambua dhamana yetu ya kuwa makini katika kufikia uamuzi na kwa uamuzi wenyewe tutakaoufanya kuhusu suala hili. Kamwe hatutafanya uamuzi ambao utavuruga mambo na kuhatarisha amani, umoja na
mshikamano wa nchi yetu, Serikali zetu na watu wake.

Hivyo narudia kuwasihi Watanzania wenzangu tuiache Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilifanyie kazi kwa ukamilifu suala hili. Tujiepushe na vitendo au kauli ambazo zitawatia watu hofu na kujenga chuki miongoni mwa raia wa nchi yetu wanaopendana na kujenga chuki na kutoaminiana baina ya raia na Serikali yao inayowapenda na kuwathamini.

Madai ya Malimbikizo ya Walimu

Ndugu Watanzania wenzangu;

Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia leo, linahusu madai ya malipo ya walimu kuhusu malimbikizo ya mishahara, nauli za likizo na posho za uhamisho na kujikimu. Kama sote tujuavyo Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kiliiarifu Serikali nia yake ya kuitisha mgomo wa walimu wote nchini iwapo madai ya walimu yapatayo shilingi bilioni 16.4 (bilioni 12.2 kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na bilioni 4.2
kwa walimu wa shule za sekondari na vyuo vya walimu) yatakuwa hayajalipwa yote ifikapo tarehe 15 Oktoba, 2008. 

Baaada ya kupata taarifa hiyo Serikali iliwasiliana na uongozi wa juu wa CWT kwa nia ya kufanya mazungumzo nao kuhusu madai yao. Bahati nzuri uongozi wa CWT ulikubali, hivyo mazungumzo yakafanyika baina ya Serikali na CWT. Upande wa Serikali uliwakilishwa na wajumbe 12 kutoka Wizara za Utumishi, Fedha na Mipango, TAMISEMI na Elimu na Mafunzo ya Ufundi na upande wa CWT uliwakilishwa na wajumbe saba (7).

Kiongozi kwa upande wa Serikali alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Hawa Ghasia na upande wa CWT kiongozi alikuwa Ndugu Yahaya Msulwa ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu, Tanzania. 

Katika mazungumzo hayo ukiacha suala la madai ya malipo yalikuwepo pia masuala mengine matano yafuatayo:

1. Kupandishwa madaraja (vyeo).

2 CWT kushirikishwa katika uhakiki wa madai ya walimu.

3. Kuundwa kwa Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Sekta ya Elimu (Teachers Joint
Staff Council).

4. Kuandaliwa kwa Taratibu za Uendeshaji wa Utumishi wa Walimu (Teachers Service
Scheme) na

5. Kuwarudisha kwenye Orodha ya Malipo (Payroll) walimu waliofutwa kwenye orodha hiyo.

Baada ya siku 15 za mazungumzo muafaka ukafikiwa juu ya masuala yote sita na makubaliano hayo ya pamoja kutiwa saini na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe kwa niaba ya Serikali na Katibu Mkuu wa CWT,Ndugu Yahaya Msulwa kwa niaba ya Walimu. 

Jambo lililotushanga na kutusikitisha sote ni kauli ya Rais wa CWT, Ndugu Gratian Mkoba tarehe 08 Oktoba, 2008 kwamba mgomo unaendelea. Tena akasisitiza kuwa mgomo huo hauna muda maalum mpaka mwalimu wa mwisho atakapokuwa amelipwa. Nilimuagiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwa, wawatafute viongozi wa CWT kuzungumza nao kuwasihi waache kuendelea na mgomo, lakini juhudi zote hazikuzaa matunda. 
Waling’ang’ania kuendelea na mgomo na ndipo tukaitumia haki yetu kwa mujibu wa Sheria ya Kazi Na. 6 ya mwaka 2004 kuomba Mahakama kuu kitengo cha Kazi iamuru mgomo usiwepo na kuwataka viongozi wa CWT warudi kwenye mazungumzo na Serikali. 

Viongozi wa CWT wanapinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu na kutaka waendelee na mgomo. Tupo mahakamani tunasubiri uamuzi wa Mahakama kuhusu rufaa ya CWT.

Ndugu wananchi;

Najua wapo walioushangaa uamuzi wa Serikali wa kwenda mahakamani na wapo pia watu waliotukejeli kwa uamuzi wetu huo. Kwanza kabisa ni haki ya mwajiri kufanya hivyo na mahakama ndicho chombo chenye mamlaka ya kuamua. Lakini, pia, tumefanya hivyo kwa nia njema ya kunusuru janga ambalo mfumo wa elimu ungelikuta nchini kwa mgomo huo ambao ungekuwa wa aina yake. Maana kuendelea kuwepo mpaka mdai wa mwisho atakapolipwa wakati inawezekana baadhi ya wadai wanaweza kuwa na vithibitisho ambavyo vinaweza kukataliwa na mlipaji kwa kutokuwa halali ni sawa na kuwa na mgomo wa kuchukua muda mrefu sana. Unaweza usiwe na ukomo kwani ubishi kuhusu uhalali wa stakabadhi ya mdai unaweza kuchukua muda mrefu. Vinginevyo ichukuliwe kuwa, kila anachodai mwalimu ni sahihi kilipwe na Serikali. Hilo nalo ni gumu kwani upo ushahidi wa kuwepo kwa stakabadhi za kughushi. 

Ndiyo maana sisi katika Serikali tumeyaafiki makubaliano ya kufanya uhakiki wa pamoja utakaoshirikisha CWT na Serikali. Nilipokuwa Tabora hivi karibuni nilielekeza kuwa uhakiki huo ufanywe shule kwa shule na mwalimu kwa mwalimu; usifanywe kwa kukagua mafaili tu katika maofisi ya Maafisa Elimu na Utumishi. Kufanya hivyo kutatupa taarifa iliyo sahihi ya nani anadai nini. Itasaidia kung’oa mzizi wa fitina. Hakutakuwepo na kudaiana kusikokwisha. 

Vilevile, itatusaidia kujua uweli wa walimu waliopo na wako wapi. Kuna minong’ono ya kuwepo walimu hewa ambao pesa zao hutolewa kila mwezi. Pia, wapo walimu waliotangulia mbele ya haki ambao bado wamo kwenye orodha ya utumishi na mishahara yao huendelea kutumwa na hairejeshwi. 

Ndugu Wananchi;

Napenda kuitumia nafasi hii kuwahakikishia walimu na wananchi wote wa Tanzania, kuwa Serikali inawathamini na kuwajali walimu. Serikali ya Awamu ya Nne inaweka kipaumbele cha juu sana kwa maendeleo ya elimu, ndiyo maana bajeti ya elimu ndiyo bajeti kubwa kuliko zote. Inachukua asilimia 19.8 ya bajeti yote ya Serikali. 

Watanzania wote ni mashahidi wa nguvu kubwa tuliyoielekeza katika elimu ya sekondari, elimu ya juu na elimu ya ufundi. Mimi na viongozi wenzangu kuendeleza elimu ni agenda yetu kuu. 

Katika juhudi hizo tunatambua nafasi na umuhimu wa Mwalimu. Hatuwezi kua watu tunaohimiza upanuzi wa elimu lakini tunampuuza mwalimu. La hasha! Mara nilipoingia madarakani, katika mkakati wa kuboresha maslahi ya watumishi, kundi tuliloanza nalo ni walimu na tumeendelea kulipa kipaumbele kila tuliposhughulikia makundi mengine. 

Katika mkakati wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma tulitambua kuwa hatutaweza kufanya hivyo kwa watumishi wote kwa wakati mmoja. Tukaona tukienda kwa makundi tunaweza. Kundi la kwanza tuliloanza nalo ni walimu. Natambua haja ya kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini, ni nia yetu kufanya hivyo. Tumekuwa tunafanya hivyo katika miaka mitatu hii na tutaendelea kufanya hivyo miaka ijayo. 
Pamoja na hayo, mwezi April, 2008, tumewalipa Walimu Shs. 7.2 bilioni, sehemu kubwa ikiwa ni madeni ya nyuma kabla sisi hatujaingia madarakani. Huu ni ushaidi kwamba tunawajali walimu. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kupuuza maslahi ya walimu.


Uchumi wa dunia

Ndugu Wananchi;

Katika hotuba yangu ya Tanga wakati wa sherehe za kuzima Mwenge na maadhimisho ya miaka 9 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, nilizungumzia hali ya uchumi wa dunia na hasa wa mfumo wa fedha unaozikabili nchi zilizoendelea. 

Nilielezea hofu yangu kuhusu athari ambazo zinaweza kutokea kwa nchi yetu ikiwa uchumi wa dunia utaendelea kuyumba kufuatia misukosuko ya kifedha ya kimataifa. Nilisema kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani huenda nayo ikakumbwa na madhara yatokanayo na kuyumba huku kwa uchumi wa dunia.

Nilieleza kuwa nchi yetu inaweza kuathirika kwa njia zifuatazo:
1. Kupungua kwa mauzo yetu ya nje kwenye masoko ya nchi za Magharibi kwa sababu ya kupungua kwa uwezo wa watu na nchi hizo kununua bidhaa na huduma. Mazao yetu ya biashara tunayouza nje yanaweza kuathirika kwa ajili hiyo; 

2. Kuna uwezekano wa kupungua kwa mapato yanayotokana na utalii, kutokana na kupungua kwa watalii kutoka mataifa hayo kwa sababu watu wa nchi hizo kuathiriwa na mgogoro wa kifedha unaozikumba nchi zao. Wapo watu wengi ustawi wao wa kifedha na kiuchumi umeshuka kwa sababu ya kuanguka kwa masoko ya hisa na mabenki na kufilisika
kwa makampuni. 

3. Kuna wasiwasi kwamba uwezo wa nchi za Magharibi kutoa misaada kwa nchi yetu utapungua, kutokana na fedha nyingi kutumika katika kuokoa vyombo vya fedha katika nchi zao. Nilitoa mfano kuwa, katika wiki chache zilizopita, nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Ubelgiji, Iceland na Sweden, zimetangaza kutoa jumla
ya dola za kimarekani trilioni 1.8 kusaidia kuyaokoa baadhi ya mabenki yaliyopata
msukosuko. 

4. Msukosuko huu unaweza kusababisha kupungua kwa mikopo ya kibiashara au kuongezeka kwa gharama za mikopo kutoka nje, na hivyo kupungua kwa uwezo wa mabenki yetu kukopesha.
5. Vilevile kuna wasiwasi wa uwezekano wa kupungua kwa uwekezaji kutoka nje. Huenda uwekezaji hapa nchini kutoka Afrika ya Kusini na Kenya ukapungua kwa kuzingatia kuwa
nchi hizo zina mahusiano zaidi na mtandao wa masoko ya fedha ya kimataifa.

6. Pamoja na hofu ya kupungua kwa uwekezaji kutoka nje, kuna uwezekano mkubwa wa kupungua kwa kiwango na kasi ya uwekezaji wa ndani kutokana na kupungua kwa uwezo wa taasisi zetu za fedha kukopesha. Wakati mwingine ni hofu ya hayo yanayotokea
duniani.

7. Na mwisho msukosuko huu unaweza kusababisha kupungua kwa fedha zinazotumwa na Watanzania walioko nje ya nchi yetu.

Ndugu Wananchi;

Tangu nilipozungumzia suala hili kule Tanga, bado hakujawa na unafuu wowote katika uchumi wa dunia licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na mataifa makubwa kurekebisha hali hiyo. Uchumi wa nchi tajiri duniani umeendelea kuyumba kwa maana ya kupungua na kudorora. Hali hiyo imeanza kuleta athari katika biashara ya kimataifa. Mahitaji ya mafuta yameanza kupungua na kusababisha kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. Hali inaweza kuwa hivyo hivyo hata kwa bidhaa zetu tunazouza nchi za nje.
Kadhalika, tunaendelea kuyasihi mataifa makubwa kiuchumi na nchi tajiri kwa jumla zinazokabilia na matatizo haya yaendelee kuchukua hatua madhubuti na za haraka kurekebisha hali iliyojitokeza katika mfumo wa kifedha wa kimataifa. Aidha, tunasisitiza umuhimu wa kuutazama upya mfumo wa kifedha wa kimataifa unavyofanya kazi kwa nia ya kurekebisha kasoro zilizopo. Naamini kufanya hayo kutatuhakikishia
kwamba msukosuko unaoikumba dunia hivi sasa utapatiwa ufumbuzi na kwamba utaepukika na hautatokea tena siku za usoni. Madhara yake ni makubwa kwa uchumi wa nchi zetu changa na maisha ya watu wetu.

Kwa mantiki hiyo napenda kutumia fursa hii kuungana na viongozi wengine duniani katika kukaribisha wazo la Rais George Bush wa Marekani la kuitisha mkutano maalum wa kimataifa wa kuzungumzia tatizo la kifedha la kimataifa. Ni matumaini yangu kwamba, mkutano huo utatoa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Bahati mbaya Afrika imesahaulika katika mkutano huo. Hii ni dunia yetu sote yanayotokea popote yanatuhusu sote.

Mauaji ya Maalbino

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;

Tarehe 19 Oktoba, 2008 nilipewa heshima ya kupokea maandamano ya kulaani na kupinga mauaji ya wenzetu wa jamii ya Maalbino. Katika maandamano hayo nilielezea kusikitishwa kwangu na matendo hayo ya kikatili na ya aibu kwa nchi yetu. Siku ile nilitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki na kushirikiana katika mapambano haya
halali ili kwa umoja wetu tuweze kukomesha mauaji ya ndugu zetu hao.

Leo nataka kuwaelezea azma ya kuwataka Watanzania kote nchini kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na mauaji ya Albino nchini. Kwa maana ya waganga, wauaji, wauzaji na wanunuzi wa viungo vya Albino. Nawataka Watanzania wawataje kwa siri watu hao ili Serikali ifuatilie kwa karibu nyendo zao, kuwabana ipasavyo na kuwachukulia hatua mwafaka. Utaratibu huu ulitusaidia sana katika mapambano dhidi ya majambazi,
naamini utatusaidia hata katika mapambano haya halali na ya haki. Baada ya muda si mrefu tutatoa maelekezo juu ya utaratibu wa kutoa na kukusanya taarifa hizo. 

Nataka kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali yenu haitakaa kimya wakati raia wasiokuwa na hatia wanaendelea kuteswa na kuuawa. Albino ni mwanadamu kama alivyo mwanadamu mwingine yeyote. Ana haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha na mali zake kutoka katika jamii. Kuwaua kwa sababu yoyote ile si haki na ni kosa kubwa. 

Isitoshe kwa sababu wanazouliwa ni aibu kwa mhusika na fedheha kubwa kwa jina zuri la nchi yetu. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kuelimisha jamii juu ya madhara ya fikra potofu zinazoenezwa na waganga wa kienyeji wenye tamaa na uchu wa kujipatia utajiri. Utajiri utapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuwa na nidhamu katika utendaji na matumizi ya mapato yako. Sote tunawajibika kuwafichua
watu hawa ambao ni hatari katika jamii yetu. Naomba ushirikiano wa kila mmoja wetu ili tuikomeshe na kuondoa aibu hii.

Fedha za EPA

Ndugu wananchi;
Jambo la mwisho ninalotaka kuzungumzia leo linahusu urejeshwaji wa fedha za akaunti ya madeni ya nje katika Benki Kuu inayojulikana kwa kifupi kama EPA. Wengi wenu mtakumbuka kuwa, nilipozungumza na Bunge tarehe 21 Agosti, mwaka huu, nilieleza kwa kirefu yaliyotokea, hatua tulizochukuwa na mahali tulipokuwa tumefikia katika kulishughulikia suala hili. Nisingependa kuwachosha kwa kurudia tena yale niliyoyasema. 

Siku ile nilieleza katika hotuba yangu kwamba niliwataka wale wote waliokuwa miongoni mwa yale makampuni 13 yaliyolipwa shilingi 90,359,078,804, waliochukua fedha ambao walikuwa bado hawajarejesha fedha hizo kufanya hivyo ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2008. Aidha, niliagiza uchunguzi kwa zile kampuni 9 zilizolipwa shilingi
42,656,107,417 uendelee. Kamati iliomba idhini ya kuwasiliana na vyombo husika vya dola vya mataifa husika ya nje ili kupata ukweli na kukamilisha uchunguzi wao.

Ndugu wananchi;

Nilielezea pia kwamba baada ya tarehe 31 Oktoba, 2008, kwa wale ambao watakuwa hawakuteleza, hatua za kisheria zichukuliwe. Leo ndiyo siku ya mwisho. Napenda kuwajulisha kuwa, taarifa nilizoletewa majira ya mchana leo, ni kuwa kiasi cha shilingi 69,326,437,650 kati ya shilingi 90,359,078,804 zilikuwa zimerejeshwa. Hii ni sawa na asilimia 76.7. 

Kesho tarehe 01 Novemba, 2008 taarifa kamili itatolewa juu ya kiasi halisi ambacho kitakuwa kimerejeshwa. 

Pamoja na kufanya hivyo, nimekwishatoa maelekezo kamili kwa wale ambao hawakutimiza malipo, Kamati ikabidhi majalada yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka mara moja, kwa hatua zipasazo za kisheria. 

Mkurugenzi wa Mashtaka ni idara huru ya Serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi. Yeye ndiyo mwenye mamlaka ya kuendesha mashtaka mahakamani baada ya kupokea taarifa za upelelezi kutoka kwa Jeshi la Polisi na Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. 

Ndugu Watanzania wenzangu;

Kuhusu uchunguzi uliokuwa unaendelea kufanywa kuhusu yale makampuni 9, nasubiri taarifa yao mpya kuhusu maendeleo ya uchunguzi huo. Taarifa niliyopewa wiki mbili zilizopita zinaonyesha kuwa polisi wetu bado hawajapata majibu kutoka kwa wenzao katika nchi walizoomba msaada. Hivyo, nakusudia kuwataka waendelee kufuatilia kwa wenzao ili hatua zipasazo ziweze kuchukuliwa.

Ndugu wananchi;

Kwa mara nyingine tena napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Kamati ya Mwanasheria Mkuu kwa kazi nzuri iliyofanya ambayo mbali na kubaini namna ya tuhuma za uhalifu zilivyofanywa, pia ilibaini wahusika na kuwabana kiasi cha kufanikiwa kurejeshwa kwa fedha ambazo vinginevyo zingepotea kabisa. 

Lakini kubwa zaidi, nawashukuru wananchi kwa uvumilivu na uelewa wao wakati wote serikali ilipokuwa inalishughulikia sakata hili la aina yake katika historia ya nchi yetu. Tumefarijika sana kwa uelewa na ushirikiano wenu. Nawaomba tuzidi kushirikiana katika mambo yote yanayohusu mustakabhali wa nchi yetu.

Aidha, utaratibu wa kuzigawa fedha hizo kwa ajili ya shughuli za kilimo na miundombinu zimekamilika.

Madai ya Wastaafu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Katika hotuba yangu ya leo, sikuweza kugusia suala la madai ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu Serikali inaandaa tamko rasmi litakalowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Mheshimiwa Mustafa Mkullo wiki ijayo. Hivyo nawaomba sote tuvute subira.


Hitimisho

Kabla ya kumaliza napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika mambo yote ya msingi yanayoihusu nchi yetu. Licha ya mawimbi ya hapa na pale ambayo tunapambana nayo katika safari yetu, tumeendelea kuimarisha umoja na mshikamano wetu ambao ndio nguzo na mhimili wa taifa letu. 

Nawaomba tuendelee kufanya hivyo kwa kutambua kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kujenga nguvu ya pamoja ya kuendeleza taifa letu. Nawasihi tujiepushe na mambo yanayoweza kutugawa na kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu na badala yake tuimarishe maelewano, mshikamano na umoja wa kitaifa. 


Mungu Ibariki Afrika;
Mungu Ibariki Tanzania.
Asanteni kwa kunisikiliza.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube